Uhuru wa Tanganyika uliamsha ari kwa Zanzibar kujitawala

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akibonyesha Rimoti kufyatua Mafataki ikiwa ni sehemu ya kuzindua rasmi Mkesha wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50 Uhuru zilizofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja usiku wa kuamkia leo. Kutoka (kushoto) ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mke wa Makamu wa Rais, Mama Zakhia Bilal na (kulia) ni Mke wa Makamu wa Rais, Mama Asha Bilal.


Na Salim Said Salim
WAKATI Tanganyika (Tanzania Bara) ilipopata uhuru nilikuwa na miaka 15, lakini nilielewa kwa kiasi mambo ya kilimwengu. Nilikuwa darasa la 10 (Fomu 2) na msomaji wa kila siku wa magazeti na nikiandika habari, fani niliyoitumikia tokea utoto wangu hadi leo. Siku siku mbili kabla ya uhuru nilimuona mmoja wa wazee walionilea na jirani, kama pua na mdomo katika mtaa niliozaliwa wa Kisimajongoo, hayati Sheikh Abeid Amani Karume, akiwaarifu wazee wenzake kuwa alialikwa kwenda Bandari ya Salama (Dar es Salaam) kuhudhuria sherehe za Uhuru.

Mzee Karume aliyekuja kuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya 1964 alikuwa kiongozi wa chama cha Afro-Shirazi ambacho kilikuwa katika harakati za kupigania uhuru. Wakati ule Zanzibar ilikuwa na utawala wa kisultani, lakini chini ya himaya ya serikali ya Uingereza.
Mfalme alikuwa Seyyid Abdulla bin Khalifa bin Haroub El-Busaidy, baba wa mfalme Jemshid aliyepinduliwa 1964. Baadaye nilipata habari kwamba viongozi wa vyama viwili vikuu vya siasa Visiwani wakati ule, the Zanzibar Nationalist Party (ZNP – Hizbu) na Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP) pia walialikwa.
Vilikuwapo vyama viwili vyengine, lakini vilikuwa na wafuasi wachache . Navyo ni Chama cha Kimonisti cha Zanzibar (Zanzibar Communist Party) ambacho viongozi na wanachama wake walikuwa vijana wa umri wa chini ya miaka 25 na Chama cha Haki za Binaadamu ambacho kilionekana zaidi kama kikundi cha burudani. Chama kingine kilichokuja kujulikana kama Umma Party kilichoongozwa na marehemu Abdulrahman Mohammed Babu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Hizbu, kiliundwa katikati ya mwaka 1963 kufuatia mfarakano ndani ya Hizbu.
Siku ya mkesha wa uhuru wa Tanganyika nilikuwa na furaha ambayo sitaisahau. Hii ilitokana na timu yangu ya soka ya New Boys (baadaye ilijulikana kama Wolverhampton Wanderers na miaka iliofuata kuitwa Ujamaa) kuwashinda wapinzani wetu wa New Generation 2-1.

Kwa kiasi fulani zilikuwapo shamra shamra Visiwani kukaribisha uhuru wa Tanganyika huku watu wengi wakizifuatia habari kupitia ha kituo cradio cha Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC). Sauti ya Unguja (sasa Shirika la Utangazaji Zanzibar) llilikuwa na taarifa mbali mbali za sherehe za uhuru wa Tanganyika.
Baadhi ya watu waliokuwa na jamaa na waliojenga urafiki na wenzao Dar es Salaam wakati wa ziara za wana michezo wa pande hizi mbili kutembeleana kila mwaka wakati wa sherehe za Pasaka walikwenda Dar es Salaam kuangalia sherehe. Baadhi ya vikundi vya ngoma, hasa vile ambavyo wanachama wake wana asili ya Bara au nchi jirani, walipiga ngoma usiku kucha .
Vile vile kulikuwa na dansi – rumba, chakacha, pachanga na mitindo mengine ya zama zile – katika ukumbi uliojulikana kama “Salim Beni’ (Salim Band) katika eneo linalojulikana hii leo kama Michenzani.
Nayakumbuka maeneo matatu mengine yaliyopigwa ngoma. Mojawapo ni mtaa uliokuwa ukiitwa Six Four (Kwa Said Kibiriti), jirani na mtaa wa Kisimajongoo. Hapo Wanyasa (watu wenye asili ya Malawi) waliovalia kaptula, mashati na soksi ndefu, zote rangi nyeupe, na wakiwa wanapunga usinga mrefu walicheza ngoma ya Beni Bati.

Maeneo mengine yaliokuwa na ngoma ni Kachorora ambapo kulikuwa na ngoma ya Kiluwa (hii huchezwa sana Mtwara na Lindi) na Miembeni ambapo kulikuwa na ile ngoma inayojulikana siku hizi kama mdundiko. Ngoma hii wakati ule ilifahamika kama “Mbwa Kachoka”. Wakati watu wa Tanganyika wakifurahia uhuru, wenzao Zanzibar walikuwa wanajiuliza : Je, na siku kama hiyo itatokea Visiwani na itakuwa katika hali gani?
Ninakumbuka mzee mmoja aliyekuwa akiitwa Yusuf Jaha umaarufu wake Sir George Mooring (jina la aliyekuwa mwakilishi wa mwisho wa Malikia Elizabeth Zanzibar) na ambaye alikuwa karibu sana na familia ya Waziri Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abdulla Kassim Hanga alisema:” Naona kiza kitupu mbele.

Tuombe Mungu atupe kheri yake”. Suala la itakuwaje Zanzibar siku za usoni lilitokana na hali ya kisiasa kuwa tete, hasa katika kisiwa cha Unguja ziliotawaliwa na chuki, uhasama, ukabila, fitna, majungu na unafiki.
Siasa hizi chafu ndio ziliopelekea mamia ya watu kuuawa kikatili na wengine kujeruhiwa vibaya sana wakati wa uchaguzi.

Machafuko makubwa yalikuwa miezi 6 kabla ya uhuru wa Tanganyika wakati ulipofanyika uchaguzi wa Juni mosi, 1961. Watu wengi. Ninawajua watu wapatao 30 waliouawa katika ghasia zile, baadhi yao wazazi wa watoto niliokuwa nikisoma nao shule. Miongoni mwa waliouawa walikuwa wazee na watoto wachanga.
Ghasia zile zilizodumu kwa zaidi ya wiki mbili na kutulizwa na kikosi cha askari wa General Service Unit (GSU) kutoka Kenya na kundi la askari wa Kiingereza (Coast Stream Guards) walioletwa haraka Zanzibar. Baada ya Tanganyika kupata uhuru, viongozi wengi wa TANU na hasa Mwalimu Nyerere na marehemu Said Tewa, ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya familia za Wangazija waliokuwapo Zanzibar, walijihusisha sana na harakati za kupigania uhuru Visiwani.
Kilichoonekana, lakini sio kwa uwazi, ni kwa viongozi wa TANU kuwa karibu zaidi na ASP kuliko Hizbu na ZPPP katika harakati za kupigania uhuru wa Zanzibar, ijapokuwa kilikuwa na mawasiliano na vyama vyote. TANU haikutaka kuonekana kuiunga mkono ASP kwa uwazi kwa sababu makubaliano ya wanaharakati wa kupigania uhuru wa Afrika Mashariki na Kati waliounda vuguvugu lilioitwa Pan African Freedom Movement of East and Cetral Africa (PAFMECA) walikuwa wanasisitiza umoja wa wapigania uhuru.
Mwalimu Nyerere alikuwa mmoja wa waasisi wa Pafmeca ambayo iliundwa katika mkutano uliofanyika Mwanza mwaka 1961.

Wapigania uhuru mashuhuri kama Dk. Kiano, Tom Mboya na Roland Ngala (Kenya), Patrice Lumumba, Maurice Mpolo na Joseph Okito wa Congo Kinshasa waliouliwa tarehe 17 Januari mwaka 1961 na Pierre Mulele aliyeuawa mwaka 1968 baada ya kurudi nyumbani akiwa mgonjwa, Milton Obote (Uganda), Joshua Nkomo, Kenneth Kaunda na Harry Nkumbula na Hastings Kamuzu Banda (Rhodesia) walisisitiza umuhimu wa wapigania uhuru kuungwa mkono bila ya upendeleo.
Hata kiongozi wa African National Congress ya Afrika Kusini, mzee Nelson Mandela, alipoalikwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Pafmeca uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwezi Januari, mwaka 1962 alisitiza umuhimu wa umoja.

Alisema kama nchi za Kiafrika zilitaka kuthibitisha kuwa zinalaani ubaguzi uliokuwepo Afrika ya Kusini basi zilikuwa zisiwabague watu wa nchi nyengine. Miezi saba baada ya hotuba ile ya kihistoria mzee Mandela alikamatwa na makaburu na kuwekwa gerezani.
Zanzibar ilipata uhuru (wengine hawaitambui tarehe hii, lakini tukio la kihistoria huwa halifutiki) tarehe 10 Desemba, mwaka 1963. Serikali ilipinduliwa usiku wa kuamkia tarehe 12 Januari, mwaka 1964.

Taarifa zinaeleza kuwa marehemu mzee Abeid Karume na Abdulrahman Babu walikwenda Dar es Salaam wakati Mapinduzi yakiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Mapinduzi nayo yalikuwa na gharama kubwa za maisha, viungo na mali. Mpaka leo haijulikani idadi kamili ya watu waliouawa. Wapo wanaosema watu kama 70, lakini wengi wanaamini ni zaidi ya 200.
Tanganyika ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Miezi mitatu baada ya Mapinduzi, Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuanzisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili ni tukio ambalo hapo kabla hapakuwepo fununu juu ya matayarisho yake.
Tunaadhimisha miaka 50 ya uhuru huku Muungano ukikaribia kutimiza miaka 48 ya mafanikio yaliotupa furaha na matukio yaliotutia huzuni. Tumeshuhudia malalamiko juu ya Muungano kutoka kwa watu na taasisi za pande zote mbili za Muungano. Hapana ubishi juu ya udugu, urafiki na maelewano ya kihistoria waliokuwa nayo watu wa pande hizi mbili za Jamhuri ya Muungano hata kabla ya uhuru wa Tanganyika.
Wakati tukisherehekea miaka 50 ya uhuru tuache kulaumiana na tujitahidi kutatua matatizo yanayotukabili. Ni vizuri kujitathmini na kurekebisha dosari zilizopo ili panapo uhai na uzima tutapoadhimisha miaka 50 ya Muungano tuwe na maelewano mazuri zaidi na matatizo ya sasa yawe sehemu ya historia ya nchi hii.
_______________________________________________
CHANZO: MWANANCHI

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s