CCM Z’bar waanza kuhofia mjadala wa Katiba

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar , Vuai Ali Vuai

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar kimesema kimegundua kuwa baadhi ya maofisa wa nchi za nje wameanza kuingiza hisia zao katika mchakato wa kuunda Katiba mpya. Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar , Vuai Ali Vuai alisema mjini hapa jana kuwa baadhi ya maofisa hao wanakutana na wanasiasa kwa lengo la kupenyeza hisia zao juu ya Katiba mpya Tanzania inatakayoundwa baada ya mchakato unaoendelea.
Vuai alisema ni kinyume kwa maofisa hao kuingilia zoezi la mchakato huo, hasa katika hatua za awali, kwa sababu Tanzania ina uwezo wa kufanya maandalizi yote kwa kutumia akili za wananchi wake.

Bila kutaja majina na nchi za maofisa hao, Vuai alisema ingawa Tanzania itaendelea kuhitaji msaada wa kiuchumi kutoka mataifa ya nje, kitendo cha maofisa hao kuingia mchakato wa kuunda Katiba mpya hakikubaliki.

“Umasikini wetu ni wa kiuchumi, sio akili. Tunahitaji msaada wa kiuchumi, lakini namna ya kuunda Katiba mpya, watupe nafasi tuendeshe mambo yetu, hasa katika hatua za awali,” alisema Vuai.

Vuai ambaye bado anashikilia nyadhifa za serikali akiwa mkuu wa wilaya huko kaskazini Unguja alisema msimamo huo unazingatiwa na mataifa yote, ndio maana hata maofisa wa Tanzania walioko nje za nje hawakuthubutu kuingilia masuala ya uundwaji Katiba ya nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Hii ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kueleza wasiwasi wa chama chake juu ya mwenendo wa maofisa wa nchi za nje wanapofanya ziara huko Zanzibar katika kipindi hiki cha Tanzania kujiandaa kuandika Katiba mpya.

Mwanzoni wiki hii akizingumza kupitia kipindi cha Nyota ya Matukio kinachorushwa na Zenj FM, Vuai alisema baadhi ya maafisa wa nchi za nje wamebainika kukutana na baadhi ya wanasiasa huko Pemba kuzungumzia suala hilo .

Licha upinzani mkubwa, muswada wa sheria ya kuunda Tume ya Katiba Mpya ulipitishwa na Bunge mwezi uliopita mjini Dodoma na Rais Jakaya Kikwete tayari inaelezwa kwamba ameusaini.

Wasiwasi wa CCM dhidi ya maofisa wa kigeni umekuja huku jumuiya tano za kiraia visiwani Zanzibar zikiwa tayari zimeungana kuunda Baraza la Jukwaa la Katiba ambalo tayari limeanza kutoa elimu ya uraia kuhusu Katiba mpya.

Taasisi hizo ni Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Taasisi ya Utafiti katika Ukanda wa Bahari ya Hindi (ZIORI) na Chama cha Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA). Miongoni mwa wafadhili wa jukwaa hilo ni taasisi moja ya kiraia yenye makao yake nchini Kenya .

_______________________________________________

Habari na Charles Mwankenja

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s