Mimi ni CUF kwa kuwa CUF ndiyo yenye visheni – Mtatiro

Na Julius Mtatiro

Kama kiongozi ambaye nimekuwa kwenye harakati muda mrefu, siku zote nimejitahidi kupambana na changamoto na kumvumilia kila mtu kwa silka yake huku nikitimiza wajibu wangu na nikiwa na visheni ambayo kwangu nadhania ni sahihi. Ndugu zangu, CUF ina mustakabli na katika hili sina shaka. Tatizo la baadhi yetu ni kuamini kuwa chama fulani kinachong’ara wakati fulani ndicho chenye mustakbali, lakini mimi siamini hivyo. Naamini katika kujenga mfumo thabiti, na mfumo thabiti hutafutwa katika kipindi kirefu. Kuna baadhi yetu hudhani CUF itakufa na kuwa imepoteza mwelekeo, lakini napenda ifahamike kuwa CUF haitakufa na haitapoteza mwelekeo.

CUF itazidiwa karata za kisiasa kutoka na mfumo mgumu wa kisiasa ambao vyama vyenye nguvu katika nchi vinau-asisi hasa katika matumizi ya fedha nyingi ambazo haieleweki vyama vinazitoa wapi na pia propaganda kali ambazo zinatumika kwa vichwa vya wananchi wengi ambao wana uelewa mdogo wa masuala ya kidemokrasia na wasio na elimu ya uraia.

Lakini CUF ikifanikiwa kupita katika changamoto za kisiasa zinazotengenezwa kimakusudi itakwenda mbali na katika mafanikio makubwa. Ninaamini hivi kwa sababu hiki ndiyo chama salama pekee kilichosalia.

Wakati najiunga CUF, tayari CHADEMA ilikuwa vibrant na ilianza dhahiri kuonekana kuwa chama chenye nguvu kuliko CUF. Hata vijaNA wengi wa vyuo vikuu walifikiria na kuchukua hatua za kuiunga mkono CHADEMA kwa kuamini kuwa ni chama chenye nguvu na maarufu na kinaweza kuleta ukombozi haraka sana.

Wakati wenzangu wana mtizamo huo mimi nilikuwa na mtizamo tofauti, KUMBUKA “for every decision there is a consequence”.
Nilijua dhahiri kuwa CUF inaweza kuwa kwenye wakati mgumu katika miaka kadhaa ijayo.

Nilitambua kwamba nina jukumu la kujiunga na chama ambacho kiko wazi katika utendaji wake, chenye falsafa niliyodhani ni sahihi, chenye viongozi imara wenye malengo ya kuikomboa nchi kwa wakati sahihi na kwa kutumia njia za wazi na sahihi. Sikujali propaganda za Udini na Upemba na uislamu na upwani na uarabu na misimamo mikali n.k.

Vitu ambavyo vilihusishwa na CUF kwa lengo la kuisaidia CCM na baadhi ya vyama ambavyo wakubwa walihitaji vishike dola baada ya CCM.

Nilihitaji chama ambacho nitakuwa na forum huru inayoweza kufanya maamuzi kwa pamoja bila shinikizo la mtu mmoja au wawili ndani ya chama(SIMAANISHI KUWA CHADEMA WANA MFUMO HUU). Kwa hiyo nilifuatilia miundo ya vyama vyote kwa muda kidogo, ufanyaji kazi wa vyama, uanzishwaji wa vyama n.k na mwisho wa siku nikaona CUF ni chama bora sana mbele ya safari hata kama kitakabiliwa na changamoto kadhaa miaka ya sasa.

Tofauti na vijana wengi ambao aidha hujikuta ni CHADEMA au CCM au CUF automatically kwa kuvutiwa na mtu fulani maarufu au kuvutia na mbwembwe za chama fulani au kutaka kuingia bungeni haraka kwa hiyo mtu anajiunga tu na chama ambacho anadhania ni shortcut ya mafanikio yake, mimi nikiri kuwa nilikaa na kuvitathmini vyama kwa muda mrefu kabla ya kufanya maamuzi kuwa najiunga na chama kipi na kwa nini, kwa hiyo sikuwa nabahatisha.

Nilifanya maamuzi ya dhati kwa kujitambua na kwa kutambua hali ya wakati tuliopo na ujao katika nchi yetu.

Lazima nikiri kuwa harakati zote ambazo wadau waliona nikizifanya wakati nikiwa WAZIRI WA MIKOPO – UDSM (2006), WAZIRI MKUU UDSM (2007) na KATIBU MKUU WA VYUO VIKUU TZ (2007-2008) nilizifanya kama mwanaharakati huru na mara nyingi nilisimama peke yangu hata pale ambapo wenzangu wengi walidhania siko sahihi.

Wakati naongoza harakati mbalimbali ndani ya nchi katika ngazi ya vyuo vikuu – vyama kadhaa vilinifuata kutaka kujua msimamo wangu wa kisiasa na kutaka kujua iwapo naweza kujiunga na vyama husika.
Nimewahi kufuatwa na mhe. Freeman Mbowe ili nijiunge CHADEMA na nilimpa msimamo wangu kuwa nitajiunga na chama chochote pale nitakapoamua kufanya hivyo, baada ya hapo alinitumia delegations mbalimbali zinishawishi lakini niliomba nipewe muda.

NCCR MAGEUZI pia wamewahi kunifuata mara kadhaa kwa kumtumia Mwalimu Nderakindo Kessy na Mwalimu Mvungi ambapo niliwajulisha pia mtizamo wangu.

Viongozi wa CCM ambao wamewahi kufanya dhahiri mazungumzo name wakiniomba nijiunge CCM kwa ahadi kemkem ni wengi mno na tena mara nyingi, amewahi kutumwa Mzee w Wassira(TYSON), NIMROD MKONO, KINGUNGE, RIDHIWANI na wakati fulani waziri Mkuu(wa wakati huo) LOWASSA- amewahi kunisisitiza sana nijiunge CCM na ku-transform harakati za vyuo vikuu katika forum za CCM ili matatizo mengi ya wanafunzi wa elimu ya juu yatatuliwe lakini nilikataa.

Baada ya maelezo haya naomba ifahamike kuwa ninavisheshimu sana vyama vyote ikiwemo CHADEMA, CCM, NCCR n.k ikiwa ni pamoja na viongozi wote wa vyama husika. Kwani naamini katika uwanja wa kisiasa tunatofautiana kimtizamo na kimaamuzi tu.

Baada ya kumaliza shahada yangu ya kwanza (sasa hivi nafanya shahada ya pili) niliamua kujiunga CUF kama mwanachama wa kawaida, baada ya mwaka mmoja niliteuliwa kuwa Mkurungenzi wa Haki za Binadamu na Sheria na Baada ya mwaka mmoja nikateuliwa kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara) na baada ya miezi 6 yaani mwezi Mei 2011 nikateuliwa na kuchaguliwa rasmi na Baraza Kuu la Chama kuwa Naibu Katibu Mkuu.

Naomba ifahamike kuwa siko CUF kimaslahi (KAMA AMBAVYO BAADHI YA WADAU WANAJARIBU KUWAAMINISHA WENZAO) kwani ningetaka maslahi ningejiunga CCM chama chenye dola na pesa za kufa mtu.

Au ningejiunga CHADEMA, chama chenye wafadhili wengi na watu wengi wenye uwezo mkubwa wa kipesa kwani ni dhahiri kuwa hata wakati CUF inapata ruzuku ya tzs 120M CHADEMA wakipata tzs 60M bado CHADEMA walifanya kampeni za uwezo mkubwa kipesa kuliko CUF.

Kwa hiyo kama shida yangu ilikuwa ni pesa nisingejiunga CUF, walau ningejiunga CHADEMA penye pesa (hata kama nisingejua nani anatoa hizo pesa). Siku zote katika maisha yangu pesa ni kitu ambacho hakininunui na hata wakati naongoza vyuo vikuu mara kadhaa serikali ilileta fedha nyingi ili nisihamasishe harakati za vyuo vikuu lakini sikuwa na shida na hizo pesa kwani mie huamini hata ukiwa na shilingi ngapi BENKI kwa kuuza matumaini ya watu, Kifo kitakuja siku moja utakufa na kuziacha pesa za dhuluma na utajiri wakona waliobaki wataponda hizo fedha kwa mwezi mmoja.

Maisha yangu hayaendeshwi kwa njaa kwani tangu utotoni mimi nimekuwa mjasiriamali mzuri.

Wakati nikiwa shule ya msingi nilitembea umbali wa Kilometa 10 kufuata miwa mashambani na kuja kuiuza shuleni bila kutumwa na mzazi japokuwa mara kadhaa niliadhibiwa na wazazi ambao hawakupenda nifanye hivyo.

Wakati nasoma Chuo Kikuu nilifanikiwa kujianzishia saloon ya kunyoa nywele na vibanda vya simu kadhaa (wakati huo mwanafunzi asiye na pupa na maisha angeweza kupunguza matumizi ya hovyo ya boom na akafungua kibanda cha chipsi cha mtaji wa 50,000 lakini kwa bahati mbaya wengi walidhania kununua TVs na redio kubwa ndiyo fasheni na walitegemea kuwa baada ya chuo ni ajira). Mimi sikuwa nategemea kuajiriwa baada ya masomo ya chuo (siwadharau watu wanaosoma ili waajiriwe- kwani ni mahitaji ya lazima).

Hadi hivi ninavyoongea ninaendesha maisha yangu bila kukitegemea chama na katika chama, nina miradi ya saloon za kiume na saloon moja ya kike, nina steshenari na miradi ya pikipiki za bodaboda na hayo yanaendesha maisha yangu bila kuhangaika sana.

Kwa hivyo, siko CUF kutafuta pesa, niko CUF nikiwa na “means” za kuendesha maisha yangu.(Mniwie radhi wale watakaoona naeleza maisha yangu bila sababu – nimezoea kufanya hivyo na hata wakati napewa unaibu CUF niliwaambia wanachama ninamiliki nini kwani ninafahamu viongozi wengi hujitajirisha kupitia nyadhifa zao lakini mie kwangu ni tofauti sana, naamini katika kujitegemea).

Naomba nikubaliane na Director kuwa CCM ndiye mgomvi wetu mkubwa na ndiye adui wetu mkubwa. Na lazima tupambane na adui huyu hadi mwisho. Na ninaomba nitoe mtizamo kuwa ikiwa tutapata katiba mpya yenye demokrasia pana, ya wazi na isiyopendelea upande wowote lazima CCM wataondoka madarakani kupitia masanduku ya kura.

Na hata wana – CCM walioko hapa wanajua kuwa hivi sasa kwa hali ya maisha ya watanzania na mfumuko wa bei, kukithiri kwa umasikini n.k. hawatakuwa na karata tena 2015 hata zikichangiwa NIGERIA hazitachangika. Na katika hili mie namshukuru ndugu Jakaya kwa sababu anaimaliza CCM vizuri na hakutakuwa na dawa ya kuifufua…HAKUNAGA DAWA!

Kwa mtizamo wangu, CUF ilipaswa kupongezwa sana kwa kuwa chama cha kwanza cha upinzani kuingia serikalini upande wa Zanzibar kwani haikuja kirahisi sana.

Badala yake wenzetu wanatangaza kuwa CUF ni CCM B na kuwa isichaguliwe. Mimi binafsi sina shaka na wasiwasi na mfumo wa SUK – Zanzibar, ninaona kama njia ya CUF kubadili muelekeo wa siasa za nchi ambapo CUF inakaa serikalini na kujipanga ikiwa serikalini, the next election utaona rais wa Zanzibar anatoka CUF.

Lakini jambo ambalo muhimu ni maendeleo ya wananchi, ikiwa pana mfumo ambao umechaguliwa na wananchi wenyewe na mfumo huo ukawaletea maendeleo makubwa, tatizo ni nini?

Mfumo wa SUK ni mfumo pia, labda kwa sababu ni mifumo mipya kwa Afrika lakini wenzetu ambao tunaiga kwao kila mfumo wanatumia mfumo huu. Leo Serikali ya Uingereza na serikali kadhaa ulaya zinatumia mfumo huu, Zimbabwe, Kenya ni mifano mingine.

Wenzetu Kenya waliunda GNU, lakini leo hii Raila haonwi kama msaliti, still wakenya wanamuunga mkono na wanajua kuwa mwisho wa siku anaweza kuwa rais wao, hapa ni suala la mtizamo tu na uelewa tu. Mfumo wa GNU ni hatua tu ya kubadilisha siasa za nchi na chama kiliona njia ya umwagaji damu sio njia ya mkato ya kuleta mabadiliko ya kweli.

Njia sahihi ya kuleta mabadiliko ni njia ya kukaa mezani na kujadiliana, ndiyo maana hata Raila na Kibaki vita haikuwasaidia, mwisho wa siku walisimamisha vita wakakaa mezani. Hata Zanzibar wamefanya hivyo kwa maslahi ya Zaznibar yao.

Wenzetu CHADEMA ambao wanageuza suala hili kuwa propaganda ya kuiua CUF hawana nguvu Zanzibar kwa hiyo hawana cha kukosa CUF ikiathirika. Wazanzibar waliamua kwa umoja wao kutengeneza serikali yao, tuwaache wasimamie mambo yao, siku wakishindwa Wazanzibari ndio watakaoamua kutafuta mfumo mpya.

Tukumbuke Zanzibar siyo mkoa wa Tanzania, ni nchi iliyoungana na Tanganyika kuunda Tanzania. Na labda usishangae mbeleni wazanzibari wakataka kubaki na Zanzibar yao na watanganyika wakataka Tanganyika yao.

Mfumo wa kisiasa tulionao ndiyo unachanganya wadau wengi. Katika nchi nyingi serikali ni moja tu na vyama ni vimoja tu. Hapa kwetu Tanzania tuna serikali mbili katika nchi mbili na vyama ni vilevile pande zote. Inapotokea nchi inabadili mfumo wake vyama haviwezi kubadilika.

CUF isingeweza kujitoa Zanzibar eti kwa sababu mfumo wa uongozi unabadilika.Mimi nachokisubiri ni maendeleo. Wananchi hawasaidiwi na hoja kuwa wanaongozwa na chama kipi, wananchi wanahitaji maji, barabara za uhakika, ajira, uchumi imara n.k.

Ikiwa SUK italeta maendeleo baada ya kuunganisha nguvu za pande zinazoongoza hutawasikia wazanzibar wakiilaumu na kuikataa SUK. Ikiwa SUK haitaleta chochote kipya wataiondoa kwa nguvu yoyote. Ni suala la wakati tu na hatimaye wakati utasema kila kitu.

Hoja ya kujiunga CHADEMA kwangu si hoja nzito sana japo sipingani na mtizamo wako. Mimi siwezi kukimbilia CHADEMA ati kwa sababu ina nguvu sana sasa. Siwezi kuwa kiongozi nisiye na visheni kiasi hicho.

Kama CHADEMA wataongoza dola 2015 hiyo pia siyo sababu ya mimi kujiunga huko kwani ikiwa watu wote tutaenda kuongoza dola kupitia basi la CHADEMA at that time nani atawasemea wananchi?
Nani anayetudanganya kuwa ati mwisho wa harakati za kuikomboa nchi ni pale ambapo CHADEMA watakuwa madarakani?

Naogopa sana mtizamo huu wa kuamini chama kama vile dini, hata CUF msije kuiamini kama dini yenu, muihoji na muifanyie uchambuzi wa kina. Mitizamo ya namna hii ni ya kuua demokrasia.

Wengi wetu tukumbuke kuwa ukiingia madarakani watu wengi huanza kukuhoji, kwa hivyo wachache kati yetu tusidhanie madarakani kuna raha, ni tafrani za hali ya juu. Kwa hiyo mie sitajiunga CHADEMA ati kwa sababu inaweza kuongoza dola kabla ya CUF na ati kwa sababu imeahidi maziwa na asali, tunaweza kuwaacha wakaongoza halafu wakashindwa na wananchi wakatafuta chaguo lingine na chaguo likawa CUF.

Jambo lingine ni hii dhana ya kuhamahama, leo CUF ikifanya vibaya hapa na pale tuhamie wanakofanya vizuri kama CHADEMA n.k. Na ikitokea huko CHADEMA wakaanza kushuka kisiasa ndo tunahamia chama kingine tena, huku ni kujikosesha mtizamo mpana wa kiukombozi na ni kujigeuza bidhaa. Kamwe mimi siwezi kugeuka bidhaa.

Ningehama CUF kama kingeacha misingi yake ya uadilifu, kuunganisha, kutetea wananchi na kutengeneza taifa la pamoja lenye maendeleo ya dhahiri. Ikiwa CUF itaanza kufuja pesa, kuongozwa kidikteta au na mtu mmoja au kikundi cha watu wachache n.k. nitafanya maamuzi tofauti.

Hata kama sisi CUF tuko kwenye SUK, serikali ambayo imeundwa kikatiba, hatujakosea popote. Ikiwa tuko SUK ili kufuja pesa za umma sawa! Ikiwa tuko SUK kula na kunywa na kusaza sawa! Lakini kwa sababu tuko SUK ili kuibadili Zanzibar na kuleta maendeleo, hakuna kosa tulilofanya.

Hizi propaganda za U-CCM B zitaisha tu iwapo nia yetu ya kuiendeleza Zanzibar itaanza kuonekana dhahiri. Kuna vitu ambavyo vimeshaanza kuonekana kama vile upandishwaji wa bei ya karafuu kutoka tzs 5000 hadi 15,000 kwa kilo.

Hili lilikuwa kwenye ilani ya CUF na tumeingia serikalini Zanzibar tumefanikiwa kulibadili na wananchi wanafahamu hivyo. Muda si mrefu yatapatikana mambo mengine kadhaa na yataonesha umuhimu wa CUF katika SUK – ZNZ.

Lakini kwa sababu CUF imeendelea kushikilia misingi yake ya uanzishwaji, kazi yangu inabakia kuwa moja tu! Kupigana kuendelea kuijenga CUF ambayo inadogoeshwa kwa propaganda za hali ya juu.

Kuna vyama haviamini kuwa vitaongoza dola CUF ikiwepo, vinapigana kufa na kupona kuona CUF inakufa. Hizo ni ndoto za mchana kabisa!

Na ninataka niwahakikishie kuwa CUF itaendelea kusimama kwa sababu ina mfumo hadi chini. Ndiyo maana hata Igunga tumepata kura 2000 ambazo wadau wanatucheka, lakini zina maana kubwa sana hata kama zimeshuka kutoka 11,000, kuwa kuna watu wanaiunga mkono CUF bila kujali propaganda wala kugawiwa fedha.

Kwa wale wanaochekelea kuwa CUF lazima iendelee kushughulikiwa wanafanya makosa makubwa sana. Hii ni kwa sababu katika uhalisia nchi haihitaji vyama vyenye misingi imara na visheni pana vife kupisha chama fulani kingie madarakani.

Nchi inahitaji tuiondoe CCM madarakani, tuweke chama kingine madarakani na tuwe na vyama kadhaa vyenye nguvu ambavyo vitakifanya chama kipya kisiwaburuze wananchi.

Kwa wale ambao wanaona huu ni mtizamo finyu na mwembamba wataona nini kitakuja kutokea iwapo moja kati ya hayo yanatokea. Na ikumbukwe kuwa CCM ikishaondoka itakufa kabisa. CCM itakufa kwa sababu ni chama ambacho kimetawala kwa muda mrefu, kikiondoka kwenye ulingo wa siasa kinaondoka kabisa, labda kifufuliwe tena baada ya miaka 100 na vitukuu vyetu.

Kwa hiyo kwa vyovyote vile panahitajika vyama vilivyojijenga na imara kama CUF vilindwe na kila mwanademokrasia ili wananchi wawe na mbadala kila chama kilichoko madarakani kitashindwa.

Mwisho nataka kusisitiza kuwa CCM lazima itaondoka 2015, hivi sasa hakuna namna ambavyo CCM itaokoka. Leo hii hata serikali haina pesa za kusimamia nchi, serikali inafilisika. Mafisadi wamepamba moto, lakini sikio la kufa halisikii dawa. Iacheni CCM ijifie, tupate chama kingine kisha baada ya hapo tutajua FUTURE ya taifa letu.

Nashukuru wa maoni na mitizamo yenu nyote hata kama iko tofauti na mtizamo wangu. Kila mtu ana mtizamo wake na huo ndio mtizamo wangu katika masuala muhimu mliyouliza.

______________________________________________________________________________________________

Julius Mtatiro ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Chama cha Wananchi kwa upande wa Tanzania Bara. Hapa alikuwa akijibu maswali mbalimbali yaliyolengwa kwake kupitia mawasiliano ya mitandao ya kijamii (Facebook na Jamii Forums). Anapatikana kwa simu namba 00255 717 536 759 na kwa barua-pepe: juliusmtatiro@yahoo.com.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s