Vurugu Zanzibar: Maalim Seif akunjua makucha tena

Na Asha Bani

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameibuka tena na kukishambulia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali zake mbili, kwa kuendelea kufanya kile alichokiita ni kuchochea vurugu Zanzibar na hususan katika Kisiwa cha Pemba.

Maalim Seif, mwanasiasa mwenye nguvu katika visiwa vya Unguja na Pemba, aliyasema hayo jana wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Akifafanua, Maalim Seif aliyeitisha mkutano huo wa waandishi kuelezea kuhusu matukio ya mapambano ya silaha za moto kati ya wananchi na vyombo vya dola Zanzibar, yanayoendelea visiwani humo hivi sasa, alisema hali hiyo ni matokeo ya kile alichokiita njama ovu za kupunguza kura za CUF wakati wa uchaguzi ujao.

‘‘Ukweli unabaki pale pale kwamba, chanzo na sababu za mgogoro uliopo ni njama ovu za CCM na serikali zake kuwazuia wananchi wengi wa Zanzibar wenye sifa za kujiandikisha kuwa wapiga kura, na ambao wanasadikiwa kuwa wanaunga mkono CUF wasiweze kujiandikisha, lengo likiwa ni kupunguza kura za upinzani,” alisema Maalim Seif ambaye alitoa matamshi ya kwanza mazito ya namna hiyo Aprili, mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, Maalim Seif aliwataka wananchi wa Zanzibar kukaza uzi ili kuhakikisha wanatetea haki yao ya kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Sambamba na hilo, Maalim Seif pia ameitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kusitisha mara moja zoezi la uandikishaji wapiga kura hadi wananchi wenye sifa watakapopatiwa vitambulisho vya kudumu vya mkaazi, vinavyowawezesha kuandikishwa kwenye daftari hilo.

“Wananchi wa Zanzibar, CUF iko pamoja na nanyi, msikate tamaa, endeleeni kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa amani, najua kwa vyovyote vile umma utashinda ingawa wanatumia nguvu za dola kuwaumiza na kuwaangamiza wananchi,” alisema.

Aliwahakikishia wananchi hao kuwa, chama hicho kipo pamoja na wananchi hao katika mapambano yao ya kupigania haki zao kwa njia za amani.

Alisema chama chake kinawapongeza wananchi wa kisiwani Pemba, kwa msimamo wao thabiti wanaoonyesha, kukataa kuendelea kudhulumiwa haki zao ambazo zimekuwa zikiporwa tangu uchaguzi wa mwaka 1995, 2000 hadi 2005.

Maalim Seif ambaye amekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF katika chaguzi kuu tatu zilizopita, alisema wanatambua mateso wanayopata wananchi wa Zanzibar kutoka kwa watawala aliowaita madhalimu, wasiojali haki za raia.

“CUF inatoa wito wa kutoyumba, bali msimame kidete kuwaambia watawala wakandamizaji wa chama tawala kuwa imetosha, tunawahakikishia kuwa nguvu ya umma itaishinda dola kandamizaji, njia hiyo wamepita wananchi wa nchi nyingine duniani,” alisema Maalim Seif.

Mbali ya hayo, Maalim Seif alisema kumekuwapo na mpango wa kuwakamata viongozi wa juu wa CUF na kuwabambikizia kesi ili kuficha ukweli wa nini kinachotokea visiwani humo.

Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema pia kwamba, mbali ya kuwapo kwa njama hizo za kuwakamata, pia kumekuwapo na mipango ya kufanya hujuma nyingine za kuwachomea nyumba wana CUF.

Aidha, alisema njama nyingine za namna hiyo ni kama zile za kuvamiwa kwa mawakala wa CUF katika nyumba zao na kuwapiga nyakati za usiku.

Pasipo kutoa ufafanuzi, Maalim Seif alilaumu kitendo cha CCM na serikali zake kuamua kuwatumia wale aliowaita waandishi mamluki kwenda Zanzibar na kuandika habari za upotoshaji kuhusu maendeleo ya kazi ya uandikishaji wapiga kura.

Mwanasiasa huyo pia alimtaka Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha anaondoa jeshi alilodai linawaangamiza wananchi, na hata kuwasababishia maafa na hasara kama ile ya kupotezea mali zao kutokana na nyumba zao kuchomwa moto.

“Rais Kikwete ndiye Amiri Jeshi Mkuu, anatakiwa kuhakikisha kuwa anaondoa jeshi na kuwaacha wananchi wakidai haki kwa amani na utulivu hadi itakapopatikana,” alisisitiza Maalim Seif.

Alisema anashangazwa na uamuzi wa serikali kupeleka jeshi lenye vifaru vya kivita na silaha nyingine za moto Zanzibar kwa gharama za walipa kodi.

Aidha, alisema kumekuwa na jitihada kubwa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kuficha ukweli wa chanzo cha mgogoro huo, kwa kudai kuwa wananchi ndio chanzo cha vurugu hizo huku wakijua si kweli.

Maalim Seif aliendelea kutilia mkazo kuwa, ZEC inajitahidi kufanya hivyo ili kupunguza wapiga kura wa Zanzibar na kuwaleta wa bara ambao alidai wameandaliwa na CCM ili kuongeza idadi ya kura katika chama hicho ambacho alidai kuwa Zanzibar hakitakiwi.

Alisema njama na upotoshwaji huo kwa pamoja zinatekelezwa na Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi, ZEC na kuratibiwa na Idara ya Usalama wa Taifa, wakitumia maofisa wao wa ngazi za juu, akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho Visiwani, maofisa watendaji wa Sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi.

“Viongozi hao kwa pamoja wameshirikiana katika kuingiza sheria ya uchaguzi ya Zanzibar, sharti linalokwenda kinyume na ibara ya saba ya katiba kisiwani humo, na kwamba mtu anayekwenda kujiandikisha ni lazima awe na kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi, wakihakikisha kuwa wastani wa Wazanzibar 175,000 wenye sifa zote kikatiba, hawapewi vitambulisho na kuwazuia kutojiandikisha,” alisema Maalim Seif.

Kutokana na machafuko hayo yanayotokea Zanzibar, Maalim Seif aliziomba nchi za Jumuia ya Madola kuingilia kati ili kusimamia haki za wananchi wa Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha wote wenye sifa, wanaandikishwa na kupata vitambulisho vya mkaazi.

Tangu kuanza kwa zoezi la uandikishwaji wa daftari la kudumu, wanachi wa Jimbo la Ole, kisiwani Pemba, walikuwa wa kwanza kukataa uandikishwaji na kusababisha ZEC kusitisha zoezi hilo baada ya wengi kuachwa kwa madai ya kukosa vitambulisho vya mkaazi.

Katika hatua nyingine, Ubalozi wa Marekani nchini, umesema hauhusiki kwa namna yoyote katika matukio ya vurugu yanayoendelea visiwani humo.

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), Hamza Hassan Juma, kuishutumu Marekani kuwa inahusika na mzozo unaoendelea katika visiwa hivyo, hasa baada ya kuwataarifu raia wake kutokwenda kisiwani huko.

Msemaji wa ubalozi huo, Dk. Ilya Levin, jana alilieleza Tanzania Daima kuwa, wao walitoa onyo kwa wananchi wake kutokana na taarifa za SMZ kueleza kwamba hali haikuwa shwari Visiwani.

“Tunachoweza kusema tena ni kwamba, onyo kwa raia wetu kuwa makini wakati wanapozuru Zanzibar lilitolewa kwa sababu Marekani inayo wajibu wa kuwalinda raia wake,” alisisitiza msemaji huyo.

Marekani inatoa tamko hilo wakati tayari nchi 14 wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani zimeshaitaka SMZ kushughulikia matatizo yaliyojitokeza kwenye kazi ya uandikishaji wapiga kura ili kuufanya uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki.

Tatizo kubwa linalopingwa na wananchi wa Zanzibar ni matumizi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kama ndiyo sifa kuu ya mtu kuandikishwa.

Chanzo: Tanzania Daima, 19 Septemba 2009

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s