CCM inaimasikinisha Tanzania

Kigezo kilichokubaliwa kimataifa kuwa matumizi ya chini kabisa kwa mtu mzima asihesabiwe kuwa ni maskini wa kutupwa ni dola moja kwa siku. Benki ya dunia inakadiria kwa kutumia kipimo hiki, umaskini Tanzania umeongezeka toka asilimia 73 ya Watanzania wote mwaka 1990 mpaka kufikia asilimia 89 mwaka 2000. Kwa kutumia kigezo hiki cha kimataifa na takwimu za uchunguzi wa bajeti za kaya wa 2007, zaidi ya Watanzania 90 katika kila Watanzania 100 ni masikini wa kutupwa. Hatuwezi kuwa na mshikamano wa kweli wa kitaifa ikiwa ukuaji wa uchumi unawanufaisha watu wachache na kuwaacha zaidi ya Watanzania milioni 36 wakiwa maskini wa kutupwa.

Hamad Rashid Mohammed, Mbunge wa CUF na Kiongozi wa Upinzani Bungeni

Hamad Rashid Mohammed, Mbunge wa CUF na Kiongozi wa Upinzani Bungeni

HOTUBA YA KIONGOZI WA UPINZANI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI, MHESHIMIWA HAMAD RASHID MOHAMED (MB) WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011

I. UTANGULIZI
1.1 Mheshimiwa Spika, Baada ya kumshukuru Mola Mtukufu kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba kuwasilisha maoni yetu kuhusu hali ya uchumi ya nchi na bajeti kwa mwaka 2010/2011 kwa mujibu wa kanuni za Bunge .
Kwa sura tunayoiona ni wazi kuwa Watanzania watapaswa kuwa macho katika kuchagua viongozi hapo Oktoba, ikiwa kweli tunahitaji maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu.

1.2. Mheshimiwa Spika, Nakushukuru wewe Mhe. Spika na wasaidizi wako pamoja na Katibu wa Bunge na watumishi wote wa ofisi ya Bunge kwa kuliongoza bunge letuhadi kuwa bunge la mfano katika Jumuiya ya Madola.. Nawashukuru sana wenzangu wote katika CUF na katika Kambi ya Upinzani hasa Mhe.Dr. Slaa kwa kusaidiana nami katika kuongoza Kambi. Aidha namshukuru Mhe. Waziri Mkullo na wasaidizi wake wote kwa ushirikiano walionipa katika kutimiza majukumu yangu..

2. TATHMINI YA MIPANGO
2.1. Mheshimiwa Spika, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ilibuniwa kwa kuzingatia maendeleo makubwa ya uchumi ya nchi za Kusini Mashariki ya Asia kama vile Malaysia na hususan ukuaji wa sekta ya viwanda, uuzaji wa bidhaa za viwanda nchi za nje na ongezeko kubwa la ajira katika sekta rasmi iliosaidia kupunguza umaskini kwa kasi kubwa.
2.2. Mheshimiwa Spika, Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ni kuhakikisha kuwa ifikapo 2025, Watanzania watakuwa na “maisha bora na mazuri, kuwa na uongozi bora na utawala wa kisheria, na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.” Tanzania itakuwa na uchumi unaotegemea sekta nyingi na ulioendelea kwa kuwa na wastani wa viwanda vingi, uchumi mpana ulio tulivu (macroeconomic stability), miundombinu imara na pato la taifa linakua kwa asilimia 8 au zaidi.

2.3. Mheshimiwa Spika, Tanzania ya 2025 itakuwa inamudu ushindani wa kikanda na kimataifa kwa kuwa na nguvukazi yenye elimu na ujuzi. Hata hivyo dira hii haijatafsiriwa na kuwekwa katika mpango mkakati wa utekelezaji. Wananchi wengi hawajui malengo ya dira ya maendeleo. Viongozi wa juu wa nchi hawaielezi na kuifanunua dira hii. Haya ni mapungufu makubwa.

2.4. Mheshimiwa Spika,Utamaduni uliokuwepo wakati wa Mwalimu wa kueleza na kuhamasisha wananchi waielewe dira na mipango ya nchi kwa mfano mpango wa kwanza wa maendeleo ya miaka mitano 1964-69 uliokuwa na kibwagizo “ It can be done, play your part” ulipigiwa debe na wananchi kuelewa madhumuni yake. Azimio la Arusha na Ujamaa ulielezwa na kusambazwa kwa wananchi.
2.5. Mheshimiwa Spika, Rais Mkapa aliandika dibaji nzuri ya Dira lakini hakusimamia kuifafanua kwa wananchi. Serikali ya awamu ya nne haina habari kabisa na suala la dira ya maendeleo. (Hii ni kasoro kubwa).

2.6. Mheshimiwa Spika, MKUKUTA ambao ni sehemu ya Dira ya Taifa, lengo lake kuu liko katika makundi “cluster” matatu ambayo ni:-
a. Kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato;
b. Kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa jamii;
c. Kuimarisha Utawala bora na uwajibikaji;
Ukadiriaji wa gharama za MKUKUTA katika baadhi ya sekta muhimu ulikamilika mwishoni wa mwaka 2006 na gharama zake zikabainika kuwa ni kubwa mno kuliko uwezo wa serikali kwa hiyo MKUKUTA umeshindwa kutekelezeka. Kwa mfano gharama za kutekeleza MKUKUTA katika sekta ya Nishati ilikadiriwakuwa wastani wad olla za kimarekani 911 kwa mwaka,sekta ya kilimo inahitaji wastani wa dola za kimarekani milioni 300 kwa mwaka,Sekta ya Afya dola milioni 476,barabara wastani wa dola 922 .

Mhe.Spika mahitaji ya sekta nne tu ni zaidi ya asilima 70 ya matumizi yote ya Serikali ya mwaka 2006/7 MKUKUTA haukutekelezwa ipasavyo kwani gharama zake hazikudiriwa mapema na ukadiriaji ulipomalizika gharama zilikuwa kubwa mno.Hata lengo la kupunguza umasikini kwa asilima 50 ifikapo 2010 halikufikiwaTathmini ya Bajeti ya Kaya kupunguza inaonesha umasikini umepungua toka asilimia 385 mwaka 1990,kufikia asilima 35.8 mwaka 2001 na asilimia33.6 mwaka 2007.Pamoja na kutokufikia lengo hili MKUKUTA 11 umeweka lengo la kupunguza umasikini kutoka 33.6 ya mwaka 2007 na kufikia asilimia 19.3 ya mwaka 2015.MKUKUTA11 haulezi mkakatiganiambayo haikutekelezwa miaka 20 iliyop[itaambayo sasa itafanikisha kupunguza umasikini kwa kasi kubwa..(Hii ni kasoro ya pili kubwa).

2.7. Mheshimiwa Spika, Kasoro ya tatu kubwa ni kuwa bajeti ya 2009/10 ilikuwa ni ya mwisho ya utekelezaji wa MKUKUTA na 2010/11 ni ya kwanza kwa kutekeleza MKUMKUTA WA Pili.(Hadi leo hakuna tathmini rasmi ya Mkukuta wa Kwanza, hivyo tunaingia Mkukuta wa Pili na kasoro zile zile za Mkukuta wa Kwanza.(Hii ni kasoro ya tatu kubwa)

3. A. KUKUZA UCHUMI NA KUPUNGUZA UMASIKINI WA KIPATO
3.1. Mheshimiwa Spika, Katika MKUKUTA wa kwanza Ukuaji wa sekta ya kilimo ulikadiriwa kutoka 5% hadi 10% mwaka 2009/10 ,Mifugo 2.7% hadi 9% mwaka 2010, uzalishaji wa chakula uwe kutoka tani 9million hadi tani12 million na tuwe na Chakula cha akiba ngalau cha miezi 4.(ESRF-Mkukuta based MDGs costing for THE agric sector, final report 2006)

3.2. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Kilimo ilitakiwa iwe na ongezeko la 23.1% kutoka Dolla za Marekani 269.3million 2005/06 ifikie 331.4Millioni mwaka 2010. Kwa ufupi ili MKUKUTA wa kwanza ufanikiwe katika sekta ya kilimo ulitakiwa uwe na wastani wa bajeti ya USD275 million kila mwaka, lakini kwa miaka mitano kuna pengo la wastani wa asilimia 42.22% . (hii ni kasoro nyingine kubwa). (ESRF-Mkukuta based MDGs costing for THE agric sector, final report 2006)

3.3. Mheshimiwa Spika, mwaka huu ambao ni wakwanza kutekeleza MKUKUTA wa Pili kilimo, pamoja na sera mpya ya KILIMO KWANZA ,kimetengewa Tshs.903.8 Billion ambazo ni asilimia 7.8% ya bajeti nzima wakati kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa SADAC ilitakiwa isipungue asilimia 10..Jee maisha bora kwa kila mtanzania yatafikiwa wakati tatizo moja kubwa la mfumuko wa bei ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeshindwa hata kulitumia soko la mchele la Kenya ambalo huagiza mchele wastani wa tani 170,000 kutoka Pakistani.

3.4. Mheshimiwa Spika, Bei ya tani moja ya mchele kwa mujibu wa (Regional Agriculture Trade Intelligence Network-RATIN) Kigali ni ni wastani wa USD952 sawa na Tshs 1,428,000/ na kwa mahindi ni USD223 sawa na Tshs.349,500/-.kama kungekuwa na umakini wa utekelezaji wa MKUKUTA wa kwanza ,na kwa kutumia vizuri soko la Afrika Mashariki leo tusingezungumzia nakisi katika bajetu zetu na hivyo uhaba wa chaukula na mfumko wa bei ingelikuwa ni hadithi. Mhe.Spika tumeshindwa hata kufikia malengo yaMKUKUTA 1 ya kuzalisha tani 12milini. (Hii ni kasoro ya nyingine kubwa).

3.5 Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Uganda huzalishaji mpunga katika “Upland rice”bila kutumia mbolea wala umwagiliaji lakini kwa kutumia mbegu bora wanazalisha wastani wa tani 2—3 .Wakati sisi katika skimu 16 za umwagiliaji maji tunazalisha wastani wa tani 1—2 kwa hekta. Jee upo ufanisi wa utekelezaji wa MKUKUTA na kwamba lengo la kupunguza umasikini wa kipato utafikiwa?(Hii ni kasoro ya sita kubwa).
3.7. Mheshimiwa Spika, RIPOTI ya Umasikini na Maendeleo ya watu iliyotolewa mwaka huu inaonyesha kuwa kwa Mwaka 2007 idadi ya watanzania waliokuwa wanakadiriwa kuwa ni masikini ni Millioni 12.9 kati ya watanzania million 38.3. Kati ya watanzania hao million 12.9 ambao ni masikini, watu milioni 10.7 sawa na asilimia 83% wanaishi vijijini.
3.8. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa tafiti hizi zilizopelekea kutolewa kwa taarifa hii zilifanywa mwaka 2007, hivyo ni ukweli uliowazi kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa idadi watanzania masikini wanaoishi mijini na vijijini imeongezeka mara dufu kutokana na hali halisi ilivyo kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, Kigezo kilichokubaliwa kimataifa kuwa matumizi ya chini kabisa kwa mtu mzima asihesabiwe kuwa ni maskini wa kutupwa ni dola moja kwa siku. Benki ya dunia inakadiria kwa kutumia kipimo hiki, umaskini Tanzania umeongezeka toka asilimia 73 ya Watanzania wote mwaka 1990 mpaka kufikia asilimia 89 mwaka 2000. Kwa kutumia kigezo hiki cha kimataifa na takwimu za uchunguzi wa bajeti za kaya wa 2007, zaidi ya Watanzania 90 katika kila Watanzania 100 ni masikini wa kutupwa. Hatuwezi kuwa na mshikamano wa kweli wa kitaifa ikiwa ukuaji wa uchumi unawanufaisha watu wachache na kuwaacha zaidi ya Watanzania milioni 36 wakiwa maskini wa kutupwa.

4.0 B. KUIMARISHA UBORA WA MAISHA NA USTAWI WA JAMII;
4.1. Mheshimiwa Spika, Ukubwa wa sekta ya uchumi isiyokuwa rasmi ni karibu mara kumi ya sekta ilio rasmi ya uchumi,taarifa ya umasikini na maendeleo ya binadmu ya mwaka 2009 inaonyesha kila mwaka ajira katika sekta isiyo rasmi ya uchumi imekuwa kwa wastani wa watu 630,000 kwa mwaka. Wakati tafiti zilizofanywa na taasisi ya “Finscope” na kugharamiwa na “Financial Sector Deepening Trust Fund (FSDT)” inaonyesha kuwa ni 9% ya wananchi ambao wanatumia huduma rasmi za kibenki, 2% ya wananchi ndio wanaopata huduma zingine za asasi ndogo za kifedha, 35% wanatumia huduma ambazo si rasmi, kwa maana kwamba wanaendesha biashara yao kiujanja ujanja tu. Aidha 34% ya wananchi hawapati kabisa huduma za kifedha.

4.2. Mheshimiwa Spika, Takwimu hizi zinatonyesha kuwa hata kama Serikali itajitahidi vipi kuongeza vyanzo vya kifedha na kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji lakini tusipofanya maboresho na kuimarisha asasi/taasisi zinazotoa huduma za kifedha kwa wananchi wa mijini na vijijini, kuondoa umasikini wa kipato litakuwa ni jambo lisilowezekana.

ASASI ZA FEDHA NA UMASIKINI WA KIPATO:
4.4 Mheshimiwa Spika, Muswada ya Sheria ya mabenki na Asasi za Fedha ya mwaka 2006 ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo kuipa Benki Kuu uwezo na uhuru zaidi wa kusimamia kikamilifu benki na asasi za fedha nchini ili kupanua huduma za sekta hii hasa kuwawezesha wananchi kupata mikopo ya masharti nafuu ili washiriki kikamilifu kujiondolea umasikini.
4.5. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inarudia tena kwa kuitaka Serikali kuziwezesha asasi ndogo za fedha kupata mikopo nafuu au kuingia nayo ubia ilikutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo kwa riba nafuu inayolipika. Kinyume na hapo bado uchumi wetu utaendelea kushikiliwa na kundi la watu wachache tu.
4.6.Mheshimiwa Spika, Waziri ametaja mifuko mingi ya mikopo ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi, Mfuko wa uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo (Small Enterpreneurs Loan Facility-SELF), Mfuko wa Udhamini wa mikopo kwa ajili ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi (ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SME’s-CGS). Tunapendekeza pafanyike tathmini huru (Independent Evaluation) ya mifuko hii kama inakidhi malengo yake na kwa kiasi gani ni endelevu, kwani bado hatujaona mafanikio yake kiasi cha kuweza kujenga kada mpya ya wafanyabiashara na wawekezaji wa kati.

4.7. Mheshimiwa Spika, Kuna Taasisi ya Serikali inayotoa mikopo kwa asasi/taasisi ndogo za fedha kwa riba ambayo ni kati ya 18% na 20% kwa mwaka. Taasisi hii inapata fedha kutoka Serikalini lakini inakopesha kwa riba kama ya mabeki ya Biashara, jee haya ndio madhumuni ya lioanzishwa taasisi hii?
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia BOT kuzilazimisha Taasisi za Fedha kuweka angalau asilimia 15% ya amana kwa kukopesha Asasi ndogo za fedha na wakulima(wafugaji na wavuvi) ili wigo wa watu wanaotumia mabeki iongezeke na uchumi uimarike.

5.0. NISHATI NA MADINI:
5.1. Mheshimiwa Spika, malengo ambayo yaliwekwa na MKUKUTA ni kwamba ifikapo mwaka 2010 idadi ya kaya/ nyumba ambazo zitakuwa zimeunganishwa kwenye grid ya Taifa ni 20% wakati malengo hayo yakiwekwa mwaka 2001 idadi ya kaya ambazo zilikuwa zimeunganishwa kwenye grid ya Taifa ni 10%

5.2.Mheshimiwa Spika, Taarifa ya umasikini na maendeleo ya watu inaonyesha kuwa Dar es salaam ambayo mwaka 2001 kaya zilizokuwa zimeunganishwa na grid ya Taifa 58.9% na kwa maeneo mengine ya mijini ilikuwa ni 29.7%. Lakini mwaka 2007, Dar Es salaam ilishuka na kuwa 50.8% na maeneo mengine ikashuka kuwa 25.9%.

5.3. Mheshimiwa Spika, Bunge lako limekwisha ipa Serikali kwa kipindi cha miaka mitano jumla matumizi ya kawaida Tshs197,207,126,900/. Matumizi ya maendeleo kwa miaka mitatu ni Tshs. 804,123,439,500/. Hii yote ni kwa ajili ya kutekeleza malengo ya Mkukuta. Lakini inaonyesha kuna mchwa wanaokula fedha hizo na hivyo kazi inashindikana, na ndio maana hadi leo tumeshindwa na kuwa na umeme wa uhakika katika taifa letu.

5.4. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza,Je pamoja na kutenga fedha hizo, hali ya upatikaji wa umeme imeimarika? Jibu tuwaachie watanzania.

5.6.Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni makampuni yanayotafuta gesi yamegundua mashapo mengine yenye hazina kubwa sana ya gesi huko Mkuranga. Jambo la kusikitisha ni kwamba hadi sasa Serikali haijakuwa na mpango madhubuti wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea katika Wilaya ya Mkuranga, badala yake inategemea ahadi aliyoitoa Mhe. Rais mwaka 2007 wakati akifungua mkutano Mkuu wa CCM – Kizota-Mkoani Dodoma kuwa kuna Kampuni kubwa duniani itakuja kujenga kiwanda cha mbolea katika mkoa wa Mtwara. Hadi sasa watanzania wanasubiri kwa hamu ujenzi wa kiwanda hicho.
5.7. Mheshimiwa Spika, Hoja hapa ni Serikali kushindwa kupanga mipango yake mapema na kukurupuka mwishoni na hapo mafisadi wanapochukua fedha za walipakodi bila huruma. Kambi ya Upinzani inasema nchi yenye wasomi wengi wanaotegemewa katika mataifa mbalimbali dunia haiwezi kuendeshwa kiholela bila ya kuwa na mipango madhubuti.
6.0. KUELEWA RASLIMALI ZA NCHI;
6.1. Mheshimiwa Spika, kutokana na kukua kwa tekinologia ulimwenguni, Kambi ya Upinzani inashauri Serikali itumie tekinologia ya “MAPING” ili kujua kwa kina raslimali zote zilizoko nchini na namna tunavyoweza kuzitumia. (teknolojia hii inapatikana hata Spain).

6.2. Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali imeshindwa kujua wingi wa madini tulionao nchini,lakini baya zaidi hata kuzigawa kwa kufuatia umuhimu wake imeshindikana.Hakuna nchi duniani Uranium inaweza kutolewa kiholela,au mkaa wa mawe,au shaba,chuma, nikle n.k. (Industrial Minerals)isipokua Tanzania. Sababu kubwa ni kwasababu hatujui thamani, wingi na pahala zilipo na kwa kiasi gani zitasaidia uchumi wetu.Huku nikukosa mipango mizuri na endelevu na kutokutumia vyema raslimali watu. Tanzania imekuwa kama shamba la viazi kila mwekezaji anakuja anachimba na kuondoka.

6.3. Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inashauri utafutwe utaalamu haraka sana kabla hatujaingia katika Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki ili Watanzania wajue raslimali zao kikamilifu ili kuepuka migongano ya kijamii baadae.
Aidha kwa Taasisi ya Uwekezaji (Tanzania Investment Centre – TIC) watakuwa wanatoa vibali kwa wawekezaji kulingana na Rasilimali zilizopo, wakijua mazingira halisi ya Uwekezaji, hii itasaidia Serikali kukusanya kodi kulingana na uzalishaji na Rasiliamali zilizopo, badala ya kutoa vibali kwa Wawekezaji bila kuzingatia maliasili zilizopo (Natural resources).

6.4. Mheshimiwa Spika, tunarudia kauli yetu ya awali kuwa ni vyema Serikali ikaipa uwezo wa kujiendesha NDC na STAMICO ili ziwe na uwezo wa kumiliki maeneo ya “industrial minerals” na kuingia ubia na makampuni ya nje bila ya kudhulumiwa.
7.0. ARDHI
7.1. Mheshimiwa Spika, ardhi ni mojawapo ya rasilimali na nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kupambana na umasikini kwani ndiyo inayotoa ajira kwa wastani wa asilimia 75 ya watanzania.

7.2. Mheshimiwa Spika, Watanzania bado hawajanufaika na rasilimali hii ambayo ina ukubwa wa kilomita za mraba 885,200 au sq km. 942,600 kwani kutokana na taarifa ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni viwanja 18,641 na mashamba 734 katika mikoa 21 ambavyo vimepimwa na wahusika kupewa Hati na viwanja 56,743 vilipimwa kupitia mradi wa kupima viwanja 20,000 kuanzia mwaka 2002/2003 hadi Juni 2008.

7.3. Mheshimiwa Spika, tukizingatia umuhimu wa rasilimali hii sio tu kumuendeleza Mtanzania kiuchumi bali kumpa urithi wa asili, ni kwa vipi kwa mwenendo huu watanzania wanaoongezeka kila mwaka wataweza kumilikishwa ardhi?

7.4. Mheshimiwa Spika, utambuzi wa ardhi ni mojawapo ya chanzo kikuu cha mapato kwa Serikali kupitia kodi ya Ardhi, na kodi hii haiwezi kulipwa kama wamiliki wa ardhi hiyo hawakusajiliwa na kupewa hati. Mfano wizara ya Ardhi ulikusanya kodi ya Ardhi ya Tshs 586,998,900/- kwa mkoa wa Dar es salaam baada ya kusajili nyumba 217,407 tu. Je kama zoezi hili la kusajili na kutoa hati kwa ardhi yote (nyumba) ni kiasi gani kama nchi itakuwa ikikusanya kwa mwaka?

Kambi ya Upinzani ilitegemea kwa umuhimu wa pekee, na kwa kuzingatia ushirikiano wa Afrika Mashariki mipango ingelikuwa wazi zaidi katika umilikishaji wa viwanja na mashamba kwa Watanzania, pia ikichukuliwa kuwa inaongeza mapato ya Serikali.
8.0 UTAMBUZI WA RASILIAMALI WATU:
8.1. Mheshimiwa Spika, Lipo tatizo la kuwa na takwimu sahihi za Rasilimali watu ambao watatoa huduma katika secta zote za Uchumi wetu. Kwa mfano Sekta ya Afya na Elimu zina upungufu mkubwa wa watumishi,na ukangalia mipango yetu hasa katika nyanja za Sayansi mahitaji ni makubwa kuliko ualishaji wa wataalamu wenywe.

8.2. Mheshimiwa Spika, Ikiwa Serikali ina lengo thabiti la kuwa na mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini unaotekelezeka Kambi ya Upinzani inaendelea na ushauri wake kwamba Serikali inastahili kujipa muda kutathmini MKUKUTA na kushirikisha na wadau wote katika kuandaa mpango mbadala wa kukuza uchumi kuongeza ajira za uhakika na kupunguza umaskini.Vyenginevyo tutaendelea kufanya makosa yale yale kila uchao. Serikali makini huwa hairudii makosa yale yale, “Once beaten twice shy”.

9.0. C. KUIMARISHA UTAWALA BORA NA UWAJIBIKAJI
9.1. Mheshimiwa Spika, Dhana nzima ya utawala bora na uwajibikaji ndio msingi mkuu wa kujenga Taifa imara na lenye uchumi endelevu. Mazingira mazuri ya ufanyaji wa biashara na uwekezaji katika ngazi zote za kiuchumi na pia katika ngazi zote za kisiasa na kiutawala huimarika.

9.2. Mheshimiwa Spika, Serikali inayoheshimiwa na raia wake hujengwa katika misingi ya utawala bora na uwajibikaji kwa viongozi wake.
Kambi ya Upinzani inaona kuwa Tanzania ni nchi inayoheshimika Duniani lakini suala la utawala bora na uwajibikaji bado liko nyuma sana na hivyo kusababisha kuwepo kwa tatizo la rushwa kuota mizizi katika ngazi zote za kiutawala. Wenzetu waliodhamiria kujenga utawala Bora, kwa mfano Rwanda,wanaochunguzwa kwa Rushwa,hupumzishwa hadi uchunguzi utakapo malizika.

9.3. Mheshimiwa Spika, Taarifa benki ya Dunia ya mwaka 2009 inaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya 127 katika suala zima la urahisi wa ufanyaji biashara. Nafasi hiyo inatokana kwa kiwango kikubwa na urasimu katika utekelezaji wa kazi zake za uendeshaji wa Serikali wa kila siku.

9.4. Mheshimiwa Spika, Pamoja msukuosuko wa uchumi Duniani, ugumu wa kufanya biashara katika nchi yetu ni jambo ambalo limesababisha kuteremka kwa uwekezaji kutoka nje(FDI) toka dola million 744 mwaka 2008 hadi dola million 650 mwaka 2009 sawa na upungufu wa 14.5%. Pamoja na mambo mengine kubwa ni urasimu kwa wawekezaji wa nje na hata wa ndani.

9.5. Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imekuwa ikitoa ahadi za kurekebisha hali hiyo lakini kila uchao hali inazidi kuwa mbaya. Kupata leseni ya biashara Rwanda inakuchukua siku 3, Tanzania katika makaratasi inatamka isizidi siku tano, lakini hali halisi ni kuwa hata kujibiwa barua ya kuthibitisha kupokea barua yako. Nalo hilo linahitaji wahisani?.
10.0. JUMUIYA YA AFRIKA YA MASHARIKI:
10.1. Mheshimiwa Spika, Tanzania ilipewa miaka mitatu na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ili ianishe maeneo gani ya kiuchumi au kibiashara inaweza kulisha soko la Jumuiya hiyo.
10.2. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika sana kwa Tanzania kupitia asasi zake za kiutendaji kuwa hadi sasa nchi husika bado hazijapewa taarifa rasmi kuhusu maeneo ambayo Tanzania ina fursa bora zaidi za uzalishaji (Comperative Advantage) na kama tukijipanga vizuri tunaweza kuuza chakula katika soko hilo.
10.3. Mheshimiwa Spika, upo wasi wasi hasa ukingalia bajetu ya mendeleo ambayo ni 3.7% ukilinganisha na Kenya na Uganda ambao ni wastani wa asilimia 9% mwaka huu wa Fedha.Tanzania itakuwa soko la Afrika Mashariki na pia itakuwa msafirishaji wa mali ghafi za viwanda vya Kenya,kwani viwanda vyetu hata vya ngano vinaagizia ngano nzima kutoka Australia na Saudi Arabia na hadi leo tumeshindwa hatakujitosheleza kwa sukari.Hii ni aibu.
10.4. Mheshimiwa Spika, Serikali kushindwa kuwataarifu Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ambao ni washirika wenzetu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuhusu uwezo wa wakulima wetu kiuzalishaji. Upo wasi wasi kuwa kama tulivyoshindwa kutumia AGO pia tutashindwa kutumia soko la Afrika ya Mashariki ipo hatari yakuwa wapokeaji tu.
10.5. Mheshimiwa Spika, Kutokana na ukimya wa Tanzania katika suala hilo sasa hivi Uganda ndiyo inayoonekana kama nchi inayoweza kuzilisha nchi zote za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2008 na 2009 Uganda imeuza tani 100,000 za nafaka kwa Kenya na 13,000 kwa Rwanda. Tanzania pamoja na miundombinu mibovu lakini wakulima wetu wana uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula tatizo nikuwezeshwa na kupatiwa bei muafaka ya mazao yao.
11.0. PESA ZA KUNUSURU UCHUMI(1.7 trilion)
11.1. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, Hakuna mtu asiyejua kuwa Serikali ilileta ombi kwenye Bunge lako Kutukufu kuomba idhini ya kutumia kiasi cha shilingi trillion 1.7 kwa ajili ya kuimarisha uchumi kutokana na mtikisiko wa uchumi wa dunia uliotokea mwaka 2009.
11.2. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani iliamini kabisa kuwa wakati Serikali inaomba idhini ya Bunge ya matumizi ya fedha hizo ilikwisha fanya upembuzi yakinifu kuhusiana na matumizi ya fedha hizo.
11.3. Mheshimiwa Spika, Hii ina maana kwamba sekta au makampuni ambayo yalikuwa yanadai kuwa yameathirika sana na mtikisiko huo yalitakiwa kwanza kufanyiwa ukaguzi ili kujua hali halisi ya kuathirika kwao na kiasi gani kitawawezesha kurudi katika biashara walizokuwa wakizifanya.
11.4. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ilitoa angalizo katika hotuba yake kuhusiana na fedha hizo kuwa inaweza kuwa ni njia nyingine ya ufisadi kama ilivyokuwa katika suala la EPA ambalo hadi sasa watanzania hawajapata majibu sahihi kutoka kwa wale wanaotakiwa kutoa majibu kuhusiana na ufisadi huo.
11.5. Mheshimiwa Spika, kuna tetesi kuwa makampuni ambayo yamepata fedha hizo yamefanya udanganyifu mkubwa na kuchukua fedha za bure kama ilivyokuwa katika suala zima la EPA.
11.6. Mheshimiwa Spika, Katika takwimu zilizotolewa na Benki Kuu zinaonyesha kuwa fedha zilizopata idhini ni Shillingi trillion 1.692 na zile zilizogawiwa ni shilling trillion 1.28. Kwa kuangalia tofauti katika ya fedha zilizoidhinishwa na zilie zilizotolewa utaona kuna bakaa (change) ya shilling billion 412. Kwa kuwa kazi waliopewa na Serikali imekwisha ,Benki Kuu inafanya utaratibu wa ku-exit. Aidha katika hilo bado ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo haujafanyika.
11.7. Mheshimiwa Spika, Aidha kwa kuwa fedha yoyote ya Serikali inayotumiwa baada ya kupata idhini ya Bunge inatakiwa ikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kambi ya Upinzani inauliza, Je ukaguzi kwa makampuni yaliyopata fedha hizo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali ameyakagua na kama tayari taarifa yake iko wapi?
11.8. Mheshimiwa Spika, Hapa Kambi ya Upinzani inataka kujua ni kwanini kila Serikali inapofanya manunuzi au kutoa huduma Fulani ni lazima fedha zibakie? Mfano katika manunuzi ya Rada ipo “change” ya billion 29, na inawezekana hata kwenye ununuzi wa ndege ya Rais kuna bakaa au “change”. Huu ni udhaifu mkubwa sana unaotoa mianya ya rushwa kubwa (grand corruption).
11.9. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inazitaka nchi za nje na mashirika yao kutusaidia kutoa taarifa za watu wetu wanaoficha mabilioni ya fedha kwenye mabenki yao na yale ya “Off shore banking”, ili tuweze kupambana na Rushwa kubwa. Sheria ya Rushwa inasema anaetoa na anaepokea pamoja na anaetunza wote ni wakosa hivyo, Banki zinazotunza fedha hii chafu nao si wasafi.
12.0. PUBLIC PRIVATE PARTNERSHIP (PPP):
12.1. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tokea mwaka 2004 kupitia hotuba zetu za bjeti tumekuwa tukiita Serikali kuweka utaratibu wa kuendesha miradi yake kwa ubia na sekta binafsi (Public Private Partnership).
12.2. Mheshimiwa Spika, Inasikitisha kuwa jambo hilo jema limepigwa danadana,hadi pale IMF na wahisani walipopunguza misaada yao ndio leo Serikali inaleta mswaada wa sharia kwa dharura ili kuanzisha mfumo huo.Mhe.Spika ni kwanini Serikali isiupokee ushauri wa Watanzania mapema hata kama ni kutoka upinzani, ili kuondokana na kutegemea wahisani kila uchao?
12.3. Mheshimiwa Spika, tunashukuru kuwa ushauri wetu kwa Serikali toka mwaka 2004 kuhimiza uanzishwaji wa PPP sasa umefanyiwa kazi na tunaamini kuwa matunda yake yataanza kuonekana hivi karibuni.
13.0. MUDA NA UKUAJI WA UCHUMI (Time management)
13.1. Mheshimiwa Spika, muda ni bidhaa ambayo pindi ikishapita basi haipatikani tena. Tanzania katika mipango yake ya maendeleo suala la muda limekuwa halitiliwi maana au kupewa kipaumbele.

13.2. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani baada ya kufanya tafiti imegundua kuwa muda unaopotezwa na watumishi wa umma au wajasiria mali kwa kujua au kutokujua ni mwingi mno. Maeneo yafuatayo ndiyo yamekuwa yakikwaza hata shughuli za maendeleo, kwanza ni kwenye mabenki yetu ambapo inasababisha hata watanzania kukata tamaa ya kufungua akaunti, pili ni misururu mirefu barabarani jambo linalosababisha kuchelewa kwa shughuli za kiuchumi, tatu ni katika vyombo vya kutoa haki, yaani mahakama na polisi, na nne ni hospitali.

13.3. Mheshimiwa Spika, kutokana na usumbufu huo, watumishi wa Umma na wajasiria mali wanajikuta kwa siku wamekwisha poteza zaidi ya saa nne. Wakati umefika sasa kwa Serikali kutambua kuwa “muda ni fedha” (Time is money) hivyo ni lazima itafiti, ichambue na kuona ni fedha kiasi gani tunapoteza kwa njia ya kutokusimamia vizuri muda wetu.
14.0. UKUSANYAJI WA MAPATO:
14.1. Mheshimiwa Spika, kwa mfano malengo ya kukusanya mapato ya ndani kwa mwaka 2008/2009 yalikuwa ni 15.9% ya pato la Taifa, mwaka 2009/2010 yalikuwa ni 16.4% ya pato la Taifa, mwaka 2010/2011 ni 17.2% ya pato la Taifa shabaha ni kufikia 18.3% kwa mwaka 2011/2012. Jee lile lengo la awali limesahauliwa au limeonekana halitekelezeki? Ni kitendawili Mhe.Spika.

14.2. Mheshimiwa Spika, Changamoto muhimu ni Mapato ya ndani hayawiani na mahitaji ya kugharamia shughuli mbalimbali za Serikali, hususan miradi ya miundombinu ya reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na umwagiliaji; huduma za jamii (elimu, afya na maji); na kilimo. Misamaha holela ya kodi inachangia kuinyima serikali mapato. Sekta ya madini haichangii mapato ya serikali inavyostahili. Matumizi mabaya ya serikali, ubadhirifu wa safari za nje na mfumko wa posho ukidhibitiwa fedha ya kuwekeza katika sekta muhimu itapatikana. Katika mapendekezo ya bajeti yetu tumeonesha maeneo ya kupata fedha hizo.

15.0. MATUMIZI YA SERIKALI
15.1. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya 2007/08 ilitumia zaidi katika matumizi ya kwaida (tshs.3.886 bl.) kuliko matumizi ya maendeleo (tshs.2,201bn.). Bajeti ya 2008/09 Serikali ilitumia zaidi katika matumizi ya kawaida (shs.4.726 trillion) kuliko matumizi ya maendeleo (shs.2.489 trillion.)
Bajeti ya 2009/2010 Serikali ilitumia shs.6.7trillion na matumizi ya maendeleo shs.2.8trillioni. Miaka 12 ya bajeti za nyuma, matumizi halisi ya maendeleo yamekuwa madogo kuliko yalivyoidhinishwa katika bajeti.
15.2. Mheshimiwa Spika, Hii ni kama tulivyo wahi kusema kuwa ukubwa wa Serikali utasababisha matumizi makubwa ya kawaida. Kambi ya Upinzani inaona kuna kasoro kubwa ya kiuwiano kati ya matumizi ya kawaida na yale ya maendeleo, hivyo kuchelewesha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini. Fedha nyingi zinatumika katika uendeshaji wa Serikali kuliko katika maendeleo na huduma za jamii na hivyo kupanda kwa pato la Taifa kutokuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida.
15.3. Mheshimiwa Spika, Ukiangalia ulinganisho wa takwimu za matumizi ya kawaida kwenye pato la Taifa (GDP) kwa Tanzania, Kenya na Uganda utaona kuwa takwimu za Kenya zina panda na kushuka toka mwaka 2007/08-2010/2011 (20.5%, 19.4%, 20.0% na 19.4%), Uganda takwimu zao za matumizi zinashuka (12.0%, 11.8%,10.3% na 9.8%) wakati takwimu za matumizi ya maendeleo zinapanda (5.6%,9.9%, 10.2% na 10.3%). Tanzania takwimu za matumizi ya kawaida zinaonyesha kupanda (14.9%, 17.7%, 21.5% na 22.7%) kwa mtiririko wa miaka, na za maendeleo Tanzania 2007/2008 hadi 2010/2011 ni (7.9%, 8.0%, 3.1% na 3.7%)Mhe.Spika utaingiaje kwenye ushindani wa kikanda wakati matumizi ya kawaida yanapanda kila uchao na ya maendeleo yanateremka?
15.4. Mheshimiwa Spika, kutokana na muundo wa bajeti ya 2010/11 matumizi ya kawaida yanazidi mapato ya ndani kwa wastani wa Tshs.1.8 trilion. Nivyema waziri atueleze atazitoa wapi katika vianzio vya ndani kulipia matumizi ya kawaida.
16.0. MATUMIZI KWENYE MANUNUZI
16.1. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika bajeti zake zote mbadala imekuwa ikitoa mwanga kwa Serikali wapi ni vyanzo wa mapato, lakini ufuatiliaji wa vyanzo hivyo umekuwa ukilegalega sana..
17.0. MISAMAHA YA KODI
17.1. Mheshimiwa Spika, Ukiangalia takwimu zilizotolewa katika maelezo ya Mhe. Waziri inaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita tu kabla ya kusoma mpango wa bajeti Bungeni, Serikali ilikwishatoa misamaha ya kodi inayofikia Tshs.324.14Billioni. Misamaha hii kwa kiasi kikubwa ndio tuliyokuwa tunaipigia kelele kwani wanapewa wawekezaji katika tasnia ya madini.

17.2. Mheshimiwa Spika, Japo kuwa kila mwaka kelele zinapigwa kuhusu misamaha ya kodi, bado hali haijawa nzuri. Zaidi ya Tshs.673billion ya mapato yametolewa kama misamaha (BAJETI 2008/09 inakadiriwa misamaha ya kodi kuwa takribani shilingi 819.9 billion na mwaka 2009/2010 misamaha ilikuwa ni 3% ya pato la Taifa). Kwa maelezo ya Bajeti ya Waziri wenzetu Kenya na Uganda misamaha ya kodi ni 1% ya Pato la Taifa kwa Kenya na 0.4% kwa Uganda wakati Tanzania ni 2.1% ya pato la Taifa, ni fedha nyingi sana hizi. Ni lazima tuandae utaratibu wa kupunguza misamaha hiyo ili kupunguza Rushwa na bajeti tegemezi, lakini pia kuwa na utaratibu ulio wazi zaidi wa kutoa misamaha.

17.3. Mheshimiwa Spika, Misamaha hii ya kodi ndicho chanzo kikuu cha kuleta nakisi (deficit) katika bajeti yetu. Hivyo basi Kambi ya Upinzani inatarajia misamaha hiyo ambayo kwa takwimu za Serikali ni asilimia 30 ya makusanyo yote ya kodi au 3.5 ya pato la nchi kupungua angalau kuwa sawa na wenzetu wa Kenya au Uganda.

17.4. Mheshimiwa Spika, inasikitisha leo kuona Serikali yetu iko tayari kuwabebesha watanzania mzigo wa madeni kwa kukopa katika mabenki ya biashara lakini inaogopa kuyabana makampuni ya nje inayo yasemehe kodi- badala yake inayabembeleza. Mtanzania kufungiwa biashara zake habembelezwi. Hii ni hatari katika kujenga taifa linalojiamini.
Mhe.Spika,Kitendo cha Serikali kurudisha msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za madini,kinavujna mantiki nzima ya marekibisho ya sheriaya madini tuliopitishahivi karibuni.Kwa kitendi hichi,kitayafanya makumpuni ya madini kuchimba madini yenyewe hivyo kuwanyima fursa makampuni ya ndani kuingia katika biashara hiyo.Huku nikua sekta ya makandarasi wa ndani.

17.5. Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani haikubaliani na pendekezo hili la Serikali.

18.0. TAARIFA YA MKAGUZI NA MDHIBITI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI
18.1. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Mkaguzi inaonyesha kuwa shs.16,785,000 ililipwa kwa makosa kwa mtumishi kama posho ya kujikimu kwa Afisa kuhudhuria kozi fupi ya siku 30 huko Swaziland.
Kambi ya Upinzani inasema malipo hayo ni sehemu ya tu ya mchezo unaoendelea kwa Wizara/Idara na taasisi zote za Serikali kupeleka watumishi nje ya nchi kwa baraka za Idara kuu ya Utumishi.
18.2. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza, Je, kwa mtindo huu wa kuwadharau wataalam wetu waliopo katika vyuo vyetu umeipotezea Serikali kiasi gani? Kama gharama kwa mtumishi mmoja kulingana na cheo chake na kozi anayoisoma ni kati ya USD 5000-8000 kama tuition fees, posho ni kati ya USD 350-500 kwa siku usafiri wa kwenda na kurudi ni kati ya USD 3000-4000. Jumla ni takriban USD 22,500 kwa kozi ya wiki tatu (siku 21). Hizi ni sawa na Tshs.29,250,000.
18.3. Mheshimiwa Spika, Kama mtumishi mmoja wa Serikali anaweza kulipiwa million hizo kwa muda wa siku 21 na ni watumishi wangapi wa Serikali wamekwisha kwenda nje? Je, fedha hizo zingeweza kuwalipia wanafunzi wangapi katika vyuo vya elimu ya Juu hapa nchini?
18.4. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tathmini ya matumizi ya fedha ambazo zimekwishatumika kwa njia hiyo kwa Wizara, taasisi,idara na wakala za Serikali.
18.5. Mheshimiwa Spika, Aidha mdhibiti na Mkaguzi Mkuu amegundua malipo ya asilimia 30 ya nyumba kwa watumishi lakini ukweli ni kwamba watumishi hao wanaishi katika nyumba za Serikali. Mdhibiti amegundua malipo ya shs.13,299,400. alizolipwa mtumishi anayeishi katika nyumba ya Serikali kama posho ya nyumba. Shs282,453,350. kama gharama za hoteli wakati walikwishapewa posho za kujikimu.

18.6. Mheshimiwa Spika, Mchezo huu wa wamatumizi ya fedha za Serikali ndio unaosababisha bajeti ya Maendeleo kuzidi kuwa ndogo siku hadi siku na matumizi ya kawaida kuendelea kupanda. Kambi ya Upinzani inachelea kuamini kama kweli wanaofanya udanganyifu huu ni kada ya chini ya watumishi.
Kambi ya Upinzani imekuwa ikilipigia kelele suala hili la manunuzi kwa muda mrefu sasa kwani ndiyo sehemu inayosababisha kuwepo kwa rushwa papa na kuyumbisha uchumi wa nchi.

ULINGANIFU WA MAPENDEKEZO YA VYANZO VYA MAPATO KWA MIAKA YA NYUMA (Tshs. Billions)
Na. Maelezo/MAPATO 2007/08 2008/09 2009/10 Utekelezaji wa Serikali 2010/2011
1. Ada za leseni uvuvi 19.0 9.5 9.5 UMEANZA 9.5
2. Mrahaba kutoka uvuvi 740.0 370.0 130.0 130.0
3. Mafuta kwa meli za uvuvi 3.0 3.0 3.0 BADO 3.0
4. Bidhaa za Misitu 100.0 100.0 100.0 BADO 100.0
5. Biashara na Comoro 2.0 4.0 BADO 2.0
6. Punguzo la misamaha ya kodi 50% 336.5 409.9 409.95 350.0
7. Kodi ya 20% posho za Semina 8.0 8.0 6.07 6.07
8. Mauzo ya hisa za Serikali (NMB)- NBC sasa 45.0 120.0 475.0 78.0
9. Ukusanyaji wa kodi ya madini isiyokusanywa 433.0 88.3 88.0 100.0
10. Ushuru mauzo ya vito na Tanzanite 100.0 100.0 150.0 BADO 100.0
11. Mapato vitalu, uwindaji wa kitalii 85.0 85.0 81.0 BADO 81.0
12. Mrahaba 4% madini 41.8 51.8 155.0
13. Ushuru katika mafuta ya petrol na diesel(makampuni 6 ya madini) 153.0 59.0 59.0 BADO 59.0
14. Mauzo ya ndege ya Rais 35.0 30.0 30.0 25.0
15. Leseni za Maderva 12.5 12.5 6.25
16. Mapato kutokana na utalii 67.5 67.5 67.5
17. Uvuvi katika mito na maziwa 45.0 UNATEKELEZWA 45.0
18. Biashara Bandari ya Mtwara 4.00 BADO 4.0
19. Elektronic Procurement(Savings) 250.0 250.0 BADO 250.0
20. Misamaha ya kodi
21. Kodi isiyokusanywa Williamson Diamond 841.0
22. Mapato toka Tansort 206.6
23. Mauzo ya hisa za celtel 25% 243.0 250.0
24 Fedha za EPA(Commitment) 131.8
25. Mauzo ya mchele soko EAC 428.4
26. Mauzo Mahindi soko EAC 104.85
27. Kodi ya Ardhi 2.5
28. Diaspora Bond 20.0

2,181.3 2,234.348 1,847.07 2,370.82

NB:Mhe.Spika,mapendekezo yetu, yamekwepa kabisa kukopa katika Mabenki ya Bishara,hatukuongeza ada za leseni kwa BODABODA ili kuwapunguzia wananchi wa kwaida gharama za usafiri ambao katika hali ya sasa ni mzigo kwao..

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa vipaumbele vyetu , tumegawa mapato kama ya bajeti hii mbadala kama ifuatavyo:-
1. Kilimo 12% = 1359.64872
2. Miundombinu 20% = 2266.0812
3. Elimu 22% = 2492.68932
4. Nishati 9% = 1019.73654
5. Afya 12% = 1359.64872
6. Maji 10% = 1133.0406
7. Mawasiliano 5% = 566.5203
8. Matumizi Mengineyo 10% = 1133.0406

USHAURI WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA SURA YA BAJETI
Mapato: shilingi bilioni
A. Mapato ya Ndani 8,380.41

B. Mikopo na Misaada ya Nje Ikijumuisha 2,777.414
I. Misaada ya kibajeti 631.808
II. Mikopo ya kibajeti 189.837
III. Misaada ya miradi 891.96
IV. Mikopo ya miradi 1,063.809
C. Mapato ya Halmashauri 172.582.

JUMLA YA MAPATO YOTE 11,330.406
D. Matumizi
Matumizi ya Kawaida 7,863.546
Matumizi ya Maendeleo 3466.86
i. Fedha za Ndani 1,511.091
(ii) Fedha za Nje 1,955.769

JUMLA YA MATUMIZI YOTE 11,330.406

19.0. MWISHO
19.1. Mheshimiwa Spika, Kubuni sera nzuri ni mwanzo tu. Sera zinazopaswa kuwekwa katika mipango ya utekelezaji na kutekelezwa kwa umakini wa hali ya juu. Utekelezaji na matokeo yake yafanyiwe tathmini ya mara kwa mara ili makosa yangunduliwe na kurekebishwa. Kujenga utumishi bora, wenye ujuzi, usiyoyumbishwa na rushwa ndani ya serikali ni changamoto muhimu.

19.2. Mheshimiwa Spika, Utumishi mzuri ulio imara haujengwi siku moja. Viongozi wa kisiasa ni wepesi kuhujumu kuwepo kwa utendaji mzuri serikalini ikiwa watawatumia watendaji wa serikali kufanikisha malengo ya kisiasa ili waendelee kubaki madarakani kwa kuiba kura wakati wa uchaguzi au utekelezaji wa miradi ya muda mfupi kwa malengo ya kuvutia wapiga kura.

19.3. Mheshimiwa Spika, Serikali inawajibika kuvutia watumishi wenye uwezo na ari ya kufanya kazi. Ni muhimu mishahara ya wafanyakazi serikalini iwe inavutia lakini utumishi serikalini uzingatie uwezo na siyo mtoto wa nani au unamjua nani!

19.4. Mheshimiwa Spika, bajeti hii ya mwaka huu ni moja ya bajeti mbaya katika historia ya nchi yetu. Ni bajeti ambayo itaumiza sekta binafsi inayozalisha mali kwa kuitoza kodi nyingi sana ili kulipia gharama za uendeshaji za serikali (sio gharama za maendeleo) na wakati huo huo ni bajeti inayoifanya serikali ishindane na sekta binafsi katika kutafuta mikopo kwenye mabenki ya biashara. Bajeti hii itaumiza ukuaji wa uchumi na kupelekea uzalishaji kupungua na hata kusababisha watu kukosa ajira au kupunguzwa kazini kwa wingi. Bajeti hii ni bajeti ya kujinyonga kwa chama kinachotawala kwani itaongeza ukali wa maisha kwa wananchi, haijibu changamoto za umma na inasaidia zaidi wenye nacho kuliko watu masikini. Hasira za wananchi hao watazionyesha katika masanduku ya kura mwezi Oktoba mwaka huu na Kambi ya Upinzani inaamini watakuwa na haki ya kufanya hivyo.

19.5.Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nawashukuru wote kwa kunisikiliza na naomba kuwasilisha.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!!!!!!!!!!!

…………………………………..
HAMAD RASHID MOHAMED (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI
11.06.2010

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s