Sheria za uchaguzi zifuatwe – Maalim Seif

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF); Maalim Seif Sharif Hamad

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF); Maalim Seif Sharif Hamad amezitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyotungwa nchini, inafuatwa na kutekelezwa kivitendo ili uchaguzi unaofanyika uwe huru na haki na usiotawaliwa na rushwa.

Maalim Seif alisema hayo jana huko Makao Makuu ya CUF Zanzibar, Mtaa wa Mtendeni mjini Unguja wakati alipotembelewa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Rajab Baraka katika ziara yake ya kawaida ya kuvitembelea vyama hivyo.

Alisema pamoja na kutungwa sheria hiyo, baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikiikiuka hadharani kwa kutoa rushwa bila kificho pamoja na kukiuka kima kilichowekwa cha gharama za uchaguzi wa jimbo, bila ya kuchukuliwa hatua zozote na mamlaka husika.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alitoa mfano wa ukiukwaji mkubwa wa sheria hiyo ni matukio yaliyojiri wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Igunga mkoani Tabora, Oktoba mwaka huu.

Alieleza kuwa wakati wa uchaguzi huo, Sheria ya Gharama za Uchaguzi ilifumbiwa macho kwa sababu licha ya sheria hiyo kuweka bayana kima cha juu cha gharama za uchaguzi wa jimbo kisizidi Sh milioni 80, kuna chama kilitangaza kwenye vyombo vya habari kitatumia Sh milioni 400 katika uchaguzi huo.
“Yaliyotokea Igunga ni uthibitisho wa ukiukwaji wa sheria hii, rushwa ilikuwa ikitolewa nje nje, Takukuru wapo wanaona, sasa kama tumeamua kutunga sheria basi tuzifuate sote,” Maalim Seif alimueleza Naibu Msajili wa Vyama.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif ameitaka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwasaidia wananchi wanaokosa haki zao kwa kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi kwa kuzishitua mamlaka zinazowawekea vikwazo wananchi hao ziache tabia hiyo kwa sababu ni kuwanyima haki zao na kuleta ubaguzi.

Alimueleza Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa hivi sasa kuna wananchi wengi wa Zanzibar wanazungushwa na kukoseshwa fomu za kuomba vitambulisho hivyo, kwa sababu za kisiasa, hali inayowasababishia wakose haki zao nyingi za msingi, mbali na shughuli za uchaguzi.

Kwa upande wake, Naibu Msajili huyo wa vyama vya siasa alisema amesikia malalamiko hayo na atayafanyia kazi, kwa nia ya kuinua hali ya demokrasia nchini. Alivitaka vyama vya siasa ambavyo havifanyi kazi zake ipasavyo viache tabia hiyo kwa sababu haisaidii kukuza uhai wa vyama na pia inadumaza demokrasia.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s