Serikali ya Mseto yanukia Zanzibar

MAPATANO ya ghafla kati ya Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, yakihusisha kumtambua rasmi Karume, na Hamad kudai hatua hiyo inafungua makubwa zaidi, ni hatua za awali kuandaa serikali ya mseto, Raia Mwema imeelezwa.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kutoka vyama vya CCM na CUF, serikali ya mseto itaundwa ikiwa ni moja ya mkakati wa vyombo vya usalama kujipatia fursa ya kubaini kasoro na namna ya kuzifanyia kazi kwa kipindi hiki cha miezi kadhaa kabla ya Uchaguzi Mkuu, mwakani.

Mara baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani, vyama vya CCM na CUF vilikubaliana rasmi kuwa Zanzibar itakuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa serikali ya mseto, lakini sasa imebainika kuwa ni vizuri zaidi kufanyia kazi wazo hilo ili kupunguza msuguano utakaoweza kujitokeza baada ya uchaguzi mkuu.

Baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM uliofanyika kijijini Butiama, mkoani Mara, Machi, mwaka jana, CCM kimsingi ilikubali kuanzishwa kwa Serikali ya mseto lakini mvutano kati ya chama hicho na CUF ulijitokeza kwa swali kwamba lini mseto uanze.

CCM walitaka mseto uanze baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani, lakini CUF wakataka uanze sasa. Wakati mvutano huo ukiendelea kulijitokeza hoja ndani ya CCM kwamba yatafutwe maoni ya Wazanzibari wote kuhusu suala hilo kwa kuwa Zanzibar si ya CCM wala CUF pekee.

Kati ya watu wanaoamini kuwa serikali ya mseto inawezekana kuundwa Zanzibar ili kumaliza mpasuko wa kisiasa ulioibuka tangu uchaguzi wa mwanzo wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995.

Viongozi waliokwishaweka msimamo wao wazi tangu Agosti mwaka jana ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Saleh Ramadhan Ferouz, alipozungumza na moja ya magazeti ya kila siku nchini.

Mapema wiki hii, Rais Karume alikutana na Maalim Seif, Ikulu ya Zanzibar katika kikao cha faragha ambacho baada ya kukamilika, Seif alifanya mkutano wa hadhara wa wanachama wa chama chake na kuwaeleza kuwa wanamtambua rasmi Karume kwa kuwa hatua hiyo inafungua milango ya makubwa zaidi, ambayo hata hivyo hakuyataja.

Hatua ya viongozi hao imetanguliwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete alipozungumza na wananchi miezi michache iliyopita kuwa suala la ufumbuzi wa migongano ya kisiasa Zanzibar bado halijamashinda Rais Karume kiasi cha yeye kuingilia kati.

Hata hivyo, wakati hayo yakijiri hali imekuwa tete katika vyama vya CCM na CUF. Wakati CCM na hususan wahafidhina ndani ya chama hicho wakianza kuratibu mikakati ya kupinga suala hilo , CUF wanaitazama hatua ya kiongozi wao kumtambua Karume kwa hadhari kubwa baadhi wakiamini hiyo ni ‘janja’ ya CCM kuweka utulivu wa nchi hususan kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Tayari viongozi mbalimbali wa kitaifa wa vyama hivyo wameunga mkono uamuzi wa CUF kumtambua Karume. Viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, na Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye alishiriki kwenye timu ya mazungumzo ya muafaka ya makatibu wakuu wa vyama hivyo.

Suala la utatuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar lilizungumzwa na Rais Kikwete katika hotuba yake ya kuzindua Bunge, Desemba 30, mwaka 2005, akisema mgogoro wa Zanzibar unamsononesha na kuahidi kuufanyia kazi.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s