CUF yafanya maamuzi mazito

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameponea chupuchupu kupigwa na wafuasi wa chama hicho, baada ya kutangaza rasmi kumtambua Rais Amani Abeid Karume.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Kibandamaiti alisema kwamba Baraza Kuu la Uongozi limekutana na kupitisha uvamuzi wa kumtambua rasmi Rais Karume, ili kutafuta muafaka wa kumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

“Mie na Mheshimiwa Karume ndio wenye dhima la kuepusha shari, yasitokee tena matatizo na mazungumzo yetu yamelenga kuimarisha umoja na mshikamano, je, mmekubali kumtambua,” aliwahoji wafuasi wake Maalim Seif na kupokea sauti ya “hatukubali.”

Baada ya tamko hilo la kumtambua Rais Karume, wafuasi CUF walinyanyuka na kuanza kuimba “Hatumtambui hatumtambui Rais Karume,” huku wakisonga mbele ya jukwaa.

Kutokana na hali hiyo, vijana wa ulinzi wa chama hicho walianza kuwarudisha nyuma wafuasi hao, lakini hali iliendelea kuwa mbaya na Maalim Seif kulazimika kukatisha hotuba yake na kwenda kukaa katika jukwaa huku akisindikizwa na walinzi.

Baada ya Maalim Seif kusitisha hotuba Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba alipanda jukwaani na kuwataka wafuasi hao kuwa watulivu huku akiendelea kuwahutubia lakini hali iliendelea kuchafuka huku wafuasi wengine wa CUF wakianguka vilio na kuwashutumu viongozi wao kuwa ni wasaliti.

“Tumepoteza nguvu zetu tumekuwa vilema leo mnatuambia tumtambue Karume nasema hatukubali kama uongozi umekushindeni ondokeni,” walisikika baadhi ya wafuasi wakipiga kelele katika mkutano huo.

Kabla ya tukio hilo wakati akihutubia, Seif alisema hatua ya kukutana na Rais Karume ilikuja baada ya kukwama kwa mazungumzo ya muafaka hasa katika utekelezaji wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na kuwataka wafuasi wake kuunga mkono azimio hilo.

Maalim Seif alisema baada ya mazungumzo ya muafaka kukwama, Baraza Kuu la Uongozi wa CUF liliweka sharti kuwa hawako tayari kuendelea na mazungumzo hadi hapo Rais Karume atakapokuwa tayari kukutana na Maalim Seif kujadili suala hilo.

Alisema kwamba mazungumzo yao yamepata mafanikio makubwa na matunda yake yataanza kuonekana baada ya miezi sita na kuwataka wafuasi wake kuwa tayari kumtambua Rais Karume.

“Suala la kukutana na Rais Karume haukuwa uamuzi wa Seif kutoka hewani nilikwenda Ikulu kifua mbele kwa kuzingatia maslahi ya nchi yetu,” alisema maalim Seif.

Alisema Zanzibar kwa muda mrefu imepita katika misukosuko ya kisiasa ambayo yamefikia kupoteza maisha ya watu kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 na baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Awali maalim Seif aliwaeleza wafuasi wake kuwa mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kukataa njia ya mazungumzo ya kumaliza matatizo ya kisiasa ya Zanzibar.

Alisema kwamba kumbukumbu zinaonyesha Wazanzibari waliokuwa wakiishi roho juu kutokana na matatizo ya kisiasa tangu mwaka 1957 na kutoa mfano mwaka 1961 watu zaidi ya 68 walipoteza maisha kutokana na matatizo ya uchaguzi.

“Baada ya kukutana na Mheshimiwa Karume, baada ya miezi sita Zanzibar itabadilika kwa nini vijana hadi leo hii hawana kazi,” alihoji Maalim Seif.
Alisema kwamba hatua ya kukutana na rais Karume imekuja wakati muafaka kwa vile tayari viongozi wa CCM Taifa wameshawahi kusema matatizo ya Zanzibar yatatatuliwa na Wazanzibari wenyewe akiwemo Makamo Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania John Samuel Malecela.

Kufuatia vurugu hizo, Profesa Lipumba alisema suala la kumtambua Karume litajadiliwa katika vikao vya ndani ili kuwapa nafasi vijana na akinamama kabla ya kufikiwa muafaka wake.
Hata hivyo, aliwaondoa wasiwasi wafuasi wa CUF kuwa viongozi hawawezi kuwasaliti katika kutetea maslahi ya chama na iwapo itatokea hivyo wako tayari kuwajibika.

“Kumbukeni Maalim Seif amepata matatizo mengi katika kutetea maslahi ya Zanzibar kutokana na tabia yake ya kuweka mbele maslahi ya Zanzibar,” alisema Lipumba huku wafuasi wengi wakiwa hawafuatilii hotuba yake wakiendelea na wimbo wa “Karume hatumtambui Karume hatumtambui,” walisikika wafuasi wakisema.

Baada ya muda viongozi hao walianza kuondoka kwa kutumia njia za vichochoroni kuhofia kushambuliwa na wafuasi waliokuwa na jazba.

Wa kwanza kuondoka alikuwa Lipumba, huku walinzi wake wakiwa wamening’inia mbele ya gari na nyuma. Alifuatiwa na Maalim Seif kupitia njia ya kichochoroni na viongozi wengine walifuatia.

Awali Baraza Kuu la Uongozi lilikutana katika Hoteli ya Mazson Mjini Zanzibar na kupokea taarifa ya mazungumzo ya rais Karume na Seif na kupitisha azimio la kumtambua Rais Karume, ili kukaribisha mazungumzo ya pande hizo mbili ya kutafuta muafaka kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.

Hata hivyo waandishi wa habari walishindwa kuwahoji viongozi hao wa kitaifa kufuatia vurugu hizo baada ya walinzi kuwazuia wakidai kutokana na mazingira yaliyojitokeza haitokuwa muafaka wa kufanya mazungumzo nao.
Chama Cha CUF kilitangaza kutomtambua Rais Karume mwaka 2005 kwa madai uchaguzi haukuwa huru na wa haki na kuingia katika mazungumzo ya muafaka lakini walishindwa kufikia kuunda Serikali ya Mseto baada ya CCM kutaka ipigwe kura ya maoni kabla ya kufikia utekelezaji wake kwa vile suala hilo linahusu katiba ya nchi.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s