“Huu si uboreshaji wa Daftari, ni uchafuzi tu”

MAELEZO YA MKURUGENZI WA OGANAIZESHENI NA UCHAGUZI THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI) KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 29/09/2009

 

Waheshimiwa Waandishi wa Habari,

 

Naomba nianze kwa kuwashukuru nyote kwa kuitikia wito wetu na kuhudhuria katika Mkutano huu.  Nitumie fursa hii pia kuwashukuru nyinyi na vyombo vyenu kwa mashirikiano mazuri ya kuwafikishia Watanzania ujumbe wetu. Ahsanteni sana.

 

Tumewaita leo hapa kuzungumzia hali inavyoendelea katika uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) katika nchi yetu, sambamba na upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

 

Tunajua kuwa si jambo geni tena katika masikio yenu, lakini ni vyema tuelezane kila hatua kuhusu mambo haya kwa mustakabali wa Zanzibar na watu wake.

 

Waheshimiwa waandishi wa habari,

Kutokana na uhusiano uliowekwa baina ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, tunawasilisha kwenu hoja zinazohusiana na namna mazoezi haya mawili yanavyoharibiwa kwa makusudi na ushirikiano wa Idara ya Vitambulisho na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

 

Zoezi la upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi bado limegubikwa na matatizo, mazonge na mizengwe mingi toka kwa Masheha na Ofisi za Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi za wilaya. Bado wananchi wengi wanasumbuliwa kupata fomu kwa visingizio vya cheti cha kuzaliwa, malipo yasiyolingana na gharama za fomu na ukiritimba wa Masheha wa kuwazungusha na kuwapotezea watu muda ili hatimaye wachoke na wakate tama. Tunaamini lengo la mzungusho wote huo ni kuwanyima haki ili kukidhi matakwa ya Ofisi ya vitambulisho ya kudhibiti ongezeko la Takwimu ya Wazanzibari waliokwishapewa vitambulisho ambavyo ndivyo vilivyolazimishwa kuwa kigezo cha pekee kwa Mzanzibari kuweza kuitumia haki ya kuandikishwa katika DKWK.

 

 

 

Katika ofisi ya vitambulisho Gamba, Mahonda, Amani na Mwera bado kuna watu wengi ambao wamepewa fomu lakini hawapewi huduma kwa sababu tulizoeleza hapo awali.  Utaratibu uliowekwa wa kuwahudumia wananchi wa kila jimbo kwa siku mbili umewaacha kwa mamia bila kuipata huduma hiyo.  Mfano katika ofisi ya Gamba zaidi ya wananchi 1,000 wa majimbo ya Nungwi, Mkwajuni na Tumbatu wameshindwa kuhudumiwa na majimbo yao yameshamaliza kazi ya uandikishaji na, kwa hivyo, wameshapoteza haki ya kupiga kura 2010.

 

 

Waheshimiwa waandishi,

Hata wale wananchi waliofanikiwa kupata fomu kupigwa picha na kupata risiti wanapewa mwezi mmoja kufuata vitambulisho vyao vya Mzanzibari Mkaazi kinyume na tamko la Mhe. Karume la kuwataka wote wanaohusika kukamilisha mchakato wa mtu kupata kitambulisho chake ndani ya siku saba.  Hii ni nini kama sio kudharau amri ya Mkuu wa nchi.

 

Waheshimiwa waandishi,

Pamoja na chama changu kulalamikia utaratibu mbaya wa upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na kuhusishwa kwake na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura, ofisi ya vitambulisho inaendelea na zoezi la kuwapatia wananchi vitambulisho ambavyo hivi sasa hatujui idadi yake pamoja na kudai kuwa Wazanzibari zaidi ya asilimia 98 wameshapatiwa vitambulisho hivyo huku wengi kwa maelfu wakiendelea kusota katika ofisi za wilaya bila mafanikio.

 

Imani ya chama changu ni kuwa ofisi ya Vitambulisho kwa kuwatumia masheha na maofisa wake mawilayani, chini ya msaada wa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, wanafanya haya ili kudhibiti idadi ya Wazanzibari watakaopewa ZAN ID kupindukia lengo na hivyo kupingana na takwimu za uandikishaji na hivyo serikali kupata aibu na kuwa ni ushahidi wa wazi wa kukitumia kitambulisho cha Mzanzibari kwa malengo ya kisiasa.

 

Hoja ya Mkurugenzi wa vitambulisho aliyoitoa katika Kongamano la Demokrasia katika Hoteli ya Mazson’s kuwa CUF inaogopa aibu ya kuwa watu wengi waliopiga kura 2005 haitofikiwa kwa kuwa walitoka Mombasa, Tanga na Dar es Salaam, haina msingi. Misururu ya wananchi katika ofisi za wilaya inathibitisha kuwa Ofisi ya Vitambulisho ilidhamiria kuwapunguza wapiga kura wa CUF, lakini sisi tukagundua na sasa imekuwa ni aibu kwao wao. Hivi sasa, baada ya matokeo mabaya ya uboreshaji wa DKWK, makelele yetu na ya Jumuiya ya Kimataifa, wimbi la utoaji wa fomu limeongezeka, ingawa hilo halimaanishi kwamba kila mwenye fomu atapatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na hivyo kuja kuwandikishwa kuwa mpiga kura. Kuna uwezekano mkubwa watu wanaopewa fomu sasa wasipatiwe kabisa vitambulisho vyao hadi baada ya uchaguzi wa 2010, kwani tunao ushahidi wa maelfu ya watu ambao wana risiti za Idara ya Vitambulisho za tangu mwaka 2006 na ambao hadi leo hii hawajapatiwa vitambulisho vyao. Watu hao wamekuwa wakikataliwa kuwa wapiga kura na ZEC kwa kuwa ZEC haitambui risiti bali kitambulisho.

 

Huu ni mkakati ambao lengo lake ni kuwanyima kura Wazanzibari na kuwapa watu ambao hawastahili ili kuisaidia CCM 2010.

 

Waheshimiwa waandishi,

Kuhusu Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, sisi katika CUF tunaamini kuwa unaofanyika sio uboreshaji bali ni uandikishaji mpya, kwani hata wale waliopiga kura 2005 wanadaiwa ZAN ID ili waandikishwe, na bila ZAN ID hawawezi kuandikishwa. Hivyo Tume inajidanganya na kuudanganya umma.  Kinachofanyika ni uandikishaji mpya uliopewa jina la Uboreshaji.

 

 Fomu 2MP kwa ajili ya watu waliopoteza shahada ya kura ya mwaka 2005 zinatumika bila utaratibu kuwaandikisha watu wapya waliokosa katika siku (2) za mwanzo za uandikishaji kwa kisingizio cha kupoteza shahada ya 2005 kwa msaada wa watendaji wa Tume wasio waaminifu katika vituo na kiburi wanachopewa na Tume cha kuwatisha Mawakala wetu hasa wanapogundua udanganyifu huo.

 

Katika kituo cha Pitanazako umefanyika mchezo huo na wakala wetu alipohoji ametishiwa kutolewa kituoni na baadae amepata simu ya wito kutoka Wizara ya Elimu na alipoitikia wito huo amepewa barua ya kusimamishwa kazi kwa kuwa eti amejihusisha na siasa.

 

Ni watendaji wangapi wa Serikali wanachama wa CCM, walimu, usalama wa taifa na wengine wengi wanaojihusisha na kazi za uandikishaji na Serikali haichukui hatua? Iweje kwa mwalimu huyu aliyeamua kukitumikia chama chake wakati  yuko likizo na uandikishaji wa shehia yake ulimalizika tarehe 27/9/09. 

 

Katika kituo cha Nungwi Msimamizi ametoa fomu tano (5) kwa watu ambao hawakuandikishwa 2005. Tumeripoti suala hili kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa wilaya, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

 

 

Waheshimiwa waandishi,

Tatizo jengine ni la uhamishaji wa vituo bila taarifa. ZEC kwa makusudi inahamisha vituo bila taarifa ili kuwazonga na kuwasumbua wananchi kwa kisingizio cha kutishiwa usalama wao.  Hii si sababu nzito, kwani serikali inalilinda Daftari hili batili kwa nguvu zote za Dola.  Mfano wakati wa uandikishaji wa Jimbo la Tumbe, vituo vya Shumba Viamboni vilihamishiwa Sizini bila taarifa yoyote kwa umma na matokeo yake ikawa ni kuwatesa wananchi.

 

Hivi sasa katika Jimbo la Mtambwe vituo vyote vimehamishiwa katika Skuli ya Daya bila taarifa yoyote.  Masafa ya kutoka Mtambwe Kaskazini hadi Mtambwe Kusini ni zaidi ya kilomita 8. ZEC inafanya kwa makusudi kuwatesa wananchi hasa Pemba ili kudhoofisha nguvu ya CUF ili kupata nafasi ya kuandikisha mamluki kwa nguvu. Mbona hawahamishi vituo katika shehia za Unguja ambako baadhi ya vituo hajaandikishwa hata mtu mmoja kwa muda wa siku zote saba (7), kuna nini hapa?

 

Waheshimiwa waandishi,

ZEC imewafundisha Wasimamizi wa vituo kuwa wafedhuli dhidi ya Mawakala wa CUF na viongozi wao (Waangalizi) kwani wanawatolea maneno machafu, dharau na kejeli, kuwatisha na kuwazuia kuhoji, kuuliza, kuandika chochote hata pale wakala anapogundua kuwa sheria na kanuni zinapindishwa kituoni. Mfano katika kituo cha Pale Jimbo la Tumbatu, Msimaizi wa kituo pamoja na Sheha walimsumbua sana wakala wetu alipohoji uhalali wa mtu wa Donge anayemjua kutaka kujiandikisha katika kituo cha Pale, jimbo la Tumbatu.

 

Wakala wetu wa Pitanazako niliyemtaja hapo juu baada ya kugundua udanganyifu wa matumizi mabaya ya fomu 2MP, yaliyomkuta ni kusimamishwa kazi. Haya yote tumemripotia Mkurugenzi wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ lakini hakuna hatua zozote wala mabadiliko vituoni.

 

Waheshimiwa waandishi,

ZEC imeamua kuzuia kutoa vitambulisho vya Waangalizi kwa viongozi wa chama chetu kwa kisingizio cha kurejeshwa vitambulisho vya Waangalizi wa majimbo yaliyokwishaandikishwa, mfano wamekataa kutoa vitambulisho vya Waangalizi wa Wete na Mtambwe eti kwa sababu Mh. Hamad Masoud na wenziwe wa Ole na Tumbe hawajarejesha vitambulisho walivyokuwa wamepewa.

 

Hii si hoja ya maana kwani ratiba ya uandikishaji inaonyesha ni majimbo gani yanafuata baada ya Ole na Tumbe na vitambulisho vyao vinaonyesha muda wa mwisho wa matumizi.  Kuwanyima vitambulisho Waangalizi wetu wa Wete na Mtambwe ni katika mkakati wa ZEC, CCM na SMZ wa kudhoofisha nguvu ya CUF ya kugundua maovu.

Waheshimiwa Waandishi,

Kwa haya yote tuliyoyataja na mengine ambayo kutokana na ufinyu wa wakati hatukuweza kuyawasilisha hapa, sisi wa Chama cha Wananchi (CUF) tunarejea msimamo wetu kama ifuatavyo:

 

Kwanza, huu unaoitwa uboreshaji wa DKWK ambao tumethibitisha kwamba ni uandikishaji mpya, usitishwe mara moja ili kutoa tena nafasi kwa Idara ya Vitambulisho kuwapa Wazanzibari wote wanaostahiki. Idara ya Vitambulisho itumie muda wote uliobakia wa mwaka huu kuhakikisha kuwa kila Mzanzibari aliyefikia umri anapata kitambulisho. Serikali pia itumie muda huu kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watu wote ambao hawana vyeti hivyo.

 

Pili, kwa kuwa tuna mashaka kwa namna vitambulisho vya Uzanzibari Mkaazi vinavyotolewa, lazima vitambulisho hivyo vihakikiwe na wahakiki huru na kwamba sote tujiridhishe kwamba kweli waliopewa ndio hasa wanaostahiki.

 

Tatu, sambamba na uhakiki wa ZAN ID, pia DKWK nalo lifanyiwe uhakiki na taasisi huru.

 

Nne, tunatangaza rasmi kuwa Daftari hili lililopo sasa ni chafu, halifai na halistahiki kuwa ndicho kigezo cha kuendesha uchaguzi ulio huru, wazi na wa haki.

 

 

HAKI SAWA KWA WOTE

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s