Hakuna mgogoro CUF, zilizopo ni chokochoko – M.Seif.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema miongoni mwa changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi katika marekebisho ya katiba mpya ya Tanzania ni utaratibu wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano, ili wazanzibari nao waweze kuitumikia nafasi hiyo.
Amesema utaratibu uliopo sasa wa kumpata mgombea wa urais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaikosesha fursa Zanzibar, na kutaka kuwepo ya utaratibu kwa nafasi hiyo kutumika kwa awamu baina ya bara na visiwani.
Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa changamoto hiyo leo katika ukumbi wa Idara ya habari Maelezo Zanzibar alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali kutoka bara na visiwani, mkutano ambao ulilenga kuelezea mafanikio na changamoto za mwaka mmoja wa Serikali ya umoja wa Kitaifa.
Amesema licha ya changamoto zilizopo tangu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar mwaka mmoja uliopita, yapo mafanikio mengi yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuendeleza maridhiano ambayo yameleta faraja kubwa kwa wananchi
Katika hatua nyengine, Maalim Seif amewataka watendaji wa Serikali kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoweya, jambo ambalo linazorotesha utendaji wa serikali.
“Wafanyakazi lazima mubadilike katika kuwatumikia wananchi na muachane kabisa na mambo ya kizamani ya kufanya kazi kwa kumuangalia mtu Fulani”, Alisema Maalim Seif
Maalim Seif ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali lililoshutumu utendaji wa Serikali ya Umoja wa kitaifa kuwa bado baadhi ya watendaji hawajaukubali mfumo huo na wanaendelea kutoa huduma kwa upendeleo, ikiwa ni pamoja na kunyimwa haki ya vitambulisho vya uzanzibari ukaazi kwa baadhi ya wananchi hasa wanaoonekana kutokea katika upande wa CUF.
Akizungumzia kuhusu shutuma mbali mbali ndani ya Chama Cha CUF ambazo zimechukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari katika siku za hivi karibuni, Maalim Seif ambaye pia ni katibu mkuu wa CUF amesema hakuna mgogoro ndani ya chama hicho bali zilizopo ni chokochoko tu.
Amesema utaratibu wa chama hicho unaruhusu kukosolewa mtu yoyote kupitia vikao vya chama na sio kupigana madongo kwenye vyombo vya habari.
“kama kuna mtu mwenye hoja aziwasilishe kwenye vikao halali vya chama na sisi tutazijadili kwa kina, kwa hiyo Mheshimiwa Hamad Rashid na wenziwe kama wana hoja tutaonana kwenye vikao, na yeyote mwengine mwenye ubavu tushindane kwenye mkutano mkuu” alisema Maalim Seif akionesha kukerwa na suala hilo.
Kuhusu shutuma za kumuandaa Mheshimiwa Ismail Jussa kuwa katibu mkuu wa Chama hicho siku zijazo, Maalim Seif amekana shutuma hizo na kusema kuwa wanaohusika kupendekeza nafasi hizo ni mkutano mkuu wenye wajumbe kutoka bara na visiwani.
“Chama hiki si Changu, na katibu mkuu kuhojiwa ndani ya chama chetu sio tatizo, anaweza kuhojiwa wakati wowote kupitia utaratibu unaokubalika, na anayetaka nafasi ya ukatibu mkuu aje anakaribishwa wakati utakapofika”, aliongeza.
Akizungumzia kuhusu vitambulisho vya uzanzibari ukaazi Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka watendaji kuheshimu agizo la Rais na kwamba kutowapa vitambulisho wazanzibari wenye sifa ni kosa la jinai.

_________________________________________________________
Na Hassan Hamad

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s