Shahada za kura zachomwa moto

Na Asha Bani

SHAHADA za kupigia kura zinazokadiriwa kufikia milioni moja, zimeteketezwa kwa kuchomwa moto katika mazingira ya kutatanisha jijini Dar es Salaam.

Shahada hizo ziliteketezwa na watu wasiojulikana ndani ya eneo la Bohari Kuu inayohusika na utunzaji wa nyara za serikali, iliyoko eneo la Keko, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya shahada hizo zilizoshuhudiwa na waandishi wa habari wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, zilikuwa za wapiga kura wa Mkoa Morogoro, Tanga, Pwani na Dar es Salaam za mwaka 2005 na 2008.

Shahada zilizoandikishwa jijini Dar es Salaam, nyingi zimetoka katika maeneo ya Manzese na Mwananyamala.

Hadi sasa haijulikani namna gani shahada hizo za kupigia kura zimekusanywa kwa wingi na kupelekwa kuteketezwa ndani ya eneo la Bohari Kuu ya Serikali.

Kuwapo kwa shahada hizo ndani ya Bohari Kuu na mpango wa kutaka kuziteketeza, kuligunduliwa na viongozi wa CUF ambao walipata tetesi kuanzia juzi.

Inasemekana kuwa, shahada hizo ambazo zinaonyesha picha na majina ya wapiga kura mbalimbali nchini, ziliteketezwa juzi, lakini baadhi yake zilibaki ndipo Profesa Lipumba aliwakusanya waandishi wa habari na kuingia nao kwenye bohari hiyo kwa siri kwa kutumia gari yake yenye vioo vya kiza.

Mara baada ya kushuka ndani ya eneo hilo la bohari, Profesa Lipumba aliwaongoza waandishi wa habari hadi lilipokuwa lundo hilo la shahada na kuanza kuzichambua moja baada ya nyingine na kisha kuzifunga kwa mafungu kwenye mifuko ya plastiki na kuzipakia kwenye gari lake.

Wakati Profesa Lipumba aliyeongozana pia na baadhi ya wabunge na viongozi wa CUF wakichambua shahada hizo, wafanyakazi wa Bohari hawakujitokeza, lakini baada ya kuanza kuzungumza na waandishi wa habari juu ya tukio hilo, baadhi yao walijitokeza katika eneo la tukio na kushangaa.

Akizungumzia tukio hilo ndani ya eneo hilo la Bohari Kuu, Profesa Lipumba, alisema tukio hilo linadhihirisha mbinu chafu zikifanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Angalieni kadi hizi, haya ndiyo matunda ya kutokuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, kila kukicha ni wizi tu hakuna uwazi wala ukweli,” alisema Lipumba huku akionyesha mabaki ya shahada zilizoungua.

Alisema vitambulisho hivyo vinatumika katika kupiga kura za utapeli na viongozi mbalimbali wa CCM wanaovinunua kwa ajili ya kurubuni na kuvuruga uchaguzi.

Alibainisha kuwa, kamwe demokrasia haiwezi kuendelea kama hila za kupata idadi kubwa ya hesabu za kura hizo zinazofanywa na CCM hazitakomeshwa.

Aliongeza kuwa, bohari ni sehemu ya kutunzia nyara za serikali, hivyo kukutwa kwa shahada hizo zikichomwa moto katika eneo hilo ni ushahidi kuwa serikali inahusika.

Alisema serikali inayopora haki ya mpiga kura kwa kupata ushindi kwa njia isiyo halali, haiwezi kuwaletea maendeleo wananchi.

Naye Mbunge wa Michewani, Shoka Hamisi Shoka, alisema hila hizo za kuwepo kwa shahada bandia, aliwahi kuzizungumzia bungeni kwamba CCM inahusika na ununuzi wa shahada za wapiga kura, lakini walipinga.

Alisema wakati akiwawasilisha hoja hiyo bungeni, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alipinga kwa nguvu hoja hiyo na kumtaka atoe ushahidi wa hicho anachokisema.

“CCM walinitolea macho, Spika wa Bunge Samuel Sitta alinitaka kutoa ushahidi wa kununua shahada za kura, na huo ndiyo ushahidi mmojawapo.

“Bohari ni mali ya serikali ambayo inaongozwa na CCM, kutokana na suala hili wanahusika moja kwa moja na ununuzi wa kura,” alisema Shoka.

Naye Mkurugenzi wa Ulinzi wa CUF, Mazee Rajabu Mazee, alisema siku zote CUF wamekuwa wakilalamika kutokuwapo kwa tume huru ya uchaguzi, lakini wamekuwa wakipuuzwa.

Alisema tukio la kukutwa shahada hizo zikiteketezwa, kumedhihirisha jambo hilo ambalo watu walikuwa hawaamini.

“Siku za mwizi arobaini, CCM walizoea kuiba na leo ndiyo wamefikia tamati, shahada hizi ni nyingi sana, zaidi ya milioni moja. Ni Watanzania wangapi wametangaziwa kiongozi asiye chaguo lao?” alihoji Mazee.

Akizungumzia sakata hilo kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Rajabu Kiravu, alisema ofisi yake haihusiki kwa aina yoyote ya uchomaji huo wa shahada za kupigia kura.

Hata hivyo, Kiravu alieleza kushangazwa na namna ujumbe wa Profesa Lipumba na waandishi wa habari walivyoweza kuingia katika eneo la tukio.

“Ofisi yangu haihusiki na uchomaji huo, kwanza mliingiaje maeneo ya Bohari?” alihoji Kiravu.

Chanzo: Tanzania Daima

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s