SMZ yaendeleza ukaidi

Na Mwinyi Sadalla, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imekataa wazo la Chama cha Wananchi (CUF) la kutaka uandikishaji wapigakura usitishe na kuundwa tume ya kuchunguza madai ya wananchi kutopewa vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi.

Wazo hilo lilitolewa baada ya maelfu ya wananchi kulalamika kuwa wanakataliwa kuandikishwa kwa kukosa vitambulisho hivyo ambavyo ni sharti kwa kila mtu kuandikishwa kuwa mpigakura.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alisema serikali haiko tayari kusitisha uandikishaji kwani imejiridhisha kuwa wananchi wengi wanavyo vitambulisho hivyo.

Hamza alisema kusitisha uandikishaji wapigakura, kutaathiri ratiba ya hatua za uchaguzi na hivyo kuja kusababisha matatizo makubwa baadaye.

Uchaguzi mkuu wa Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani, unatarajiwa kufanyika Oktoba, mwakani ambapo Wazanzibari watamchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wabunge.

Waziri alisema msimamo unaotolewa na CUF hauwezi kutekelezwa kwa sasa kwa vile umelenga kuchelewesha utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Uchaguzi (ZEC), wakati idadi kubwa ya wananchi tayari wanazo sifa za kuandikishwa katika daftari hilo .

Alisema masuala ya uchaguzi huenda kwa kalenda na kuzingatia katiba ya nchi kwa vile hivi sasa umebakia mwaka mmoja kabla kufanyika uchaguzi mkuu.

Aliongeza kuwa zoezi la uandikishaji litaendelea katika awamu ya pili na ya tatu basi wale ambao hawajapata vitambulisho vya ukaazi wakamilishe taratibu ili waandikishwe katika awamu zinazofuata.

Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema kama serikali inasisitiza kuwa imetoa vitambulisho vya kutosha kwa wananchi, basi inafaa watu wote waitwe kwa majina kwa kila kitambulisho kilichotolewa.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali, amesema uandikishaji unaendelea vizuri kisiwani Pemba ikilinganishwa na siku za mwanzo.

Alisema amethibitisha hali hiyo baada ya kutembelea vituo mbalimbali vya uandikishaji Pemba na kuongeza kwamba hakuna sababu ya kuahirisha zoezi hilo wakati wananchi wanajitokeza vituoni.

Naye Mbunge wa Mkanyageni Pemba, Mohamed Habibu Mnyaa, amesema matatizo ya umasikini yamesababisha wananchi wengi kisiwani Pemba kutopata vitambulisho vya ukaazi.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi, amesema anamuachia Mwenyezi Mungu aliyehusika kuchoma nyumba yake eneo la Mlandege, mjini hapa juzi usiku.

Kamanda Bugi alisema amesikitishwa na tukio hilo ambalo alijulishwa na wanafamilia wake usiku wa manane Jumanne muda mfupi baada ya moto huo kugundulika. Alisema ndani ya nyumba yake, kulikuwa na watu 11, akiwemo mkewe wa kwanza na watoto wao, pamoja na watoto wa mjomba wake.

Alisema hawezi kufikiria ni maafa kiasi gani yangetokea iwapo nyumba hiyo ingeteketea yote kwa moto.

Alisema kwamba katika maisha yake hana ugomvi na mtu yeyote na amekuwa akiishi kwa mashirikiano makubwa na makundi ya aina mbalimbali katika jamii.

“Sijawahi kugombana na mtu na katika maisha yangu nimekuwa nikishirikiana na watu wa matabaka tofauti ndio maana naona nimwachie Mwenyezi Mungu mwenyewe suala hili,” alisema Bugi.

“Mwenyezi Mungu aliyetuumba ndiye atakayemfichua mtu aliyefanya jaribio la kuteketeza familia yangu,” aliongeza Kamanda Bugi alipoulizwa kama anadhani kuna mtu anamshuku kuhusika na tukio hilo . Alisema kitendo cha Polisi kudhibiti watu walioonekana mara baada ya tukio hilo ni jambo la kushukuriwa, kwa vile iwapo moto huo usingewahiwa ungeweza kuleta maafa makubwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Khatib Shaaban, alisema hadi jana hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

CHANZO: NIPASHE 18 Septemba 2009

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s