Kificho: Kura ya maoni serikali ya mseto Z`bar kabla ya uchaguzi

Na Mwinyi Sadallah
19th February 2010

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, amesema kura ya maoni itakayoamua kuundwa kwa Serikali ya Mseto Zanzibar itafanyika kabla ya uchaguzi Mkuu kama ilivyoamuliwa na Wajumbe wa Baraza hilo Januari, mwaka huu.

Akizungumza na Nipashe jana Zanzibar, Spika Kificho, alisema hakuna mtu mwenye ubavu wa kubadilisha maamuzi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi zaidi ya wenyewe waliopitisha uamuzi huo.

Aliyasema hayo baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichomalizika Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, kiliamua kura ya maoni kuhusu Serikali ya Mseto ifanyike baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar.

Alisema kura hiyo ya maoni ndio itakayotoa uamuzi wa kuundwa serikali shirikishi baada ya uchaguzi mkuu iwapo wananchi watakuwa wamefikia muafaka wa kuundwa Serikali ya Mseto.

Alisema hivi karibuni atatangaza majina ya wajumbe sita watakaounda kamati ya kufuatilia utekelezaji wa hoja binafsi ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alisema kamati hiyo itakuwa na wajumbe watatu kutoka CCM na watatu kutoka CUF na ndio watakaopewa jukumu kwa niaba ya Baraza ya kufuatilia hatua za utekelezaji kabla ya wananchi kufikia hatua ya kushiriki katika kura ya maoni.

Spika Kificho alisema jambo linalosubiriwa hadi sasa ni kuwasilishwa kwa muswada wa marekebisho ya sheria utakaoipa mamlaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kusimamia suala la kura ya maoni kabla ya kufikia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani.

Hata hivyo, alisema bado ni mapema kueleza kwamba muswada huo utawasilishwa katika kikao cha Machi 24 au baadaye kwa vile bado unaendelea kutayarishwa na Mwanasheria Mkuu.

Suala la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa limefikiwa baada ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitisha hoja binafsi iliyowasilishwa na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakar.

Hata hivyo, Wajumbe wa Baraza hilo wameitaka Serikali kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuitishwe kura ya maoni, kwa vile suala hilo linahusu katiba ya Zanzibar kama ilivyoamuliwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Butiama mwaka 2008.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu na iwapo suala hilo litakubalika kupitia kura ya maoni itakuwa ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kuundwa kwa Serikali ya Mseto tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi Visiwani mwaka 1992.

SOURCE: NIPASHE

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s