Hatimae mrithi wa Rostam ajulikana, Igunga

  • Kafumu aibuka kidedea
  • Amzidi mgombea wa CHADEMA kura 3,224
  •  Mahona wa CUF aambulia kura 2, 104
  • Mabomu ya machozi yafunika mji wa Igunga
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM)Bw. Wilson Mukama akiwa amemshikilia Dkt. Peter Kafumu wakati akitangazwa kuwa mbunge wa Jimbo la Igunga kwenye Viwanja vya Halmashauri ya wilaya hiyo jana. Kulia ni mke wa Dkt. Kafumu,Bi. Maria-Magdalena.

CHAMA cha Mapinduzi CCM kimeiubuka kidedea katika Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga baada yamgombea wake Dkt. Peter Kafumu kumzidi mpinzani wake wa karibu, Bw. Joseph Kashindye wa CHADEMA kwa kura 3,224. Akitangaza matokeo mjini hapa jana mchana Msimamizi wa Uchaguzi huo, Bw. Protace Magayane alisema Dkt. Kafumu amenyakuwa kiti hicho baada ya kupata kura 26,484 (asilimia 47) dhidi ya Bw. Kashindye aliyepata kura 23,260 (asilimia 41). Mgombea wa CUF, Bw. Leopold Mahona alipata kura 2,104 (4%) akifuatiwa na mgombea wa (SAU), Bw. John Maguma kura 83, Bw. Saidi Cheni (DP) 76, mgombea wa Bw. Steven Nushuyi (AFP) kura 235, Bw. Hassan Lutengama (CHAUSTA) 182, Bw. Hemed Ramadhani (UPDP) (63). Jumla ya kura zilizopigwa ni 53,672 na zilizoharibika ni 1,185. Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mbunge mteule wa Jimbo la Igunga, Dkt. Kafumu alisema atahakikisha anawatumikia wananchi wa jimbo hilo kama Ilani ya CCM inavyomuagiza kufanya. Matokeo hayo yalitangazwa saa 9:15 alasiri tofauti na ilivyokuwa imeelezwa jana na Bw. Magayane kuwa yangeweza kutolewa juzi usiku. Ucheleweshaji wa matokeo hayo kulisababisha wafuasi wa chadema ambao tangu juzi walikuwa wamekusanyika na kuanza kushangilia ushindi, kuanza kujikusanya katika ofisi za halmashauri kushinikiza kutangazwa, ndipo wakakabiliana na polisi na kuanza kutawanywa kwa mabomu. Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Wilson Mukama alisema pamoja na ushindi huo hakufurahishwa na siasa za baadhi ya vyama za kumwagiana tindikali na kuchomeana nyumba. Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Bw. Julius Mtatiro alisema uchaguzi huo ulinuka rushwa na wapiga kura kugawiwa fedha. Bw. Mtatiro alisema wapiga kura walishawishiwa kutokipigia kura chama chake kwa sababu ya hadaa ya fedha walizopewa, hali inayoonesha kuwa siasa za Tanzania hivi sasa zitakuwa kwa watu wenye fedha. Aliyekuwa mgombea wa CUF, Bw. Leopold Mahona alisema hatakuwa na muda wa kukata rufaa kupinga matokeo ya Dkt. Kafumu bali atahakikisha anajiandaa kwa ajili ya chaguzi zijazo. Alisema kwa sasa jambo moja ambalo lipo mbele yake ni kuhakikisha anajiandaa kwenda masomoni kwani anaamini pamoja na kufanya siasa bado anao uwezo wa kuendelea na masomo. “Nimejipanga kuendelea na masomo yangu ya juu na nikimaliza nitakuja kuendelea na shughuli za siasa,” alisema Bw. Mahona. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjrao, Bw. Basil Lema alisema uchaguzi huo ulikuwa na vitisho vingi ikiwa ni pamoja na magari ya polisi kuingizwa kwenye vituo vya kupigia kura. Alisema hatua hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kuogopa kujitokeza kupiga kura na badala ya kukaa majumbani mwao bila kupiga kura na pia kulikuwa na kasoro nyingi, hivyo kutangaza waziwazi kuwa chama hicho hakukubali matokeo hayo. Awali, mgombea wa CHADEMA Bw. Kashindye alisema hatakubaliana na matokeo ya kukosa jimbo hilo kwa sababu CCM imetumia mbinu nyingi ambazo si halali katika uchaguzi huo.

Vurugu kabla ya matokeo

Awali wakati wananchi wakisubiri kupata matokeo ya uchaguzi huo hali ilikuwa tete hivyo kuilazimu Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya kurejesha hali ya utulivu. Hali ya mji wa Igunga iligeuka kuwa tisho kwa kusikika kwa milio ya risasi na yowe kutoka kwa wananachi waliokuwa wakikimbizana na polisi hivyo kusababisha wafanyabishara kufunga maduka, hoteli na huduma zote kwa muda. Ilidaiwa kuwa vurugu hizo zilitokana na malori yaliyosadikiwa kuwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia mitaani yakiimba nyimbo za ushindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, huku wenzao wa Chadema nao wakifanya hivyo hivyo tangu juzi jioni. Baada ya burudani hiyo inayodaiwa kuwa ya CCM, CHADEMA nao wanadaiwa kujibu mapigo kwa kuingia barabarani wakiwa na lori la muziki kuelekea Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Ilidaiwa kuwa gari hilo ilipofika katika hoteli ya Peak walimofikia viongozi wote wa CCM ghafla vijana zaidi ya 30 walianza kuwashambulia hivyo kusababisha vurugu kuanza. Vurugu hizo zilidumu kwa nusu saa hivyo polisi
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasi (FFU) walilazimika kuzingiara hoteli hiyo kufanya oporesheni ya ukaguzi wa silaha mbalimbali za jadi na kuwakamata wahusika wa vurugu hizo. Mbunge wa Mbinga Magharibi, Bw. John Komba alitoka nje ya hoteli hiyo na kuzungumza na kiongozi wa FFU kusitisha shughuli hiyo ya ukaguzi kwa maelezo kuwa kulikuwa na viongozi wa kitaifa hivyo si vizuri kuwavuruga. Wakati Bw. Komba akizungumza na askari huyo
ghafla vijana walimzonga na kutaka kumshambulia. Katika vurugu hizo gari la CCM lenye namba T 162 BLW lilipasuliwa vioo huku watu wawili wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CHADEMA wakijeruhiwa. Vurugu hizo zilihamia Halmashauri hivyo kuilazimu polisi kuimarisha ulinzi kwa kuweka kamba mita 100 kutoka katika ofisi hizo ili kusubiri matokeo kutangazwa. Hata hivyo vijana wa Igunga walishindwa uvumilivu na kutaka kamba ya polisi, kuvunja miti yote iliyopandwa na kuzingira gari la polisi la maji ya kuwasha huku wengine wakitaka kuruka uzio wa waya. Hali hiyo ilisababisha Mkuu wa FFU, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Telesphory Anaclet, kuamuru askari kuwatuliza kwa maji ya kuwasha na mabomu ya machozi. Hali hiyo ilisababisha tafrani kwa watu mbalimbali wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi na waandishi wa habari ambapo kila mmoja alianza kulia na kutafuta maji ya kunawa. Operesheni ya kuwatawanya vijana hao iliendelea maeneo karibu yote ya mji wa Igunga hadi kituo cha mabasi yaendayo mikoani.Kamishna Anaclet aliwataka viongozi wa CHADEMA kuwatuliza wafuasi wao ili kuepusha madhara lakini  huku malori ya muziki yakiendelea kupita mitaani na kuwataka wafuasi kwenda ofisi za chama hicho kutoa tamko. Vijana wanaidaiwa kuwa ni wa CHADEMA waliibuka wakiwa wamebeba jeneza likiwa limefunikwa bendera ya CCM na kuingia barabarani kuandamana kabla ya kukumbana na nguvu ya dola na kuliacha njiani na kutokomea kusikojulikana. Waandishi wa habari nao walionja joto la jiwe kwa kuvamiwa na watu waliodhaniwa kuwa ni wafuasi wa CHADEMA kutokana kwa madai kuwa ni kushabikia CCM. Waandishi hao ni wa vyombo vya Uhuru, Mzalendo, Habari Leo, Jambo Leo, TBC, ITV na Shirima la Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye kuokolewa na Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s