CUF ‘kidedea’mdahalo Igunga

.CHAMA cha Wananchi (CUF) juzi usiku kiliibuka ‘kidedea’ katika mdahalo wa wagombea wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda ubunge wa Igunga, huku CCM na Chadema wakijikuta katika wakati mgumu wa kujibu tuhuma zinazowakabili wagombea wao.

Hata hivyo, katika mdahalo huo uliotawaliwa na vurugu za mashabiki wa vyama hivyo tangu mwanzo hadi mwisho, mgombea wa CCM, Dk. Dalaly Kafumu, aliwashangaza wana CCM kwa utulivu na uwezo wake wa kutumia Ilani ya CCM, usomi na ufahamu wake wa jimbo hilo kujibu tuhuma zilizomwandama kuhusu mikataba mibovu ya madini.

Wagombea katika kiti cha ubunge wa jimbo la Igunga wakiwa wameshikana mikono mara baada ya kumalizika kwa mdahalo wa pamoja uliofanyika ukumbi wa Sakao mjini Igunga juzi usiku, kutoka kulia ni leopad Mahona wa CUF, katikati ni Dk. Dalay kafumu na wa kushoto ni joseph Kashindye wa CHADEMA.Mgombea wa Chadema, Peter Kashindye, aliyetarajiwa kung’ara kutokana na mtindo wa siasa za chama hicho wa kutumia tuhuma kupata mashabiki, alijikuta katika wakati mgumu wa kunyong’onyesha mashabiki wake, baada ya siasa hizo kumgeuka.

Mgombea wa CUF, Leopold Mahona, ambaye hakuwa na tuhuma, ndiye aliyegeuzia kibao cha ufisadi kwa mgombea wa Chadema pale alipomtaka Kashindye aeleze alivyoshiriki kula fedha za mradi wa majengo ya kituo cha elimu katika tarafa ya Simbo akiwa Mratibu wa Elimu, huku akishangaa ilikuwaje akapandishwa cheo kuwa Mkaguzi wa Shule.

Mahona alisema wagombea wa Chadema na CCM wanajuana, kwa kuwa wametoka nyumba moja; serikalini huku akihoji iweje mgombea wa Chadema, Kashindye ‘avute’ mshahara wa Serikali ya CCM mwisho wa mwezi na baada ya hapo tarehe moja mwezi uliofuata ajiite mpinzani.

Siasa za ufisadi, vurugu Chadema
Kashindye aliingia ukumbini na kitabu cha madini kumtuhumu Dk. Kafumu kwa kutangaza kwa lengo la kuuza maeneo ya madini ya Igunga nje ya nchi na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka uliopita, ikieleza Sh milioni 800 zilivyopotea katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.

Hata hivyo, hakutarajia pale Dk. Kafumu kwa utaratibu aliposema “nimetupiwa madongo mengi, ngoja nami ingawa si kilichotuleta hapa, nirushe kidogo madongo kwa Kashindye, kwa kushiriki kutafuna Sh milioni 800 alizozisoma katika taarifa ya CAG.”

Katika majibu kuhusu alivyokula fedha za mradi wa tarafa ya Simbo, Kashindye alisema anamwona Mahona aliyekuwa mwanafunzi wake, anajaribu kumrushia madongo na kuongeza kuwa mgombea huyo wa CUF hajui kitu, kwa kuwa wakati yeye akiwa msimamizi wa mradi huo, Mahona alikuwa mwanafunzi asiyejua kitu.

Kuhusu kushiriki kula Sh milioni 800 za Halmashauri akiwa Mkaguzi wa Elimu na mmoja wa maofisa wa halmashauri hiyo, Kashindye alijikuta akikana kuwa ofisa wa halmashauri hiyo na kujiita kuwa ofisa wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye akasahau na kujiita ofisa wa Wizara ya Elimu.

Alipoulizwa kwa nini hakusema kuwa kuna wizi wa fedha mpaka akasubiri wakati wa kampeni, alijibu kuwa yeye amesomea lugha na anajua anavyopaswa kusema kitu sahihi kwa wakati sahihi na mahali sahihi.

Huku akiwa amesahau kuwa alikana kuwa ofisa wa Halmashauri, alijikuta akikubali akisema asingeweza kusema kuwa kuna wizi wa fedha katika halmashauri, kwa kuwa alihofia kuharibu uhusiano ofisini.

Alipotuhumiwa kuhusika kuporomosha kiwango cha elimu Igunga ili CCM izidi kulaumiwa, Kashindye alisema yeye ni kama mpimaji wa maabara, anapima ugonjwa na kutoa ushauri, watekelezaji ambao ni halmashauri ndio wa kulaumiwa.

Kuhusu Chadema kutumia alama ya V, inayotumiwa na makundi ya kigaidi duniani kikiwamo cha Al-Qaeda, Al-Shabaab na vingine, Kashindye alisema alama hiyo si ya kigaidi bali ya ushindi.

Alifafanua, kuwa alama hiyo imetumika Libya, Tunisia na Misri kukomboa wananchi kutoka serikali kandamizi na kwa Tanzania Serikali ya CCM ni kandamizi na iko mbioni kuondolewa.

Kuhusu vipi atatetea wanawake wasionewe, wakati Chadema ilimshambulia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, Kashindye alisema Mkuu huyo hakushambuliwa, bali alihujumu uchaguzi na alitolewa tu katika jengo alimokuwa akifanyia mkutano wa kuihujumu Chadema.

Kafumu awashangaza CCM
Wakati mpaka saa 10 jioni kulikuwa na taarifa kuwa Dk. Kafumu asingeshiriki mdahalo huo,
baadaye aliingia ukumbini na wagombea wengine wa Chadema na CUF, na kuonesha umahiri wa kutumia ilani ya CCM kwa utulivu kujibu tuhuma dhidi yake na hoja mbalimbali na kuwaamsha wana CCM vitini kwa shangwe.

Kuhusu hoja kuwa alihusika kusaini mikataba ya madini inayoinyima nchi mapato, Dk. Kafumu alisema yeye alikuwa Kamishna wa Madini kwa miaka mitano na kazi yake ilikuwa ni
kushauri na kusimamia sheria na anayesaini mikataba ni Waziri na anayetunga sheria ni Bunge, ambamo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto alishiriki.

Alipotakiwa aeleze alishindwa nini kusaidia wachimbaji wadogo wa Igunga wakati akiwa jikoni kama Kamishna wa Madini na sasa atafanya nini akiwa Mbunge, Dk Kafumu alisema hakushindwa bali kuna mambo alifanya.

Alisema alitoa vibali vya uchimbaji mdogo maeneo ya Igunga na kuwaanzishia soko la kuongeza thamani madini yao Nzega. Alifafanua kuwa katika nafasi ya

ukamishna, alikuwa akishughulikia nchi nzima na ilikuwa vigumu kusaidia Igunga peke yake, lakini akiwa Mbunge, atashughulikia Igunga pekee na kutumia utaalamu wake kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo zaidi.

Alipotakiwa kueleza atafanya nini kujenga daraja la Mbutu, linalozungumzwa kama moja ya vigezo vya kuinyima CCM kura, Dk. Kafumu alisema lipo katika Ilani ya Uchaguzi na tayari
limetengewa fedha katika Bajeti ya mwaka huu na mkandarasi wa kulijenga ameshatangazwa.

Hata hivyo, Kashindye aliema Dk. Kafumu amedanganya, kwa kuwa zabuni ya ujenzi wa daraja hilo ndiyo imetangazwa na anashangaa kusikia mkandarasi amepatikana.

Lakini Dk. Kafumu aliomba radhi kuwa ulimi uliteleza.

Kwa upande wa Mahona, alisema ataanza ujenzi wa daraja hilo bila kutegemea bajeti ya Serikali siku 100 baada ya kuchaguliwa kwa kutumia rasilimali za Igunga, lakini Dk. Kafumu alimwambia hajui utaratibu wa uwekezaji, ndiyo maana anazungumzia nadharia ambayo ni tofauti na utekelezaji.

Vurugu na ushindi wa CUF
Awali kabla ya kuanza kwa mdahalo huo wenye jina la ‘Uchaguzi Mdogo wa Igunga na Tanzania Tunayoitaka’, mashabiki wengi wa CUF walifika mapema ukumbini na kuchukua nafasi zote za mbele kabla ya mashabiki wa CCM na Chadema.

Baada ya kuchukua nafasi hizo, mabango mengi ya mgombea wa CUF na bendera za chama hicho, viligawiwa kabla Chadema na CCM hawajafika na wachache waliokuwapo, walikuwa mikono mitupu bila mabango wala sare za vyama vyao.

Mbinu hiyo ya CUF, ilisababisha mashabiki wengi wa CCM na Chadema wakiwamo wabunge wao, kulazimika kukaa viti vya nyuma, huku wakituma magari yao kwenda kutafuta mabango ya wagombea wao na kuchangia kutokea kwa vurugu za mara kwa mara kati ya CCM na Chadema waliokuwa wamekaa pamoja.

Wagombea walipoingia ukumbini, mashabiki wa CUF walisimama na mabango ya Mahona na kumsifu, jambo lililosababisha mashabiki wa Chadema na CCM kutoka nyuma ya ukumbi nao kuja mbele kushangilia wagombea wao.

Mratibu wa Mdahalo huo, Rosemary Mwakitwange, alilazimika kusitisha matangazo na kuomba viongozi wa kitaifa wa vyama hivyo, Mwigulu Nchemba wa CCM, Zitto wa Chadema na Julius Mtatiro wa CUF kuzungumza kutuliza mashabiki wao.

Mdahalo ulipoanza, ghafla kuliibuka mzozo kati ya mashabiki wa Chadema na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage na kusababisha mdahalo usitishwe tena, ambapo Zitto alilazimika kwenda kumchukua Rage na kumhamishia viti vya mbele na kumtoa nje mmoja wa mabaunsa wa Chadema.

Baada ya kumalizika kwa mdahalo, viongozi hao wa kitaifa walipewa nafasi ya kusema neno la kufunga, akaanza Nchemba, akafuatia Zitto lakini alipoanza kuzungumza Mtatiro, alimtuhumu Nchemba kwa kuweka kambi za vijana kwa ajili ya vurugu na kutishia kuwa CUF, ndio wanaoziweza na kila mtu anajua.

Tuhuma hizo zilimwamsha Nchemba akitaka kujibu mapigo na alipopewa kipaza sauti, mashabiki wa CUF walisimama na kupiga kelele, huku wakivamia eneo rasmi la kuzungumzia na kumzuia, ikabidi mdahalo ufungwe kuepuka vurugu zaidi huku nje ya ukumbi polisi wakiwa na mabomu ya kutoa machozi wakijiweka sawa.

NEC yalaani uhuni
Naye Halima Mlacha anaripoti kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imelaani vitendo vya kihuni na visivyo vya kistaarabu vinavyofanywa na baadhi ya vyama katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Mwenyekiti wa Muda wa Tume hiyo, Profesa Amon Chaligha, alisema vitendo hivyo ambavyo ni pamoja na kumwagiana tindikali,
kurushiana matusi na risasi na kuvuliwa nguo kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, vinakwenda kinyume na Sheria na Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

“Vitendo hivi pia ni kinyume na utamaduni wa Mtanzania wa kuheshimiana na kujenga umoja uliodumu kwa miaka 50 ya uhuru wa Taifa letu,” alisema Profesa Chaligha.

Alisema tangu kampeni za uchaguzi huo zianze mapema mwezi huu, Msimamizi wa Uchaguzi wa Igunga, amepokea malalamiko matatu ambayo ni kumwagiwa tindikali, kudhalilishwa kwa DC na kujeruhiwa kwa mapanga aliyoyawasilisha katika Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ngazi ya jimbo.

“Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka kila chama cha siasa nchini, iliyapitia malalamiko hayo na kuyatolea uamuzi ili kuipa uhuru Mahakama iyashughulikie bila kuingiliwa,” alisema.

Hata hivyo, baada ya Kamati hiyo kumaliza kujadili malalamiko hayo, muda mfupi baadaye, matukio mengine ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi yaliripotiwa; ambayo ni kurushiana risasi za moto, kuwa na silaha katika mikutano ya kampeni, kuharibu mali na kutumia lugha ya
matusi na ukabila badala ya Kiswahili katika kampeni.

Profesa Chaligha alisema baadhi ya matukio hayo yameshawasilishwa katika Kamati ili yajadiliwe na kutolewa uamuzi, lakini pia alisisitiza kuwa timu ya makamishna wa Tume hiyo inajiandaa kwenda Igunga kukutana na vyama vya siasa vinavyofanya kampeni jimboni humo, ili kuvikumbusha umuhimu wa kufuata maadili ya uchaguzi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s