Igunga kumekucha

WAKATI leo wananchi wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora wanapiga kura kumchagua Mbunge wao mpya, vituko, vijembe na shamrashamra viligubika mikutano ya mwisho ya kampeni kwa vyama vinane vilivyosimamisha wagombea jana.

Moja ya makosa ambalo lingeweza kuchafua ufungaji wa kampeni za uchaguzi mdogo
Igunga jana, ni uamuzi wa vyama vya CCM, Chadema na CUF, kufanya mikutano yao katika viwanja vilivyo jirani na Igunga mjini kiasi kwamba mgombea akizungumza uwanja mmoja, viwanja vingine vinamsikia.

Hali ilikuwa tete pale Chadema ilipoamua kwenda katika uwanja wao wa kufunga kampeni wa Barafu kwa maandamano kupitia katika uwanja wa kituo kidogo cha mabasi cha Igunga
walipokuwa CUF na Uwanja wa Sokoine, walipokuwa CCM.

Hata hivyo katika uwanja wa CUF, kulikuwa na maandalizi ya awali ya mkutano huo lakini katika uwanja wa Sokoine, CCM walikuwa wameshaanza mkutano wao uliokuwa ukiongozwa na kada wa chama hicho, Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu mstaafu, Philip Mangula.

Maandamano ya Chadema yaliyokuwa yakichagizwa na helikoptayao iliyokuwa imesimama
juu ya maandamano hayo, yalipofika katika mkutano wa CCM, umbali wa meta zisizozidi 10, helikopta ya chama hicho ilisimama juu ya uwanja wa mkutano wa CCM.

Kitendo hicho kilisababisha vijana mabaunsa wa chama hicho tawala kuanza kupandisha
munkari kutaka kukabiliana na wa Chadema waliokuwa wakilinda maandamano hayo yaliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.

Vijana hao wakiongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya waliamua kwenda kukabiliana na wa Chadema na kusababisha polisi waliokuwa katika mkutano wa CCM, kujipanga katikati ya makundi hayo kuzuia vurugu yoyote isijitokeze.

Ilipofika saa 11.48 jioni, helikopta ya CUF ilipita katika anga la Igunga na kushuka katika uwanja ambao kabla ya hapo ulikuwa na viongozi tu wa CUF.

Mara baada ya helikopta hiyo kutua, huku mwendeshaji kampeni wa CUF akitangaza kuwa
Mgombea wa CUF, Leopold Mahona ndiyo anatua, baadhi ya watu walihama kutoka mkutano wa Chadema uliokuwa karibu na kwenda kuangalia helikopta ya CUF.

Wakati hayo yakitokea Igunga mjini, katika Kata ya Nyandekwa, mgombea wa CUF, Mahona na Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Magdalena Sakaya, nusura wapigane na Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk. Anthony Mbassa (Chadema), kwa madai
kuwa Mbunge huyo aliwatukana.

Sakata hilo lililotokea katika kata hiyo ambako vyama hivyo viwili kwa mujibu wa ratiba vilikuwa na mikutano kijijini hapo kwa nyakati tofauti, lakini CUF wakachelewa kuanza mkutano jambo lililowafanya vijana wa Chadema wakiongozwa na Dk. Mbassa kwenda kuzuia mkutano huo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), CUF ilitakiwa kuanza mkutano wake wa hadhara wa lala salamakatika kata hiyo, saa nne asubuhi katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyandekwa na baadaye saa tano asubuhi Chadema walikuwa na mkutano katika kata hiyo katika viwanja vya Sungusungu. Saa sita kasoro wanachama wa
Chadema walikuwa tayari wamejikusanya wakimsubiri Dk. Slaa na mgombea wa chama hicho Kashindye, lakini ghafla helikopta ya CUF ikatokeza na kuwachanganya wanachama hao wakidhani kuwa ni ya Chadema.
Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya helikopta hiyo kutua kwenye viwanja vya shule ya msingi Nyandekwa na Mahona akiongozana na Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Ismail
Jussa Ladhu, walipanda jukwaani na kuanza kumwaga sera
jambo ambalo liliwachukiza wafuasi wa Chadema. Dk. Mbassa akiongozana na baadhi ya vijana wa chama hicho waliwafuata polisi waliokuwa wakilinda usalama wa mikutano hiyo na kuwataka wausimamishe mkutano huo wa CUF kwa kuwa umeingilia mkutano wa Chadema uliotakiwa kuanza muda mfupi na kwamba muda wa mkutano wao tayari ulishapita. Mbunge huyo wa Chadema aliingia katika uwanja huo wenye mkutano wa CUF na kutaka kupanda jukwaani lakini polisi waliokuwapo walimzuia na kujaribu kuzungumza na Naibu Katibu Mkuu bara wa CUF Julius
Mtatiro wakimtaka wafanye haraka kumaliza mkutano huo na kuondoka. Wakati sakata hilo la mabishano baina ya Mtatiro, polisi na Dk. Mbassa likiendelea Jussa na Mahona waliendelea kumwaga sera zao huku Jussa akiwataka wakazi wa Nyandekwa kuepuka kuchagua chama cha fujo cha Chadema na kutolea mfano vurugu hizo za kutaka kuvurugwa kwa mkutano wao. Sakata hilo lilimalizika kwa CUF kuondoka eneo hilo chini ya usalama wa polisi lakini gari iliyokuwa imebeba spika za matangazo za CUF ilijikuta katika wakati mgumu kutokana na wafuasi wa Chadema kuitaka iondoke haraka eneo hilo huku ikionekana wazi kuwa na hitilafu. Polisi walifanikiwa kuisogeza mbali na eneo la mkutano wa CUF, na muda mfupi baadaye helikopta ya Chadema iliwasili kwenye mkutano na Dk. Mbassa akajitapa kuwa Chadema siku zote lazima itadhibiti wale wote wanaowaingilia na kutolea mfano walivyofanikiwa
kukatisha mkutano wa CUF. Mkapa afunga kampeni za CCM Rais mstaafu Benjamin Mkapa akifunga mkutano wa mwisho wa kampeni wa CCM alisisitiza kwamba wapinzani wa kiafrika ni watu ambao wamejijengea tabia ya
kupinga kila kitu na kwamba wanachokifanya ni kuwahadaa wananchi kwa sera zao za matusi na kejeli.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha Chama cha (CHADEMA) kumshambulia Mkuu wa Wilaya ya Igunga Fatuma Kimario na kwamba kama angekuwa yeye Rais kama ilivyokuwa wakati ule asingekubali kuwaachia kama alivyofanya Rais Jakaya Kikwete ambapo alimsifu kwa uvumilivu wake. Alitumia nafasi hiyo kuwaambia wananchi kuwa uvumilivu una mwisho wake na kitendo ambacho kimefanywa na CHADEMA kuna siku Serikali itashindwa na kutumia nafasi hiyo kuwaambia wananchi kazi ya wapinzani kila siku ni kusema wameibiwa kura wakati hakuna
uchakachuaji kazi yao kubwa ni kulalamika kwa mabwana zao. Akizungumza katika mkutano huo wa mwisho wa kampeni za CCM katika Kata ya Nkinga, Mkapa alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wapinzani wanatoa lugha ambazo hazina msingi wowote kwa Watanzania na wananchi wa Igunga na kuongeza kuwa ndimi za wapinzani zimejaa hila, vinywa vyao vimejaa maneno ya uongo. Mkapa wakati anawahutubia wananchi hao ambao walifurika
kwa wingi katika mkutano huo, alisema kuwa ni mambo ya ajabu kuona wapinzani wakizunguka na kutoa lugha za kudhalilisha na kutukana watu wakati hawana lolote la kufanya na hawana sera mbadala. Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli aliwahakikishia wananchi wa Igunga kuwa huu ni wakati muafaka kwao kuhakikisha wanamchagua Dk.Kafumu katika uchaguzi unaofanyika leo. Akizungumza na wananchi wa Igurubi jana mchana, Dk.Magufuli alisema wananchi wa Igunga wanafanya uchaguzi wa kuchagua mbunge wao baada ya kufanyika kwa kampeni lakini ana uhakika mkubwa kuwa Dk.Kafumu atakuwa Mbunge wa jimbo hilo. Kwa upande wa Chadema, Dk. Slaa akihutubia katika mkutano wa mwisho wa kampeni Igunga Mjini aliwataka wakazi wa Igunga kujitokeza kwa wingi kupiga kura lakini akawasihi kutokwenda mbali na vituo vya kupigia kura ili kulinda kura zitakazopigwa. Alisema chama hicho kimejipanga kiasi cha kutosha kuhakikisha kuwa kinatumia kila mbinu ili kuhakikisha kuwa kinalinda kura zake zitakazopigwa ili mgombea wa chama hicho aweze kushinda uchaguzi huo.
Alisema katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru, serikali ya CCM imeshindwa kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na umasikini kwa wananchi wakati Taifa likipoteza mabilioni ya fedha kutokana na vitendo vya ufisadi,
rushwa na wizi wa fedha za umma. Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) aliwataka
wananchi kutokwenda mbali na vituo watakavyopigia kura ili kulinda kura hizo zisiweze kuibwa.
Nao Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umeeleza kusikitishwa na kitendo ilichodai kuwa ni uamuzi wa viongozi wa Chadema wa kutumia ndugu na marafiki zao kula fedha za uwakala wa kusimamia uchaguzi mdogo wa Igunga.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s