Mwakilishi akanusha uongo wa vyombo vya SMZ

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 13 OKTOBA 2009

CUF YAKANUSHA UONGO WA VYOMBO VYA HABARI VYA CCM NA SMZ

Kufuatia matangazo ya Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), kama yalivyosikikana kwenye taarifa yake ya habari ya leo ya saa 1.00 magharibi, ambayo yamedai mwakilishi wa jimbo la Gando (CUF), Mheshimiwa Said Ali Mbarouk, ameipongeza Idara ya Vitambulisho kwa utendaji kazi wake, Mhe. Mbarouk ametoa kauli ifuatayo kwa umma:

“Si kweli kabisa kwamba nimempongeza Mkurugenzi wa Vitambulisho, Bwana Mohammed Juma Ame, kwa kazi yake. Sijaona ikiwa anafanya kazi yake kwa uadilifu na kitaalamu, na hivyo hastahili pongezi za mtu mwenye heshima zake, ambaye ni mtunga sheria na ambaye anaona wazi sheria zikivunjwa na Idara inayoongozwa na Mkurugenzi Ame.

“Kile hasa nilichomwambia Mkurugenzi Ame, katika mkutano huo uliofanyika saa 4.00 asubuhi hadi saa 6.00 mchana katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Wete na kuhudhuriwa na wakuu wa wilaya za Wete na Micheweni, viongozi wa vyama vya CCM na CUF, mkuu wa Usalama wa Taifa wilaya ya Wete na yeye mwenyewe (Mkurugenzi Ame) akiwa na kundi la waandishi ‘wake’ wa habari, ni kuwa Idara yake inafanya kazi kinyume na sheria.

“Nilimpa mifano miwili kuthibitisha hilo : mmoja ni kuwatumia masheha katika utoaji wa vitambulisho vipya, ambao hawamo kwenye Sheria ya Vitambulisho. Nafasi pekee ya sheha katika suala hili ingelikuwa ni pale tu ambapo mkaazi wa shehia yake amepoteza kitambulisho hicho na akataka barua ya uthibitisho ili kuiwasilisha Polisi na Idarani. Mfano mwengine ni hatua ya upotoshaji wa Idara yake ya kulazimisha kwamba watu waende na vyeti virefu vya kuzaliwa.

“Katika mifano yote miwili, Idara yake inajua tatizo lilipo: kwenye nafasi ya masheha, inajua kuwa pamoja na kwamba si halali kisheria kuwatumia kudai kitambulisho kipya, lakini pia masheha hao hutumia ukereketwa wa kisiasa katika suala hili kama ambavyo mifano kadhaa imeendelea kuthibitisha. Kwenye suala la vyeti virefu, Idara yake inajuwa kuwa utaratibu wa kuvipata ni mrefu pia na una gharama kubwa ambazo wananchi wengi wa kawaida hawawezi kuulipia. Kwa hivyo, inapoweka vigingi hivi inafanya makusudi ili kuzuia Wazanzibari wengi wenye haki ya kuwa na vitambulisho wasiwe navyo!

“Kwa yote mawili, Mkurugenzi Ame alikiri kuwepo kwa kosa na tatizo, kwani kwa maneno yake mwenyewe ni kweli kwamba sheria haikumpa nafasi sheha wala idara yake haijapewa nguvu za kudai cheti cha kuzaliwa, lakini akasema hizo ni “kanuni za Waziri.”

“Nikiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na, hivyo, mtunga sheria, nafahamu kuwa ‘Kanuni ya Waziri’ wa Mkurugenzi Ame haitakiwi ikiuke Katiba wala Sheria na kwamba inapofanya hivyo, huo unakuwa ni ubatili mtupu. Kwa hivyo, ni wazi kuwa Mkurugenzi Ame anasimamia ubatili, na hilo si jambo la kumsifia, bali ni lawama ya kumlaumu.

“Hayo niliyabainisha kwenye mkutano huo na, angalau kwa maneno, Mkurugenzi Ame alikubaliana na lawama nilizozitoa na kuahidi kwamba angelikaa na wenzake (labda alikusudia wenzake serikalini) na kuhakikisha kuwa gharama za upatikanaji cheti zinashuka na kwamba Mrajis aliyeko Pemba anapewa nguvu na mamlaka ya kusaini vyeti ili kupunguza urefu wa muda wa kupata cheti kirefu. Kuhusu masheha, ufafanuzi pekee alioutoa ni kwamba wao (masheha) ndio wanaowajua zaidi watu wanaokaa nao.

“Kwa hivyo, kwa umma, ningependa kueleza kwamba kilichotangazwa na STZ kilikuwa ni uongo mtupu, ambao lengo lake ni kunichafulia hadhi na heshima yangu. Watu wengi wamesumbuka kunipigia simu na kutaka uhakika kutoka mdomoni mwangu mwenyewe. Nami ingawa nimejitahidi kuwafahamisha, huenda kuna wengine ambao wamesikia na ambao wangetaka kujua ukweli lakini hawawezi kunipigia simu. Taarifa hii itosheleze kuwa hakikisho la msimamo wangu.

“Kwa STZ, nimempigia simu Juma Mohammed kutoka Idara ya Habari Maelezo kumtaka asahihishe makosa hayo na aeleze ukweli. Ninawaonya wafuate maadili ya taaluma yao ya uandishi wa habari ambayo yanawataka waseme ukweli na ukweli mtupu!

“Nirudie tena msimamo wangu kwamba Idara ya Vitambulisho inayoongozwa na Mkurugenzi Ame haijafanya chochote kinachostahiki kusifiwa katika hili, kwani bado kuna maelfu ya Wazanzibari wenye sifa ambao hawana vitambulisho na ambao mtandao wa Idara hiyo na masheha unawazuia kwa makusudi wasivipate.

“Siku Mkurugenzi Ame na Idara yake watakayostahiki sifa zangu, ni pale watakapowacha vituko vyao vya makusudi na wakampa kila Mzanzibari anayestahiki kitambulisho chake cha Mzanzibari. Na hadi siku hiyo ifike, yeye na idara yake wataendelea kubeba lawama zote zinazohusiana na Wazanzibari kunyimwa haki yao ya kimsingi, ya kiraia na ya kisheria.”

Imetolewa na:

Said Ali Mbarouk (Mwakilishi wa Gando)

Simu: +255 777 411 739

Imesambazwa na:

Kurugenzi ya Habari na Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF

Simu: +255 777 414 112

cufhabari@yahoo.co.uk

http://www.hakinaumma.wordpress.com

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s