Tamko la Maalim Seif kuhusu hali ya Pemba

MAELEZO YA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA WANANCHI (CUF), MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI, 16 SEPTEMBA, 2009

Waheshimiwa Waandishi wa Habari,

Nawashukuru nyote kwa kuitikia wito wetu na kuja kujumuika nasi katika mkutano huu wa waandishi wa habari ambao ni wa pili kuuitisha mimi tokea kuanza kwa kile kinachoitwa uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar tarehe 6 Julai, 2009.

Kwa niaba ya Chama Cha Wananchi (CUF) na kwa niaba yangu binafsi, naomba pia niwashukuru nyote pamoja na vyombo vya habari mnavyoviwakilisha kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwafahamisha Watanzania na ulimwengu kwa jumla yale yanayotendwa katika visiwa vya Unguja na Pemba katika kipindi hiki cha uendelezwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Bila ya kutekeleza wajibu wenu wa kuripoti ukweli wa yale yanayotokea, Watanzania na ulimwengu usingelijua udhalimu unaofanywa na CCM na Serikali zake dhidi ya wananchi wasio na hatia ambao kosa lao pekee ni kudai haki yao ya kidemokrasia na ya kikatiba ya kuandikishwa kuwa wapiga kura. Tunawashukuru sana kwa uzalendo wenu huo.

Mtakumbuka nilifanya mkutano nanyi tarehe 08 Agosti, 2009 ambapo niliwaeleza juu ya njama zilizoandaliwa za kulivuruga Daftari hilo zikishirikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika kipindi chote hiki yanathibitisha yale yote niliyowaeleza katika mkutano ule.

Leo hii basi nimeona kuna haja ya kuzungumza nanyi tena ili kuwaeleza wananchi wapenda amani na utulivu wa Tanzania na ulimwengu kwa jumla kile kinachoendelea kufanyika Zanzibar na mwisho kutafakari hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuinusuru hali isiendelee kuzorota.

MSIMAMO WA WANANCHI

Kumekuwa na jitihada kubwa za CCM na Serikali zake kujaribu kuficha ukweli wa chanzo na sababu za mgogoro uliopo. Imefika hatua ya baadhi ya waandishi mamluki kukodiwa na kupelekwa Pemba ili kupotosha ukweli wa kile kinachofanywa na Serikali za CCM dhidi ya wananchi na badala yake kujaribu kuonyesha kwamba eti wananchi hao wanafanya vurugu.

Ukweli unabaki pale pale kwamba chanzo na sababu za mgogoro uliopo ni njama ovu kabisa za CCM na Serikali zake kuwazuia wananchi wengi wa Zanzibar wenye sifa zote za kujiandikisha kuwa wapiga kura na ambao wanasadikiwa kuwa wanaunga mkono CUF wasiweze kujiandikisha, lengo likiwa ni kupunguza kura za upinzani. Sambamba na hilo, njama hizo zinahusisha kutumia idadi hiyo ya wapiga kura halali inayopunguzwa kwa kuwajaza watu wasio na sifa ambao ni pamoja na watu wanaoletwa maalum kutoka Tanzania Bara kuja kuandikishwa na baadaye kuipigia kura CCM, vijana malum walioandaliwa na CCM (maarufu kama Janjaweed) waliosajiliwa na chama hicho na baadaye kupelekwa kuandikishwa zaidi ya mara moja katika majimbo tofauti ya uchaguzi, na watoto wadogo wa umri wa chini ya miaka 18.

Njama hizi zinatekelezwa kwa pamoja na Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na zinaratibiwa na Idara ya Usalama wa Taifa wakiwatumia maofisa wao wa ngazi za juu ambao ni pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame, na sehemu kubwa ya maofisa na watendaji wa Sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salim Kassim Ali.

Kilichofanyika ni kuingiza katika Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar sharti linalokwenda kinyume na Ibara ya 7 ya Katiba ya Zanzibar kwamba kila mtu anayekwenda kujiandikisha ni lazima awe na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi huku wakihakikisha kuwa wastani wa Wazanzibari 175,000 wenye sifa zote za kikatiba hawapewi vitambulisho hivyo na kwa hivyo kuwazuia wasiweze kujiandikisha. Wakati huo huo, watu wengine wasio na sifa kwa idadi kama hiyo wamepatiwa vitambulisho hivyo ili kujaza pengo hilo na hivyo kujiongezea wapiga kura mamluki wengi watakaohakikisha ushindi haramu wa CCM katika chaguzi zote zijazo kwa kutumia Daftari la Kudumu linaloandaliwa sasa.

Njama hizo zimejulikana na wananchi na ndiyo maana wameamua kutumia njia za amani kupinga mpango huo muovu. Msimamo huo thabiti wa wananchi unaonekanwa na CCM na Serikali zake kuwa umefichua aibu wanayojaribu kuificha, na hasira zinazotokana na kufedheheka kwao ndiyo zinazopelekea kutumia nguvu za kupindukia mipaka kuwatesa wananchi hao wakidhani wataogopa na kurudi nyuma. Ni mfano wa mbinu zile zile zinazotumiwa na madikteta ulimwenguni kujaribu kuwanyamazisha wananchi wanaokataa kuonewa na nkukandamizwa.

Chama Cha Wananchi (CUF) kinawapongeza sana wananchi kwa msimamo wao thabiti wanaouonyesha kukataa kuendelea kudhulumiwa haki zao ambazo zimekuwa zikiporwa tokea katika chaguzi za 1995, 2000 na 2005. Tunajua wanapatishwa mateso makubwa na watawala madhalimu wasiowajali raia zao lakini hiyo ndiyo gharama ya kudai haki zao. Tunatoa wito kwamba wasiyumbe na wasimame kidete kuwaambia watawala wakandamizaji wa CCM kwamba imetosha, sasa basi! Tunawahakikishia kwamba nguvu ya umma itaishinda dola kandamizaji. Njia tunayopita pia wamepita wananchi wa nchi nyengine waliokandamizwa na kunyimwa haki zao lakini waliweza kuhimili na mwishowe walishinda. Na wananchi wapenda haki na demokrasia wa Zanzibar na Tanzania watashinda tu.

MATUMIZI YA VITISHO NA NGUVU ZA KIJESHI DHIDI YA RAIA

Inasikitisha kwamba wakati wananchi wanatumia njia za amani kudai haki zao za kiraia, vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano na vile vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vimekubali kutumiwa kufanya kazi ya CCM ya kuwanyanyasa na kuwakandamiza wananchi hao. Nguvu kubwa ya kijeshi vikiwemo vifaru vya kivita vimepelekwa visiwani Zanzibar kwenda kukabiliana na raia wanyonge wasio na hatia.

Inasikitisha kwamba silaha nzito nzito za moto zilizonunuliwa kwa fedha za walipa kodi wananchi masikini wa Tanzania ili kuihami nchi yetu dhidi ya uvamizi kutoka nje au wahalifu, leo hii zinatumika dhidi ya walipa kodi hao masikini wasio na hatia yoyote.

Watu kadhaa wamepigwa, kukamatwa na kuwekwa ndani katika zoezi hili. Wananchi wakiwemo wanawake waja wazito na watoto wachanga wanapigwa mabomu ya machozi mfululizo na kumwagiwa maji ya kuwasha ili wasithubutu kudai haki zao. Wengine wameshaathirika na hata kulazwa hospitali kutokana na athari hizi. Nyombo kadhaa hapo jana zimechomwa moto kutokana na fukuto la mabomu ya machozi lililowasha mapaa ya makuti na hatimaye moto wake kuenea na kuunguza nyumba hizo. Hata risasi za moto zimeshapigwa hewani na kwa jinsi mambo yanavyokwenda na kumbukumbu za matukio ya nyuma zinavyoonyesha haitashangaza iwapo zitatumika dhidi ya raia. Nyote mnashuhudia hali hii kupitia taarifa zinazoonyeshwa na kurushwa na vituo vya televisheni vya hapa nchini. Uandikishaji wa wapiga kura ambayo ni shughuli ya kiraia imegeuzwa zoezi la kijeshi. Halafu watawala wetu wanaimba nyimbo za kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki.

Chama Cha Wananchi (CUF) kinalaani kwa nguvu zote matumizi haya ya nguvu kubwa ya kupindukia mipaka ya vikosi vya ulinzi na usalama katika shughuli ya kiraia. Tunamtaka Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete kuacha kuruhusu vikosi vyake kuwakandamiza na kuwatesa raia wasio na hatia. Na pia tunatoa wito kwa taasisi za kutetea haki za binadamu za ndani na nje ya nchi na jumuiya ya kimataifa kuingilia kati hali hii na kupeleka wachunguzi wake visiwani Pemba na Unguja ili kutathmini hali na kuchukua hatua zianzofaa kulinda haki za binadamu za Wazanzibari.

VITISHO KWA WAANDISHI WA HABARI

Mbali ya wananchi wanyonge, kipindi hiki pia kimeshuhudia vitisho na kutishiwa usalama na maisha ya waandishi wa habari walioko kazini na ambao wanafuatilia shughuli za uendelezwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hususan kisiwani Pemba. Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salim Kassim Ali, alimtishia mwandishi Muhibu Said wa IPP Media kuwa atamchomea nyumba yake kama zinavyochomwa nyuma za Masheha. Waandishi wengine pia walioko Pemba wamekuwa wakikumbana na vitisho mbali mbali katika utekelezaji wa kazi zao.

Chama Cha Wananchi (CUF) kinalaani vitisho hivyo na kinazitaka Serikali zote mbili na vyombo vya dola kuheshimu haki ya waandishi kufanya kazi zao bila ya bughudha au vitisho.

UTAWALA KUINGILIA TUME

Katika kipindi chote hiki, tumeshuhudia pia viongozi wa Serikali (Utawala) hasa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame, na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wakiingilia shughuli za Tume hadi kufikia kutoa matamko na maagizo na kutolea ufafanuzi mambo ambayo yangepaswa kutolewa na Tume.

Hali hii ililalamikiwa hata na Tume ya Uchaguzi iliyomaliza muda wake katika Taarifa yao Rasmi ya Kazi na inaonekana kuendelea katika Tume hii bila ya Tumne yenyewe kuikemea.

CUF tunawataka viongozi hao wa Serikali kuacha kuingilia kazi za Tume na pia tunaitaka Tume iakatae kuingiliwa iwapo kweli inataka iaminiwe kama ni Tume huru.

MIPANGO YA VURUGU NA NJAMA ZA KUWAKAMATA VIONGOZI WA CUF

Wakati haya yakiendelea, kumekuwa na majaribio ya kufanya hujuma za kuchoma moto nyumba za wana-CUF na wana-CCM na pia kuvamiwa mawakala wa CUF katika nyumba zao na kupigwa usiku wa manane. Mojawapo ya matukio hayo liliongozwa na AFisa Tawala wa Wilaya ya Wete, Khamis Silima Juma.

Tuna wasiwasi kwamba hujuma hizi zinafanywa kwa makusudi ili kuongeza joto la kisiasa na hatimaye kufanikisha mipango inayozungumzwa kwa muda sasa ya kutaka kuwakamata viongozi wa CUF na kuwabambikizia kesi. Njama hizi hazitosaidia chochote zaidi ya kuifanya hali kuwa mbaya zaidi na ni vyema Serikali za CCM zikajifunza kutokana na matendo kama hayo waliyoyafanya huko nyuma.

WITO WETU

Hali inayoendelea katika zoezi la uendelezwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura si nzuri na hatua zinapaswa kuchukuliwa kurekebisha mambo. Mimi nilimuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kumsihi asitishe zoezi hilo mpaka hapo atakapojiridhisha kwamba zile sababu zilizopelekea kukwama hapo awali zimepatiwa ufumbuzi. Kutokana na hali iliyopo CUF inatoa wito kwa

1. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kusitisha zoezi hili mpaka hapo wananchi wote wenye sifa watakapopatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ili waweze kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

2. Serikali ama iharakihe mpango wa kuwapatia Wazanzibari wote wakaazi vitambulisho vyao au iliondoshe sharti la kuwa na kitambulisho hicho katika uandikishaji.

3. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zichukue hatua za kurejesha hali ya amani na utengamano kwa kushirikiana na wananchi badala ya kupambana na wananchi wake wenyewe wanaodai haki zao kwa njia ya amani.

4. Taasisi za kiraia na zile za haki za binadamu hapa nchini kuingilia kati hali hii na kutetea haki za Wazanzibari.

5. Jumuiya ya Kimataifa iingilie kati suala hili na kuona haki inatendeka na amani inadumu.

6. CUF inalaani matumizi yote ya nguvu kutoka kwa yeyote na inawataka wanachama na wapenzi wake na Wazanzibari wote kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu na wasijibu vitendo vya uchokozi na badala yake waendelee kudai haki zao kwa njia za amani na utulivu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s