Tamko la MUWAZA juu ya kiapo cha Rais wa Zanzibar katika baraza la mawaziri la muungano

Mwenyekiti wa MUWAZA Dr Yussuf S. Salim alieko Copenhagen nchini Denmark

MUWAZA imepata mshangao na kusikitishwa na hatua ya rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuamua kula kiapo kwa minajili ya kuingia katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tunakiona kitendo hiki kama ni muendelezo wa udhalilishaji kwa Serikali ya Zanzibar pamoja na wananchi wake. Pamoja na kuwa suala hili limetajwa katika katiba ya Muungano, lakini haikuwa ni mazoea kwa ma Rais waliopita kuhudhuria kiapo hiki.

Kwa mnasaba huo, tunapata masuala mengi kuliko majibu. Ni kwa nini Rais wetu amefanya kitendo hiki wakati huu ambapo utaifa wa Zanzibar unazidi kuchomoza kutokana na muamko, umoja, na nguvu ya Wazanzibari.

MUWAZA inaamini kwamba, masuala yote yanayohusu Zanzibar yatajadiliwa na Wazanzibar wenyewe kupitia Serikali yao na Baraza lao la Wawakilishi. Endapo vyombo hivyo vitashidwa, basi Wazanzibari wenyewe wanayo nguvu yao ya kikatiba kuamua mambo yao kwa kupitia kura ya maoni.

Uwezo huo upo na ni hiari ya Wazanzibar kuutekeleza wakati wowote, aidha kwa kutumia katiba iliyopo sasa au ye yote ile ya Muungano itakayokuja. Katika hali hiyo,
Rais wa Zanzibar anahudhuria katika Baraza la Mawaziri la Muungano kwa kujadili masuala gani?

MUWAZA inaamini kwamba Rais wa Muungano na Serikali yake ya sasa inayo haki ya kuendesha mambo yote ya Tanganyika na yale yahusuyo Muungano. Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Serikali ya Zanzibar wanayo mamlaka yote ya kushughukilia mambo yahusuyo Zanzibar na pia kazi ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Zanzibar na uhuru wake ndani na nje ya Muungano yanaheshimiwa. Panapo tokea mvutano, ni wajibu wa Marais wawili kukaa pamoja na kutafuta ufumbuzi kwa kutumia miongozo ya Serikali zao.

Kwa vyovyote vile, hakuna mantiki na si haki kwa Baraza la Mawaziri la Muungano kujadili na kuamua mambo mazito yanayohusisha masuala muhimu ya Zanzibar ati tu kwa sababu Rais wa Zanzibar amehudhuria au ni mwanachama katika Baraza hilo. Kiini macho hicho hakikubaliki.

MUWAZA inamnasihi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dk. Mohammed Ali Shein, kuchukua hatua za haraka za kuwafahamisha Wazanzibari juu ya uamuzi wake wa kuhudhuria kiapo hiki hasa kwa vile hakuomba ridhaa yao kabla ya kutenda kitendo hicho. Aidha, tunamkumbusha juu ya umuhimu na mamlaka aliyonayo akiwa kama Rais wa
Nchi kamili inayozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatuoni sababu ya Rais wetu kuhudhuria katika Baraza la Mawaziri la Muungano akiwa aidha kama waziri au Rais wa Zanzibar. Hatutegemei kumuona anaendelea kuhudhuria vikao hivyo. Venginevyo, tutakilaani kitendo chake hiki kwa nguvu zote. Kwa niaba ya MUWAZA
Dr. Yussuf S. Salim
Mwenyekiti
Copenhagen

Advertisements