Wananchi Pemba wazuia uandikishaji

Na Salim Said Salim, Pemba

ZOEZI la uandikishaji wapiga kura kisiwani Pemba, jana liliendelea kupambana na vikwazo kutokana na wananchi kuzuia uandikishaji kuendelea kutokana na wengi wao kutopatiwa vitambulisho, hivyo kutoweza kupata haki ya kupiga kura.

Vikundi vya watu kati ya 200 na 300 vilikaa karibu na milango ya vyumba vya kuandikisha wapiga kura wakisisitiza wapewe vitambulisho na kuandikishwa au yeyote yule mwenye kitambulisho haandikishwi.

Katika kituo cha Kiuyu Minungwini, Jimbo la Ole, hakuna hata mtu mmoja aliyeandikishwa jana, ukilinganisha na kuandikwa watu wanane juzi.

Vituo vingine vitatu vya Kambini, Mjini Kiuyu na Tume watu walioandikishwa kwa kutumia ujanja hawakuzidi watano kila kituo.

Kumekuwapo mabishano makali kati ya wananchi na askari polisi walipowazuia kusonga mbele, lakini walirudi nyuma baada ya baadhi ya vijana na wazee kupiga kelele kuwaambia askari kuwa wamezoea kuwaua Wapemba wanapodai haki yao na kama walikuwa na uchu wa kuendeleza mauaji, basi wasiouogope hata Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mwakilishi wa Ole, Hamad Masoud aliongoza kundi la watu wapatao 100 kwenda kuzuia uandikishaji wapiga kura na kueleza kwamba hataandikishwa mwana CCM yeyote hapo kwa vile ndio waliopewa vitambulisho mpaka kila mtu apatiwe kitambulisho.

Alipotakiwa na askari polisi asiwashawishi wananchi kuweka kizuwizi, aliwaambia askari kwamba vizuwizi vya demokrasi vimewekwa na serikali ya CCM kwa kuwabagua watu na kuwanyima haki ya kuandikishwa kupiga kura.

Baadaye Mbunge wa Ole, Bakari Shamis Faki, naye aliongoza kundi lake la watu wengine wapatao 100 na alipotakiwa awarudishe masafa ya mita 200 kutoka kwenye kituo, alimwambia walichoamua watu anaowawakilisha ni kusonga mbele kudai haki yao ya kupiga kura na si kurudi nyuma..

Alipotakiwa afanye tathmini ya hali ya namna anavyoona zoezi la uandikishaji wapiga kura linavyoendelea, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Khatib Mwinchande , alisema hali aliyoiona vituoni haimfurahishi na angependa kuona kila mwenye haki ya kupiga kura anaandikishwa.

Hata hivyo, alisisitiza tume hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na moja ya sheria hizo ni kwa mtu kuwa na kitambulisho cha uraia, ili aandikishwe.

Mkuu wa Wilaya ya Wete, Omar Ali, jana alirudia tena kauli yake ya kuwalaumu viongozi wa upinzani kwa kuzuia zoezi la uandikishaji wapiga kura lisiendelee na kusisitiza kwamba, hapakuwepo tatizo katika utoaji wa vitambulisho na kwamba watu wanapatiwa kama kawaida.

Lakini kundi la waandishi wa habari lilipowataka kinamama waliojaribu kupata vitambulisho na kukosa kusimama, zaidi ya kinamama 50 walisimama na baadhi kusema wamefika ofisi za usajili zaidi ya mara tatu.

Katika kituo cha Kiuyu Minungwini walikuwepo askari polisi zaidi ya 50 wakiwa na bunduki na mabomu ya machozi na wengine wakiwa katika magari yaliyokuwa yamebeba bendera nyekundu huku pembeni likiwepo gari linalomwaga maji yenye kuwasha.

Mara gari hilo lilipofika likitokea Wete saa tano asubuhi, kinamama walionekana kufurahia na kuwataambia askari: “Siku nyingi hatujaoga…njooni mtuoshe, lakini kwa heshima na adabu.”

Tafauti iliyojitokea jana, ni kutoonekana askari wa KMKM wenye sare nyeupe ndani na nje ya vituo vya uandikishaji kutokana na waandishi wa habari na viongozi wa CUF kuuliza kwa nini askari wa KMKM walijazana vituoni wakati kazi zao kisheria ni baharini.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s