Nikiingia Ikulu hata mwanangu atafungwa – Maalim Seif

Na Mwinyi Sadallah

19th September 2010

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema iwapo ataingia Ikulu ya Zanzibar mwezi ujao hakuna mtu atakayekuwa juu ya sheria na iwapo mwanawe au Waziri wake akibainika ametenda kosa atakwenda jela.
Aidha, Maalim amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi ujao ataunda taasisi ya kupambana na rushwa na amewaonya watendaji serikalini wanaotoa zabuni kwa upendeleo au kujinufaisha mwisho wao Novemba 5 atakapoapishwa.
Mgombea huyo alisema hayo jana katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika viwanja vya Tibirizi, kisiwani Pemba.
Alisema katika serikali ya umoja wa kitaifa atakayoiongoza akichaguliwa viongozi, wananchi wote pamoja na yeye mwenyewe watakuwa chini ya sheria.
“Hata mwanangu Suleiman Seif atafungwa kama atabainika mbele ya sheria kuwa amefanya kosa, na hata awe Waziri akivunja sheria atafungwa,” alisema Maalim Seif.
Alisema ahadi hiyo itatekelezeka kwa vile wakati wa uongozi wake vyombo vyote vya sheria, zikiwemo mahakama zitafanya shughuli zake kwa uhuru mkubwa na hakutakuwa na nafasi ya kusema huyo ni mtoto wa Rais. Kuhusu rushwa mgombea huyo alisema vitendo hivyo vipo kwa wingi Zanzibar na vimeenea katika zabuni za serikali na ununuzi wa mali, kutokana na zabuni kutofanywa kwa uwazi.
Aliwaeleza wafuasi na wanachama wa CUF kuwa atahakikisha shughuli zote serikalini zinafanywa kwa uwazi kwa mujibu wa misingi ya utawala bora.
Aidha, alisema iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu Zanzibar atapinga aina zote za ubaguzi, ikiwemo vitendo vya baadhi ya wananchi wenye sifa kunyimwa vitambulisho vya Uzanzibari ukaazi, vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa (Masheha).
Alisema ubaguzi wa aina yoyote utakuwa haramu na Wazanzibari wote watakuwa sawa na serikali ya umoja wa kitaifa itagusa matabaka na itakuwa na uwakilishi wa vyama vyote vya siasa vyenye wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Alieleza kwamba atahakikisha wananchi wote watapata hati za kusafiria bila ya usumbufu wowote kinyume na hali inayojitokeza hivi sasa, ambapo wale wanaotafuta hati hizo wamekuwa wakikumbana na usumbufu mkubwa.
Aliendelea kuwaahidi wananchi wote wa Zanzibar watarajie mabadiliko makubwa ya upatikanaji wa huduma za jamii, ikiwemo usafiri wa uhakika kati ya visiwa vya Unguja na Pemba utakaowawezesha wananchi kufanya shughuli za kibiashara kwa urahisi kati ya visiwa hivyo.
Aliwaahidi wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa atawapandishia mshahara na kuwalipa sh 150,000 kwa mwezi kwa wafanyakazi wa kima cha chini, na wale wa kima cha juu wataongezewa kwa uwiano huo.
Mapema mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho, na kiongozi wa upinzani bungeni anayemaliza muda wake, Hamad Rashid Mohammed amewataka wananchi wa Pemba kutomuangusha Maalim Seif kwa vile alipitia misukosuko mikubwa akiwa na CUF kwa nia ya kuwaletea maisha bora Wazanzibari.
Kiongozi huyo alisema miongoni mwa misukosuko aliyoipitia Maalim Seif pamoja na CUF ni chama hicho kusingiziwa kinahusika na ugaidi, ambapo Marekani na Canada baadaye zilithibitisha kwamba madai hayo yalikuwa uongo mtupu.
Alisema Maalim Seif ndiye kiongozi anayeweza kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo Zanzibar kwa vile muda wake wote ameutumia kutetea haki za Zanzibar na hata alipotimuliwa CCM aliwahidi wananchi katika uwanja huo huo wa Tibirinzi kwamba atakuwa pamoja nao akiwa ndani au nje ya serikali.
Naye, Makamo Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali aliwataka wanachama na wafuasi wa CUF kisiwani Pemba wasibabaishwe na vyama vyengine vinavyojipenyeza na kuwahadaa wananchi.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s