‘Serikali ya Muungano haiheshimu Mkataba wa Muungano’

“Kamati ya Makamu wa Rais haina uhalali wa kisheria. Katiba yetu haisemi popote kwamba chombo hiki kipo na kwamba kina nguvu gani. Ni chombo cha ushauri tu ambacho ufanyaji kazi na mafanikio yake yanategemea zaidi dhamira njema. Na, kama tulivyosema kwenye hotuba yetu ya mwaka juzi, dhamira hiyo njema haionekani kuwepo, hasa hasa kwa upande wa Serikali ya Muungano. Hii ndiyo sababu, katika hotuba yake ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka huu, Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Uchumi wa SMZ alisema wazi kwamba SMT bado haijawa tayari kuzungumzia masuala ya gawio la SMZ kwenye EACB, faida ya Zanzibar kwenye mtaji ulioanzisha Benki Kuu ya Tanzania, haki ya Zanzibar kupata zaidi ya asilimia 4.5% ya gawio la misaada ya nje, na mengine mengi yenye manufaa ya moja kwa moja ya kiuchumi kwa Zanzibar, na Serikali ya Muungano. Tunachokisisitiza hapa ni kwamba msingi wa Muungano unapaswa kuwa ni haki sawa kwa wote.”

Mhe. Riziki Omar Juma

Mhe. Riziki Omar Juma

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI, MHE. RIZIKI OMAR JUMA (MB), KUHUSU MAKADIRIO NA MATUMIZI YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MAMBO YA MUUNGANO) KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011

1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kwa idhini yako napenda kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Masuala ya Muungano) kwa mwaka wa fedha 2010/2011, kama inavyoelekezwa na Kanuni za Bunge toleo la Mwaka 2007, kanuni ya 99 (7).

Mheshimiwa Spika,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutujaalia sote kuwa hapa kwenye kikao cha mwisho cha bajeti katika awamu hii. Aidha,natoa shukrani za dhati kwako wewe binafsi kwa kunipa fursa hii ya kutoa mtazamo wa Kambi hii. Pia naushukuru uongozi mzima wa chama changu, Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na viongozi na wanachama wa wilaya ya Wete kwa kunipa mashirikiano makubwa katika kufanikisha kazi zangu. Mwenyezi Mungu awazidishie imani na upendo juu yangu. Amin. Aidha nawashukuru viongozi wangu wa Kambi chini ya Mhe. Hamad Rashid Mohammed na Mhe. Dk. Wilbrod Slaa kwa imani na ushirikiano wao kwangu, bila kuwasahau waheshimiwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani kwa ushirikiano wa hali ya katika kutimiza majukumu yangu na ya Kambi.

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu napenda nitumie nafasi hii kumshukuru mume wangu na watoto wangu kwa kunivumilia katika kipindi chote cha miaka mitano kwa kuwa mbali nao wakati nikitekeleza majukumu yangu.

2. MAJUMUISHO YA MIAKA MITANO
Mheshimiwa Spika,
Wakati tunamaliza Bunge hili, ni muhimu kujitathmini ikiwa miaka yetu mitano ya kuwamo humu ilikuwa na maana yoyote kwenye mustakabali wa Muungano wetu, hasa panapohusika jukumu letu sisi kama Kambi ya Upinzani. Kwa heshima, naomba nilikumbushe Taifa kupitia chombo chako hiki kitukufu kwamba jambo la msingi ambalo tulilipigania na kulisimamia ni kuwa na Muungano wenye ridhaa ya pande zote husika na wenye uadilifu. Tulipigania Tanzania Moja yenye Tanganyika Imara na Zanzibar Madhubuti. Kwetu, tuliamini na tunaendelea kuamini kuwa Tanzania ya aina hiyo inawezekana, ingawa kwa masikitiko tunakiri kwamba wenzetu walioshikilia madaraka hawajapata kuamini kuwa na Tanzania ya aina hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Sisi wa Kambi ya Upinzani, tulijaribu kutumia nafasi yetu na uwezo wetu kupigania umoja wa kweli na sio utengano, imani sio unafiki, na juu ya yote tulitaka kuona uwazi unatawala Muungano huu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa miaka yote hii mitano, Serikali hii imekuwa ikifikiri na ikitenda mambo yake bila ya kutilia maanani pande nyengine husika za Muungano huu. Katika hili, tathmini yetu inahitimisha kwamba miaka hii mitano imekuwa awamu nyengine ya kuudhoofisha Muungano wetu, kwani kwa mara nyengine suala la msingi halikuzingatiwa. Ni Mkataba wa Muungano, ambayo ni hati ya kimataifa iliyosainiwa na wawakilishi wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano, na ambao hauwezi kubadilishwa kwa namna yoyote ile bila ya pande hizo kuamua hivyo katika misingi ya usawa na uadilifu.

Mheshimiwa Spika,
Tunataka raia wa Jamhuri hii ya Muungano watambue kwamba katika miaka hii mitano, sisi wa Kambi ya Upinzani tulipigania kuona kwamba Mkataba huu unaheshimiwa kikamilifu. Tulithibitisha kwa hoja na mifano ya wazi kwamba Serikali katika vipindi mbalimbali vya historia ya Muungano huu, imeukiuka, imeuvunja na kuudharau kabisa Mkataba huu.

Mheshimiwa Spika,
Kwani ukiwauliza Serikali watakupa mifano ya kero ambazo zimetatuliwa katika kipindi hiki, watakuambia kwamba mwezi uliopita paliwekwa saini baina ya Serikali mbili kwamba masuala ya Uvuvi wa Bahari Kuu na Tume ya Haki za Binaadamu yametatuliwa na kuondoshwa katika Orodha ya Kero hizo.

Mheshimiwa Spika,
Ukweli ni kuwa hata mifano hii yenyewe inaonesha namna ambavyo moyo wenyewe wa Muungano unavyovunjwa. Kwa sababu: Kwanza, kutokana na mifano hii, tafsiri halisi inayopatika ya kutatua kero za Muungano ni kuyafanya mambo yasiyo ya Muungano yawe ya Muungano. Kwa maneno mengine, ni kuendelea kudhoofisha mamlaka na madaraka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pili, ikumbukwe kwa miaka yote hii minne si kwamba juu ya meza palikuwa na kero hizo mbili tu za Muungano. Zipo nyingi tu, zikiwemo:
• Mafuta na Gesi Asili
• Kuongezeka na Tafsiri ya Mambo ya Muungano
• Ajira za Wazanzibari katika Taasisi za Muungano
• Uwezo wa Zanzibar Kukopa Nje
• Gawio la Zanzibar katika Mali za Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB)
• Utozwaji Kodi mara mbili kwa Wafanyabiashara wa Zanzibar
• Utaratibu wa Zanzibar kuwa na ushirikiano wa kimataifa na nchi za nje na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kunufaika na fursa za kichumi
• Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya na hatimaye Shirikisho la Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika,
Hata kama tutakubiliana na kujiaminisha kuwa kinachofanywa na Serikali ni kutatua kero za Muungano, hivi Serikali ya CCM itwambie inahitaji miaka mingapi mengine kutatua kero zilizokwisha orodheshwa ikiwa kasi yake ya utatuzi ni wastani wa kero moja tu kwa miaka miwili mizima?

Mheshimiwa Spika,
Sababu ya tatu, ni ule ukweli tuliousema mwaka jana hapa, kwamba Kamati ya Makamu wa Rais haina uhalali wa kisheria. Katiba yetu haisemi popote kwamba chombo hiki kipo na kwamba kina nguvu gani. Ni chombo cha ushauri tu ambacho ufanyaji kazi na mafanikio yake yanategemea zaidi dhamira njema. Na, kama tulivyosema kwenye hotuba yetu ya mwaka juzi, dhamira hiyo njema haionekani kuwepo, hasa hasa kwa upande wa Serikali ya Muungano. Hii ndiyo sababu, katika hotuba yake ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka huu, Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Uchumi wa SMZ alisema wazi kwamba SMT bado haijawa tayari kuzungumzia masuala ya gawio la SMZ kwenye EACB, faida ya Zanzibar kwenye mtaji ulioanzisha Benki Kuu ya Tanzania, haki ya Zanzibar kupata zaidi ya asilimia 4.5% ya gawio la misaada ya nje, na mengine mengi yenye manufaa ya moja kwa moja ya kiuchumi kwa Zanzibar, na Serikali ya Muungano. Tunachokisisitiza hapa ni kwamba msingi wa Muungano unapaswa kuwa ni haki sawa kwa wote.

Mheshimiwa Spika,
Kwa sababu hizo tatu, Kambi ya Upinzani haiwezi kuwa sehemu ya wawakilishi wa wananchi wanaoyaongeza matatizo ya wananchi hao badala ya kuyatatua.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki cha miaka mitano, tulijaribu kuonesha khofu yetu kuu tuliyo nayo kwamba Serikali ya Muungano inajifanya kutia pamba masikioni na kuudharau kabisa historian a uhalisia wa Muungano wenyewe, kwamba ni matokeo ya madola mawili huru kukasimu baadhi ya mamlaka yao katika mamlaka ya pamoja, huku madola hayo yakibakia na sehemu nyengine za mamlaka yake. Hili la Tanganyika na Zanzibar kukasimu baadhi tu ya madaraka yao kwa Muungano tulilisema na kulirudia kwa kujiamini, maana hivyo ndivyo ilivyo unapoangalia Mkataba wa Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Tunataka pia raia wa Jamhuri hii ya Muungano watambue kwamba katika kipindi hiki tulipigania kuona kwamba hoja ya Muundo mpya wa Muungano wenye Serikali Tatu, yaani ile ya Tanganyika, ya Zanzibar na ya Muungano, inarudi Bungeni na inakuwa sehemu ya kumbukumbu za chombo hiki kitukufu. Tulilikumbushia na tulilitukuza kundi la Wabunge 55 wa Bunge hili tukufu ambao katika miaka ya ’90 waliwahi kupitisha hoja ya haja ya kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika.

Mheshimiwa Spika,
Tunataka raia wa Jamhuri hii ya Muungano wafahamu kwamba katika kipindi walichotuweka humu Bungeni tuliyaweka wazi mapungufu ya Katiba ya 1977 panapohusika Muungano. Miongoni mwa mapungufu tuliyoyaweka wazi ni lile la nafasi ya Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo tulisema wazi kwamba Mabadiliko ya 11 ya Katiba yaliyomuondoshea nafasi hiyo Rais wa Zanzibar yalikuwa batili kwa dhati yake. Tunafahamu kwamba mabadiliko yale yalifanywa kwa khofu ya Serikali ya Muungano kukiogopa kivuli chake chenyewe. Vyenginevyo, hapakuwa na hoja wala haja ya kuuvunja Mkataba wa Muungano kwa kisingizio cha kuwa eti ingeliwezekana pande hizi mbili za Muungano zikawa na marais kutoka vyama tafauti baada ya kurudi tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kwa hivyo, tulidai na bado tunadai kwamba Rais wa Zanzibar arudi katika nafasi yake ya kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kama yalivyo matakwa ya Mkataba wa Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Tunataka raia wa Jamhuri hii ya Muungano wazingatie kwamba tuliihoji nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano tukieleza namna ambavyo nafasi hiyo isivyokuwa ya Muungano kama vile tulivyohoji matumizi ya jina la ‘Tanzania Bara’ badala ya Tanganyika ndani ya Muungano, Akaunti ya Pamoja ya Fedha, Mahakama ya Katiba na nafasi na uwezo wa Jaji Mkuu na Mahakama ya Rufaa. Mote humo hoja yetu ilikuwa rahisi kufahamika na ya wazi. Mambo mengi yamevungwa vungwa ndani ya kijaluba kimoja hata sasa ni shida kusema, kipi ni cha Muungano na kipi si cha Muungano. Imekuwa haitegemei tena Makubaliano ya wenye Muungano huo kama yanavyoelezwa kwenye Mkataba, bali kinategemea watunga mikakati wa Serikali ya Muungano wamelalia na kuamkia ubavu gani. Na huko, kwa hakika, ni kwenda kinyume kabisa na ari hasa ya Muungano. Ndio maana hakuna la ajabu kwamba hakuna jirani hata mmoja wa Jamhuri hii ambaye amewahi kutamani kujiunga nasi kwa miaka yote hii 46, maana Muungano wetu unawatisha.

Mheshimiwa Spika,
Mwisho tungetaka raia wenzetu wa Jamhuri hii ya Muungano waelewe kwamba tulihoji uhalali wa kisheria na wa kisiasa wa vikao vya pamoja kati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Zanzibar vinavyoratibiwa chini ya Ofisi wa Makamo wa Rais. Hoja yetu ilijengeka juu ya dhana halisi ya Muungano wenyewe. Kwamba, kwanza, huu ni Muungano wa madola mawili huru ya Tanganyika na Zanzibar na hivyo, pili, ingawa Ofisi ya Waziri Kiongozi inaweza kuwa inawakilisha upande wa Zanzibar kama mshirika wa Muungano, Ofisi ya Waziri Mkuu haiwezi kuwa inawakilisha upande wa Tanganyika, ambaye ni mshirika mwengine wa Muungano; maana hii tunavyoambiwa ni ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni mshirika wake. Kwa ufupi ni kusema wanaokutana kuzungumza sio hasa waliopaswa kuzungumza.

Mheshimiwa Spika,
Naomba nimalizie nukta hii kwa kuwathibitishia Watanzania wenzetu kwamba sisi wa Kambi ya Upinzani tulitimiza wajibu wetu. Tulihoji pa kuhoji, tulikosoa pa kukosoa na tulielekeza pa kuelekeza. Bila ya shaka, lilipotokea la kusifu na kuunga mkono, tulifanya hivyo, lakini lazima tukiri kwamba hayo yalikuwa ni machache sana, maana katika suala la Muungano huu, Serikali imeharibu mengi kuliko kutengeneza. Sisi tulitimiza wajibu wetu kwa kadiri ya nguvu na mipaka yetu.

3. MTIKISIKO WA MUUNGANO 2005 – 2010
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba maarufu ya Rais Jakaya Kikwete hapa Bungeni ya Disemba 30, 2005, alizungumzia dhamira yake ya kuulinda, kuudumisha na kuuimarisha Muungano. Miaka miwili baada ya hotuba hiyo, Muungano ukaanza kukumbwa na dharuba ya kwanza ikitokea ndani ya Chama na Serikali yake mwenyewe. Ilikuwa ni pale Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda alipotamka humu Bungeni kwamba Zanzibar si nchi. Pili na pale, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipoamua kuzungumzia kwa uwazi suala la nishati za mafuta na gesi asilia na kutaka liondolewe kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Mambo haya mawili ndiyo migogoro mikuu ya waziwazi iliyoutikisa Muungano wetu ndani ya awamu hii. Yote mawili yalizua miito ya ukinzani kutoka pande husika na kila upande uliamini kwamba unasimamia jambo la haki na, au, la kisheria.

Mheshimiwa Spika,
Bahati nzuri ni kuwa msimamo wetu katika masuala kama haya huwa unajulikana wazi na hata unaweza kutabirika. Kwa sababu ya sera ya mfumo wa Shirikisho la Serikali Tatu tunayoisimamia, Kambi yetu imekuwa kila siku ikizitambua hadhi mbili za Zanzibar kama nchi na kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano. Tunaitambua Tanganyika katika upeo huo huo. Na kwa sababu ya sera ya kiuchumi tunayoitetea, tunaamini pia kwamba nchi yenye sifa hizo ya Zanzibar, ina jukumu la kusimamia rasilimali zake yenyewe kwa mustakbali wa watu wake na vizazi vyao. Juu ya yote, tunataka kuona kuwa mjadala mpana, wa kiadilifu, na wa wazi na wenye dhamira ya kujenga unaendelezwa kuhusu masuala haya, kusudi hatimaye papatikane Muafaka wa Kitaifa kuhusu Muungano mzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,
Ni maoni yetu kwamba, tutakuwa tunajidanganya wenyewe tukidhani kwamba mambo haya mawili yamepitwa na wakati. Ni makosa zaidi kuamini kuwa yalipozuka yalizuka kwa bahati mbaya na kwamba yalikuwa masuala ya jazba. Kwa kuwa yenyewe hayakuzungumzwa yakamalizwa, tukae tukijua kwamba tunamaliza miaka yetu mitano ya kuwepo kwenye nafasi tulizo nazo tukiwa tumeuwacha mgogoro mmoja mkubwa sana kuwahi kutokea kwenye Muungano huu.

4. MUUNGANO NA WAZANZIBARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa siku nyingi huko nyuma, ufahamu wa wengi ulikuwa ni kwamba muingiliano wa kisiasa baina ya Tanganyika na Zanzibar ulianza baada ya Muungano huu, Aprili 1964. Lakini kutokana na rekodi za kihistoria ambazo sasa zimekuwa zikikusanywa na kuwekwa wazi na wanahistoria, ufahamu huu unatanuka na leo inajuilikana kwamba muingiliano huo ulianza kabla ya Muungano wenyewe na kwamba ambacho kimekuwa kikitokezea ndani ya miongo hii minne na nusu ya sasa ni muendelezo tu wa kile kilichoanzishwa hapo kabla. Hivi sasa kuna maandiko kama vile kitabu cha ”Kumbukumbu za Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo”, ”The Partner-ship” cha Mzee Aboud Jumbe, ”Pan Africanism or Pragmatism” cha Profesa Issa Shivji na cha karibuni zaidi ni ”Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!” cha Dkt. Harith Ghassany. Maandiko yote haya yanataja kwa namna moja ama nyengine, namna siasa au viongozi wa siasa wa upande mmoja wa Muungano walivyowahi kuwa na athari kwenye upande mwengine.

Mhseshimiwa Spika,
Athari njema na mbaya za muingiliano huu zinaweza kuorodheshwa kwa kadiri muorodheshaji anavyodhamiria. Si lengo la hotuba yetu ya leo kuzizungumzia kwa undani athari hizo, lakini itoshe kusema kwamba kila upande kati ya pande mbili hizi za Muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar, una nafasi ya kuzisawiri au kuziathiri, kuzitengeneza au kuziharibu, siasa za upande mwengine. Kwa hivyo, linabakia kuwa jukumu la kila upande kuuangalia upande mwengine wa pili kwa jicho la urafiki, udugu, huruma na upendo. Kwamba wetu ni Muungano wa washirika na wala sio Muungano wa wapinzani. Ni Muungano wa marafiki uliotokana na ridhaa zao wenyewe na wala si Muungano wa wababe wa kivita ambapo mmoja alimshinda mwenzake na kumuweka chini ya himaya yake kwa lengo la kumdhibiti asije akanyanyuka tena.

Mheshimiwa Spika,
Sisi tunatambua kwamba kwetu ni kuungana sio kutawaliana, kwa hivyo hatuna na wala hatutakiwi tuwe na ushindani na ukinzani wa kudhibitiana na kuwekana katika wakati mgumu. Sote, Tanganyika na Zanzibar, tunapigania khatima ya pamoja, ambayo ni kuliona eneo hili la Afrika ya Mashariki likipiga hatua za kimaendeleo ya kiuchumi, ya kisiasa na ya kijamii ambayo yatakuwa kioo cha kuwavutia wengine wa Bara letu la Afrika.

5. ZANZIBAR, MUUNGANO NA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika,
Mwisho tungependa kuweka msimamo wetu juu ya nafasi ya Zanzibar iliyo kwenye Muungano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika,
Mambo matatu ndiyo yanayoleta utata: kwanza, maeneo yaliyoorodheshwa kuwa ya mahusiano kwenye Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni 17, ambapo kati ya hayo ni manne tu ndiyo mambo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa yale yaliyobaki 13, Zanzibar ina mamlaka yake kamili juu ya mambo hayo kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 102. Pili, uhusiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaingia katika kigawe (category) cha mahusiano ya kimataifa, ambalo lenyewe si jambo la Muungano. Tatu, hata itokezee kwamba Jumuiya hii inaingia katika kigawe cha Mambo ya Nje, ambalo ni jambo la Muungano, basi bado Serikali ya Muungano haina uhalali wa kuiwakilisha Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, angalau katika yale mambo ambayo si ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Khofu kubwa inayojengeka sasa kwa Zanzibar ni kwamba, mwenendo wa kulazimishana unaonekana kuchukuliwa kwenye kasi ya kuelekea Shirikisho utaishia kwenye kuzusha mfumo wa Serikali Moja kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maana ikiwa tutaendelea hivi na kukichukua kila cha Zanzibar na kukiwakilisha chini ya mwamvuli wa Muungano, mwisho wa siku hapatabakia na chochote cha Zanzibar. Jumuiya hii ya Afrika Mashariki inathibitisha hilo.

Mheshimiwa Spika,
Ripoti ya Kituo cha Katiba cha Afrika Mashariki chenye makao makuu yake mjini Kampala, Uganda iliyochapishwa mwezi wa Aprili mwaka huu inaonya kwamba nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanapaswa kujifunza makosa makubwa yanayofanyika ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiwa kweli wanataka Jumuiya hii idumu na iimarike.

Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa makosa yanayotajwa na ripoti hiyo ni ukweli kwamba hisia na mawazo ya upande mmoja wa Muungano hazipewi nafasi katika kuuendesha na kuutawala Muungano wenyewe. Tabia hii ya kuyachukulia mambo kifichoficho au kwa kuyavungavunga ni mbaya sana kwenye ushirikiano wa pande zaidi ya moja. Unapokosekana uwazi wa kutosha katika mahusiano, shaka na dhana mbaya ndio huchukua nafasi badala ya nia njema na kuaminiana.

Mheshimiwa Spika,
Kutokuipa nafasi Zanzibar kama Zanzibar ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni tatizo jengine linalosubiri kuchipuka kwenye siasa za nje na mashirikiano ya kimataifa za Tanzania. Kwa upande mmoja, Wazanzibari wanataka kuiona nafasi yao wenyewe ndani ya Jumuiya ili waweze kusimamia vyema maslahi yao kwa yale mambo yasiyo ya Muungano. Kwa upande mwengine, siasa za Muungano kuelekea Zanzibar zinazosimamiwa na Serikali ya Muungano haziruhusu kuiona Zanzibar inajenga mashirikiano yake yenyewe nje ya mipaka ya Tanzania hata kwa yale mambo yasiyo ya Muungano huku ikieleweka kwamba hata unapoangalia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ushirikiano wa kimataifa si jambo la Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Khofu ambayo inajengeka kwa mkabala huu wa Serikali ya Muungano kuelekea Zanzibar inaweza kuwaathiri washirika wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wanaweza nao kukhofia jaala za mamlaka yao kama wataingia kwenye ushirikiano wa ndani zaidi na nchi ambayo imezowea kujifanya kaka mkubwa na kuwachukulia majirani zake kama watoto wadogo ambao hawawezi kujisimamia wenyewe.

Mheshimiwa Spika,
Inaweza kufahamika kwamba kuna khofu pia kwa upande wa Serikali ya Muungano, ambao unaona hatua yoyote ile ya Zanzibar kutumia haki yake ya kuingia kwenye mashirikiano ya kimataifa kutaathiri mamlaka ya Serikali yenyewe ya Muungano; na hivyo kuhatarisha au kuuvunja kabisa Muungano wenyewe. Ndiyo hoja iliyotumiwa wakati ule Zanzibar ilipolazimishwa kujitoa kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC), hoja ambayo imeshafafanuliwa kwamba ilikuwa potofu.

Mheshimiwa Spika,
Kuwepo kwa khofu hii isiyo na msingi kwa upande wa Serikali ya Muungano kunaathiri sana mfumo wa Muungano, maana ule msingi wa ukweli na ridhaa ya hiyari wa Muungano unakosekana. Msingi huo ni mapenzi na kuaminiana. Tunapofika pahala, sisi wenyewe tukiwa kwenye Muungano hatuaminiani na badala yake tunategana mitego na kuviziana, tujuwe kwamba tumefika katika kilele cha udhaifu wa Muungano huo.

6. MARIDHIANO YA WAZANZIBARI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka uliomalizika wa 2009 ulimalizika kwa matumaini mapya na mwaka huu wa 2010 ukaanza kwa matarajio ya milango ya kheri kufunguka Zanzibar. Hii ni baada ya viongozi wakubwa wa vyama viwili vya siasa vyenye ushawishi wa siasa za nchi hii kuamua kukutana na kuanzisha mazungumzo ambayo sasa yamezaa kile kinachoitwa Maridhiano. Sisi wa Kambi tunawapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kuongozwa kwao na maslahi makubwa na mapana ya kinchi na kizalendo na kuamua kuweka nyuma hisia na maslahi binafsi.

Mheshimiwa Spika,
Kwa muktadha huu wa Muungano, tunachukua fursa hii, na kwa namna ya pekee, kumshukuru sana sana Rais Jakaya Kikwete, ambaye akiwa kama Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha uelewa wa hali ya juu na akaziunga mkono jitihada za viongozi wenzake wa Zanzibar. Tunaamini kauli zake za mara kwa mara za kutia moyo ambazo amekuwa akizitoa kuhusiana na Maridhiano ya Wazanzibari zinatoka moyoni mwake na kwamba kutokana na na kuziunga mkono kwake kwa kila hali basi nchi hii itajikwamua kutoka jinamizi la miaka zaidi ya hamsini la mgogoro wa kisiasa Zanzibar. Tunaamini Rais Kikwete anaongozwa na hekima yenye kuiona Zanzibar iliyoungana na iliyotulia kuwa ina maslahi zaidi kwa Muungano kuliko Zanzibar iliyogawika na kuchafuka.

Mheshimiwa Spika,
Niruhusu nichukuwe nafasi hii kupitia Bunge hili tukufu, kuwaomba Watanzania wenzangu popote walipo na katika chama chochote cha siasa walicho, waisaidie Zanzibar iondokane na balaa na badala yake, kwa kutumia Maridhiano haya, iinuke na istawi vyema. Nina hakika kwamba Zanzibar ya aina hiyo ndiyo inayotakiwa na kila mwenye nia njema na Muungano wetu. Nitumie fursa hii basi kutoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar waongozwe na hekima, busara na moyo wa umoja na upendo wakati watakapokuwa wanapiga kura ya maoni tarehe 31 Julai, 2010 kuhusu Maridhiano.

Mheshimiwa Spika,
Maridhiano ya Wazanzibari yametupa fundisho moja kubwa sana, kwamba penye nia na dhamira ya kweli na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele, hakuna lisilowezekana. Hakuna asiyejua miongoni mwetu kiwango cha uhasama na kutoaminiana kilichokuwepo kati ya viongozi na wanachama wa CCM na CUF. Leo tumeweza kuibadilisha hali hiyo na kila mwenye kuitakia kheri Zanzibar na Tanzania hawezi kufanya juhudi za dhahiri au za chini chini za kutaka kuturejesha kule tulikotoka. Naomba basi, tutumie mfano huu, na kwa misingi hiyo hiyo niliyoitaja hapo juu, ili sasa baada ya kuwa na Maridhiano ya Wazanzibari, tuwe pia na Maridhiano ya Muungano yatakayoupa Muungano wetu haiba na sura mpya katika hali ya umoja wa dhati na upendo wa kweli uliojengeka juu ya udugu wa asili wa watu wa pande mbili hizi za Muungano. Hili linawezekana ikiwa tutakuwa tayari kutimiza wajibu wetu.

7. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Kama nilivyotangulia kusema, hiki ni kikao cha mwisho cha Bajeti kwa kipindi hiki cha Bunge. Huenda tukarudi tena hapa mwakani, huenda tusirudi. Turudi ama tusirudi, ni muhimu sana kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wakati aliotupa wa kuwatumikia Watanzania wenzetu katika kiwango hiki cha kuwawakilisha katika chombo kinachohusika na maamuzi ya kuiendesha nchi yao.

Mheshimiwa Spika,
Naomba nimalizie kwa kukumbusha kwamba Muungano huu ni kitu kizuri ambacho kinastahiki kuendelea kuwepo na kudumishwa, lakini kuulinda na kuuimarisha Muungano hakumaanishi kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano na kupunguza mamlaka ya upande husika bali kunahitaji kuheshimiana na kuheshimu mamlaka ya kila upande.

MUNGU IBARIKI AFRIKA
MUNGU IBARIKI JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha

……………………………………..
RIZIKI OMAR JUMA (MB)
Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani
Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano.
21.06.2010

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s