Ubabe wa Karume ulimuaibisha Nyerere na taifa

Ahmed Rajab

Hayaati Mwalim Julius K.Nyerere

SIKU moja nilipokuwa nikiongea na rais mmoja wa Zanzibar sebuleni Ikulu, Unguja, alinigeukia ghafla na kuniuliza: ‘Unafikiri Ukarume utarudi hapa?’ Sikudiriki kumjibu na wala sidhani kama alitaraji nimjibu maana mbiombio alijijibu mwenyewe, tena kwa mkazo, kwa kusema: ‘Hautorudi tena.’ Alipoutaja ‘Ukarume’ nilijua alichokikusudia: Ubabe wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.
Moja kati ya mambo yaliyomponza Mwalimu Julius Nyerere kimataifa tangu Tanganyika ipate uhuru mwaka 1961 ulikuwa huo ubabe wa Karume, aliyekuwa makamu wake wa kwanza walipoziunganisha nchi zao Aprili mwaka 1964. Ilikuwa ni aibu ambayo Nyerere aliishi nayo hadi mwaka 1972 wakati Karume alipouawa.
Pamoja na kuitia dosari Tanzania, huo ubabe wa Karume uliwafanya wenzetu wa Tanganyika walalamike, kwa kipindi hicho cha miaka minane, kwamba Zanzibar ilikuwa mzigo thakili juu ya migongo yao. Huo lakini ulikuwa mzigo ambao Nyerere alikuwa tayari kuubeba juu ya huo uzito wake bila ya kujali jinsi ulivyokuwa ukimdhalilisha na kumharibia jina.
Miaka hiyo, Zanzibar ilinuka duniani. Ilipokuwa inanukuliwa kwenye vyombo vya habari basi mara nyingi ilikuwa ni kwa mabaya. Jina ‘Zanzibar’ lilikuwa kisiwa cha mateso, madhila, ubaguzi, kukamatwa watu ovyo, kuwekwa watu vizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na mauaji.

Kulikuwako pia vioja na vichekesho kwenye utawala huo ingawa hivyo navyo vilikuwa na uovu wake.
Bila ya shaka Nyerere akiuona uovu huo na akiusema kichinichini lakini hakuthubutu kuuzima kwa sababu akimcha Karume. Na si pekee aliyekuwa akimuogopa Karume au utawala wake. Wazanzibari wa itikadi tofauti za kisiasa wakiishi kwa woga. Haikuwa ajabu kusikia watu wakilala na suruali na miswaki mifukoni wakihofia wasije kukamatwa usiku wa manane.
Hayo ni miongoni mwa masaibu waliyokuwa wakiyapata Wazanzibari kutokana na ubabe wa utawala huo; ubabe ambao haukuchagua nani wa kumuonea.Uliwaminya waliokuwa na wasiokuwa maadui wa Mapinduzi ya mwaka 1964. Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa kiongozi mpigania haki. Hilo halina shaka. Alikuwa kiongozi wa wengi, aliyepigania haki za wengi. Bahati mbaya aliposhika madaraka alizikanyaga hizo haki alizokuwa akizipigania na aliteleza. Kwa ufupi, alikuwa dikteta. Pingine mazingira aliyojikuta nayo na hasa fitna alizokuwa akipelekewa na wale waliomzunguka hayakumruhusu awe vingine.
Inamkinika pia kwamba si yeye aliyekuwa akitoa amri ya maovu yaliyokuwa yakitendeka. Nasema hivi kwa sababu Sheikh Karume alikuwa akiwasaidia aliowapenda bila ya kujali kabila zao au hata misimamo yao ya kisiasa hali ambayo ilibadilika aliposhika hatamu za uongozi wa nchi.

Official portrait of Sheikh Abeid Amani Karume issued by the Zanzibarian government probably in 1972

Bahati nyingine mbaya ni kwamba Karume pamoja na kuwa dikteta aliongoza utawala wa kikatili uliowategemea mahabithi kuwatia hofu wananchi. Kati ya hao ni wale waliokuwa kwenye mtandao wa ‘viwavi’ — watu waliokuwa wakilipwa pesa mbili tatu ili kuwapeleleza wananchi wenzao na kuwaripoti kwa Serikali kwa yaliyokuwa ya kweli na yasiyokuwa ya kweli.
Mbali na hivyo wivavi, kulikuwa na watumishi wa Idara ya Usalama waliofunzwa wakafunzika. Waalimu wao walitoka Idara ya Stasi, yaani idara ya polisi wa siri iliyokuwa ikitikisa nchini Ujerumani ya Mashariki. Vitimbi na uovu wa hao wanaoitwa ‘watu wa usalama’ wa Zanzibar ulikuwa sawa na ule wa akina Ton Ton Macoute, majahili waliokuwa wakitumiwa na dikteta wa zamani wa Haiti, Papa Doc Duvalier.
Ala kuli hali, kimsingi utawala wa Karume haukutofautiana sana na zile tawala za madikteta wa kimabavu wa siku hizo kama vile Idi Amin Dada wa Uganda au Jean-Bedel Bokassa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliyefurutu ada kuwapita wenzake alipojitangaza kuwa ni ‘mfalme’ wa taifa hilo.
Mithili yao, Karume naye aliifanya nchi yake kuwa kama milki yake. Katika siku za mwisho mwisho za uhai wake kulikuwa na ripoti kwamba aliamua kuhaulisha akiba nono ya sarafu za kigeni ya Serikali ya Mapinduzi kutoka akaunti ya Serikali na kuiweka kwenye akaunti yake binafsi katika benki moja ya Kirusi jijini London, Uingereza.
Tamko lake lilikuwa amri na hakuthubutu mtu, si Nyerere si mwingine, kumkosoa seuze kumpinga. Wala hakuthubutu mtu kumwingilia katika mambo ya ndani ya Zanzibar. Safari moja Nyerere alimpeleka Zanzibar waziri wake wa fedha, Amir Jamal, amuombe Karume aziingize katika mfuko wa Tanzania fedha za sarafu za kigeni ilizokuwa nazo Zanzibar. Mzee Karume alimtisha na kumtimua Jamal.
Mwishowe ilimbidi Mwalimu ende mwenyewe kuonana na Karume. Inasemekana kwamba alipolitaja suala hilo la kutaka fedha za sarafu za kigeni za pande hizo mbili za Muungano zichanganywe, Sheikh Karume alimjibu kwa kumuuliza: ‘Pesa zipi? Ikiwa hizi zenye picha yako, sawa. Lakini zenye kichwa cha queen (Malkia wa Uingereza) haiwezekani kwani hizo si zetu.’
Si Jamal pekee aliyetimuliwa na Karume. Aliwahi pia kulifukuza Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuusimamisha mradi wake wa kupiga vita Malaria. Alihoji kwamba mradi huo hauhitajiki Zanzibar kwani Malaria si tishio kwa vile Waafrika ni ‘Malaria proof’ yaani ni sugu kwa ugonjwa huo wa Malaria. Matokeo yake ni kwamba ugonjwa wa Malaria ambao ulikuwa unatoweka kutokana na juhudi za mradi huo ulirudi kwa nguvu Visiwani.
Kama nilivyokwishagusia waathirika wa ubabe wa utawala wake hawakuwa wote wapinzani wa Mapinduzi au watu wasioyapenda Mapinduzi ya mwaka 1964 kwani haikuchukuwa muda Mapinduzi hayo yalianza, kuwameza watoto wake wenyewe. Watu waliouliwa inadhaniwa tu kwamba wameuliwa kwani haikuwahi kutangazwa kwamba waliuliwa au hata kuwa wamehukumiwa kuuliwa. Wala hapakuwa na watu waliouliwa hadharani. Watu walipotea tu; haikujulikana walipotelea wapi na vipi.
Sio wote waliokamatwa waliouliwa. Kuna waliobahatika. Bahati yao ni kwamba badala ya kuuliwa waliteswa gerezani. Kuna walioachwa na chatu korokoroni. Kuna waliopigwa mpaka wakazirai. Kuna waliolawitiwa. Waliokuwa wakitenda hayo walikuwa watu waliobobea katika tasnia ya utesajiwa binadamu wenzao.
Wasiokuwa kifungoni au kizuizini walikabiliwa na mateso ya aina nyingine. Ukosefu wa vyakula ulisababisha foleni refu za watu waliokuwa wakijipanga kutoka hata kabla ya majogoo kuanza kuwika wakisubiri wauziwe mkate, unga au sukari. Karume alikataa msaada kutoka Bara akihoji kwamba kulikuwa na foleni refu hivyo kwa sababu wananchi walikuwa na pesa nyingi za kutumia.
Safari moja pale bei ya samaki ilipopanda kupindukia kiasi alisema kuwa sababu ilikuwa kufungwa kwa Mfereji wa Suez baada ya kuzuka vita baina ya Israel na nchi za Kiarabu mwaka 1967. Kulikuwa na mingine mbali na ukosefu mkubwa wa vyakula yaliyowasibu Wazanzibari. Kwa mfano, Karume alitoa amri kwamba asiyeMzanzibari hawezi kumuoa binti Wakizanzibari mpaka kwanza ailipe Serikali ya Zanzibar Shilingi 64,000 — siku hizo huo ulikuwa ni mkwiji mkubwa mno.
Halafu kulikuwa na ile kadhia — kashfa kwa hakika — ya mabinti Wakizanzibari wenye asili ya Kiajemi na ya Kiarabu walioolewa kwa nguvu bila ya ridhaa zao au idhini za wazee wao, kinyume na maamrisho ya dini ya Kiislamu. Visa hivyo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ndivyo vilivyoifanya Zanzibar inuke duniani.
Jumuiya ya kupigania haki za binadamu ya Amnesty International ilikuwa haishi kupiga makelele kuilaani Zanzibar kwa vitendo hivyo. Ilikuwa mstari wa mbele katika kuujulisha ulimwengu kuhusu wasichana wanne wenye asili ya Kiajemi, mmoja akiwa na umri wa miaka 14, wengine miaka 16, 17 na 20, walioshikwa kwa nguvu na wanajeshi waliokuwa na silaha na kuozeshwa wakubwa wa Mapinduzi.
Malalamiko yalifikishwa hadi Umoja wa Mataifa. Umoja wa Wanawake wa Tanzania nao ulipiga kelele ukisema kwamba ndoa hizo za kulazimishwa ziliiharibia jina Tanzania. Nilishangaa miaka kadhaa baadaye kumsikia kiongozi mmoja mswalihina wa taifa hili akitueleza mimi pamoja na Balozi Anthony Nyakyi kwenye hoteli moja jijini London kwamba ilikuwa sawa kwa Mzee Karume kuzishadidia ndoa hizo eti kwa sababu akitaka watu wachanganye damu ili iondoke fitina ya ukabila huko Zanzibar.
Hatua nyingine iliyokiuka haki za binadamu ni ile ya kuzivunja mahakama za kisheria na badala yake kuwekwa ‘Mahakama za Umma’ zilizokuwa na majaji wasio na elimu ya sheria. Washtakiwa hawakuwa na ruhusa ya kuajiri mawakili wa kuwatetea.
Visa hivyo na mateso mingine viliwafanya watu waikimbie nchi kwa wingi. Kutoka Zanzibar kwa njia halali ilikuwa shida kubwa. Kwa hivyo, watu walikimbilia sehemu za pwani za Tanzania Bara kwa mitumbwi, walioipagiza jina la VC10, aina ya ndege kubwa za siku hizo.
Mwenyekiti Mao aliyeongoza Mapinduzi ya China ya mwaka 1949 hakukosea alipoandika kuwa: ‘Mapinduzi si karamu ya chai. Si kama kuandika insha, kuchora picha au kutia nakshi…mapinduzi ni kitendo cha matumizi ya nguvu, ni kupinduliwa kwa nguvu kwa tabaka moja na tabaka jingine…’ Huku kwetu maneno hayo ya Mao yamegeuzwageuzwa kuwa ‘mapinduzi si lelemama.’
Alichokusudia Mao ni kwamba katika mapinduzi — ambayo ni machafuko makubwa ya kijamii — hali ya mambo kamwe haiwi shuwari. Watu huuliwa kwa lengo la kuyalinda mapinduzi. Historia lakini imetuonyesha kwamba mara nyingi watu huuliwa bure kwa kuonewa bila ya kuyazingatia mapinduzi. Hamna shaka yoyote kwamba moja ya makosa makubwa ya Mao ni kusababisha mamilioni ya watu kuuliwa bure.
Vivyo hivyo, moja ya makosa makubwa ya awamu ya mwanzo ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ni ubabe uliosababisha mauaji ya bure na vitendo vingine vilivyokiuka haki za binadamu na vilivyotendwa kwa sababu za kibinafsi kwa kutumia nguvu za kibabe.
Tunapoadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika hatuna budi pia kukumbuka jinsi ubabe huo ulivyolitia doa taifa hili.

____________________________________________________________________
CHANZO: RAIA MWEMA

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s