Karume endelea kutusukia bomu la 2010, ila utabeba lawama

Na Ally Saleh

Kule kwetu Pemba, japo mie sio kindakindaki lakini najiitakidi kuwa ni Mpemba, kuna neno moja linalooitwa “kujipumbaza” ambalo husishwa na mtu kujua kitu halafu kujifanya kama hajui kwa dharua, bezo au kedi tu.

Nataka nilihusishe neno hili moja kwa moja na tabia ya Rais Amani Karume juu ya suala la vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN-ID) ambavyo kwa sasa vimekuwa kesi kubwa katika suala la uandikishaji wa Daftari la Kuduma la Wapiga Kura (DKWK) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2010 (UM2010).

Karume anajua kwa undani juu ya tatizo la ZAN-ID tokea kipindi hiki zilipoanzwa kuhusishwa na uandikishwaji wa kupiga kura, lakini amekuwa akijipumbaza na kutoa kauli ambazo yeye kama Rais hazimuwajibikii hata kidogo na hazisaidii kulimaliza tatizo hilo zaidi ya kutengeneza bomu litalokuja kuripuka 2010.

Lakini pengine uzi wa bomu hilo unaweza ukawa unauungua kwa haraka zaidi na maripuzi yake yasifike 2010 bali kwa mtizamo wangu linaweza kuripuka pale uandikishaji DKWK litapofikia Mkoa wa Mjini Magharibi lakini hasa katika majimbo ya Wilaya ya Mjini.

Dalili kuwa bomu analotengeneza Karume kwa kushindwa kuchukua nafasi yake kama Rais ziko wazi hivi sasa. Anafanya hivyo kwa sababu analitizama zoezi hilo kwa macho ya chama chake yaani kutengeneza mazingira ili CCM ipate ushindi kwa njia ya kuandikishwa wanaodhaniwa kuwa ni wanachama wachacheau ambao watapigia kura upinzani.

Kukwama uandikishaji hatua ya kwanza na kukwama tena hivi sasa zoezi hilo lilipoanza kurejewa, ni kauli ya wananchi kuwa hajatimiza wajibu wake kama Rais au anajipumbaza. Ni kauli kuwa hawatakubali tena, na umma unapofika hapo, hata ikiwa ni sehemu ndogo tu, basi kuna hatari.

Ni wazi Karume anajua kuwa tatizo lilipo na kama halijui basi leo nitamuambia na kama hatanielewa niko tayari anikaribishe Ikulu nimfahamishe kadri ya ninavyolijua ili pengine apate mawazo nje ya watu waliozunguka ambao pengine wanamnyima taarifa sahihi.

Siamini kuwa Karume hajui kuwa kuna maelfu ya Wazanzibari hawana vitambulisho vya Mzanzibari ambapo maelfu hayo yamegawika katika mikoa, wilaya, majimbo hadi katika shehia. Anajua fika hilo, na kama atapata mawazo nje ya watu waliomzunguka, basi ataambiwa.

Na maelfu hayo anajua kuwa yamepatikana kwa vile Idara ya Vitambulisho haikufanya wajibu wake kama ilivyohitajika kugawa vitambulisho kwa vijana walioanza kutimiza miaka 18 hapo 2006, wakachanganyika na wa 2007, na wa 2008 na hawa wa sasa wa 2009.

Idara ya Vitambulisho laiti ingekuwa na program nzuri na ya dhati, na hapa napenda nisisitize neno dhati, maana kwa hali nyingi inaonekana kuwa chanzo cha tatizo lote ni Idara hiyo kukosa udhati, ama iwe ni kwa hiari yake, shindikizo au ushaiwishi.

Kisha pia kuna wale ambao walipewa risiti za vitambulisho lakini hadi hivi leo kwa sababu zinazoeleweka zaidi na wahusika – wenyewe wenye vitambulisho na Idara ya Vitambulisho, hawajapewa kadi zao za ZAN-ID hadi leo.

Hata hivi karibuni baada ya uandikishaji kukwama mara ya kwanza, hasa huko Pemba, Idara ya Vitambulisho ilifanya danganya toto kwa kuwaruhusu Masheha watoe barua na hivyo baadhi ya watu wakafika kujiandikisha.

Ila la ajabu, uandikishaji wa DKWK umeanza tena, na walioandikishwa na Idara ya Vitambulisho bado hawajapewa ZAN-ID na kwa hivyo hawawezi kuandikishwa na kwa hivyo ni kama Idara hiyo haikufanya lolote zaidi ya kupiga danadana na kununua muda na kuchezea akili za watu.

Lakini pia nikiri kuwa kuna watu wengine ambao walikuwa wamefikisha umri lakini hawakuona umuhimu wa kuchukua vitambulisho huko nyuma na hao wako hata waliozaliwa miaka ya 1950, 1960 hata 1970. Wapo na tunao mitaani.

Ila vyovyote iwavyo naamini Rais Karume unajua kuwa kuwa na kitambulisho ni jambo la lazima kisheria, kwa hivyo iwe kwa sababu yoyote ile, ama uzembe wa raia au mbinu za Idara ya Vitambulisho, kila Mzanzibari aliyetimia umri wa miaka 18 lazima awe na kitambulisho hicho.

Siamini kuwa Rais Karume ndani ya kilango cha moyo wake anaamini kuwa zogo lote liliopo ni la propaganda ya kisiasa bila ukweli. Mimi nakubaliana na yeye kuwa kuna ukweli kwamba propaganda ipo, lakini ni ukweli mkubwa zaidi kuwa watu hawana vitambulisho.

Naamini iwapo Rais Karume atatoa amri kuwa kwa mfano watu wasio na vitambulisho wa Jimbo la Mji Mkongwe wakusanyike Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, au wa Kikwajuni wakusanyike Skuli ya Haile Salasie au wa Raha Leo wafike Elimu Mbadala, kama hatapigwa na bumbuazi.

Kwa utafiti mdogo tu ambao nimekuwa nikiufanya na takwimu za vizazi na vijana wanaomaliza masomo naamini hakuna hata Jimbo moja Unguja na Pemba ambalo linakosa watu 300 kwa uchache kabisa ambao hadi sasa hawana ZAN-ID na kwa hivyo hatarini kukosa kupiga kura mbali ambao wataongezeka mwakani.

Kama kila Jimbo ni uchache wa watu 500, ambao ni kiwango cha chini kabisa jee si kwa nchi nzima ina maana ni watu 20,000? Nilitangulia kusema kuwa kuna gau la propaganda katika suala hili zima kama vile CUF kunadai wasio vitambulisho wanafika 90,000, lakini jee kwa nini hata hawa 20,000 Karume hataki kuamini?

Karume anajua kuwa idadi hiyo ni wapiga kura wa kiasi cha Majimbo matatu na kwa vyovyote wanaamua bila ya wasi wasi wowote ushindi wa chama kimoja au kushindwa kwa chama chengine katika uchaguzi wa Rais.

Naamini pia Karume anajua kuwa Masheha wamekuwa wakilalamikiwa kuwa ndio chanzo kikuu cha watu kukosa vitambulisho kwa sababu wanatumika kuwazuia watu wasifike kwenye Idara ya Uandikishaji ambako huko pia hukwamishwa kwa kubandikwa risiti bila ZAN-ID hivi sasa kukiwa na watu wana risiti kwa miaka mine.

Fikra zangu kwa Rais Karume ni hizi. Uandikishaji wa DKWK kwa ajili ya UM2010 unasuasua na una hatari ya kukwama tena. Na kila ukikwama tunasogea katika mazingira ya kuandikisha wapiga kura wachache au mazingira ya kutokuwepo Uchaguzi Mkuu mwakani.

Jee Rais Karume anataka amalizie muda wake kama alivyoanza? Sote tunajua alianza muda wake kwa mikiki mikubwa ya matokeo ya hali ya kisiasa na kilele kikawa ni maandamano ya Januari 26 na 27, 2001 ambapo zaidi ya watu 30 walifariki. Jee anataka kumalizia muda wake kwa staili hiyo pia?

Nimesema mara nyingi kama ambavyo wengine wengi wamesema, haitawezekana kabisa kwa kiasi kikubwa cha watu wakose haki yao, haki ambayo nchi hii ilifanya Mapinduzi ili ipatikane – haki ya kupiga kura- halafu iwe bure tu hivi hivi watu walale chali wakubali kupokwa haki hiyo.

Nimesema mara nyingi kuwa Rais Karume lazima achukue uongozi wa suala hili. Asilitizame kwa maslahi ya chama chake tu bali kwa taifa ambapo kwa hali ya sasa kubwa analolifanya kwa msimamo wake ni kutengeneza bomu ambalo sote tunajua litaporipuka halitachagua.

Imani yangu ni kuwa bado tuna muda. Karume akikamata uongozi kama Rais inawezekana ZAN-ID zikatoka kwa kila mwenye haki, inawezekana kuondoa urasimu na dana dana zote ziliopo – maana Serikali hilo halitalishindwa, iwapo ipo nia?

Sipendi kuhukumu nia ya Rais Karume, lakini kama hali ikiendelea hivi, nitaamini kuwa hana nia na nitajua kuwa antutayarishia bomu ambalo uripukaji wake hakuna anaeweza kuutabiri dhidi ya kujua kuwa madhara hayatasemeka, huo ndio ukweli ambao lazima tuukubali.

Chanzo: Mwananchi, 16 Septemba 2009

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s