Nitaupaisha uchumi wa Zanzibar

Na Mauwa Mohammed, Zanzibar

MGOMBEA wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad, amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataifanya ipanuke kiuchumi na kuwa kama mji wa Hong Kong uliopo nchini China.

Alibainisha kuwa ataviunganisha visiwa vya Unguja na Pemba kiuchumi kwa kuanzisha usafiri wa boti ziendazo kasi ili wananchi waweze kufanya shughuli za kibiashara kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

Ahadi hiyo aliitoa jana alipokuwa akihutubia mkutano wa ufunguzi wa kampeni wa chama chake zilizofanyika katika uwanja wa Tibirindi, Chake Chake, kisiwani Pemba, ambao ulihudhuriwa na idadi kubwa ya wananchama na wapenzi wa chama hicho.

Maalim Seif alisema atajenga Bandari ya Mkokoto na Mkoani Pemba ili kuweka usafiri wa haraka wa boti ziendazo kasi, ambazo zitatoa huduma za haraka za usafiri, hasa kwa wafanyabiashara ambao watakuwa na uwezo wa kwenda Unguja na kurudi kisiwani Pemba.

Aliongeza kuwa sababu ya wananchi wa Pemba kuhama hama itakuwa imepatiwa tiba, kwani watapata fursa za kufanya shughuli zao za kibiashara Unguja na kurejea makwao kutokana na kuwapo kwa usafiri wa uhakika.

Alibainisha kuwa serikali atakayoiongoza itashughulikia ujengaji wa bandari za Wete, Mkoani Pemba na kuimarisha Bandari ya Malindi Unguja na kuweka bandari kuu itakayojengwa Mkumbuu, Chake chake Pemba.

Maalim Seif, alisema serikali yake inachangamoto kubwa ya kujenga uchumi imara utakaowanufaisha wananchi wote, hivyo ana matumaini Zanzibar itakuwa na bandari huru itakayowafanya wafanyabiashara kwenda kufanya biashara zao kwa ufanisi mkubwa.

Aliongeza kuwa serikali atakayoiunda itakuwa ni ya utumishi wa umma ambapo wabunge na mawaziri watakuwa watumishi wa umma watakaotumikia kwa mujibu wa sheria.

Alisema waziri yeyote akivunja sheria vyombo vya sheria vitambana bila kujali wadhifa wake, kwa sababu serikali yake itazingatia usawa mbele ya sheria na ubaguzi wowote hautakuwa na nafasi.

Maalim Seif alisema ataheshimu na kuulinda Muungano kwa misingi ya kuheshimiana, ataunda serikali tatu kila nchi itakuwa na seikali yake na kuzungumzia na kuondosha kero za Muungano na kuzipatia ufumbuzi.

Wakati Maalim Seif akiunguruma katika visiwa vya Pemba, mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohammed Shein, jana alizindua kampeni za chama hicho kisiwani Unguja huku akiwataka wananchi wa Zanzibar wasimchague mtu kwa majaribio, bali waendelee kukipa ridhaa Chama Cha Mapinduzi kiongoze kwa kuwa uongozi haujaribiwi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni huko katika viwanja vya Kibandamaiti mjini Zanzibar, alisema kwamba CCM ndiyo chama chenye uwezo na uzoefu wa kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na kulinda amani na utulivu, hivyo wananchi waendelee kuwachagua wagombea wake.

Alisema akichaguliwa kushika wadhifa wa urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, atadumisha Muungano wa Tanzania katika utaratibu uliopo wa serikali mbili, kwa vile ndivyo ilani ya CCM inavyoelekeza.

Alisema ana uzoefu mkubwa katika kutatua kero za Muungano alioupata kutokana na wadhifa wake wa Makamu wa Rais pamoja na kuongoza kamati ya kushughulikia kero hizo.

Alibainisha kuwa ataendelea kulinda azima ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwa vile ndiyo yaliyoleta hadhi na heshima kwa wananchi wa Zanzibar na hakuna sehemu yoyote iliyobaguliwa na itkayobaguliwa katika maendeleo.

Alisema kwamba mapinduzi hayo ndilo chimbuko la muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ulikuja kwa ridhaa ya wananchi wenyewe, hivyo CCM ina jukumu la kuulinda muungano huo ambao pia umeipa heshima kubwa Tanzania katika uso wa dunia.

“Zipo nchi Afrika, kule Afrika Magharibi na kwingineko zimejaribu kuungana, lakini zimeshindwa, muungano wetu ni wa kupigiwa mfano na umetupa heshima kubwa, hivyo lazima tutaulinda.
Alisema katika uongozi wake akiwa Ikulu Zanzibar, vijana wategemee mambo poa, kwa vile ilani ya CCM imeelezea mipango madhubuti ya kuleta ajira kwa wananchi pamoja na kuwaendeleza.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, ambaye alihudhuria uzinduzi huo, aliwataka wanachama wa CCM waendelee kumuomba Mungu, Zanzibar CCM iendelee kuongoza na si upinzani.

Viongozi wengine wa CCM waliohudhuria mkutano huo ni mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha.

Katika mkutano huo, Dk. Bilal alisema Zanzibar katika kipindi cha miaka 46 tokea mapinduzi, imeweza kupiga hatua kubwa na hivyo, wananchi wa Zanzibar wasifanye makosa na wampe kura Dk. Shein ili kuendeleza mafanikio hayo.

SOURCE: TANZANIA DAIMA

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s