Muungano ni kama koti likikubana unalivua – Sheikh Karume…

Hayati Mwalim Julius Kambarage Nyerere akichanganya udongo wa Zanzibar na wa Tanganyika kama ishara ya Muungano mnamo mwaka 1964 nchi mbili hizi zilipo ungana

ALASIRI moja nikiwa kwenye hoteli niliyoshukia mji mkuu wa Sudan, Khartoum Hilton, nilishuhudia vurumai kubwa katika sehemu ya karibu na lifti. Watu wakikimbilia huko wakiambizana kwa msisimko kuwa ‘sheikh amefika, sheikh amefika.’

Afisa wa serikali ya Sudan aliyekuwa na jukumu la kunihudumia (ambaye pia huenda alikuwa shushushu) naye alipiga mbio kumkimbilia huyo sheikh na mimi sikuwa na budi ila kupiga mbio na kumfuata.

Tulipofika kwenye lifti nilimwona huyo sheikh akiwa amevaa kanzu na bushti jeupe. Uso wake uliokuwa na ndevu kama za tambi ulikuwa mwembamba na ukiangaza chini. Nakumbuka alipiga kilemba lakini chake kilikuwa kidogo si kama ile milemba inayopendwa na Wasudani.

Kwa nukta chache sana nilimshuhudia huyo sheikh akiingia kwenye lifti na ndevu zake za tambi huku akizungukwa na kundi la waliokuwa wakimyenyekea.
Huyo sheikh alikuwa Osama bin Laden. Siku hizo hakuwa na umaarufu, au sifa ya uovu, aliyoipata miaka michache tu baadaye.

Wakati huo Rais Omar Hassan al-Bashir alikuwa akiandaa mijadala mbalimbali ya kuleta demokrasia na katiba mpya nchini humo. Lakini sidhani kama Osama bin Laden aliwasili Sudan kwa minajili hiyo kwani sikumbuki kumshuhudia tena kwenye vikao mbalimbali vilivyofanywa kwa zoezi hilo.

Kwa hivyo, siwezi kusema kwamba niliwahi kuonana na bin Laden lakini mtu niliyemuona mara kwa mara na niliyebahatika kuzungumza naye kwa faragha kwa muda wa saa mbili alikuwa sheikh mwengine, Hassan al Turabi ambaye wakati huo alikuwa na mahusiano mazuri na bin Laden.

Hapa wanaonekana Baba wa Taifa,Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(kushoto) akibadilishana na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume(kulia), nyaraka rasmi za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar miaka 44 iliyopita.

Tukiwa kwenye chumba cha maktaba yake nyumbani kwake katika sehemu za kaskazini za Khartoum, Turabi alizungumza kuhusu mahusiano ya Zanzibar na Oman. Katika masimulizi yake alinihadithia mengi kuwahusu Mwalimu Julius Nyerere na Mfalme Qaboos bin Said wa Oman. Sitoyanukuu aliyoniambia kumhusu Qaboos.

Ama kumhusu Nyerere, mwanasiasa huyo wa Sudan ambaye sasa ni mpinzani mkubwa wa serikali ya huko ambaye juzi tu alifunguliwa gerezani, alionyesha kuitilia shaka dhamira ya Nyerere ya kuziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar.

Turabi aliniambia kuwa dhamira halisi ya Nyerere kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar ilikuwa ni kuuvunja Uislamu katika Afrika ya Mashariki.

 Hiyo ni shtuma nzito na nyeti hasa sasa ambapo udini umeingia katika siasa za Tanzania. Ulimi wangu niliufyata.

Sina shaka yo yote kwamba Nyerere mwenyewe angeliisikia shtuma hiyo angekasirika bila ya kiasi. Yeye akishikilia kwamba kuziunganisha nchi hizi mbili ilikuwa hatua ya kuelekea lengo la kuleta umoja wa nchi zote barani Afrika.

Nyerere alianza kuuimba wimbo huo kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika uliofanywa Cairo mwaka 1965 alipozikaribisha nchi nyingine za Kiafrika ziingie kwenye Muungano huo. Kwa bahati, sijui nzuri au mbaya, hakuna nchi yo yote iliyomsikiliza. Hata Zambia iliyokuwa na fungamano kubwa na Tanganyika haikujiunga.

Historia inamsuta Nyerere. Inaonyesha kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuundwa kwa dhamiri ya kuleta umoja wa Afrika. Kwa mfano, nyaraka za Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, zinaonyesha ushahidi wa jinsi Marekani na Uingereza zilivyomtaka Nyerere auunde huo Muungano kwa manufaa ya nchi za Magharibi.

Nchi hizo, hasa Marekani na Uingereza, zikihofu Zanzibar, chini ya serikali ya Mapinduzi, kugeuka na kuwa ‘Cuba ya Afrika.’ Kwa ufupi, madola hayo ya Magharibi yakihofia kwamba Zanzibar ingeweza kuyasambaza mapinduzi ya Kikoministi katika bara la Afrika.

Si kwamba mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ya Kikoministi lakini hizo ndizo zilizokuwa fikra finyu za madola hayo katika enzi hizo ambapo Marekani na washirika wake walikuwa wakichuana na maadui zao Wakikoministi.

Mzee Abeid Amani Karume, wakati wa uhai wake

Maelezo ya uundwaji wa Muungano ni mengi — ya kweli na ya uongo yamekuwa yakitiwa sana hewani kiasi cha kwamba waliozaliwa baada ya Muungano kuundwa wanababaika; hawajui wayashike yepi wayaache yepi.

Visiwani Zanzibar, kwa mfano, kuna wenye kuamini kwamba viongozi wa Tanganyika walikuwa na njama ambayo hadi leo wanayo. Nayo ni njama ya kuiona Zanzibar inatoweka, kwamba wakitaka, na eti bado wanataka, kuifanya Unguja iwe sehemu ya Mkoa wa Pwani na Pemba iwe sehemu ya Mkoa wa Tanga. Yaani kwa ufupi wanataka kuimeza Zanzibar.
Lililo bayana ni kwamba waasisi wa Muungano, yaani Nyerere na Karume, hawakuwa na misimamo sawa kuhusu Muungano.

Nyerere aliwahi kuulizwa na mwandishi Colin Legum wa gazeti la Observer la Uingereza mwaka 1968 iwapo ataridhia pindi Zanzibar itataka kujitoa kutoka kwenye Muungano huo. Alijibu kwamba hatotumia nguvu na hatowapiga mabomu Wazanzibari waukubali Muungano ikiwa hayo yatakuwa matakwa yao.
Nyerere aliyasema hayo wakati Karume akiwa hai. Ingawaje, miaka baada ya Karume kufariki Nyerere alisema kwamba angeweza kuvumilia watu wake waangamize kila kitu ikiwa pamoja na Azimio la Arusha, lakini hakuwa tayari kuuona Muungano unavunjika.

Mzee Karume, kwa upande wake, aliufananisha Muungano na koti. ‘Unalivaa unapolihitaji na unalivua likikubana,’ aliwahi kusema. Juu ya tofauti hizo, hamna shaka yo yote kwamba waasisi wa Muungano wakitambua vyema kwamba Muungano waliouunda ni wa mataifa mawili yaliyo huru.

Siku mbili hizi kumekuwa na tetesi nyingi kwenye magazeti mbalimbali nchini Tanzania kuhusu Muungano na hatima yake. Kwa bahati si uhaini kulizungumza suala hilo wala kuzungumzia uwezekano wa kuvunjika kwa Muungano.

Hali kadhalika tunaona wenye kulijadili suala hili kwa jazba na wenye kuliangalia kwa makini. Kuna wenye kutaka pawepo na serikali moja tu nchini Tanzania, wakimaanisha kwamba serikali ya Zanzibar ifutwe. Kuna wenye kutaka Muungano uvunjwe. Na kuna wenye kushikilia kuwa muundo wa sasa wa Muungano usigeuzwe.

Lakini huu muundo wa sasa ambao umekuwako kwa muda unaokaribia nusu karne ndio uliowafanya Wazanzibari wengi walalame kwamba wamemezwa na Tanganyika.

Hayati Mwalim Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Muundo huo pia umewafanya watu wa iliyokuwa Tanganyika walalamike kwamba Zanzibar imekuwa mzigo mkubwa kwao kuubeba. Kwa hakika ni jambo la kusikitisha kusikia kuwa kuna viongozi Tanzania Bara ambao bado hawataki kukubali kuwa Wazanzibari wana hisia za uchungu dhidi ya Muungano.

Kwa mwenye macho ni wazi kwamba mfumo uliopo sasa hauridhishi na kwamba umezusha mashakil mengi kuliko natija. Hivyo, panahitajika mfumo mpya wa mahusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar, nchi mbili zilizo huru katika Muungano huu.

Wazanzibari wengi wanahisi kwamba ili udumu Muungano utabidi ubadili muundo wake na uwe na muundo wa serikali tatu. Tena katika mfumo mpya pasiwe na nchi moja itayojipa jukumu la kuiongoza nyingine, yaani pasizuke hali kama iliyozuka karibuni pale serikali ya Muungano ilipojaribu kuufikisha muswada wa kuipitia katiba bila ya kuishauri serikali ya Zanzibar.

Na kwa hili la katiba viongozi wa serikali ya Muungano lazima watambue kuwa mjadala tu wa kukusanya maoni ya wananchi hautoshi. Unahitaji kufuatiliwa na kongamano la kitaifa litakalowajumuisha wanasiasa, viongozi wa kidini, wawakilishi wa jumuiya na asasi za kiraia na jumuiya za kupigania haki za binadamu.

Katika nchi zote kulikofanyika mkutano wa kitaifa wa kuandika katiba mpya, kumewezekana kuwekwa misingi imara ya demokrasia na utawala bora.
Mfano mzuri ni Benin. Hii ni nchi ambayo iliwahi kujinata kuwa ya kwanza Afrika kufuata nadharia ya Marx na Lenin wakati wa utawala wa Mathieu Kerekou mnamo miaka ya 1970.

Licha ya hayo, Benin iliibuka kuwa nchi ya kwanza barani humu kulikubali wimbi la mabadiliko. Pakafanywa mkutano wa kikatiba mwaka 1990 uliofuatiwa na uchaguzi ambao ulimuangusha Kerekou 1991.

Miaka mitano baadaye Kerekou alirudi madarakani alipomshinda Nicephore Soglo. Mbali na Benin, kuna nchi pia kama vile Botswana na Mauritius, ambazo zinaweza kuzifunza nchi nyengine kuhusiana na demokrasia na utawala bora. Zinaweza kufanya hivyo kwa vile zina katiba zinazofuata misingi ya kisheria na si matakwa ya anayetawala. Na katiba hizo zinafanya kazi sawasawa.

Kwa Tanzania pamoja na hayo kuna haja kubwa ya kuzingatia utungwaji wa katiba utakaokwenda sambamba na suala la Muungano kwa pande zote mbili. Masuala haya mawili ni chanda na pete. Haitowezekana kupata katiba bila ya kupata suluhisho la suala la Muungano.

Inavyoonyesha ni kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaweza tu kuokolewa endapo katiba ya Muungano itafanyiwa marekebisho ili pawepo mfumo wa serikali tatu. Kilicho muhimu zaidi ni madaraka na mamlaka gani itapewa serikali ya Muungano na gani yatapewa serikali za kila moja ya nchi mbili katika Muungano huo.

Itakuwa kosa kuiendeleza ile dhana ya kwamba hakuna njia au mfumo wo wote mwengine wa kutetea na kuhami maslahi ya Tanganyika na maslahi ya Zanzibar nje ya Muungano kama ulivyo sasa.

Itakuwa pia ni upuuzi mtupu kushikilia kuwa urekebishwaji wa katiba utaoipa Zanzibar madaraka na mamlaka zaidi utahatarisha amani, usalama na ufanisi wa Tanganyika au kwamba Zanzibar itaweza kutumiwa na madola ya nje kuyadhuru maslahi ya Tanganyika.

___________________________________________________________

Makala ya Ahmed Rajab katika gazeti la Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s