Wazanzibari hawautaki Muungano

Vijana wa Kizanzibari wakipinga Rasimu ya Muswaada wa Uundaji wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya Kamati ya Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Samuel Sitta mapema mwaka huu.

Hakika ni ajabu kuwa baada ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, leo wanajitokeza vijana huko Zanzibar ambao wanaukataa huu Muungano. Kama kungetokea wazee ndio wamekuwa na rai hiyo labda kungekuwa na mantiki kuwa hao wanaukumbuka Uzanzibari wao ule ambao si sawa na ulivyo leo.

Hawa vijana wanachojua ni Muungano tu na Zanzibar huru kwao ni historia; ubaya wake na uzuri wake hawakuuona. Wanayoyajua ni ya kuhadithiwa tu ambayo yanaweza kuwa na chumvi nyingi ama yameungwa pilipili kichaa kali sana kiasi kwamba kama kingekuwa ni chakula basi wangekitema. Lakini sivyo ilivyo.

Wasomaji watakumbuka wakati fulani hata waziri mmoja wa Zanzibar alitamka kuwa ingawa yeye kazaliwa na kukulia katika Muungano alikuwa na maoni yake binafsi ambayo hayakupendelea huo Muungano, ingawa aliongeza kuwa hasa katika mfumo uliopo sasa.

Watanganyika na Wazanzibari wamekuwa na uhusiano wa siku nyingi sana kiasi kwamba kuna watu wa Kigoma na hata wa Songea, ikiwa mifano mizuri, ambao wana ndugu zao ama Pemba au Unguja.

Imekuwa ni jambo la kawaida walio na hali nzuri kuwa na nyumba Kisangani Kigoma na Zanzibar, na hizo ni nyumba kamili zikiwa na familia. Huko ni mbali hivyo ikifikiriwa pwani ya Tanganyika basi uhusiano kama huo ndio kabisa upo.

—Hawa ni wanafunzi wa skuli za Zanzibar ambao ni miongoni mwa vijana wanaoinukia katika elimu wanasoma wanafahamu mambo mbali mbali ya kilimwengu, ikiwemo siasa ya nchi yao. Ndio hawa basi ambao kesho na kesho kutwa wanakuja kuwa viongozi wa nchi hii jee ikiwa wazazi wao hajawaamulia mustakabali wa nchi yao na maslahi yao mazuri kisaisa kisiasa wataweza kuishi kwa usalama?

Kwa sababu hizo ulipotangazwa Muungano wa nchi hizi mbili kuna watu wengi walioona kuwa hilo ni jambo la busara, hao walikuwa wengi wa Bara. Inafahamika sasa kuwa wananchi wa Zanzibar tangu hapo walikuwa na mawazo tofauti.

Linaloweza kusikitisha zaidi miongoni mwa wa-Zanzibari ni kule kufahamika sasa kuwa kwanza Muungano wenyewe haukuhalalishwa na vyombo vinavyohusika kule Zanzibar.

Profesa Pir Issa Shivji ameliandikia sana somo hilo kwa marefu na mapana. Hivi sasa kumetokea maandiko mengine ya Al Marhum Sheikh Muhsin Baruwani na kingine kitabu kilichotolewa hivi karibuni “KWAHERI UKOLONI, KWAHERI UHURU”,kilichoandikwa na Dkt Harith Ghassany, huyu ni mzaliwa wa Zanzibar.

Yeye kapata udaktari wake Chuo Kikuu cha Havard huko Marekani. Kutokana na utafiti aliopitia ili kupata yale aliyoandika ni wazi kuwa yale mapinduzi yanayosemekana kuondoa utawala wa Sultani ulikuwa ni kitu kingine kabisa.

Hazikuwa njama za wananchi wa Zanzibar za kutaka kuleta mapinduzi yale na kuwa na utawala kama ule uliotawazwa (?) baada ya hayo yaliyoitwa mapinduzi.

Haya ni kutokana na maelezo ya baadhi ya wale waliokuwa jikoni kuyatayarisha na kuyapika mapinduzi yale. Jina ambalo linajitokeza sana ni lile la Hayati Mzee Victor Mkello. Huyu alikuwa ni kiongozi shupavu wa wafanya kazi katika mashamba ya mkonge huko Tanga na alikuwemo pia mstari wa mbele katika kupigania uhuru chini ya uongozi wa TANU.

Maelezo yake ya mapinduzi ya Zanzibar hayafai kubezwa, labda mpaka pale atakapotokea mtafiti mwingine atakayetoa maelezo ama hadithi mbadala.
Imetajwa huko nyuma kuwa katika kitabu alichoandika Al Marhum Sheikh Muhsin Barwani kuna maelezo juu ya hayo yanayoitwa mapinduzi.

Maelezo hayo yanakingana na yale yanayofahamika na watu wengi kuwa ni wananchi wa Zanzibar wenyewe ndio waliotaka kuung’oa utawala wa Sultani. Baada ya kitabu hicho kutoka na kusomwa na watu wengi Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliombwa ajibu shutuma dhidi yake zilizomo katika kitabu hicho.

Mpaka kafariki hakutaka ama hakuweza kuzijibu shutuma zile. Bila shaka hayo yote yanafahamika miongoni mwa wa-Zanzibari wengi, wale wa jana na wale wa leo.

Inawezekana kabisa kuwa hiyo ni sababu moja inayowafanya wa-Zanzibari, vijana kwa wazee, wasiukubali huu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Inawezekana kabisa kuwa kuna sababu zingine pia zinazowafanya wa-Zanzibari wachoke na Muungano. Kwa mfano wamekuwa wanalalamika sana kuwa uchumi wao umeathirika sana kutokana na Muungano.

Huko nyuma kulikuwa na malalamiko kuwa Banki Kuu ya Tanzania kwa mfano ilkuwa ikichukua maamuzi mazito kuhusu sarafu (shilingi) bila hata kuwaatarifu Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kuna wakati Zanzibar, ikiwa chini ya Rais Dr Salmin “Commando” Amour, nchi hiyo ilikuwa na biashara kubwa sana ya kimataifa, kiasi kwamba wafanya biashara kutoka sehemu nyingi za Afrika ya Mashariki na ya Kati walikuwa wakifurika Zanzibar kupata mahitaji yao.

Zanzibar ilivuma kweli kweli; lakini inasemekana kuwa Serekali ya Muungano (Bara) iliingilia kati na msimu huo ulikatishwa ghafla. Hapa sio kudai kuwa Serekali ya Muungano ilifanya kusudi ama kosa, la; bila shaka walitumia sheria zilizopo zilizowaruhusu kuvunja nguvu hiyo iliyoipata Zanzibar ghafla tu.
Kumekuwa na malalamiko halikadhalika kuwa maamuzi mazito kuhusu Zanzibar yanapitishwa Dodoma badala ya wananchi wenyewe wa Zanzibar kuyashughulikia na kutoa maamuzi yenye manufaa kwao.

Mfano mzuri ni ule wa “kuchafuka hali ya hewa” kiasi kwamba Rais aliyechaguliwa na watu wa Zanzibar aliweza kutakiwa “kujiuzulu” akiwa Dodoma na sio Zanzibar kule alikochaguliwa na wananchi.

Kweli kunaweza kuwa na kipengele cha kisheria kilichowezesha hatua hiyo kupitishwa Dodoma na sio Zanzibar, likini kuwepo na sheria kama hiyo pia kunaweza kuwa ni sababu ya malalamiko.

Ni vigumu kuzungumzia mambo ya uchumi wa Zanzibar bila kutaja sakata la mafuta yanayosemekana yako chini ya bahari ya Zanzibar.
Bahati mbaya sana kuwa wakati wa-Zanzibari na Serekali ya Mapinduzi wameweza kutoa mawazo na sera zao kinagaubaga mpaka sasa Serekali ya Muungano haijatoa matamshi ya wazi wazi kuhusu suala hilo nyeti. Hili haliwaridhishi wa-Zanzibari.

Hakika yako mengi mengine mojawapo likiwa dhana ya kuwa wa-Bara mara nyingi huonyesha dharau kwa ndugu zao wa Zanzibari hasa katika yale ya kiserekali ama ya kiofisi. Mwandishi huyu huko nyuma amewahi kushuhudia hisia za namna hiyo pale wa-Bara wanapozungumzia taarifa zinazowahusu “kina yakhe” maofisa wa Zanzibar.

Haya yanafahamika wazi na wa-Zanzibari wenyewe; lakini kama hilo si zito sana kiasi cha kuathiri Muungano ni shauri lingine.
Ukweli pia kwamba kwa sababu ya Muungano ulivyoanzishwa, Zanzibar ilipoteza kwa kiasi kikubwa ule utamaduni wao wa ki-Zanzibari.

Ingawa kweli Serekali ya Mapinduzi imekuwa ikijiita ya kisekula isisahaulike pia kuwa wananchi wa nchi hiyo wengi wao ni Waislamu.

Yuko ndugu yangu mmoja, bahati mbaya sasa ni Al Marhum, alikuwa na pendekezo kuwa bora Muungano ufe ili Zanzibar irudi kuwa nchi ya Kiislamu. Muungano umewezesha Ukristo kuingia Zanzibar kwa nguvu sana.

Wasomaji wajaribu kutafakari maandishi ya Bwana Ibrahim Mohammed Hussein makala zake zikitokea lkatika gazeti hili. Pia yale maoni ya mwandishi wa siku nyingi Bwana Ahmed Rajab anayoyatoa takriban kila wiki katika gazeti la RAIA MWEMA yatiwe maanani.

Ila mimi ningetahadharisha jambo moja tu ambalo ni la maana na muhimu sana. Hivi sasa nchi nyingi sana duniani zinajaribu kutafuta umoja ama muungano. Udugu walio nao waTanganyika na wa Zanzibari ni wa siku nyingi sana.
Pande zote za Muungano wa Tanzania wakumbuke kuwa UMOJA NI NGUVU UTENGANO NI UDHAIFU. Hasa miongoni mwa wanandugu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s