Ngunguri Mahita aumbuka Mahakama yasema mtoto aliyemkana ni wake

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemwamuru aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Omar Mahita kulipa malimbikizo ya gharama za matunzo ya kumhudumia mtoto Juma Omar Mahita (12) baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa mtoto huyo ni wake.

Hukumu hiyo ilitolewa jana majira ya saa mbili asubuhi na Hakimu Suzan Kihawa katika mahakama ya siri (chamber), ambapo siku zote wanaoruhusiwa kuudhuria kesi hiyo ni mlalamikaji, Rehema Shabani na wakili wake toka Kituo cha Haki za Binadamu, Fredrick Mkatambo na wakili wa mdaiwa, Charles Semgalawa na mdaiwa Omar Mahita kutokana na mazingira ya kesi hiyo kumhusisha mtoto.

Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Kinondoni, Mkilya Daudi, muda mfupi baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mahakama hiyo imeutazama ushahidi wa mazingira na maneno, uliotolewa na mlalamikaji na ushahidi uliotolewa na Mahita na kuridhika kuwa mtoto huyo ni wa mkuu huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi.

Katika ushahidi wake, mlalamikaji Rehema ambaye ni mama wa mtoto Juma, aliithibitishia mahakama kuwa, alianza uhusiano wa kimapenzi na Mahita mwaka 1996 mjini Moshi akiwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba yake wakati huo akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Rehema, wakati wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi na IGP huyo mstaafu, alipata ujauzito na mwaka 1997 alijifungua mtoto ambaye Mahita alimkana kwa madai kuwa si wake na hajapata kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mlalamikaji.

Rehema katika ushahidi wake, alidai kuwa wakati akiwa na ujauzito, Mahita alikuwa akimhudumia kwa kumpa sh 40,000 kila mwezi na siku chache baadaye alimpatia nauli ili aende nyumbani kwao Kondoa kwa ajili ya kujifungua.

Alidai kuwa, tangu aliporejea nyumbani kwao Kondoa kwa ajili ya kujifungua, Mahita alisitisha kutoa gharama za matunzo, hali iliyosababisha mama huyo kuishi katika mazingira magumu na hatimaye kuanza kutafuta haki yake kwenye vyombo vya sheria.

“Hakimu Kihawa ameridhika kwamba Juma Omar Mahita ni mtoto wa nje ya ndoa wa Omar Mahita na mahakama imemtaka mdaiwa kwa sababu tangu mtoto huyo azaliwe alikuwa anaishi na mama yake, ataendelea kuishi na mama yake ambaye awali alikuwa mfanyakazi wa ndani wa mdaiwa,” alisema Daudi.

Alisema pia mahakama imemwamuru Mahita amlipe sh 100,000 kila mwezi kama gharama za matunzo ya mtoto huyo, kulipa malimbikizo ya gharama za matunzo toka mwaka 2003 hadi sasa kwa kiwango cha sh 100,000, na alipie gharama za masomo ya mtoto huyo hadi atakapoanza kujitegemea.

“Pia mahakama imeona kwamba mlalamikaji hajawahi kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo, hivyo imetoa amri kwamba asilipe gharama za kesi na kumtaka Mahita kukata rufaa katika mahakama za juu kama ataona inafaa,” alisema Daudi ambaye aliwaonyesha waandishi wa habari amri hizo zilizotolewa na mahakama hiyo.

Baada ya kumaliza kuzungumzia hukumu hiyo, mwanasheria huyo wa kituo cha haki za binadamu, aliwaeleza waandishi kwamba Februari 26 mwaka 2007, Rehema alikwenda kituoni kwao kuomba msaada wa kisheria, akidai kuwa mzazi mwenzake Mahita, amemtelekeza mtoto wake na amekataa kutoa gharama za matunzo ya mtoto.

“Baada ya kupokea malalamiko hayo, tulifikia uamuzi wa kupeleka suala hilo mahakamani, lakini kabla ya Rehema kufika katika kituo chetu Agosti 10 mwaka 2006, alishapeleka lalamiko lake kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii na hata maofisa wa Ustawi wa Jamii walivyojitahidi kumwita Mahita, alikataa kuitikia wito huo, na ndiyo ofisi hiyo ilipoamua kuiandikia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiiarifu mahakama hiyo isuluhishe.

“Lakini sisi kituo chetu tuliona Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya aina hiyo ya madai ya matunzo ya mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kutokana na Sheria ya Watoto waliozaliwa nje ya Ndoa Na. 278 ya 1949, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

“Februari 26 mwaka 2007, kituo chetu kilimsaidia mama huyo kwa kupeleka kesi Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na Mahita akaweka wakili wake na wakati kesi ikiendelea, mdaiwa alitaka kesi hiyo ifutwe kwa sababu imefunguliwa nje ya muda na mahakama ikatupilia mbali ombi hilo na badala yake mahakama hiyo Aprili 24 mwaka huu, ilitoa amri mlalamikaji na mdaiwa na mtoto, wakapime kipimo cha DNA na gharama za kipimo hicho zitolewe na pande zote mbili,” alisema Daudi.

Alisema jumla ya sh 300,000 zilitakiwa kwa ajili ya kufanyia kipimo hicho, lakini Mahita alikaidi amri hiyo ya mahakama ya kuchangia sh 100,000, ndipo kituo hicho kikaamua kubeba jukumu hilo kwa kutoa fedha taslimu sh 300,000 ili watu wote watatu wakapime kipimo hicho, lakini pia Mahita aligoma tena kwenda kufanyiwa kipimo hicho.

Daudi alisema baada ya Mahita kugoma kwenda kupima kipimo hicho, mahakama hiyo iliendelea kusikiliza kesi hiyo na kupokea ushahidi wa pande zote mbili hadi jana ilipotoa hukumu.

Akizungumzia jinsi kituo chake kilivyopokea hukumu hiyo, alisema kesi hiyo imeangukia katika utekelezwaji wa sheria mbovu ya Sheria ya Watoto Wanaozaliwa Nje ya Ndoa ya 1949, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ambayo inasema mtoto wa nje ya ndoa, baba atapaswa atoe sh 100 kwa mwezi kwa ajili ya matunzo.

“Sisi tunatumia mahakama zetu kuanza kutamka kiasi cha sh 100 hakitoshi kulingana na mazingira ya sasa, kwa hiyo kiasi hicho cha sh 100,000 kilichotamkwa na mahakama hiyo jana, ni kiasi kikubwa na angalau kinaendana na gharama za maisha ya sasa.

“Hivyo tunaamini hukumu ya kesi hii italeta mabadiliko ya kitabia kwa wanaume wenye tabia kama Mahita, za kuwapachika mimba wanawake nje ya ndoa zao na kisha kuwatelekeza, na pia kituo hiki kinatoa pongezi kwa mlalamikaji Rehema, kwani ni mwanamke jasiri ambaye ameweza kutetea haki yake bila woga kwani hasingekuwa jasiri, hivi sasa mtoto wake Juma hasingekuwa na baba na angekosa haki zake za msingi kama mtoto, na tunawahamasisha wanawake wasio na uwezo wanaohitaji msaada wa kisheria, wajitokeze kwenye vituo vyetu, tuwapatie msaada wa kisheria,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s