Tutaijenga Zanzibar Mpya – Maalim Seif

Kwa hakika, nataka kutumia fursa hii kutoa wito hasa kwa wananchi wote wa Zanzibar, walio CUF, CCM, wa vyama vyengine na wasio wafuasi wa chama chochote, wote kwa ujumla wao wajitokeze kwa wingi siku ya tarehe 31 Julai, na wapige kura ya NDIO ili kwa pamoja tuijenge Zanzibar Mpya; Zanzibar shirikishi na siyo Zanzibar tenganishi; Zanzibar itakayokuwa na neema kwa wote. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu, mmenichagua niinue juu bendera ya CUF kwa madhumuni ya kuwaomba Wazanzibari ridhaa yao ili niiongoze Zanzibar Mpya tuliyoazimia kuijenga. Naamini tutafanikiwa.

Maalim Seif akihutubia mkutano mjini Zanzibar

Maalim Seif akihutubia mkutano mjini Zanzibar

HOTUBA YA SHUKRANI YA MGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR KWA TIKETI YA CUF, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU MAALUM WA TAIFA WA CHAMA CHA WANANCHI (CUF) LANDMARK HOTEL, DAR ES SALAAM – 27 JUNI, 2010

Mheshimiwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Mheshimiwa Makamo Mwenyekiti, Waheshimiwa Manaibu Katibu Mkuu, Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, Waheshimiwa Wageni wetu waalikwa, Mabibi na Mabwana, Kwa mara nyengine tena, namshukuru kwa namna ya pekee Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia afya njema na uzima hadi tukaweza kukamilisha kazi kubwa iliyotuleta hapa ya kuwachagua Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama chetu.

Nawashukuru nyinyi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa pia kwa imani yenu kubwa mliyonipa ya kunichagua kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama chetu. Imani yenu kwangu naithamini sana. Naithamini sana kwa sababu ni dalili ya mapenzi makubwa kwangu ambayo naamini yametokana na jinsi nilivyoweza kufanya kazi nanyi kwa kipindi chote ambacho tumekuwa pamoja katika hali ya uaminifu na kujituma wakati natekeleza majukumu mliyonipa. Siipati kauli nyengine ya kueleza shukrani zangu zaidi ya kuwaambia Ahsanteni sana.

Natumia fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Prof. Ibrahim Lipumba kwa kuchaguliwa kwake kwa kura nyingi na nyinyi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha CUF.

Nimemjua Prof. Lipumba kwa miaka mingi sasa na pia nimefanya kazi naye kwa ukaribu katika kipindi cha takriban miaka 15 sasa, kwanza akiwa Mgombea wetu mwaka 1995 na baadaye kama Mwenyekiti wangu kuanzia 1999 hadi sasa. Sina shaka wala wasiwasi kwamba Prof. Lipumba ni ndiye mtu anayefaa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inahitaji kiongozi atakayejenga uchumi imara utakaotoa ajira na neema kwa wote kwa kuwainua Watanzania masikini na kuwongezea kipato chao mwaka hadi mwaka badala ya kujenga uchumi legelege unaowanufaisha wachache na kuendelea kuwafukarisha walio wengi.

Hongera sana Prof. Lipumba na naamini utaipeperusha vyema bendera ya CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambao naamini utaleta mabadiliko makubwa kwa Chama chetu. Nampongeza pia Mheshimiwa Juma Duni Haji kwa kuteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa kuwa Mgombea Mwenza wa Prof. Lipumba. Naamini kutokana na uzoefu na umahiri wake wa kazi, atashirikiana vyema na Mgombe Urais kuwadhihirishia Watanzania kuwa CUF ina timu imara ya kuleta mabadiliko yanayohitajiwa sana na Watanzania.

Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu, nimesema kwamba naithamini sana imani mliyoionyesha kwangu. Mmenipa imani kama hii huko nyuma lakini mara hii mmefanya hivyo katika mazingira tofauti ya kisiasa. Maridhiano ya Wazanzibari yaliyoanzishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, na mimi tarehe 5 Novemba, 2009 yamebadilisha kabisa sura na mahusiano ya kisiasa baina ya wananchi wa Zanzibar na hasa baina ya wafuasi wa vyama vyetu viwili, CUF na CCM.

Kuna uwezekano wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka huu kufanyika katika mazingira ya uhuru, haki na uwazi. Rais Karume amekuwa akisisitiza mara kadhaa kwamba hilo ndilo lengo lake na la Serikali yake kuona uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na wa haki ambao utawafanya washindani wote waridhike na kusiwepo na malalamiko ukiondoa yale ya kibinadamu. Ni imani yangu kwamba Rais Karume ataisimamia kauli yake hiyo kwa vitendo. Hivyo basi, naamini katika mazingira hayo na tukishirikiana wanachama wote wa CUF kufanya kampeni kabambe, za kisasa na za kistaarabu hapana sababu kwa nini tusishinde uchaguzi huu na kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Lakini uchaguzi wa mwaka huu pia utakuwa ni tofauti kwa sababu matokeo yake yatapelekea Zanzibar kuanzisha muundo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Najua kuwa hili litategemea maamuzi ya wananchi kupitia kura ya maoni itakayofanyika Zanzibar tarehe 31 Julai, 2010, lakini mimi naamini kabisa Wazanzibari wamechoshwa na hali ya magomvi, uhasama na chuki iliyodumu kwa takriban miaka 50 sasa, na hivyo basi naamini kwa umoja wao na kwa asilimia kubwa sana watapiga kura ya NDIO kuridhia muundo huo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa hakika, nataka kutumia fursa hii kutoa wito hasa kwa wananchi wote wa Zanzibar, walio CUF, CCM, wa vyama vyengine na wasio wafuasi wa chama chochote, wote kwa ujumla wao wajitokeze kwa wingi siku ya tarehe 31 Julai, na wapige kura ya NDIO ili kwa pamoja tuijenge Zanzibar Mpya; Zanzibar shirikishi na siyo Zanzibar tenganishi; Zanzibar itakayokuwa na neema kwa wote. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu, mmenichagua niinue juu bendera ya CUF kwa madhumuni ya kuwaomba Wazanzibari ridhaa yao ili niiongoze Zanzibar Mpya tuliyoazimia kuijenga. Naamini tutafanikiwa.

Lakini nilitaka basi niyataje japo kwa ufupi tu mambo kumi (10) ambayo yatakuwa ndiyo msingi wa maongozi yangu katika kipindi cha miaka mitano ijayo, na ambayo yatakuwa ndiyo pia msingi wa Ilani ya Uchaguzi ya CUF kwa upande wa Zanzibar. Mambo hayo kumi (10) ni haya yafuatayo:

1. Kuyaendeleza Maridhiano ya Kisiasa tuliyoyaasisi mimi na Rais Amani Karume yakiwa ndiyo njia sahihi ya kujenga umoja wa kweli miongoni mwa Wazanzibari na kuendeleza amani na utulivu uliopo kwa kufuata misingi ya ukweli na mapatano.

2. Kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa mujibu wa makubaliano ya CUF na CCM yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo ya Bagamoyo na ambayo yaliridhiwa na vyama vyetu viwili kupitia vikao vya juu vya maamuzi vya vyama vyetu.

3. Kuuimarisha Muungano wetu kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuendeleza mazungumzo yenye nia ya kweli ya kuyapatia ufumbuzi wa dhati matatizo yanayoukabili chini ya misingi ya haki, usawa na kuheshimiana baina ya pande mbili zinazounda Muungano huu.

4. Kujenga uchumi imara kwa kuzingatia mfumo wa soko huria unaotoa fursa ya ushiriki kwa wananchi wote na ambao unaratibiwa vyema na Serikali ili kuhakikisha kuwa wananchi wetu wote wanafaidika na fursa hizo na kunyanyua hali zao za maisha katika hali ya neema na tija kwa wote. Sekta za Kilimo, Utalii, Biashara, Viwanda na Uvuvi zitapewa kipaumbele katika ujenzi wa uchumi wa kisasa kwa Zanzibar Mpya.

5. Kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi Serikalini na ubora wa huduma zinazotolewa na utumishi wa umma kwa kusimamia ipsavayo kanuni za kazi, kuwapatia mafunzo ya kazi kadiri inavyowezekana na kuwaongezea mishahara wafanyakazi wetu ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuwa mfano kwa umma.

6. Kwa kufuata mfumo wa uchumi wa soko huria, kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake ya kituo kikuu cha biashara na huduma katika eneo lote la Afrika Mashariki kwa kutekeleza sera zitakazoweka mazingira mazuri na yanayovutia ya kufanyia biashara na kuleta uwekezaji mkubwa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha bandari zetu na viwanja vya ndege vitakavyoweza kutuunganisha na nchi za nje na nchi jirani.

7. Kukiendeleza kilimo na kukirejeshea hadhi yake kama moja ya njia kuu za uchumi inayotegemewa na wananchi wetu walio wengi hasa wa vijijini. Mkazo utawekwa katika kilimo cha viungo na mboga mboga ili tuendelee kutumia vyema soko linaloweza kupatikana kutokana na jina maarufu la Zanzibar kama visiwa vya viungo.

8. Kuweka msukumo maalum katika kuinua viwango vya elimu katika skuli zetu za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ili Zanzibar iwe ndiyo kituo kikuu cha elimu na mafunzo stadi katika eneo lote la Afrika Mashariki. Mkazo utawekwa katika kusomesha walimu kwa viwango vya kimataifa, kuwapatia maslahi bora ili kuirejeshea hadhi fani na kazi ya ualimu, kuboresha mazingira ya skuli zetu na taasisi za elimu ya juu kwa kuzipatia huduma zote muhimu zinazohitajika kwa ukuzaji wa elimu, kujenga na kuimarisha maabara za kisasa, na kupunguza ukubwa wa madarasa na idadi ya wanafunzi ili walimu waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuipitia upya mitaala yetu ili iendane na mahitaji ya Zanzibar ya leo kulingana na sera za uchumi tutakazozifuata.

9. Kuinua na kuimarisha huduma za afya katika hospitali, zahanati na vituo vya afya kwa kuweka vifaa vya kisasa vya matibabu, kuvipatia madawa yote muhimu, kusomesha na kuajiri madaktari na wauguzi wapya, kuboresha maslahi ya madaktari na wauguzi, kuwawekea mazingira bora ya kufanyia kazi na kuhakikisha usafi katika sehemu hizo.

10. Kurejesha maadili mema ya Wazanzibari kwa kuhuisha mila, silka na utamaduni wetu na kuwarejeshea Wazanzibari hadhi na fahari yao iliyotokana na mila, silka na utamaduni huo. Katika kurejesha maadili hayo, Serikali nitakayoiongoza itapambana vikali na uingizaji na utumiaji wa madawa ya kulevya ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi visiwani Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa sheria zinatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo ili kudhibiti uingizaji na pia kuanzisha na kuviendeleza vituo vya kuwasaidia waathirika wa madawa hayo ya kulevya ili waache utumiaji huo.

Ndugu zangu, wajumbe wa Mkutano Mkuu, haya niliyoyaeleza hapa siyo mambo pekee yatakayotekelezwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa nitakayoiongoza. Haya ni mambo nitakayoyapa umuhimu wa kipekee lakini yatajenga msingi wa kuyaendeleza mambo mengine katika sekta na nyanja zote za maisha. Haya na mengine yataelezwa na kufafanuliwa kwa upana zaidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu tutakayoizindua wakati wa kampeni ukifika. Kwa ufupi, tunakusudia kujenga Zanzibar mpya ili ifikie kule ambapo Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alitaka kila Mzanzibari afikie na kujinasibu nako ikiwa ndiyo malengo ya Uhuru waliokuwa wakiupigania wazee wetu hao. Katika Ilani ya Uchaguzi ya ASP ya mwaka 1961, Mzee Karume aliieleza vyema Zanzibar hiyo kwa maneno yafuatayo: “UHURU ndio msingi wa siasa ya chama chetu. Unachanganya bila ya shaka kumalizika kwa Serikali ya Kikoloni na mwisho wa utawala wa nje.

Kadhalika UHURU unakusanya ukunjufu kutokana na ujinga na haja zisizokwisha. UHURU wa kuwa na pato la kumwezesha mtu kuyatekeleza yaliyombidi, kustarehe na kuwa mtu, uhuru wa kuishi kama watu katika nchi yetu. Huu ndio UHURU ambao daima tukiutaka, huu ndio UHURU ambao daima twaupigania, huu ndio UHURU ambao tumejitolea kuutumikia na siku zote tutautumikia kwa nguvu zetu zote na kwa uwezo wetu wote.

Tunadhani kuwa kila mmoja wetu katika visiwa hivi aendelee mbele kwa mujibu wa uwezo wake, jambo ambalo ni gumu lakini kabisa si jambo lisilowezekana. Na iwapo wewe Kilillahi huyapingi haya tuliyoazimia na wewe mwenyewe ndiye uwezaye kujua, basi tafadhali karibu uungane nasi twende pamoja na kuutia mkononi huu UHURU.” Wazee wetu waliupigania na kuutia mkono UHURU huu.

Sasa ni wajibu wetu sisi kuendeleza pale walipotuachia ili tuyafikie kweli malengo ya UHURU huo walioupigania kama alivyoyaeleza Marehemu Mzee Karume. Naamini tukiyasimamia na kuyatekeleza vyema mambo haya kumi (10) niliyoyataja hapa, basi tutaweza kuyafikia malengo hayo.

Ahsanteni sana.

Dar es Salaam

27 Juni, 2010

Advertisements

9 thoughts on “Tutaijenga Zanzibar Mpya – Maalim Seif

 1. Maalim Seif,mimi napata shaka na chama chako,binafsi sio kama nachukia CUF au labda napendelea CCM,napata hofu juu ya uwezo wa chama chako kuweza kuleta umoja wa kitaifa Zanzibar has nikiangalia idadi kubwa ya wanachama pamoja uongozi wa chama chako ni ule ambao unatoka upande mmoja wa Zanzibar,hofu ninayopata ni kubwa sana kiasi cha kwamba bado sijashawishika kwenda kukipigia kura chama chako,pamoja na kura tuliopiga ya NDIO na mimi Allah alinishuhudia nilipiga NDIO ili tupate amani kule kwetu Zanzibar lakini bado nashindwa kushawishika utaijenga vipi zanzibar ikiwa chama chako kinaonekana wazi na dhahir kina nguvu sana upande mmoja na hata huo upande wa pili basi idadi kubwa ya wafuasi ni kutoka upande huohuo nliousema kwanza,naomba uniondoe hofu hii tafadhali ili nihue kura yangu naitumia vipi!!!

 2. Assalaam Alaykum…nakutakieni kila la kheri ktk mbio zenu za kutaka kuikomboa zanzibar…InahaAllah Mola atakusaidieni.
  Ila ningekuombeni mufanye na Zanzibar iwe na mtawala wake wa elimu ya juu, hiyo ni njia moja ya kuikomboa Zanzibar kielimukwa kizazi cha sasa na kijacho.
  Nakutakieni kazi njema.

 3. wewe muunguja unotaka maalim akutoe hofu au kumuuliza vipi ataikomboa zanzibar jiulize suala moja tu halafu ujijibu hicho chama chako sicho hicho kilichoizamisha zanzibar mpaka leo ikafikia ikombolewe? jee haitoshi ccm kuwa haina maana tena tuwape wengine wajaribu?? acha chuki za kiccm

 4. Hivi hii website / glob ndo imekufa????? Mbona hakuna updates?????
  Mmeridhika na nini???? Hakuna cha kuandika????
  Tutasoma wapi habari za CUF????
  NAOMBA MAJIBU
  Kambi

  • Ni kutokana na fitna za wale wachache, wanaojaribu kukisaliti na kukitilia fitna, lakini bado tuko imara na tunasonga mbele kwa uwezo wake Allah.

 5. Maalim tunaomba utweke wazi kuhusiana na mwenendo mzima wa mchakato wa marekebisho ya katiba, sababu kutokana na kauli za viongozi wa ccm znz, tayari nimeshavunjika moyo ,na kupoteza mwelekeo mzima wa kupata mamlaka kamili znz yametoweka, je utfanya nini juu ya hili?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s