CHADEMA yaingiza vijana 120 Igunga

SIKU moja kabla ya uchaguzi mdogo wa Igunga, Chadema imepeleka zaidi ya vijana 120 na inadaiwa kuwa na mpango wa kufikisha vijana 1,200 katika wilaya hiyo kutoka majimbo ambayo wana wanachama wengi, kwa madai ya kwenda kupiga kampeni na kufanya kazi ya uwakala.

Vijana hao ambao baadhi yao gazeti hili limewashuhudia katika ofisi za Chadema, wanadaiwa kutoka Mwanza lakini inadaiwa wengine wako njiani kutoka Tarime, Dar es Salaam, Moshi, Arusha na Singida na wataingizwa Igunga wakiwa katika mabasi madogo aina ya Toyota Coaster, Hino na wengine wanadaiwa kuingizwa na Fuso.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Siasa na Mambo ya Nje, January Makamba alisema wao walipata taarifa hizo kutoka kwa wanachama wa CCM katika mikoa hiyo.

“Tuna mtandao mkubwa nchi nzima, tulipigiwa simu kutoka Mwanza tukaambiwa kuna watu katika makundi makubwa wanapanda mabasi manne wakiimba nyimbo za Chadema, tukatoa taarifa kwa vyombo vya usalama.

“Baada ya hapo tuliomba kwenda kushuhudia na tukaenda Tinde kule Shinyanga tukakuta polisi wameshaweka kizuizi…kwenye muda wa saa saba wakaingia watu tulipowahoji wakasema ni makada wa Chadema wanakuja katika kampeni,” alisema Makamba.

Katika kundi hilo la Mwanza, walikuwa na mabasi aina ya Coaster matatu na Hino moja, mawili yaliingia saa tisa usiku na mengine mawili asubuhi na yote yanamilikiwa na Kampuni ya Mukesh ya Mwanza.

*Madai ya CCM
Kwa mujibu wa January, taarifa walizonazo ni kwamba Chadema wana mpango wa kuleta vijana 1,200 na lengo lao ni kufanya vurugu kwa wapiga kura wa CCM ambao ni watu wazima na wanawake ili wasiende kupiga kura.

January alisema kwa sasa vijana hao wameshafikia 600 na wamekuja kwa njia mbalimbali; wako mmoja mmoja kwa njia ya mabasi ya kawaida ya abiria na wako walioletwa kwa makundi kama hao wa Mwanza.

Vijana hao kwa mujibu wa January, si mawakala kwa kuwa mawakala Sheria inataka majina yao yawe yameshapelekwa kwa msimamizi wa uchaguzi na waapishwe siku saba kabla ya uchaguzi.

“Unaleta watu hao, hawapigi kura, hawana shughuli yoyote huko si kufanya vurugu?” alihoji January na kuongeza kuwa Chadema kimeonesha kuwa kinataka ushindi kwa bei yoyote.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa chama cha SAU kilikataliwa kuweka mawakala kwa kuwa kilichelewa kwa siku moja kupeleka mawakala wake na kukuta mawakala wengine, wakiwemo wa Chadema, CUF na CCM wameshaapishwa Septemba 27 mwaka huu.

“Hivi katika hali kama hii ya kuomba kura kutoka Igunga, kwa nini ulete vijana wengi kama hawa? Na katika mantiki ya kawaida kama ni mawakala, kwa nini uamini wana Igunga wakupe kura na usiwaamini wawe mawakala? Alihoji January.

Alivitaka vyombo vya usalama na Msimamizi wa Uchaguzi kuhakikisha hali ya usalama inakuwepo wakati wote wa uchaguzi mpaka atakapopatikana mshindi na wananchi wa Igunga waachiwe wachague kiongozi wao kwa uhuru.

January pia alitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi ihakikishe kuwa mawakala wana vitambulisho vyenye picha zao na wana barua za vyama wanavyoviwakilisha.

*Chadema wakiri
Akizungumzia madai hayo, Mratibu wa Kampeni za Chadema, Mwikabe Mwita alikiri kuingiza vijana aliodai wako 120 kutoka Mwanza na kuongeza kuwa kazi zao ni mbili; kupiga kampeni na uwakala.

Alifafanua kuwa pamoja na kuwa mawakala wao walishaapishwa, lakini hawawezi kuwaamini baadhi ndio maana wameleta wengine wanaowaamini na watapelekwa maeneo aliyoita korofi.

Alipoulizwa kuhusu suala la Sheria kutaka mawakala hao wawe wameapishwa siku saba kabla ya siku ya uchaguzi, Mwita alidai kuwa Sheria hiyo hiyo imeruhusu mawakala kubadilishwa ndani ya saa 48.

*Nahodha akiri kuwa na taarifa

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha amekiri jeshi la polisi mkoani Shinyanga kushikilia mabasi manne yanayodaiwa kubeba vijana wa Chadema na kuwapeleka mjini Igunga kwa ajili ya uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa alisema kwa sasa kinachofanyika ni kuchunguza watu waliokuwamo kwenye mabasi hayo ni akina nani na wanatoka wapi.

“Ni kweli nafahamu kuwa polisi inashikilia mabasi manne yaliyobeba vijana wa Chadema, tuacheni suala hili tulifanyie kazi, tunataka kuchunguza ni akina nani na wanatoka wapi,” alisema Vuai.

Hata hivyo, mabasi hayo na watu hao waliachiwa kwa kuwa gazeti hili liliyashuhudia yakiwa na watu hao katika ofisi za Chadema Igunga.

Aliendelea kusisitiza juu ya mkakati wa polisi wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani ambapo jeshi hilo litaweka doria katika maeneo mbalimbali mjini Igunga, ikiwa ni pamoja na kutoa namba ya simu za dharura za simu kwa ajili ya kuripoti matukio ya uhalifu.

Namba hizo ni 0784 396484, 0787 027021, 0754 492545, 0769 406323, 0784 769263, 0718 646131 na 0787 940449. Hata hivyo mapema jana, Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo hilo, Protace Magayane, alieleza sheria kuruhusu mawakala kutoka katika maeneo nje ya Jimbo la uchaguzi.

Alisema kutokana na sheria hiyo, Chadema wanaruhusiwa kuweka mawakala ambao wanatoka nje ya Jimbo la Igunga na kueleza kwamba kwa vile Chadema walipendekeza majina ya mawakala wapya, mawakala hao wangeapishwa baadaye jana.

Alipotafutwa jioni jana ili kuzungumzia hatua zaidi zilizochukuliwa ili kuwaapisha mawakala hao, Magayane alisema alikuwa nyumbani kwa mapumziko na kwamba atazungumzia zaidi suala hilo leo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s