Tupe nafasi tuibadilishe Tanzania

Kuwepo kwa maendeleo au kukosekana kwake kuna uhusiano wa moja kwa moja na hali ya uchumi wa nchi. Kutokana na uhusiano huu ni dhahiri kuwa anayehitaji maendeleo hana budi kuwapa wataalamu wa uchumi nafasi kubwa kabisa katika kubuni, kupanga, kurekebisha, na kuratibu sera za kiuchumi. Pili, amani na utulivu haviwezi kushamiri katika mazingira ambayo haki ni adimu na hazifanyiki juhudi za makusudi kubadili hali hiyo. Hatuhitaji mtaalamu wa kutueleza kuwa umasikini umekithiri, mfumo wa huduma za jamii umesambaratika, na ajira badala ya kukua inazidi kupungua.

PROF. LIPUMBA: "RAIS KIKWETE AMEZUNGUKWA NA WAHAFIDHINA WANAOMSHAURI VIBAYA KUHUSU ZANZIBAR"

PROF. LIPUMBA: “RAIS KIKWETE AMEZUNGUKWA NA WAHAFIDHINA WANAOMSHAURI VIBAYA KUHUSU ZANZIBAR”

Naanza kwa salamu za chama, ‘Haki sawa kwa wote’.

Kwa mara nyingine tena ifikapo Oktoba 2005 wananchi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tutapiga Kura kuchagua Rais, Wabunge, na Madiwani wa nchi yetu. Huu utakuwa ni Uchaguzi Mkuu wa tatu chini ya mfumo wa vyama vingi ambapo kila Mtanzania mwenye sifa ya Kupiga Kura, na aliyejiandikisha atakuwa na wajibu wa kumchagua yule anayedhani anamfaa.

Chaguzi kuu mbili zilizotangulia, yaani ule wa kwanza uliofanyika Oktoba 1995 na wa pili uliofanyika Oktoba 2000 zimetupa uzoefu wa kutosha juu ya nini cha kutarajia kutoka kwa viongozi, makada, wanachama, washabiki, na mawakala wa CCM waliopandikizwa katika vyombo mbalimbali vya umma. Kwa kifupi chaguzi hizi zimetufunza kutarajia wizi wa Kura, Rushwa, Vitisho, Ghilba na Ulaghai wa kila aina kutoka kwa CCM na mapandikizi wake ndani ya vyombo vya dola.

Kwa mara nyingine tena ifikapo Oktoba 2005 Watanzania tutakuwa na fursa ya kuamua juu ya mustakabali wa nchi yetu. Tunaweza tukaamua kulegea na kuachia wizi, rushwa, vitisho na udanganyifu vitawale na hivyo kuwa washirika katika kuendeleza maovu yanayoididimiza nchi yetu. Lakini pia tunaweza kusimama kidete kuhakikisha tunakuwa ngangari kuzuia vitendo vyote vya wizi wa Kura ili watakaochaguliwa wawe kweli ndio chaguo halisi la Wananchi.

Tukumbuke kuwa tusipokuwa imara Taifa letu litaendelea kupata viongozi ambao malengo yao si kuleta maendeleo katika nchi na kustawisha haki na usawa, bali kuwagawa watu na kuleta upendeleo wa makundi bila kujali ni kiasi gani sera za aina hiyo zinaididimiza nchi. Ni muhimu tukumbuke kuwa Viongozi wa aina hii ndio ambao tumekuwa nao tangu uhuru – wanahubiri umoja lakini matendo yao ni ya kuwagawa watu kati ya wanaostahili na wasiostahili; wanasema Wananchi wabane zaidi mikanda yao, lakini ya kwao wanazidi kuilegeza kwa rushwa na wizi wa fedha za Wananchi; wanahubiri uwazi na ukweli lakini wanauza mali na ardhi ya Watanzania kwa mikataba iliyojaa utapeli mtupu, n.k.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kujiuliza kwa makini kabisa ni kitu gani hasa tunachokihitaji. Kuendelea kubaki na jamii iliyojaa migongano, shutuma, kulaumiana na kutambiana na huku tunaogelea katika dimbwi lililokithiri umasikini, maradhi, ujinga, dhulma, na rushwa ya hali ya juu; au kujenga jamii mpya itakayozingatia haki, usawa, na maendeleo bila kujali tofauti zetu za kivyama, kikabila au kidini?

Wananchi, kikubwa kabisa tunachokihitaji ni maendeleo na amani ya kutosha ili tuweze kunufaika na matunda ya hayo maendeleo. Lakini ni muhimu tuelewe kuwa maendeleo ya nchi hayaji kwa kubahatisha na utulivu katika jamii hauji kwa hotuba za kisiasa, vitisho, wala matumizi ya nguvu. Hivi ni vitu ambavyo vinapatikana kwa kuwepo kwa nia njema na mipango madhubuti ya kuvijenga.

Kuwepo kwa maendeleo au kukosekana kwake kuna uhusiano wa moja kwa moja na hali ya uchumi wa nchi. Kutokana na uhusiano huu ni dhahiri kuwa anayehitaji maendeleo hana budi kuwapa wataalamu wa uchumi nafasi kubwa kabisa katika kubuni, kupanga, kurekebisha, na kuratibu sera za kiuchumi. Pili, amani na utulivu haviwezi kushamiri katika mazingira ambayo haki ni adimu na hazifanyiki juhudi za makusudi kubadili hali hiyo. Hatuhitaji mtaalamu wa kutueleza kuwa umasikini umekithiri, mfumo wa huduma za jamii umesambaratika, na ajira badala ya kukua inazidi kupungua.

Aidha sisi sote ni mashahidi wa jinsi vijana wetu wanavyobandikwa ‘lebo’ za uzururaji na kuhukumiwa kwenda jela wakati ni Taifa lenyewe limeshindwa kuwapatia cha kufanya. Ni nani asiyejua kuwa leo hii katika jamii yetu kufaulu usahili (interview) au kupandishwa cheo kunahusishwa na itikadi za kisiasa, dini, kabila, nasaba, jinsia, au tabaka la kiuchumi analotoka mtu?

Aidha ni nani asiyefahamu kuwa siku hizi Mahakamani sheria hutafsiriwa kwa kuangalia ni nani amesimamishwa kizimbani? Ni nani ambaye mpaka leo hajaelewa kuwa askari wanatumika kugawa vipigo kwa kishawishi cha itikadi za kisiasa, imani za kidini, na hali za watu kiuchumi? Mafanikio ya kiuchumi sasa yanapimwa kwa ahadi za kusamehewa madeni na siyo uboreshaji wa miundo mbinu, ongezeko la uzalishaji, ongezeko katika pato la Mwananchi na kukua kwa huduma za jamii.

Kigezo cha mtu kupata haki kwenye jamii yetu siyo tena Uwananchi wake bali ni uwezo wake wa kiuchumi, nasaba yake, itikadi yake ya kisiasa, imani yake ya kidini, n.k. Kwa kweli mazingira ya aina hii ni sawa na bomu linalosubiri muda kulipuka na kuleta maangamizi makubwa.

CCM imetufikisha pabaya sana. Hivi sasa nchi yetu iko njia panda; na inahitaji mabadiliko makubwa. Ni wajibu wetu sote kutafakari kwa makini kabisa kabla ya kuamua kuiachia hali hii iendelee. Hata kama sisi wenyewe tumekata tamaa, bado tuna wajibu mkubwa wa kuwaonea huruma watoto wetu. Watoto wetu wanaweza wakaishi maisha bora tofauti na tunayoishi sisi wazazi wao, kaka zao, na dada zao.

Hata hivyo tunawajibika kwanza kuwa majasiri na tushiriki kikamilifu katika harakati za kuwang’oa wale ambao kwa zaidi ya miaka arobaini sasa kazi yao kubwa imekuwa ni kutawala kwa visingizio, vitisho na ahadi za uongo. Miaka arobaini ni muda wa kutosha kabisa kujua kwa uhakika kuwa hawa wameshindwa kukidhi matarajio yetu.
Waheshimiwa Wananchi, Uchaguzi Mkuu Oktoba 2005, itakuwa ni nafasi nyingine adhimu kufanya mabadiliko ya msingi. Ushauri wetu ni kwamba ni muhimu kulenga kuiweka kwenye madaraka serikali mpya itakayohakikisha yafuatayo:

• Kuleta umoja wa kweli miongoni mwa Watanzania kwa kuhakikisha kuwa HAKI SAWA KWA WOTE si suala la kuombwa bali ni wajibu wa serikali.
• Kutengeneza utaratibu wa kudumu utakaohakikisha kuwa haki za binadamu zinazingatiwa na kuheshimiwa. Sheria za nchi zinakuwa wazi na zinazoeleweka, na kuasisi Mahakama zilizo huru zenye watumishi waadilifu na vitendea kazi vya kutosha; na ambazo ndio zitakuwa na mamlaka ya mwisho katika kutafsiri sheria hizo.
• Kutengeneza utaratibu utakaohakikisha kwamba Taifa linajenga uchumi imara, unaoongeza ajira na utakaotuhakikishia neema kwa wote.
• Elimu ya msingi na ya sekondari inakuwa ni haki ya kila mtoto wa Tanazania.
• Huduma za msingi za afya ni haki ya kila Mtanzania

Waheshimiwa Wananchi, tukumbuke kuwa SIASA SI BURUDANI ila ni suala la kufa na kupona. Katika shughuli za burudani kama vile michezo, muziki, nakadhalika, ushabiki unaruhusiwa. Timu unayoishabikia hata ikifungwa mabao 100 mathalan, athari kubwa kabisa unayoweza kuipata ni kuumwa na roho tu. Timu yako ikiwa imeshinda au imeshindwa hakutakupunguzia au kukuongezea ugali, mavazi, malazi au uwezo wa kuwapeleka wanao shule. Tofauti na inavyokuwa katika masuala ya burudani, katika siasa unapofanyika uzembe wakapatikana viongozi wabovu madhara yake yanafika hadi mvunguni.

CUF – Chama Cha Wananchi kina nia ya kuunda serikali itakayosimamia uundwaji wa mfumo utakaofanya kazi kwa kuzingatia mambo haya manne yaliyoorodheshwa hapo juu. Tutafanikisha hili kupitia misingi mikuu ya sera zetu ambayo ni HAKI SAWA KWA WOTE na UTAJIRISHO.

Haki Sawa kwa Wote
Tafsiri ya sera hii ni kwamba ili jamii isonge mbele na kustawi, inawajibika kujenga mazingira ambayo yatauhakikishia Umma kwamba haki siyo mali ya mtu fulani, tabaka fulani, au kikundi fulani- mazingira ambayo siyo tu kuwa ni lazima kuwepo na taasisi madhubuti za kusimamia haki, lakini pia jamii iridhike kuwa ni kweli haki inatendeka.

Utajirisho
Tafsiri ya itikadi hii ni kwamba jamii inayojali ustaarabu, uadilifu, haki na maendeleo inawajibika kujenga mazingira yatakayoacha wazi milango ya neema na ustawi kwa watu wote. Itikadi hii inawapa nafasi na kuwahimiza Wananchi wote watumie uwezo wao waliopewa na Mwenyezi Mungu kujijengea maisha bora, kwa upeo wa uwezo wao. Kwa mujibu wa itikadi hii, sio uadilifu kabisa kwa serikali kuwazuia wale ambao wana nia ya kweli ya maendeleo yao, – kwa kufanya kazi kwa bidii, kubana matumizi na kuwa wabunifu, – wasisonge mbele kwa sababu tu katika jamii yetu kuna wengine ni magoigoi, wazembe, wafujaji na wengine wote ambao hawaoni thamani ya maendeleo.

Hali kadhalika kwa mujibu wa itikadi hii, ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu amejengewa mazingira mazuri ya kumsaidia kusonga mbele katika juhudi za kujiletea maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia magoigoi, wazembe, na wengine wote ambao hawaoni thamani ya maendeleo kubadili mienendo yao.

Manifesto hii ya CUF itakuonyesha ni jinsi gani hatua kwa hatua mabadiliko ya msingi yanaweza yakapatikana. Lakini hatua hizi hazitakuwa na maana bila ya wewe Mtanzania kutambua fika kuwa hapa tulipofikia tunalazimika kuacha ushabiki wa kisiasa na kuwa na dhamira ya pamoja ya kuleta mabadiliko.

CUF imejibebesha dhima ya kuongoza kuleta mabadiliko yanayohitajika; kutoka kwako tunahitaji idhini na mamlaka ya kuyatekeleza yale yaliyomo katika manifesto hii. Idhini na mamlaka hayo ni kura yako ya siri, bila kusahau kuwa jasiri katika kuilinda kura hiyo mpaka imehesabiwa na kuorodheshwa.

HAKI SAWA KWA WOTE

Profesa Ibrahim Haruna Lipumba

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano

CUF – Chama Cha Wananchi

Bonyeza hapa kusoma Ajenda ya CUF kwa Maendeleo 2005

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s