Barua ya wazi kwa Mheshimiwa Rais Karume na Maalim Seif

Ninawaaandikia barua hiyo ya wazi kwa sababu nimeguswa kwa karibu sana na jinsi mijadala kufuatia mkutano wenu inavyoendelea na inavyoendelezwa. Mijadala hii imepotoshwa, ama kwa kutokuelewa au kwa makusudi. Kwa maoni yangu, swali la msingi kabisa katika hali ya Zanzibar leo ni: Je, uchaguzi mwaka huu, bila kutanguliwa na mabadiliko katika hali ya kisiasa ya Zanzibar, utakuwa wa amani, haki na huru? Na nini ifanyike ili kujenga mazingira yatakayowezesha uchaguzi wa amani, haki na huru? Nitafupisha chimbuko la matatizo ya kisiasa ya Zanzibar katika vifungu vitatu:
• Jamii ya Zanzibar kisiasa imegawanyika kati-kati, yaani ‘it is split in the middle’. Na jambo hilo limedhihirishwa katika takriban kila uchaguzi.
• Kwa hivyo, hakuna mazingira ya ushindani katika Zanzibar; badala yake kuna mazingira ya uhasama. Katika mazingira ya uhasama, haiwezekani kabisa kuwa na siasa za kishindani, ambayo ni kiini cha mfumo wa vyama vingi.
• Jitihada zote zilizochukuliwa, pamoja na miafaka miwili, hazikuzaa matunda kwa sababu mbalimbali, ambazo sinahaja kuzichambua katika barua hii. Isipokuwa sinabudi niweke wazi kwamba, kwa maoni yangu, sababu kuu ya jitihada hizi kutokuzaa matunda ni wanansiasa kuweka maslahi yao ya muda mfupi mbele ya maslahi ya taifa/jamii.
Kwa mara ya kwanza, katika kipindi cha karibu miongo miwili, maridhiano kati ya viongozi wakuu wa CCM na CUF wa Zanzibar, na sio wengine (na hili lazima lisisitizwe) imetoa kamatumaini kadogo ka uwezekano – sio uhakika – wa kutatua matatizo ya Zanzibar. Kinachotakiwa, tena bila kupoteza muda, ni kuiimarisha hatua hii iliyochukuliwa na kujenga juu yake. Na hili ifanyike kabla mijadala potofu inayoendelea haijawa sugu na kuwapotoshea malengo wananchi, hususun lengo la kuweka msingi wa amani.
Naposema mijadala potofu ninamaanisha hoja kama zifuatazo:
• Karume asiongezewe muda wala kipindi kingine cha urais. Hii ni kinyume cha katiba ya nchi na katiba/sera ya CCM.
• Katiba isichezewe kwa kubadilisha, badilisha.
• Yaliyoanzishwa na Karume, yanaweza kuendelezwa na mrithi wake.
• Huwezi kuwa na serikali ya umoja wa kimataifa bila ridhaa ya wananchi, kwa maana ya bila kuwa na kura za maoni.
Kwa hivyo, ifanyike nini:
Kama sote tunafahamu kwamba uchaguzi ujao hauwezi kufanyika katika hali ya uhasama tuliyanayo, na hali hiyo haiwezikubadilika au kubadilishwa katika muda uliobaki, basi ni wazi kwamba uchaguzi usogezwe.

Madhumuni ya kusogeza uchaguzi ni kutoa muda wa kutosha wa kuchukua hatua za awali lakini za lazima kujenga mazingira yatakayowezesha uchaguzi wa amani, haki na huru.

Kwa hivyo, kinachohitajika ni kipindi cha mpito (tuseme kama miaka miwili) kutekeleza hatua maalum, yaliyoainishwa na kukubaliwa kisheria. Kipindi hiki ni cha mpito (transitional period) kati ya mazingira ya uhasama tuliyonayo, na mazingira ya ushindani, tunayotaka.
Hatua gani ambazo ni muhimu na zinatakiwa kuzichukuliwa:
• Kuunda serikali ya umoja wa kimataifa, (sio serikali ya mseto) mara baada ya sheria ya mpito (transitional law) kupitishwa na Baraza la Wawakilishi. Bila shaka washiriki wakuu wa serikali hii watakuwa CCM na CUF.
• Kujadili na kukubaliana kuweka kikatiba vyombo huru vitakavyosimamia uchaguzi.
• Kujadili na kukubali marekebisho mengine ya kikatiba na sheria yatakayowezesha mazingira ya ushindani.
• Kujadili na kukubali, kati ya pande zote zinazohusika, marekebish ya Katiba ya Jamhuri katika vifungu vinavyohusika na muungano.
• Kuweka taratibu na ratiba ya hatua zilizikubalika kuchukuliwa.
Kwa mantiki ya hoja yangu ya kuaahirisha uchaguzi, suala ambalo linajitokeza moja kwa moja ni kwamba hatutakuwa na rais, kiongozi wa nchi na serikali, kwa kuwa rais aliyoko madarakani atakuwa amemaliza muda wake. Sasa je, nani atachukuwa nafasi ya mkuu wa nchi na kiongozi wa serikali? Kuna njia tatu:
Moja, mtu ateuliwe na Baraza la Wawakilishi kushika hatamu wakati wa mpito. Hili kwa kweli ni kinyume na hulka ya kidemokrasia na huwa haifanyika wakati wa kawaida isipokuwa tu kama kuna hali ya dharura (emergency) na Katiba imewekwa kando. Kisiasa, mteule kama huyo hatakuwa na uhalali hata kama ikikubaliwa kwamba asiwe mwanachama wa chama chochote.
Pili, Jaji Mkuu achukuwe nafasi hiyo. Ninafikiri hii pia haina mantiki kwa sababu anyetakiwa kuongoza katika kipindi hichi ni yule ambaye, kwa kiasi fulani, ana uhalali wa kisiasa. Na vyovyote vile sio vizuri kwa demokrasia kumingiza mkuu wa muhimili wa mahakama katika mambo ya kisiasa.
Tatu, ni kumongezea muda (sio kipindi kingine) rais aliyopo madarakani kuedelea wakati wa kipindi cha mpito. Hii inawezekana kisheria, na njia pekee, itakayokuwa na uhalali wa kisiasa kwa sababu (a) alichaguliwa, (b) chama chake kina wawakilishi wa kutosha katika Baraza, (c) chama kikuu cha upinzani (CUF) kimemkubali, na (d) inaelekea wananchi kwa kiasi kikubwa kimeridhia kwamba amalize kazi aliyoanza. Ni kweli, wanasiasa wenzake katika chama chake wasipendezwe na hatua hii, lakini kwa wale ambao wanajiona marais-matarajiwa, bila shaka, hawawezi wakapendezwa. Wana haraka ya kuingia ikulu!
Mwishowe, je, kitaaluma, nini ifanyike na nini inawezekana?
Baada ya makubaliano kati ya CCM na CUF, waandishi wa sheria wataanda sheria maalum ambayo inakuwa na hadhi sawa na Katiba na huitwa ‘constituent act’. Kwa hivyo Baraza la Wawakilishi wataipitisha sheria (labda nitaje jina: The Constitution (National Unity Government) (Transitional and Temporary Provisions) Act, 2010) ambayo itaorodhesha hatua zote muhimu, pamoja na kuweka muundo wa serikali ya umoja wa kimataifa. Pia, itaweka kando (suspend) vifungu vinavyohusika na uchaguzi na kipindi cha urais kwa muda wa mpito, n.k. Sheria hiyo itatamka wazi kwamba uhai wake ni wa muda wa, tuseme, miaka miwili tu na kwamba baada ya miaka miwili, itapoteza nguvu yake ya kisheria. Sinahaja kuzungumzia mambo mengine ya kitaaluma isipokuwa kusisitiza kwamba muhimu ni utashi wa kisiasa na hakuna upingamizi wowote wa kitaaluma.
Waheshimiwa, nimesema mambo haya hadharani kwa sababu mbili. Moja ni jambo lenyewe ni muhimu mno kwa wanajamii wa Zanzibar na Watanzania kwa jumla. Kamwe, hatuwezi kustahimili machafuko mengine katika nchi yetu. Pili, ni maaridhiano yenu yanatuhusu sisi sote na yasiwe ya siri wala yasichezewe kwa maslahi ya wanasiasa.
Kila la heri.
Issa Shivji
Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
15/01/2010.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s