CCM yakaliwa pabaya Igunga

UPEPO wa kisiasa si shwari kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa Igunga baada ya wafanyabiashara mashuhuri walioombwa na chama hicho kuchangia sh milioni 300 kugoma kutoa fedha hizo.

Habari za uhakika kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara hao waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina, zinasema wafanyabiashara hao wamegoma kwa sababu wamegundua CCM kinafuja pesa kwa anasa badala ya kampeni.

Mmoja wa hao waliogoma, ambaye yuko ndani ya timu ya kampeni, amesema kikao cha CCM kuchangisha wafanyabiashara hao kilifanyika katika Hoteli ya Peak, Septemba 10, na kilihudhuriwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, na viongozi wengine wa CCM. Kila mfanyabiashara alikubali kuchanga sh milioni 5.

Hata hivyo, habari zimesema kuwa sasa wafanyabiashara hao wamegoma kutimiza ahadi zao na wengine waliokuwa wametoa kiasi cha fedha wamechukua fedha hizo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao aliliambia Tanzania Daima kuwa uamuzi wa wafanyabiashara hao umekuja baada ya kutoridhishwa na matumizi mabaya ya chama hicho, hasa baada ya mmoja wa viongozi wa kampeni za CCM kukabiliwa na tuhuma za ngono.

“Ni kweli tulikutana na Mkapa na Mukama hapo hotelini, tarehe 10, kuanzia saa tatu asubuhi na tulikubali kuchangia. Lakini tumeamua kutoendelea na zoezi hili kwa sababu hatuwezi kutoa fedha zetu ambazo zinatumika hovyo,” alisema.

Imedaiwa kwamba baada ya kudhihirika kwa tukio la fumanizi linalomhusisha kiongozi huyo na tuhuma kwamba baadhi ya viongozi wanagawa fedha kwa wananchi, wafanyabiashara hao waliamua kusitisha michango yao.

Wengine waliamua kudai fedha zao kutoka kwa mtu waliyekuwa wakimkabidhi.

Habari zinasema fumanizi hilo lililomkumba kigogo huyo, limekigharimu chama chao kiasi cha sh milioni 14 ili kumnyamazisha mume wa mwanamke huyo aliyefumaniwa.

Polisi wakana taarifa za CCM

Wakati hayo yakijiri, polisi wilayani hapa wamekanusha madai ya Mukama kwamba jeshi hilo limekabidhiwa majina ya makomandoo 33 walioletwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kufanya fujo na ghasia kwa lengo la kuvuruga uchaguzi mdogo wa ubunge.

“Chama chetu kinazo taarifa za CHADEMA kuleta jimboni hapa makomandoo 33 waliopata mafunzo katika nchi za Afganistan na Libya ambao ndiyo vinara wa vitendo vya uhalifu vinavyotokea wilayani hapa wakati huu wa kampeni za uchaguzi mdogo.

Hawa ndio wanaomwagia watu tindikali, wanaochoma moto nyumba zao na kukata watu mapanga,” alidai Mukama.

Mukama alisema kuwa makomandoo hao wamepiga kambi katika wilaya za Igunga, Nzega na Kahama, na kuyataja maeneo hayo kuwa ni kata za Itobo, Bulinde, Bukene, Isaka na kwingineko.

Mukama alionya kuwa njia zinazotumiwa na CHADEMA kuendesha siasa zake zinatengeneza mazingira ya uhaini na ugaidi na kukilinganisha na kilichokuwa kikundi cha kigaidi cha Renamo cha Msumbiji.

Lakini Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu, alisema jeshi lake halijapata taarifa za watu hao wanaopewa sifa ya ukomandoo kama ilivyotangazwa na Mukama jana.

“Sisi jeshi la polisi hatuna taarifa kama hizo, labda wamepeleka katika vyombo vingine vya usalama,” alisema Kamanda Mungulu.

Hata alipoambiwa kwamba CCM imethibitisha kufikisha habari hizo katika jeshi hilo, bado kamanda Mungulu alikanusha kujua jambo hilo.

“Nimesema sijui lolote. Kama ni kweli wangetuambia, maana sisi ndio tunaowajibika kulinda usalama wa watu wote. Leo asubuhi tulikuwa na kikao, lakini hakuna taarifa kama hiyo iliyoletwa, na sijaisikia popote. Kama ingekuwapo ningewaambia maana hakuna la kuficha, hasa katika tuhuma nzito kama hiyo,” alisema Mungulu.

Alionya wanasiasa wasijaribu kulihusisha ama kulitumia jeshi la polisi kwa manufaa ya kisiasa.

Kamanda huyo aliongeza kuwa katika kusimamia usalama, hawataogopa kumkamata yeyote anayevuruga amani bila kujali hadhi yake na chama anachotoka,” alifafanua.

Mukama akerwa na Tanzania Daima

Katika hatua nyingine, Mukama alionyesha kukerwa na habari za tathmini ya uchaguzi wa jimbo hilo iliyofanywa na CHADEMA na kuandikwa na baadhi ya magazeti likiwemo Tanzania Daima, zikionyesha kuwa chama hicho kitashinda kwa kura kati ya asilimia 55 na 74.

“Hivi mtu na akili yako ambaye uko hapa Igunga unasema CHADEMA inashinda kwa asilimia 74, heee? Hizo kura watakuja nazo? Labda zimekuja na hao makomandoo walioko Chuma cha Nkola, Bukene, Bulinde, Isakamaliwa na Itobo,” alisema Mukama..

Aidha, Mukama aliyashambulia magazeti yaliyoandika habari zilizowapa sifa za ushujaa, wabunge wawili wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya kumweka chini ya ulinzi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

Aling’aka: “Waandishi wa habari mnashabikia uhalifu; watu wamefikishwa mahakamani kwa uhalifu wanarudi mnasema wamepokelewa kishujaa!”

CHADEMA nao waionya CCM

CHADEMA nayo imeionya CCM kuacha kupandikiza mbegu za udini kwa kuwatumia waumini wa dini ya Kiislamu katika kampeni za jimbo la Igunga.

Onyo hilo lilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Zanzibar), Saidi Issa Mohamed, akisema CCM imeanza kuwatumia baadhi ya viongozi wa Kiislamu kueleza kuwa chama hicho kimemdhalilisha mkuu wa wialaya ya Igunga kwa kumvua Hijab, hivyo wananchi wakikatae.

Alisema viongozi wa dini, kwa bahati mbaya bila kutafakari, wamejikuta wakiwa sehemu ya timu ya kampeni za CCM ambacho hivi sasa kina hali mbaya katika kampeni hizo.

“Naliomba Baraza la Maulamaa kuwa makini na wanasiasa,” alisema na kuwaomba wavute subira juu ya jambo hilo kwa kuwa liko mahakamani.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Mkoa wa Tabora, Kansa Mohamed, alisema serikali ya CCM imekuwa ikizitumia taasisi za dini na viongozi wake kufanikisha ushindi wake kwenye chaguzi mbalimbali.

Alisema mwaka 2000, CCM ilieneza propaganda kuwa CUF ni chama cha kidini lakini hakuna hata kiongozi mmoja wa Kiislamu aliyesimama na kupinga kauli hiyo.

Alisema mwaka 2010 CCM ilikuja na propaganda kuwa CHADEMA ni chama cha kidini na Waislamu wakahimizwa kumchagua Kikwete ambaye leo hii amebainika kuwa aliwahadaa juu ya Mahakama ya Kadhi na shule zilizotaifishwa.

“CCM inataka kuwagawa Waislamu na Wakristo ili iendelee kutawala; Watanzania wawe makini na jambo hili,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima, 23.09.2011

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s