Polisi wawatawanya CHADEMA

 

  • matokeo ya kura
  • Mchuano wabaki kwa CHADEMA na CCM, CUF vyama vyengine hoi!
  • Awali CHADEMA walifurika mitaani kushangilia
  • CCM yageuza kibao matokeo ya vijijin
  • Utulivu watawala katika upigaji kura

WAKATI matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga yakionyesha kuwapo kwa mchuano mkali kati ya CCM na Chadema, jana jioni Polisi walilazimika kuwatawanya wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani ambao walikuwa wakishinikiza kubandikwa kwa matokeo kwenye vituo huku wengine wakiimba nyimbo za hamasa kushangilia kile walichokiita ushindi wa mgombea wao, Joseph Kashindye.

Mbali ya kushangilia ushindi pasipo mgombea wao kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), baadhi ya wana Chadema hao usiku wa kuamkia leo walikesha katika ofisi za Tume hiyo Mjini Igunga, ambako kazi ya kujumlisha matokeo inafanyika ikiwahusisha maofisa wa tume, halmashauri ya wilaya, wagombea na mawakala wao.

Makundi ya vijana yalianza kuonekana katika maeneo vilikokuwa vituo vya kupigia kura mnamo saa 11:00 jioni jana na pale kulipokuwa na dalili za matokeo kuchelewa kubandikwa katika vituo, walianza kupiga kelele.

Hata hivyo, baada ya kubandikwa yalidhihirisha kuwepo kwa mchuao mkali baina ya vyama hivyo viwili.

Katika eneo la Stoo ya Pamba kulikokuwa na vituo vitano vya kupigia kura, vijana hao wakiwa katika makundi makubwa waliingia katika eneo la wazi lililopo hapo na kuanza kushangilia huku wakiimba nyimbo za hamasa baada ya kuwa yamebandikwa matokeo ya vituo viwili ambayo yalionyesha kuwa Kashindye alikuwa akiongoza kwa kura chache.

Hali hiyo ni kama ilianza kuwaogofya wasimamizi wa uchaguzi na baadhi ya polisi waliokuwa katika eneo hilo na baada ya muda gari la polisi likiwa na bendera nyekundu na askari wapatao tisa, lilifika na kudhibiti shamrashamra hizo.

Wakati vijana hao wakiwa bado wanazungumza na mmoja wa polisi hao, lilifika kundi jingine kubwa likitokea katika maeneo ya makazi huku wafuasi hao wakiimba. Kundi hilo nalo lilizuiwa na Polisi kuingia katika eneo la Stoo ya Pamba na baadhi yao kutimua mbio baada ya kuwaona polisi.

Hali kama hiyo iliripotiwa kutokea katika maeneo mengine kikiwamo Kituo cha ujenzi, ambako zilizuka vurugu ambazo hata hivyo, zilidhibitiwa baada ya muda mfupi na polisi wa doria.

Baadaye majira ya saa nnne usiku, kulikuwa na wafuasi wengi wa Chadema ambao walikuwa wamezunguka eneo la ofisi za NEC wakisubiri kutangazwa kwa matokeo ya jumla.

Pamoja na rabsha hizo, hadi jana saa 5:00 usiku, hakukuwa na taarifa zozote za kipolisi zilizotolewa kuhusu maandamano hayo ambayo yalipita karibu katika vituo vyote vya kupigia kura Mjini Igunga.

Hadi muda huo pia, kazi ya kujumlisha kura ilikuwa bado haijaanza kutokana na masanduku ya kura kuchelewa kufika, hivyo kushindwa kutekelezeka kwa ahadi ya Msimamizi wa Uchaguzi, Protase Magayane ambaye alisema ujumlishaji ungeanza saa 2:00 usiku na matokeo rasmi kutangazwa usiku wa jana.

Kuchelewa kuwasili kwa masanduku hayo kulitokana kwa kiwango kikubwa na mvua kubwa iliyonyesha jana jioni hivyo kusababisha baadhi ya barabara kupitika kwa tabu.

Ofisi za vyama
Ofisi za Chadema na CCM ndizo ambazo wafuasi wake walionekana wakiwa kwenye harakati za kupokea na kujumlisha matokeo ya kura kutoka kwa mawakala wao, waliokuwa wametawanywa katika vituo mbalimbali.

Katika viwanja vya Ofisi za Wilaya za Chadema, wafuasi wengi wa chama hicho walikuwa wakifuatilia kwa makini taarifa za mawakala, ambazo zilikuwa zikiratibiwa na timu iliyoongozwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.

Katika kambi ya CCM, hali ilikuwa hivyohivyo ambako January Makamba ambaye ni Katibu wa Mambo ya Nje na Siasa wa chama hicho alikuwa akiratibu matokeo hayo.

Katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya televisheni, redio na mitando ya intaneti, vilitumia matokeo hayo ya vyama kama taarifa za awali kwa umma, hali ambayo ilionekana kama ni kuingilia kazi za NEC ambayo kisheria, ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza matokeo hayo.

Hali ilikuwa tofauti katika ofisi za CUF, ukimya ulikuwa umetawala kwa kiasi kikubwa huku baadhi ya viongozi wake wakuu wakielezwa kuwa walikuwa wameshaondoka Igunga, kurejea walikotoka.

Chama hicho kama ilivyo kwa Chadema na CCM kilikuwa kikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika uchaguzi huo, kutokana na kumsimamisha mgombea, Leopold Mahona ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana alipata kura zaidi ya 11,000, nyuma ya aliyeshinda kiti hicho Rostam Aziz wa CCM.

Baadhi ya matokeo ambayo yalipatikana kwenye Kata za Igunga ni Kituo cha Bigadilele ambako CCM ilipata kura 135 na Chadema (96), Choma Bwangamila CCM (193) na Chadema (58).
Katika katika kata ya Nanga, yalionyesha CCM kupata kura 845 dhidi ya 915 za Chadema, CUF 45 ,DP sita, AFP 1, Sau 2, UPDP tatu na 1.

Kwa upande wa matokeo yaliyojumlishwa kwa Kata ya Nkinga yalionyesha CCM kilipata kura 1,266, Chadema 1,205, CUF 64 Chausta 2 na AFP 2.

Matokeo ya Kata ya Bukoko yalionyesha CCM kilipata kura 828, Chadema 726, CUF kura 7, wakati vyama vya SAU, DP, CHAUSTA, AFP na UPDP vikibaki patupu.

Katika Kata ya Sungwizi, CCM kilikuwa na kura 1,318 huku Chadema kikiwa na kura 671 na CUF kikiambulia kura 14.
Katika Kata ya Simbo, Chadema kilionekana kuwa mbele kwa kupata kura 861 huku CCM kikiwa na kura 553, CUF 268 na SAU kura 1.

Hali ya Upigaji kura
Kwa ujumla, hali ya upigaji kura ilikuwa shwari licha ya kuwapo kwa baadhi ya watu waliodai kuyakosa majina yao kwenye vituo.

Mgombea UPDP hakupiga kura
Mgombea ubunge kupitia UPDP, Hemedi Ramadhani Dedu hakupiga kura kwa kuwa hakujiandikisha katika Jimbo la Igunga.

“Sikupiga kura ndugu yangu kwa sababu sikujiandikisha hapa, nimejiandikisha Dar es Salaam.”

Chausta bila mawakala
Magayane alisema vyama karibu vyote vilijitahidi kuweka mawakala isipokuwa Chausta ambacho kilishindwa kuweka mawakala katika vituo vya kupigia kura.

“Unajua hili suala ni mkataba baina ya vyama vyenyewe na mawakala hao, sasa inawezekana kwamba hali ya kifedha si nzuri katika vyama hivi, hivyo utakuta ni vyama vichache ambavyo vilimudu kuwa na mawakala sehemu zote,” alisema.

Upigaji kura
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema saa 12.00 asubuhi na ilipotimu saa 1:00 asubuhi, upigaji kura ulianza wakati ambao tayari baadhi ya wananchi walikuwa wamejipanga katika mistari wakisubiri kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.

Sura za wapiga kura zilikuwa zimejawa na matumaini na kila aliyekuwa akiingia katika chumba cha kupigia kura alionekana akiwa na shauku ya kumpata kiongozi mpya.

Hata hivyo, watu walikuwa wakijitokeza katika vikundi vidogovidogo na wakati wa asubuhi kati ya saa 1:00 na 3:00 wengi waliojitokeza walikuwa ni kinamama, wazee na watu wenye ulemavu wakati vijana walijitokeza baadaye.
Katika kituo cha Shule ya Msingi Mwenge, Mjini Igunga, Mpiga kura, Rehema Damson alisema uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na ule wa mwaka jana kutokana na kuwapo vurugu nyingi zilizosababishwa na wingi wa vyama vinavyoshiriki.

Katika Kituo cha Ujenzi, Ngeso Mitimingi alieleza kufurahishwa kwake na utaratibu wa upigaji kura akisema mwaka huu kumekuwa na mwamko wa kushiriki katika uchaguzi tofauti na mwaka jana kutokana na kuongezekwa kwa uelewa wa masuala ya demokrasia.

“Mwaka huu tunapiga kura kumchagua mbunge, miaka iliyopita hali haikuwa hivi kwa sababu tulikuwa tukipiga kura tukijua nani atashinda, lakini leo kuna tofauti kubwa, ndiyo maana huu ni uchaguzi tofauti,” alisema Emiliana Edson baada ya kupiga kura katika Kituo cha Shule ya Msingi ya Azimio.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s