Maalim Seif akana kumuandaa Jussa

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akiwasilisha hotuba yake kwa waandishi wa habari wa vyombo mbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar hapo Rahaleo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) amesema yeye binafsi hana chama bali anayetaka kuwania nafasi yeyote ya uongozi ndani ya chama afuate utaratibu wa chama unavyoelekeza. Sambamba na hilo amekanusha kumuandaa Ismail Jussa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kwa siku za baadae.

Maalim Seif ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Idara ya habari Maelezo Zanzibar alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali kutoka bara na Zanzibar, mkutano ambao ulilenga kuelezea mafanikio na changamoto za mwaka mmoja wa Serikali ya umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Katika maswali ya waandishi wa habari walitaka ufafanuzi juu ya kile kinachoonekana katika siku za hivi karibuni kubebea nafasi kubwa katika vyombo vya habari ndani na nje ya nchi juu ya mgogoro uliopo ndani ya chama chake cha CUF.

Akijibu shutuma mbali mbali ndani ya Chama Cha CUF ambazo zimechukua kweli kursa kadhaa za magazeti na vituo vya radio na televsheni, Maalim Seif amesema hakuna mgogoro ndani ya chama hicho bali zilizopo ni chokochoko tu zinazofanywa na baadhi ya watu bila ya kuzingatia utaratibu wa chama.

Amesema utaratibu wa chama hicho unaruhusu kukosolewa mtu yoyote kupitia vikao vya chama na sio kupigana madongo kwenye vyombo vya habari kama inavyoonekana hivi sasa ambapo baadhi ya viongozi wamekosa uvumilivu na kuanza kurushiana maneno katika vyombo vya habari.

“Kama kuna mtu mwenye hoja aziwasilishe kwenye vikao halali vya chama na sisi tutazijadili kwa kina, kwa hiyo Mheshimiwa Hamad Rashid na wenziwe kama wana hoja tutaonana kwenye vikao, na yeyote mwengine mwenye ubavu tushindane kwenye mkutano mkuu” alisema Maalim Seif akionesha kukerwa na suala hilo.

Kuhusu shutuma za kumuandaa Mheshimiwa Ismail Jussa kuwa katibu mkuu wa Chama hicho siku zijazo, Maalim Seif amekana shutuma hizo na kusema kuwa wanaohusika kupendekeza nafasi hizo ni mkutano mkuu wenye wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Chama hiki si changu, na katibu mkuu kuhojiwa ndani ya chama chetu sio tatizo, anaweza kuhojiwa wakati wowote kupitia utaratibu unaokubalika, na anayetaka nafasi ya ukatibu mkuu aje anakaribishwa wakati utakapofika”, aliongeza Maalim Seif.

Katika hatua nyengine Maalim Seif alisema changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi katika marekebisho ya katiba mpya ya Tanzania ni utaratibu wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano, ili wazanzibari nao waweze kuitumikia nafasi hiyo.

Amesema utaratibu uliopo sasa wa kumpata mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaikosesha fursa Zanzibar, na kutaka kuwepo ya utaratibu kwa nafasi hiyo kutumika kwa awamu baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema licha ya changamoto zilizopo tangu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar mwaka mmoja uliopita, yapo mafanikio mengi yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuendeleza maridhiano ambayo yameleta faraja kubwa kwa wananchi kwa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif amewataka watendaji wa Serikali kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoweya, jambo ambalo linazorotesha utendaji wa serikali. kauli hiyo ya Maalim Seif sio ya mara ya kwanza ni mfululizo wa agizo la kuwataka watendaji wafanye kazi zao kwa uadilifu na kuzingatia majukumu yao ambapo tayari Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein mara kadhaa ameshasikikika akitoa agizo hilo lakini bado watendaji wa serikali wanaonekana kusuasua katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Wafanyakazi lazima mubadilike katika kuwatumikia wananchi na muachane kabisa na mambo ya kizamani ya kufanya kazi kwa kumuangalia mtu fulani, tunataka serikali yenye kuaminiwa na wananchi wake na pia tunataka kuona wananchi wanaiamni serikali yao na viongozi wao na bila ya shaka tukiamua kubadilika basi wananchi wataiunga mkono serikali yao, kwani lengo la serikali ni kuwatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi na hilo ndio lengo letu tunataka kufike huko. bila ya kufanya hivyo wananchi watapoteza iamni na serikali yao ”, Alisisitiza Maalim Seif

Maalim Seif ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu maswali mbali mbali kutoka kwa waandishi wa habari ambapo suali moja lilishutumu utendaji wa Serikali ya Umoja wa kitaifa kuwa bado haijafanya kazi ipasavyo na kuonesha baadhi ya watendaji hawajaukubali mfumo huo na wanaendelea kutoa huduma kwa upendeleo, ikiwa ni pamoja na kunyimwa haki ya vitambulisho vya uzanzibari ukaazi kwa baadhi ya wananchi hasa wanaoonekana kutokea katika upande wa CUF.

Akizungumzia kuhusu vitambulisho vya uzanzibari ukaazi Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka watendaji kuheshimu agizo la Rais na kwamba kutowapa vitambulisho wazanzibari wenye sifa ni kosa la jinai.

_____________________________________________________________

Habari na Hassan Hamad, Picha na Salmin Said (OMKR)

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s