Sababu 10+ za Prof. Lipumba kugombea tena Urais

Hotuba ya Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi), Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, kuelezea sababu za kugombea tena urais

Waheshimiwa wananchi

Kwa mara nyengine nachukua fomu ya Urais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi). Nimeamua kuchukua fomu ya kuwa Mgombea Urais baada ya Chama changu kuniteua kwa kuamini kua nina nia, sababu na uwezo wa kutoa ushawishi kwa Watanzania kunichagua kuwa Rais wa Serikali itakayopambana na saratani ya ufisadi na rushuwa, kusimamia upatikanaji wa haki sawa kwa wananchi wote, kukuza uchumi utakaoongeza ajira na kuwa na manufaa kwa wananchi wote, kuharakisha maendeleo yetu na kuondoa umasikini. Kama mnavyojua mzigo mzigo hupewa Mnyamwezi.

Waheshimiwa wananchi

Tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wakati nchi yetu iko njia panda. Watanzania wamechoshwa na hadaa na ngulai za CCM. Umasikini unaongezeka, ajira zimetoweka, ufisadi na rushwa vimekithiri. Ahadi ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania” imeishia kuwa maisha bomu kwa kila Mtanzania. Serikali ya CCM imeshindwa kuwaonyesha ni vipi maisha ya Mtanzania yameboreshWa na badala yake sasa inajikurupusha kwa kuwalisha watanzania takwim zisizo na kichwa wala miguu. Wanachosahau nikwamba watanzania hawali takwim. Hali halisi wanaiona wao wenyewe na wala hawategemei kuambiwa na CUF. Hivi CCM wanadhani Mtanzania anahitaji kuambiwa kuwa mwaka 2005 kilo ya sukari iliuzwa shilingi 500/- lakini hivi sasa inauzwa shilingi 1800/- na vijijni ni zaidi ya shilingi 2000/-: mchele wa kyela ulikuwa unauzwa shilingi 450/- lakini hivi sasa ni shilingi 1700/-kilo ya sembe shilingi 250/- lakini hivi sasa ni shilingi 900/-. Wafanya kazi wanapodai kuongezwa mishahara kwa sababu ya kupanda kwa gaharama za maisha wana sababu za msingi. Badala ya Rais kukutana na wafanyakazi na kuwasikiliza anawatishia kuwatoa ngeu na kutumia risasi za moto.

Rais Kikwete amefanikiwa kuigawa CCM mapema. Usanii na ukwepaji wa kuchukua maamuzi magumu, na kuchukulia mambo mazito ya nchi kimzaha unatishia kuisambaratisha nchi. Watanzania tutajua ikiwa tutaruhusu wizi wa kura kumpa fursa nyingine kuwa kiongozi wa nchi. Ameshindwa kuweka dira na kusimamia utawala bora katika kipindi chake cha kwanza. Alichofanikiwa ni kuweka rekodi za safari za nje na kuifanya Tanzania kuwa omba omba na Matonya wa kimataifa. Chonde chonde watanzania ikiwa Mheshimiwa Kikwete atapewa kipindi cha pili na kwa kua hatakuwa na Uchaguzi mwingine unaomkabili, safari za nje zitaongezeka mara dufu na atakuwa CCM kweli kweli na chukua chako mapema.

Waheshimiwa wananchi, Watanzania wameweka matumaini yao katika Chama cha CUF na misingi yake ya sera ya kuleta ”Haki sawa kwa wote” na kujenga uchumi imara unaowaongezea ajira na utakaoleta neema na tija kwa wote”.

Tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu 2010 baada ya kufikia Maridhiano ya wazanzibari yaliongozwa na Rais Amani Abeid Karube kwa upande wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad kwa upande wa CUF. Wazanzibari kupitia kura yao ya maoni ya tarehe 31 Julai 2010 wameafiki kuundwa kwa Serikali ya umoja wa kitaifa mara baada ya uchaguzi wa oktoba 2010. ni matumaini yangu kuwa Maridhiano ya wazanzibari yatazaa matunda mazuri na kuufanya uchaguzi Mkuu 2010 usiwe wa mizengwe kama zilivyokuwa chaguzi za 1995, 2000 na 2005.

Rais Amani Karume amepata fursa ya kihistoria ya kuwa muasisi wa siasa za kidemokrasia na kistaarabu kwa kuhakikisha kuwa uchaguzi wa 2010 unakuwa huru na wa haki na wa kuwaunganisha wazanzibari badala ya kuwagawa. Hii ni fursa adimu na adhibu asiipotezwe. Akitumia vizuri fursa hii, kama ambavyo amefanya hadi sasa, historia ya Zanzibar, Tanzania na Afrika kwa ujumla itamkumbuka kama shujaa wa demokrasia.

DIRA YA MABADILIKO (VISION FOR CHANGE)

Kama mjuavyo Chama chetu kimekuwa ni Chama kikuu cha upinzani nchini kwa muda mrefu sasa na wananchi wanaendelea kuteseka kwa kuona matatizo yao yakizidi kuongezeka bila ya hatua zozote za msingi kuchukuliwa. Hali hii inawafanya wananchi wengi hasa vijana na wanawake kuwa katika shauku kubwa ya kuona utawala wa nchi yetu unabadilishwa kwa amani kupitia karatasi za kura. CUF kwa kutambua nafasi yake katika kuyaongoza mabadiliko yanayoohitajika kikiwa siyo tu Chama kikuu cha upinzani hapa nchini bali pia kutokana na mjengeko wake wa kuwa kweli ni Chama cha kitaifa chenye kukubalika na chenye mtandao mpana katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano, ilizindua mwaka jana DIRA YA MABADILIKO kupitia Operesheni Zinduka.

Dira ya Mabadiliko tunayowapelekea watanzania, ambayo ndiyo itakuwa msingi wa ilani ya Uchaguzi wa CUF kwa mwaka huu wa 2010, na ambayo tutawaomba waiunge mkono kupitia uchaguzi Mkuu huu inatilia mkazo mambo 22 ambayo tuaamini chini ya Serikali ya CUF yatatujengea Tanzania Mpya inayojili haki sawa kwa wananchi wote na itakayojenga uchumi imara unaoongeza ajira na utakaoleta neema na tija kwa wote. Mambao hayo 22 ni haya yafuatayo:-

1. Kila raia popote alipo awe na haki ya kuchagua na kuchagukiwa kuwa kiongozi toka ngazi kitongoji/kijiji mtaa mpaka uongozi wa taifa

2. Kujenga umoja wa kitaifa wa kweli ambapo hakutakuwa na ubaguzi wa aina yeyote wa jinsia, kabila, rangi, dini au ulemavu. Kuhakikisha kuwa serikali inaheshimu dini zote na inajenga mazingira ya waumini wa dini mbali mbali kuheshimu na kuvumiliana

3. Kuhakikisha kuwa kila mwananchi ana uwezo au anawezeshwa kupata milo mitatau kwa siku. Hatua za makusudi zichukuliwe kuhakikisha kuwa kinamama wajawazito na watoto wachanga wanapanga lishe bora kwani mtoto mchanga asiye na lishe bora ananyimwa haki na kujenga mwili, kinga ya mwili na ubongo wake ili aweze kushiriki kikamilifu katika kujielimisha na kujiendeleza na kufikia uwezo wake aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

4. Kuhakikisha kuwa kila raia ana haki na anapata huduma za msingi za afya. Hatua maalum zichukuliwe kuhakikisha kua huduma za uzazi anapatiwa kila mama mjamzito ili kupunguza vifo vingi vya kusikitisha vya kina mama wajawazito

5. Wazee wengi badala ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu wanaishi katika umasikini wa kutisha. Watoto wao hawana kipato cha kutosha na maadili ya kuwalea wazee yameporomoka. Kama taifa ni muhimu turejeshe na kujenga maadili ya kuwaheshimu na kuwaenzi wazee wetu. Tuweke utaratib wa kitaifa wa hfidhi ya wazee itakayohusisha jamii kuwalea wazee wetu

6. Watanzania milioni 4.2 sawa na asilimia 10 ya watanzania wote ni watu wenye ulemavu. Watu wenye ulemavu wana mahitaji sawa na watu wengine, akini pia wanakuwa na mahitaji wengine zaidi kulingana na aina ya ulemavu walio nao. Kipimo cha utu wa taifa ni namna kinavyowajali walemavu wake. Serikali itayoongozwa na CUF itatenga fungu maalum la kuwasaidia walemavu wapate elimu, matibabu na vifaa vya kuwapunguzia dhiki ya ulemavu wao na mafunzo stahiki waweze kuajirika na kuajiriwa katika fani mbali mbali

7. Elimu ndio ufunguzi wa maisha. Ili kujenga taifa linalojiamini, watoto wote wa Tanzania wawe na haki ya kupata elimu bora ya msingi, ya sekondari na elimu ya juu. Taifa lijenge utamaduni wa kuamini kuwa elimu haina mwisho na kila raia ajiendeleze kielimu hasa kwa kutumia vizuri teknolojia ya habari na mawasiliano

8. Elimu ya wasichana ni nyenzo muhimu ya kuleta haki sawa kwa wananchi wote na kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa na kufsa sawa katika kuleta na kuneemeka na maendeleo. Wasichana wengi hawamalizi masomo yao kwa sababu ya uwezo mdogo wa fedha wa wazazi, mila zilizopitwa na wakati zinazowabagua wasichana na wanawake, mazingira mabovu ya shule kama vile kutokuwa na vyoo vya wanawake mashuleni na mambo mengine kama hayo. Motisha maalum itolewe kwa wasichana na familia zao ili wasichana wamalize elimu ya shule ya msingi na waendelee na elimu ya sekondari na ya vyuo vikuu na hivyo kuwawezesha kufika uwakilishi wa kujiamini wa 50 kwa 50 wanawake wenye vyombo vya juu vya maamuzi

9. Kuwaelimisha wasichana na wanawake kushiriki katika soko la ajira ni nyenzo muhimu ya kuvunja mduara wa umasikini unaorithisha umaskini toka kizazi kilichopo na kinachofuata

10. Ili kufanikisha mabadiliko ya kiuchumi, kuongeza tija na ajira, Tifa litoe kipaumbele maalum katika kuendeleza elimu ya hisabati, sayansi na teknolojia

11. Kujenga uchumi wa kisasa wenye ushindani kimataifa na utakaohimili misukosuko ya utandawazi, unaokua kwa kasi bila kuharibu mazingira na wenye manufaa kwa wananchi wote kuweka misingi ya utawala bora na utekelezaji wa sera utakaohakikisha kuwa uchumi unakua kwa asilimia 8 – 10 kwa miongo mitatu (miaka 30) ijayo

12. Wananchi wahisi na waone kuwa uchumi wa taifa unatoa fursa sawa kwa wananchi wote. Tofauti za vipato vya wananchi wisiwe vikubwa mno huku tukizingatia kutoa motisha kwa raia kuwa wabunifu na wajasirimali hodari. Mikakati ya kufaidi matunda ya kukua kwa uchumi

13. Bila kukuza uchumi umasikini uliokithiri utakuwa tatizo la kudumu katika suala la kukuza uchumi hakuna miujiza. Uchumi unakua kwa kuongeza elimu, ujuzi na utaalamu wa wafanyakazi, ongezeko la rasilimali na vitendea kazi, na kuongezeka kwa ufanikishaji na tija katika uzalishaji na huduma. Kukua kwa uchumi kunahitaji uongozi imara za utawala bora, mikakati na mipango mizuri ya maendeleo na utekelezaji mzuri wa mikakati na mipango hiyo. Kazi ya kukuza uchumi itakuwa rahisi ikiwa tutatumia rasilimali na maliasili ya nchi hii kwa manufaa ya wote

14. Nchi ambazo zimefanikiwa kukuza uchumi kwa kasi ya juu na kuwa na maendeleo kwa muda mrefu zimefanya hivyo kwa kuwa na uongozi adilifu, wenye dira na ulio imara katika kufanya maamuzi, utekelezaji na kujifunza toka kwenye makosa waliofanya na kujirekebisha. Uongozi wa nchi unawajibika kubuni sera kwa kuzingatia uhalisia na hali ya uchumi wa nchi, fursa zilizopo na vikwazo vinavyoikabili nchi katika kukuza uchumi wake. Baada ya kubuni sera, uongozi unawajibika kuzieleza sera hizo kwa wananchi na kuwahamasisha waziunge mkono na waelewe kuwa ili kujinasua toka dimbwi la umasikini wanawajibika kuchapa kazi kwa bidii, kuweka akiba kuwa wajasirimali wabunifu na kukubali kasi ya mabadiliko itawapo fursa watanzania kupata uongozi adilifu, wenye dira, na ulio imara katika uamuzi na utekelezaji

15. Tunapaswa kukipa kilimo nafasi ya pekee katika mikakati ya kukuza uchumi na hivyo kuwaondolea umasikini wananchi wa vijijini ambao wameumizwa vibaya na sera mbovu za CCM zisizotoa kipaumbele kwa kilimo. Katika miaka mitano ijayo, bajeti ya sekta ya kilimo itamuwa asilimia 10 – 15 ya bajeti yote na italenga katika kuimasisha utafiti na elimu kwa wakulima na huduma za ugani, upatikanaji wa mbolea na pembejeo nyingi kwa bei nafuu, bei nzuri kwa wakulima, msoko ya uhakika, kutengeneza barabara za vijiji, kusambaza umeme vijijini kwa kutumia nishari mbadala kama vile biogas inayotokana na mabaki ya mimea na vinyesi vya mifugo, jua na upepo

16. Ukuaji wa uzalishaji wa mazao ya chakula ndio unaoweza kupunguza kasi ya kuongeza kwa bei za vyakula. Kilimo kitaendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato ya fedha za kigeni. Tanzania ina ushindani wa biashara katika soko la dunia siyo tu kwa mazao kama vile kahawa, chai, korosho, katani, tumbaku na karafuu lakini pia katika mazao ya vyakula yakiwemo mahindi, mpunga, alizeti, ufuta, jamii ya kunde, mboga mboga na matunda na mibono inayoweza kutumiwa kutengenezea dizeli mbadala na inalinda mazingira. Sekta ya kilimo ni kiungo muhimu cha kukuza sekta nyingine. Mapato ya wakulima yanatumiwa kununua bidhaa za viwanda na huduma nyengine. Wakulima wenye kipato kikubwa watanunua nguo, vyakula vilivyosindikwa kama vile mafuta ya kupikia, mabati, saruji, samani, magodoro na bidhaa nyingine. Ongezeko la mahitaji ya bidhaa hizi vitaongeza ajira viwandani.

17. kuna changamoto mpya ambazo zinaongeza vikwazo lakini pia kutoa fursa za kukuza uchumi. Ongezeko la joto duniani limeanza kuongeza ukame, litaongeza maji baharini kutoka thekuji inayoyeyuka katika bara la Afrika na Arctic na kuleta mafuriko katika fukwe za pwani, kuongezeka mafuriko, na milipuko ya maradhi. Nchi masikini ambazo zimechangia kidogo sana katika ongezeko la joto duniani ndizo zitakazo athirika zaidi. Mkakati wa kukuza uchumi uzingatie changamoto ya ongezeko la joto duniani. Ulinzi wa mazingira, upandaji wa mashamba ya miti na utumiaji wa nishati mbadala viwe vyanzo vya wananchi kujipatia kipato

18. Hakuna nchi iliyofankiwa kukuza uchumi kwa kiasi ya juu kwa muda mrefu bila serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu, barabara, nishati, reli, bandari na mawasiliano. elimu na afya. Uwezekano wa serikali katika sekta ya miundombinu, elimu na afya unajenga msingi imara unaovutia sekta binafsi kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na biashara. Uwekezaji wa sekta ya umma katika maeneo hayo unatengeneza njia ya kuwezesha viwanda na makampuni mapya kuanzishwa na kuongeza faida ya shughuli zote za kibiashara zinazofaidika kwa kuwepo wafanyakazi wenye afya njema na walioelimika, kuwepo kwa barabara nzuri zinazopitika wakati wote, na kuwepo kwa umeme wa uhakika. Tutawekeza katika miundombinu kwa kutumia vizuri fedha za umma na kukusanya alau asilimia 20 ya pato la taifa kama mapato ya ndani ya serikali

19. Mapinduzi ya kilimo yatayoongeza uzalishaji na tija ni muhimu katika kuanzisha ukuaji wa uchumi endelevu. Lakini kilimo peke yake hakiwezi kukuza pato la taifa kwa muda mrefu. Kuongezeka kwa tija katika kilimo kutaruhusu nguvu kazi kubwa iweze kuajiriwa katika sekta nyengine hususan viwanda. Sekta ya madini kwa ujumla haitoi ajira kwa wingi. Kwa nchi ndogo kuendelea, hakuna njia nyenginwe bali kujijengea uwezo wa kuzalisha bidha za viwanda na kuziuza nchi za nje. Hakuna nchi iliyoendelea na kukuza uchumi wake kwa muda mrefu bila kuwa na maendeleo ya viwanda. Mabadiliko ya mfumo wa uchumi ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi. Nguvu kazi ya nchi inahama toka sekta zenye tija ndogo na kwenda kwenye sekta zenye tija kubwa. Viwanda kwa kawaida vina tija ya juu. Nchi ambazo uchumi wake haukui kwa kasi kubwa zimeshindwa kuhamisha rasilimali ya nguvu kazi kwa wingi zinatioa ajira. Kuongezeka kwa mahitaji ya wafanya kazi viwanda husaidia kuongezeka mishahara. Viwanda vingi vinavyohitaji wafanyakazi wengi hupata fursa wanawake kuajiriwa na hivyo kuchangia katika kuleta usawa wa kijinsia

20. Nchi ambazo hazina maendeleo ya viwanda na zinataka kuanzisha viwanda na kuuza nje bidhaa za viwanda zinakabiliwa na ushindani, siyo tu wa nchi zilizoendelea za Ulaya, Marekani na Japan, kalini ushindani mkubwa ni kutoka nchi nyingine za Asia na hasa China. Bidhaa kutoka china zinashindana na makampuni yanayotengeneza bidhaa za viwandani na kuuza soko la ndani. Je Tanzania tunaweza kumudu ushindani wa china katika kuzalisha bidhaa za viwanda?. Gharama za uzalishaji viwandani china zinapanda kwa sababu uchumi wa china unakua kwa kasi ya juu mno. Tayari china inakabiliwa na migogoro ya wafanyakazi wanaodai kuongezwa mishahara. Serikali ya china inashindikizwa na Jumuia ya kimataifa kuongeza thamani ya sarafu yake na kutegemea zaidi soko la ndani katika kukuza uchumi wake. Ikiwa tutajipanga vuziri tunaweza kupenya katika soko la dunia la bidhaa za viwandani

21. Jambo moja linalokwaza sana maendeleo ya viwandani ni ukosefu wa miundombinu ikiwa ni pamoja na umeme wa uhakika, maji, mawasiliano, barabara, reli, bandari n.k Matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na matumizi yanayofadhiliwa na misaada ya nje yalenge katika kuimarisha na kuboresha miundombinu. Ni muhimu pia kuimarisha utaratibu wa usafirishaji wa bidhaa na matumizi ya TEKNOHAMA kupunguza gharama za kufanya biashara. Tunahitaji pia kuanzisha maeneo maalumu ya viwanda ya kutengenezea biadhaa za kuuza nje na kuyasheheni maeneo haya na huduma za umeme, maji, mawasiliano, barabara n.k. katika hilo, tunapaswa kuchagua eneo maalumu kuzingatia hali halisi ya kuwafanya wawekezaji wa sekta binafsi wavutiwe na maeneo hayo

22. Fedha nyingi za umma zinaibiwa au kutumiwa vibaya. Tathmini na uhakika wa kina wa fedha za msaada wa dola milioni 60 uliotolewa na serikali ya Norway katika wizara ya maliasli na utalii katika lipindi cha miaka 12 uliofanyika mwaka 2006 unaonyesha kuwa nusu ya fedha hizo, yaani dola milioni 30, ziliibiwa au kutumiwa kifisadi. Tatizo la matumizi mabaya ya fedha haliko wizara ya maliasili na utalii tu bali limetapakaa serikalini kote. Tukidhibiti matumizi mabaya ya feha tunaweza kuokoa fedha zitakazotumiwa katika ujenzi wa miundombinu. Rais Kikwete alipokuwa anafungua Mkutano wa TAKUKURU alieleza asilimia 30 ya matumizi yote ya serikali kila mwaka yanaibiwa au kutumiwa kifisadi. Hii ni sawa na shilingi trilioni 11.8 kwa bajeti ya serikali ya mwaka 2006/7- 2010/11, fedha inayotosha kukamilisha mradi ya kufua umeme MW 2000 na kujenga bara bara za lami km 4000 na kuongeza kima cha chini cha mshahara wa watumishi wa serikali

Serikali ya Umoja wa Kitaifa:

Ili kupambana na matatizo makubwa ya ufisadi na rushwa, umasikini na ujenzii wa demokrasia nitaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa. Demokrasia ya kweli na ushindani wa kisiasa unaotoa haki sawa kwa washiriki wote, uhuru wa kusema na uhuru wa vyombo vya habari, ni msingi wa utawala bora. Demokrasia ni lengo la maendeleo ya kisiasa lakini pia ni nyenzo ya kujenga uchumi kwani inasaidia sana kuzuia kuenea kwa saratani ya rushwa. Demokrasia ya kweli inawafanya viongozi wawajibike kwa wananchi. Ili kujenga misingi imara ya demokrasi ya kudumu tunahitani katiba nzuri inayowapa uhuru wa kweli watanzania wa kuchagua na kuchaguliwa. Muungano wetu utaimarika ikiwa watanganyika na wazanzibari watahisi sana haki sawa katika Muungano huo. Katiba ya sasa haikidhi maendeleo ya demokrasia nchini mwetu. Serikali ya umoja wa kitaifa itaandaa utaratibu wa kupata katiba ya wananchi yenye misingi imara ya demokrasia.

Nikichaguliwa kuwa Rais nitajiwekea lengo la kuijengea heshima nchi yangu kwa kuimarisha utawala bora na adilifu na kukuza uchumi unaoongeza ajira kwa wingi na kuleta neema kwa wananchi wote. Kazi hii nitaifanya kwa uadilifu wa hali ya juu na kuhakikisha kuwa kwa mara ya kwanza Rais wa Tanzania atakapostaafu aweze kupata tunzo ya Mo Ibrahim ya Kuongoza nchi vizuri kwa kuheshimu na kulinda haki za binaadamu, kupambana na ufisadi kwa mafanikio, kukuza uchumi na kuutokomeza umasikini.

ZINDUKA MTANZANIA, CHAGUA CUF,
LA SIVYO MAFISADI WATATUMALIZA

HAKI SAWA KWA WOTE

PROF. IBRAHIM HARUNA LIPUMBA
Agosti 5, 2010

Advertisements

2 thoughts on “Sababu 10+ za Prof. Lipumba kugombea tena Urais

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s