Upinzani waonesha njia

Kambi ya Upinzani inaona kuwa kwa ajili ya kutoa motisha zaidi kwa wafanyabiashara kusafirisha korosho ambazo tayari zimebanguliwa na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa tunazouza nje na pia kutoa ajira kadhaa kwa wananchi ni bora wangepewa unafuu kadhaa katika kodi za ndani. Kwani ushuru wa usafirishaji wa korosho ghafi nje wa kulipa USD 160 kwa tani moja ingekuwa ni bora uongezwe ili kusitisha usafirishaji wa korosho ghafi. Wakati huo huo, Serikali ikae na viwanda vya kubangua korosho, ili visaidiwe kutoka tani 17,000 zinazobanguliwa sasa ifikie angalau tani 50,000 kwa mwaka. Maana kuzuia usafirishaji wa korosho ghafi, hakusaidii kama hakuna ongezeko la viwanda vya kubangua korosho.

Hon. Hamad Rashid Mohammed, Opposition Leader in the National Assembly

Hon. Hamad Rashid Mohammed, Opposition Leader in the National Assembly

HOTUBA YA MHESHIMIWA HAMAD RASHID MOHAMMED (MB) KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI – WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA FEDHA YA MWAKA 2010 (THE FINANCE ACT, 2010)

I: UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote ningependa kutumia fursa hii kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2010 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kanuni ya 86(6), Toleo la 2007.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani pamoja na watu wote ambao kwa njia moja ama nyingine wametoa mchango wao katika kufanikisha hotuba yetu ya Bajeti Mbadala kwa mwaka wa fedha 2010/2011. Kupitia Bunge hili tukufu, ninatoa ahadi kwa niaba ya Kambi nzima kuwa tutaendelea kutetea maslahi ya Watanzania wote kwa ujumla kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuzungumzia vifungu mahsusi vya Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2010, napenda kueleza maoni ya jumla ya Kambi kuhusiana na maudhui ya muswada huu.

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2009 (Uk. 5), sehemu ya Ongezeko la Ukusanyaji Kodi inasema: “Wahusika wote katika ukusanyaji wa kodi wanatakiwa kufanya kazi hiyo kwa juhudi kubwa zaidi ikizingatiwa kuwa hadi sasa makusanyo ya mapato yako chini ya asilimia hamsini (50%) ukilinganisha na fedha inayotakiwa kukusanywa kutoka kwenye vianzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na migodi, utalii, bidhaa za kilimo, biashara na kadhalika. Ukwepaji wa kulipa kodi pamoja na kulipa kodi kidogo, kutumia mianya ya udhaifu wa sheria zilizopo imekuwa ni desturi ambayo inastahili kupigwa vita”.

Mheshimiwa Spika, kwa kuthibitisha hayo kwa mujibu wa Taarifa ya Msajili wa Hazina iliyonukuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, hadi kufikia tarehe 30.6.2009 kulikuwa na mashirika ya umma yenye madeni yaliyofikia Tsh. 102.5 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 25 ya bakaa yote ya madeni iliyodhaminiwa na Serikali ambayo yalitakiwa yalipwe ifikapo tarehe 30.09.2009. Wakati huo kulikuwa na bakaa ya mapato ya Tsh. 110.1 bilioni ikijumuisha na Tsh. 93.4 bilioni ya deni la zamani ambalo hadi leo halijalipwa, hivyo kufanya jumla kuwa Tsh. 203.5 bilioni.

Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa hiyo, matumizi yote ya Serikali ya kawaida na maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2007/2008 na 2008/2009, hesabu za matumizi (Expenditure Account) iliongezeka kutoka Tsh. 3.7 trilioni 2007/2008 hadi Tsh. 4.9 trilioni, sawa na ongezeko la 34% wakati matumizi ya maendeleo yaliongezeka kutoka Tsh. 1.3 trilioni hadi Tsh.1.6 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 20.

Mheshimiwa Spika, lakini taarifa ya mapato yasiyokusanywa yameongezeka kwa kiwango cha kutisha kutoka Tsh. 789.2 milioni kwa mwaka wa 2007/2008 hadi kufikia Tsh. 10.02 bilioni sawa na asilimia 1,170. Mheshimiwa Spika, hiki ndicho kiwango cha udhaifu wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nimeanza na utangulizi huu kwa sababu Serikali imekuwa inaongeza kodi kila uchao hasa kwa Watanzania masikini, lakini inashindwa kubana mianya ya kukwepa kodi hadi kufikia kiwango hicho cha kutisha cha asilimia 1,170. Katika hali kama hii, ni dhahiri nyongeza hizi ni za kumuongezea mzigo mlaji, Mtanzania masikini, badala ya kumuendeleza.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imekuwa ikiishauri Serikali wakati wote kuwa ipunguze misamaha ya kodi kwa angalau asilimia 50. Mara zote Serikali imekuwa ikidai kuwa wanalifanyia mkakati suala hili lakini ukiangalia hali halisi hakuna kinachofanyika.

Mheshimiwa Spika, naomba nirejee kauli ya CAG kwamba, ili Serikali iweze kuongeza mapato inapaswa ipunguze misamaha ya kodi, hasa ukizingatia ukweli kwamba misamaha hiyo ya kodi jumla yake ni Tsh. 752 bilioni.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali ingalikuwa na nia ya dhati ya kuwaondolea kodi kama za pikipiki na gari za “Boda Boda”, ingeliweza kufanya hivyo kwa kufidia kiwango hicho cha mapato kwa kupunguza angalau asilimia 50 ya misamaha, ambayo itafanya si chini ya Tsh. 376.2 bilioni. Maelezo ya CAG yanaonyesha mchanganuo wa misamaha hiyo ya kodi kama ifuatavyo:

Taasisi Idara ya Forodha (shs) Idara ya Kodi ya Ndani (shs) Jumla (shs)
Taasisi za Serikali 21,617,300,000.00 21,617,300,000
Mashirika ya Umma 7,125,600,000.00 7,125,600,000
Taasisi za kidini 408,000,000.00 408,000,000
Taasisi zisizo za Kiserikali 37,237,700,000.00 37,237,700,000
Miradi ya wafadhili 21,552,700,000.00 21,552,700,000
Makampuni na watu binafsi 51,236,400,000.00 51,236,400,000
Kituo cha Uwekezaji (TIC) 380.090,500,000.00 380,090,500,000
Misamaha ya kodi na ongezeko la thamani 170,097,500,000 170,097,500,000
Misamaha ya kodi katika maduka yasiyotozwa kodi 3,892,400,000 3,892,400,000
JUMLA 578,408,900,000.00 173,989,900,000.00 752,398,800,000.00

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani haikubaliani na hatua ya kusamehe kodi makampuni ya madini kama inavyopendekezwa na Serikali kwa kutaka kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 148.

Mheshimiwa Spika, katika Kitabu cha Mapato (Revenue Book) fungu la 137, hakuonekani mapato yoyote mwaka huu kutokana na leseni za uvuvi. Uvuvi wa kanda wa pwani huwa na wastani wa meli 15-20 zinazovua kamba (prawns) ambazo kila moja inalipia leseni ya wastani wa USD 18,000. Na kuvua wastani wa tani 80 -100 kwa mwaka, Serikali hutoza asilimia 5 kama mrahaba kwa samaki wanaovuliwa. Kambi ya Upinzani tunajiuliza ni kwa nini kitabu cha Mapato kisionyeshe angalau mapato haya? Umakini wa kukusanya mapato uko wapi?

Mheshimiwa Spika, hata katika uvuvi unaofanyika kwenye bahari kuu, Serikali haikusanyi mapato kwenye meli zinazovua huko. Wastani wa meli zinazovua huko ni 150 – 170 na zina uwezo wa kuvua wastani wa tani 500 – 2,000.

Mheshimiwa Spika, Hivyo basi, kama Serikali ingeliiwezesha Wizara ya Uvuvi na Mifugo ingeliweza:
a. Kuongeza mapato kutokana na leseni za uvuvi wa bahari kuu na bahari ndogo ambao kwa mujibu wa ‘Revenue Book’ mwaka huu hakuna makusanyo kabisa pamoja na kwamba zipo meli zinazovua.
b. Tungeweza kupata levy ya asilimia 5 kutokana na mauzo ya wastani wa tani 100 za kamba (prawns).
c. Tungeweza kuongeza ada ya leseni kutoka USD 18,000 hadi USD 30,000 ambazo hazikusanywi kwa sasa.
d. Tungeweza kupata levy ya asilimia 2 ya samaki wanaovuliwa bahari kuu ambapo wastani wa meli 150-170 zenye uwezo usiopungua tani 500 – 2,000 zinavua na kuondoka.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa kama Serikali ingelikuwa sikivu tungeweza kukusanya si chini ya Tsh. 130 bilioni. Serikali haifanyi hivyo na badala yake inakimbilia kuongeza leseni ya “Boda Boda” ya Tshs 10,000.

MAPITIO YA MUSWADA

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Muswada wa Fedha wa mwaka 2010 kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mabadiliko katika Sheria ya Korosho, sura ya 203, Kambi ya Upinzani inaona kuwa kwa ajili ya kutoa motisha zaidi kwa wafanyabiashara kusafirisha korosho ambazo tayari zimebanguliwa na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa tunazouza nje na pia kutoa ajira kadhaa kwa wananchi ni bora wangepewa unafuu kadhaa katika kodi za ndani. Kwani ushuru wa usafirishaji wa korosho ghafi nje wa kulipa USD 160 kwa tani moja ingekuwa ni bora uongezwe ili kusitisha usafirishaji wa korosho ghafi. Wakati huo huo, Serikali ikae na viwanda vya kubangua korosho, ili visaidiwe kutoka tani 17,000 zinazobanguliwa sasa ifikie angalau tani 50,000 kwa mwaka. Maana kuzuia usafirishaji wa korosho ghafi, hakusaidii kama hakuna ongezeko la viwanda vya kubangua korosho.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mabadiliko katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa za Ndani, Sura ya 147, kifungu cha 9 cha muswada kinachofanyia marekebisho Jedwali la Nne, H.S. Code No. 2201.10.00 na 2202.90.00 vinavyohusiana na kupandishwa kwa sh. 5.00 kwa kila lita ya maji na vinywaji baridi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona pendeezo hili la Serikali badala ya kuviinua viwanda vyetu hasa vile vinavyotengeneza juice za matunda kwa bidhaa zake kuweza kununuliwa na wananchi wa kada zote za maisha, inavikandamiza. Hali ya umasikini kwa wananchi inazidi kuwa mbaya hivyo bei kupandishwa kidogo maana yake ni kwamba kundi kubwa la watumiaji watashindwa kununua, na wakishindwa kununua viwanda vitashindwa kuendelea na uzalishaji kwani mzunguko wa bidhaa utasimama. Je, tunavilinda viwanda vyetu au tunaviua?

Mheshimiwa Spika, mabadiliko yanayofanywa katika Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332, kifungu kipya cha 80A kinachoongezwa cha kumtaka yeyote atakayenunua bidhaa za zaidi ya sh. 5000/- kupatiwa risiti ambapo risit hiyo inatakiwa pia iwe na anuani ya mnunuzi. Sote tunaelewa Watanzania walio wengi ambao ndiyo watakaofanya manunuzi haya ya sh. 5,000/- hawana anuani halisi za makazi kutokana na ukweli kuwa utaratibu wa anuani za mitaa haujawekwa na nchi yetu, hivyo basi kifungu cha 80A(2)(d) utekelezekaji wake utakuwa ni mgumu sana kama si kutotekelezeka kabisa, jambo ambalo tunaona litasababisha kughushi nyaraka husika. Mwisho wake ni kutiwa hatiani na kifungu kipya cha 17(3).

Mheshimiwa Spika, pili kwa kuwa kuna utaratibu wa kutumia mashine za kutoa risiti (electronic fiscal receipts) ambao umekwishatangazwa kuanzishwa na TRA, hivyo basi tunadhani TRA iweke utaratibu wa kuwakopesha wafanyabiashara wadogo ambao hawana uwezo wa kununua mashine hizo ili wawe wanalipa kidogo kidogo kadiri biashara zao zitakavyokuwa zinakua.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Magari (Usajili na Uhamisho wa Miliki), Sura ya 124, vifungu vya 24(a) na 24(b) vya Jedwali la Kwanza, vinavyoongeza viwango vya ada za usajili wa magari na pikipiki, Kambi ya Upinzani haikubaliani na jambo hili kabisa kwani badala ya kumpunguzia mwananchi adha ya usafiri, ongezeko hili litazidisha gharama za bei ya nauli kwa pikipiki na bajaji na pia taxi. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inaliona ongezeko hili halileti tija katika kumsaidia mwananchi wa kawaida wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, katika mabadiliko yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148, kifungu cha 43 kinachofanya marekebisho kwenye Jedwali la Pili, kwa ujumla marekebisho hayo ni kuwanufaisha zaidi wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta za kilimo na mifugo. Kambi ya Upinzani inataka kuelewa unafuu huo unamnufaisha vipi mzalishaji (mkulima na mfugaji) ili na yeye aweze kuzalisha kwa moyo? Au Kilimo Kwanza kimekusudia kuwanufaisha wawekezaji na wafanyabiashara wa sekta hizo badala ya wakulima na wafugaji walioko vijijini?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona ingekuwa ni vyema unafauu unaopatikana kutokana na punguzo hilo au msamaha wa VAT basi mfanyabiashara katika sekta husika, nusu yake irudi kwa mkulima kama motisha ya kuzalisha zaidi. Lakini ukiacha hayo, Kambi ya Upinzani ingependa pia kuona sekta ndogo ya uvuvi pia inajumuishwa katika unafuu ili kuwanufaisha wananchi wanaoishi kando ya bahari au maziwa ambao wanajishughulisha na uvuvi kama njia ya kuendesha maisha.

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho la kulizungumzia ambalo ni muhimu sanani lile linalohusu mabadiliko yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 148, ili kutoa msamaha wa ushuru wa bidhaa za petroli kwa Kampuni za Madini zilizosaini mikataba na Serikali. Kambi ya Upinzani imeshangazwa na hatua hii kwani misamaha hii ilikuwepo na iliondolewa katika bajeti ya mwaka jana lakini sasa Serikali imeamua kuirudisha. Hoja iliyotolewa na Serikali ni kwamba inafungika na mikataba iliyosaini yaani MDA’s. Kambi ya Upinzani siyo tu kwamba inashangazwa kwamba Serikali haikuiona hoja hii wakati inafuta misamaha hii mwaka jana bali pia inashindwa kuamini kama Serikali ikidhamiria kweli inashindwaje kujadiliana na kampuni zinazohusika ili waone haja ya Watanzania pia kufaidika na sekta hii ya madini. Hivi mikataba ya MDA’s imekuwa na nguvu hata ya kulinyang’anya Bunge mamlaka yake ya kuanzisha na kufuta kodi katika nchi yetu?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa msamaha huu unasaidia Kampuni za Madini kuzalisha umeme wao kwa kutumia mafuta (kampuni zimetoa zabuni kwa kampuni binafsi za kuzalisha umeme kutoka nje), hapatakuwa na vivutio vya kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na kulifanya Shirika la TANESCO kuuza umeme wake kwa migodi ya umeme. Msamaha unaua dhana nzima ya fungamanisho la sekta ya Madini na sekta ndogo ya Umeme. Katika muundo wa gharama za Kampuni za Madini (cost structure), gharama za umeme ni asilimia 13 ya gharama za uzalishaji ambazo kwa kuwarejeshea misamaha hii sasa fedha hizi zitakwenda kwa kampuni binafsi za nje zilizopewa zabuni za kuzalisha umeme kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwengine, kwa kuwa msamaha huu hautahusisha wakandarasi wa ndani wanaofanya biashara na Kampuni za Madini (local contractors), hivyo hapatakuwa na vivutio kwa kampuni za madini kutumia wakandarasi wa ndani. Kampuni za madini zitaona ni rahisi zaidi (less costly) kufanya shughuli ya kuchimba wenyewe (owner mining). Hii itaua dhana ya fungamanisho kati ya sekta ya madini na sekta ya ujenzi (construction) ambayo ilikuwa ni madhumuni mojawapo ya Sheria mpya ya Madini iliyopitishwa na Bunge lako tukufu katika mkutano uliopita tu, ili kujibu changamoto ya fungamanisho dogo la sekta ya Madini na sekta nyingine za Uchumi (low integration of the mining to other sectors of the economy). Katika muundo wa gharama za uzalishaji kwa Kampuni za madini, takribani asilimia 30 ni gharama za kuchimba.

Mheshimiwa Spika, ili kuifanya nchi yetu na watu wake wafaidike na rasilimali za madini yaliyomo nchini na pia kuifanya sekta ya madini ichangie zaidi katika Pato la Taifa, Kambi ya Upinzani inapendekeza msamaha huu wa bidhaa za mafuta uendelezwe pia kwa kampuni za ujenzi katika migodi ambazo ni wakandarasi wa ndani (local contractors). Utafiti unaonyesha jumla ya kampuni hizo za wakandarasi wa ndani ni 7 na hivyo kuwa na uwezo wa kutoa mchango wa kutosha katika pato la nchi.

Mheshimiwa Spika, katika kuzidi kuifanya nchi inufaike na sekta ya madini na kuongeza mapato ya Serikali, Kambi ya Upinzani inaitaka pia Serikali isimamie vizuri utekelezaji wa Sheria ya Usajili wa Wakandarasi (The Contractors Registration Act) ya 1997 ambayo inataka Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (Contractors Registration Board) kusajili kampuni za nje zinazotaka kutoa huduma hapa nchini kama matawi ya kampuni zao mama zilizosajiliwa nje ya nchi badala ya kuziruhusu kujiandikisha hapa nchini kama kampuni tanzu (locally incorporated as a subsidiary company). Kumekuwa na mwanya mkubwa kwa upande wa CRB kuruhusu kampuni hizo kujisajili kama kampuni tanzu zilizosajiliwa hapa nchini na hivyo kutambuliwa kama kampuni za ndani na hivyo kuikosesha Serikali mapato kwa kukwepa kulipa kodi ya zuio (withholding tax) ya asilimia 15 wanayopaswa kulipa kama wakandarasi wa nje na badala yake kulipa kodi hiyo ya zuio kwa asilimia 5 tu wanayopaswa kulipa wakandarasi wa ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa kuruhusu ukiukwaji wa Sheria hii ya Usajili wa Wakandarasi ya 1997, Serikali inapoteza mapato mengi kutoka kwa wawekezaji wa sekta ya madini na badala yake inakimbilia kuwakamua wananchi masikini. Mfano ni kwamba ukiwa na wakandarasi 10 wa nje waliachiwa kujisajili kama wakandarsi wa ndani na hivyo kulipa kodi ya zuio ya asilimia 5 badala ya asilimia 15, na hawa kila mmoja akafanya kazi yenye gharama ya USD 30 milioni, jumla yake itakuwa ni USD 300 milioni. Wanapokwepa kulipa tofauti ya kodi ya zuio ya asilimia 10 kutoka kiasi hicho cha jumla, hiyo maana yake Tanzania imekosa mapato ya USD 30 milioni ambazo ni kiasi cha Tsh. 45 bilioni.

Mheshimiwa Spika, hiki ni kiasi kikubwa sana kwa nchi yetu kupotea hivi hivi. Ni sawa na ile hadithi ya kuruhusu kulipwa kwa midimu na mibaazi huku utajiri wa nchi ukiendelea kumalizika. Nchi yetu haimudu upotevu huu na tunazihitaji fedha hizi kwa kuziba nakisi iliyopo katika vyanzo vyetu vya mapato ya ndani.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hili pengine kuna haja pia ya Sheria hii ya Fedha kuanzisha kodi ya zuio (withholding tax) ya asilimia 15 kwa huduma za kiufundi kwa kampuni za madini zitakazofanya uchimbaji wenyewe (owner mining). Kwa kuwa wakandarasi wa ndani wanatozwa asilimia 5 ya kodi ya zuio kwa shughuli kama hizi za kiufundi, itakuwa ni rahisi (cheap) kwa kampuni za madini kutoa zabuni kwa kampuni za ndani.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa Kambi ya Upinzani inapenda kulikumbusha Bunge lako tukufu kwamba Watanzania wamechoka kuishi kwa matumaini chini ya sera zinazowakatisha tamaa za Chama Cha Mapinduzi huku wakiendelea kusota katika umasikini wakati nchi yao ni tajiri wa rasilimali zinazoweza kuanzisha vianzo vingi vya mapato badala ya kuendelea kuwakamua wao kupitia vyanzo hivyo hivyo kila mwaka vya soda na vinywaji vyengine baridi, vileo, sigara na ada za leseni za magari na pikipiki. Kambi ya Upinzani inadhani wakati umefika wa Serikali ya CCM kuacha kumkama ng’ombe ambaye sasa anatoa damu badala ya maziwa. Tuwe tayari kutumia vyanzo vyengine vya mapato ambavyo vitamnufaisha Mtanzania badala ya kuendelea kumkandamiza. Vyenginevyo, watakuwa na haki ya kutafuta mbadala utakaowaletea maisha yenye neema kwao na kwa vizazi vyao chini ya misingi ya haki sawa kwa wote na uchumi imara unaotoa ajira na tija kwa wote.

Mheshimiwa Spika, iwapo Serikali itakubali kufanya marekebisho tuliyoyapendekeza kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake, Kambi ya Upinzani itaiunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

………………………
Hamad Rashid Mohammed (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani –
Wizara ya Fedha na Uchumi.
15.06.2010

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s