Umasikini wa Watanzania hauelezeki kwa rasilimali zao

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE: MAGDALENA H.SAKAYA (MB) KUHUSU BAJETI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KWA MWAKA WA FEDHA 2009/2010

I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika awali ya yote nachukuwa nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu na hekima tele kwa kunipa afya njema na kuendelea kunipigania katika kila jambo. Hakika yeye ni mwaminifu anastahili kutukuzwa na kuabudiwa milele.

2. Mheshimiwa Spika, kadhalika nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2009/2010 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(3) na (7) toleo la 2007.

3. Aidha napenda kuchukua nafasi hii kukishukuru Chama changu cha wananchi CUF Chama Kikuu Cha upinzani nchini Tanzania kwa ushirikiano wanaonipatia, pia niwawashukuru wananchi wa Mkoa wa Tabora hususani wale wa Wilaya Urambo kwa kuendelea kuniunga mkono katika kutetea maslahi yao na ya watanzania wote kwa ujumla. Ushirikiano wanaonipa umenisaidia kutekeleza majukumu yangu ya kila na kwa ufanisi mkubwa. Ninawaahidi kwa uwezo anaonipa Mwenyezi Mungu nitaendelea kuwatumikia kwa uaminifu tena kwa juhudi zangu zote, na kwamba sitowaangusha.

4. Mheshimiwa Spika, Kadhalika natoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote, kunipitisha bila kupingwa na kuniwezesha kuwa mjumbe wa Tume ya utumishi wa Bunge nawashukuruni sana. Aidha, nawashukuru Wabunge wa Kambi ya Upinzani kwa mashirikiano makubwa wanayonipa yanayonipelekea kuzifanya kazi zangu kwa wepesi na kwa ufanisi zaidi.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuchukuwa fursa hii kuwashukuru viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani kwa kutuongoza, kutuelekeza na kutusimamia vyema katika shughuli zetu za kila siku. Ufanisi mkubwa unaoonekana katika Kambi yetu ni kutokana na Uongozi wao mahiri.

6. Mheshimiwa Spika, nitakuwa sijatenda haki kama sitowashukuru Mhe.Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa utendaji wao katika kuhakikisha sekta hii ya Maliasili na Utalii inakuwa miongoni mwa sekta kiongozi katika mchango wake kwa pato la Taifa.

II. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BAJETI YA MWAKA 2008/09
Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu mwaka jana lilipitisha kiasi cha Shilingi 71,975,518,000/= kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya wizara hii ya maliasili na utalii na matumizi yake ya utawala. Kati ya fedha hizo Shilingi 33,799,851,000/=zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

WANYAMAPORI
7. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi mojawapo iliyobahatika kuwa na wanyamapori wa kila aina ambao ni rasilimali kubwa kwa nchi yetu na ni muhimu sana katika kuchangia pato la Taifa. Mapato halisi yaliyokusanywa inaonyesha kuwa ni shs. 14,079,878,856/= (14billion), kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwenye kamati, lakini takwimu za kitabu cha hali ya uchumi cha mwaka 2008 zinaonyesha kuwa mapato yatokanayo na shughuli za wanyamapori yalikuwa shilingi 18.4 billioni. Kambi ya Upinzani inataka Waziri alieleze Bunge hili ni takwimu ipi ni ya uhakika kati ya hizo mbili ambazo zote zimetolewa na Serikali
8. Mheshimiwa Spika, mapato hayo yaliyopatikana bado ni kidogo sana ukilinganisha na rasilimali tuliyo nayo. Kuna mianya mingi sana ya upotevu wa fedha za wananchi ambao unasababishwa na serikali kushindwa kuwa na mipango mizuri ya kusimamia mapato kikamilifu.
Mwaka jana tumeeleza kwenye hotuba yetu jinsi gani serikali inakosa mapato kutokana na ukwepaji wa ulipaji wa kodi kwa baadhi ya camp Operators. Kuna Camps ambazo hazikulipa Concession fees na park fees kwa miaka zaidi ya 10 na zimeendelea kufanya biashara. Tuliainisha Jumla ya fedha zote ambazo hazikulipwa ni USD 1,542,000 ambayo ni sawa ni Tshs 1,850,400,000/=

Serikali ilikiri na kuahidi kufuatilia na kutuletea majibu. Hadi leo hakuna majibu na bado hali inaendelea vilevile.

9. Mheshimiwa Spika, Kwa Takwimu hizi tunaweza kuona ni kiasi gani nchi yetu inavyoporwa. Watumishi tuliowapa dhamana ya kusimamia na kutunza rasilimali zetu badala yake wakiangaliana au kushirikiana na wawekezaji wasio waadilifu, au kwa kushindwa kuweka miongozo sahihi yenye maslahi kwa Taifa.

10. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri atueleze ni kwanini Serikali haijachukua hatua yoyote kwa wahusika na wanaendelea kufanya biashara bila kulipa fees zinazotakiwa kulipwa?

11. Mheshimiwa Spika, Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) waliweka makisio ya bajeti yao ili waweze kutoa huduma nzuri kwa watalii, kulipa mishahara mizuri kwa wafanyakazi na kuendeleza uhifadhi katika maeneo wanayosimamia. Katika makusanyo yaliyotarajiwa ni pamoja na kupokea kodi (concession fees) kutoka kwa mahoteli yaliyojengwa ndani ya hifadhi hizi.

11. Mheshimiwa Spika, Kuanzia mwaka 1990 wakati malipo ya kitanda yakiwa dolla 40, concession fee ilikuwa dolla 7. Pamoja na malipo kupanda kati ya dolla 200 hadi 300 bado serikali imeendelea kukumbatia mahoteli haya ya wawekezaji na wameendelea kulipa dola 7 tu kwa kitanda.
12. Mheshimiwa Spika, Kuna usiri mkubwa wa kodi zinazolipwa, wawekezaji wa mahotel haya wamekuwa hawajadiliani na uongozi wa TANAPA lolote kuhusiana na kodi wanazotakiwa kulipa, badala yake wao wanakwenda moja kwa moja kuongea na watendaji wizarani. Matokeo yake wanalipa wanavyotaka wao,shirika linakosa mapato yake stahiki na serikali inakosa mapato .

13. Mheshimiwa Spika, zipo hotel katika mbuga ya Serengeti na Selous kwa zaidi ya kipindi cha miaka 10 sasa hawajawahi kulipa concession fees na hakuna mtu yeyote anayefuatilia kuona kuwa Nchi inapata kile inachotakiwa kupata kihalali. Baya na la kusikitisha ni pale Serikali inaposhikilia mtikisiko wa uchumi kwa kila kitu na kushindwa kufuatilia malipo ya kodi zetu halali toka kwenye mahotel.

14. Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na TANAPA lakini bado kuna matatizo makubwa yanayotokana na matumizi makubwa ya fedha yasiyokuwa na udhibiti.

15. Mheshimiwa Spika,Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kwa mwaka wa Fedha 2007/2008 yalionekana matumizi mabaya ya fedha kwenye akaunti ya Amana ya kiasi cha Dola za Marekani 4,088,801 sawa na Tshs 4,906,561,200 (kwa rate ya wakati ule ya $=1200), Amana zingine zenye thamani ya Dola za Marekani $ 2,044,655.25 sawa na Tshs 2,453,586,324 pia hazikuonekana kwenye vitabu kwa kipindi kinachoishia 30 Juni, 2008. Hii ni jumla ya Tshs 7,360,147,524. kwa mujibu wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali.

16. Mheshimiwa Spika kambi ya Upinzani inamtaka Mhe.Waziri atueleze hatima ya fedha hizi, na kama kuna ubadhirifu au wizi pia kuutolea tamko ikiwa ni pamoja na hatua zilizochukuliwa kwa wahusika.

17. Mheshimiwa Spika, hali hii imetokea kabla ya Mtikisiko wa Uchumi wa Dunia. Hapa ni ushahidi tosha kuwa tatizo letu ni ukosefu wa uadilifu kwa baadhi ya watendaji wa Mashirika yetu na Idara zetu mbalimbali na Serikali katika ujumla wake. Hata baada ya Taarifa kama hizi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, na hata Taarifa za Kamati za Bunge bado hazijafanyiwa kazi.

18. Mheshimiwa Spika, Waziri wa Utalii mwaka 2007 alitoa Taarifa Bungeni kuwa TANAPA imeingia mkataba na Shirika la utangazaji la CNN kutangaza Biashara ya Utalii na nchi yetu kwa ujumla. Kutekeleza hilo Mwenyekiti wa TANAPA alitia saini Mkataba husika. Lakini ilipofikia taratibu za utekelezaji wa Mkataba huu na ununuzi, nyaraka zote husika zimewekewa saini na Wizara ya Mali Asili na Utalii, kwa kiwango cha Dola za Marekani 750,000 (Tshs 900,000,000) kwa mwaka 2007 na mkataba kuongezwa mwaka 2008/2009 kwa kiwango cha Dola za Marekani 800,000 (Tshs 1,040,000,000).
19. Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kabisa huu ni mfano wa Mkataba mbovu, katika kipindi ambacho Bunge lako Tukufu limekuwa likipigia kelele sana uwekaji saini mikataba mibovu. Hali iko hivyo hivyo kwa malipo yaliyofanywa kwa Jambo Publication Ltd kiasi cha Dola za Marekani 272,006.45 (Tshs 353,608,385), na kiasi cha Dola za Marekani 68,373.23 (Tshs 88,885,199) kama gharama ya matangazo kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow (London) kwa miezi 6 kuanzia Januari hadi June 2008, na malipo mengine ya US $ 203,633.20(Tshs 264,723,160).

20. Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa malipo kwa CNN Mikataba kuhusu malipo haya haikuonekana, na hakuna ushahidi kama matangazo haya yalitolewa kwa kiwango na utaratibu uliotakiwa.

21. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako tukufu nini hasa kilitokea hadi sheria, taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za Serikali vikavunjwa. “Value for money” kwa matumizi ya fedha hizo imepatikana?

22. Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Ngorongoro ni hifadhi ya kipekee yenye vivutio vya aina yake vilivyopelekea hifadhi kupata hadhi ya urithi wa dunia (World Heritage site). Hifadhi hii kupata hadhi hii ya kimataifa ni heshima kubwa kwa Taifa letu. Hadhi hii inavuta wageni wengi watalii kuja nchini, kuona vivutio vilivyopo na pia kutumia fursa hiyo kutembelea mbuga nyingine.

23. Mheshimiwa Spika, hadhi ya hifadhi hii imeanza kushuka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu haswa kilimo na kutishia eneo la Ngorongoro Creta kuondolewa kwenye urithi wa Dunia.

24. Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa hapa ni Serikali kuingiza siasa kwenye masuala ya msingi ambayo yanahitaji ushauri wa wataalam hali inayoathiri hata utajiri wetu na uchumi wa Taifa kwa ujumla. Sheria ya mwaka 1959 iliyoanzisha hifadhi hii na baadae kufanyiwa marekebisho mwaka 1975, inapiga marufuku kilimo ndani ya hifadhi.

25. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe ufafanuzi ni kwanini kunatolewa matamko yanayopingana na sheria ambayo yanawachanganya watendaji na bodi hata kushindwa kutekeleza majukumu yake?

SEKTA YA MISITU NA NYUKI

26. Mheshimiwa Spika,Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa misitu na mapori mengi ya asili yenye mchanganyiko mkubwa wa mimea. Pamoja na kwamba mimea hii imekuwa ikichangia uchumi wetu kwa kiasi fulani, bado mkazo wa kutosha haujawekwa kuhakikisha kwamba faida yote iliyomo kwenye mimea hii inapatikana. Mathalani, madawa asilia ambayo nchi nyingine, kwa mfano Costa Rica, ni sekta inayoingiza mabilioni ya Dola kwa mwaka, hapa kwetu sekta hii bado haijaangaliwa kwa upana wake.

27. Mheshimiwa Spika, mti wa mng’ongo unaotumika kwa kutengeneza kinywaji ama mvinyo wenye umaarufu mkubwa duniani aina ya Amarula ni moja ya rasilimali za asili zilizomo kwa wingi katika nchi yetu. Kutokana na wingi wa miti hii bado matumizi yake hayajaweza kufanyika kwa kuwawezesha wananchi kunufaika na mti huo.

28. Mheshimiwa Spika, wataalamu wa utafiti wa misitu kutoka taasisi mbalimbali za misitu nchini ikiwamo Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori), wamebaini na kuthibitisha kuwamo kwa utajiri mkubwa wa miti aina ya mng’ongo (Sclerocarya Birrea) inayopatikana kwenye misitu yetu hapa nchini.

29. Mheshimiwa Spika, “Utafiti huo uliofadhiliwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU), Kambi ya Upinzani inaona kuwa kutokana na tafiti hiyo ni dhahiri kama watakuja wawekezaji watakuwa na uelewa mkubwa kwenye sekta ya miti hiyo, jambo litakalo sababisha kuwazidi uelewa watu wetu kwenye majadiliano ya kiuwekezaji na hivyo rasilimali zetu kuvunwa kwa bei ya bure kama inavyofanyika kwenye shamba la miti la mufindi.

30. Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ubinafsishaji wa shirika la Mkata Saw Mills –Handeni toka 16.3.1998 hadi sasa toka kiwanda kibinafsishwe hakijawahi kuzalisha chochote na Serikali imeendelea kukosa stahili yake ya kodi. Pia kiwanda cha Sao Hill Saw Mills Ltd-kilichopo Iringa serikali haijapata pato lolote tokea kiwanda hiki kibinafsishwe na mbaya zaidi inaonyesha kuwa Mwekezaji ana lengo tofauti na lile lililomo kwenye mkataba.

31. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwani tunaendelea kuwa na wawekezaji ambao hawafuati masharti ya mikataba yao? Na cha kusikitisha zaidi kwa upande wetu ni pale rasilimali zetu zinapovunwa na kupelekwa nchi jirani na baadae tunalazimaka kununua vyetu toka kwa jirani zetu.

32. Mhe spika Tunaomba ufafanuzi wa hili la Tanesco kununua nguzo za umeme toka nje ya nchi tena kwa gharama kubwa wakati miti ya nguzo za umeme tunazo kwa wingi. Aidha tunaomba tuelezwa kwa kipindi chote hicho, kwa makampuni mawili ya mazao ya misitu Serikali imepoteza kiasi gani cha fedha? Mbaya zaidi ni kuwa hata fedha za mrahaba stahiki ya Serikali toka Sao Hill shilingi 181,165,465/= hazikuwekwa benki, hii ni kwa mujibu wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

33. Mheshimiwa Spika, ubinafsishaji wa shamba la mitiki la Longuza lililoko mkoani Tanga kwa kampuni ya Kilombero Valley Teak Co Ltd (KVTC) inayomilikiwa na Shirika la Maendeleo la Jumuiya za Madola (CDC) na ilianzishwa mwa 1992 haukufanyika kwa kuzingatia masalahi ya Taifa.

34. Mheshimiwa Spika, kiasi cha Tsh. bilioni 7 kwa ajili ya kuuziwa msitu huo wa Longuza ni kidogo sana ukilinganisha na thamani halisi ya mitiki yenyewe. Ni wazi kama taratibu zingefanywa kihalali na si kienyeji kama ilivyotokea thamani yake ingekuwa si chini ya Tsh. bilioni 38.7 ukiacha miti ya Misaji ambayo ina umri wa chini ya miaka 30 ambayo ina ukubwa wa karibu hekta 440. Thamani ya shamba la Longuza kwa miti ya Misaji ni takribani sh. bilioni 60 ukiacha aina nyingine za miti, hii ni kwa mujibu wa tafiti za wataalam wa misitu.

35. Mheshimiwa Spika, Serikali imepata hasara kutokana na uuzwaji huo uliofanyiwa tathimini ya chini. Idara iliuza miti ya mitiki kutoka shamba la Mtibwa yenye mita za ujazo 42,000 na kupata sh. bilioni sita.
Hivyo basi kwa nini shamba lenye zaidi ya mita za ujazo 400,000 litolewe kwa sh. bilioni saba tu? ”Je tunatoa zawadi kwa Commonwealth Development Corporation (CDC)?

36. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani siku zote tumekuwa tukisema kuwa utajiri wetu unaibiwa kwa udhaifu wetu kwa kutokuthaminisha mali zetu kwa bei za soko. Mfano serikali inauza ujazo wa mita moja kwa Tsh. 50,000 badala ya bei ya soko ambayo kwa wanunuzi wa hapa Tanzania si chini ya sh. 140,000 kwa mita moja ya ujazo kwa miti ya mitiki.

37. Mheshimiwa Spika Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe.Waziri atueleze ni hadi lini nchi yetu itaendelea kuwavumilia watendaji wasiokuwa na uzalendo na uaminifu pale wanapouza maliasili za Taifa kwa kuweka mbele maslahi yao? Na je ni hatua gani za nidhamu zinachukuliwa kwa watu hao?

38. Mheshimiwa Spika, kwa sasa licha ya Serikali kupiga marufuku uvunaji wa misitu kwa kukata magogo na upasuaji wa mbao lakini kwa masikitiko zoezi hilo bado linaendelea na Serikali imekaa kimya tu. Kumezuka wawekezaji wezi ambao wanajifanya wanawekeza kwenye kilimo cha mibono na hivyo kupata fursa hiyo, lakini wakifika tu wanaanza kufyeka na kuvuna misitu katika maeneo husika.

39. Mheshimiwa Spika, mfano ulio hai ni wawekezaji wa kilimo cha mibono walioingia mkoani Lindi, wilaya ya Kilwa katika vijiji vya Mavunji, Liwiti na Migeregere. Watu hawa wamefyeka na kuvuna msitu wote na kusafirisha kila kitu kwa njia ya mashua kupitia bahari ya Hindi na barabara kwenda Dar Es Salaam. Mbaya zaidi hata kilimo kilichokusudiwa haionyeshi dalili kuwa kipo.

40. Mheshimiwa Spika, Jambo la kusikitisha ni kuwa Serikali inazo taarifa zote lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Kambi ya Upinzani inataka Mhe.Waziri alieleze Bunge ni kwanini watendaji hao wanaoshirikiana na wawekezaji wezi wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kuhujumu uchumi?

41. Mheshimiwa Spika, uharibifu mkubwa wa misitu hapa nchi unachangiwa kwa kiasi kikubwa na watendaji wasio waadilifu wa Serikali waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali hizi. Ipo mifano mingi halisi, mmoja upo Wilaya ya Urambo kata ya USINGE kitongoji cha MABOHA ambapo wananchi wametenga eneo lao la msitu, lakini viongozi wa Serikali wameanza kuuza eneo hilo na kukata vipande kuwa mashamba. Eneo lingine ni kitongoji cha MAKANYA kata hiyo hiyo ya USINGE ambapo watu walihamishwa na kuchomewa nyumba zao kwamba wapo ndani ya hifadhi, jambo la kusikitisha maeneno waliyohamishwa wananchi yanayopata 14,000ha yanafuatiliwa na baadhi ya viongozi wakuu Serikalini ili kujimilikisha kuyafanya mashamba. Tunaomba kauli rasmi ya Serikali kuhusiana na maeneo hayo wananchi.

42. Mheshimiwa Spika,kitendo cha Serikali kuendelea kukumbatia watendaji wabovu ndio chanzo cha kuzorotesha utendaji mzima wa Wizara hii, pia tabia ya kuhamisha mtumishi anapoharibu na kumpeleka kwenye kituo kingine au hata kumpandisha cheo kinasababisha matatizo yasiyoisha. Haiwezekani mtumishi aliyekuwa menaja wa pori la akiba la ugalla, akaharibu hata kushindwa kufanya kazi na wananchi, viongozi wa Wilaya, Viongozi wa Mkoa leo akapandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi msaidizi! tunategemea nini hapa?.

43. Mheshimiwa Spika, hivi sasa ujangili kwenye maeneo mbalimbali katika mapori ya akiba umeongezeka kutokana na kukosekana kwa usimamizi makini na mahusiano mabaya yaliyopo kati ya mtendaji mkuu wa Idara ya Himasheria (Ant-poaching) na wale anaowasimamia. Hali hii imepelekea watumishi kukata tamaa, kukosa motisha wa kazi, na hata wengine kuacha kazi. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufuatilia suala hili kwa makini na kulipatia ufumbuzi ili kunusuru rasilimali zetu na kuboresha utendaji wa kazi.

44. Mheshimiwa Spika, sekta ya ufugaji nyuki bado ina fursa kubwa sana kwa maendeleo ya watanzania na uchumi wa nchi kwa ujumla. Ni ukweli ulio wazi kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na kampuni inayojihusisha na maendeleo ya sekta kilimo inayoitwa (PASS), inaonyesha kuwa Tanzania inauwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali zenye thamani ya shilingi 133.3billion kila mwaka na kuzalisha nta tani 9,200 zenye thamani ya shilingi 35.5billioni kwa mwaka.

45. Mheshimiwa Spika, kwa sasa Tanzania inazalisha asali tani 4,860 kwa mwaka zenye thamani ya shilling 4.9 billion na nta tani 324 yenye thamani ya shilling 648million kwa mwaka. Hii ni sawa na 3.5% ya uzalishaji mzima katika tasnia ya ufugaji nyuki.

46. Mheshimiwa Spika, tafiti zinaonyesha kuwa kuna zaidi ya hekta 34Million za mapori yanayofaa kutunza makoloni 9.2millioni ya nyuki wa asali. Aidha tafiti zinaonyesha kuwa ukanda wa Magharibi mikoa ya Tabora,Rukwa,Kigoma na Shinyanga ndio ukanda muhimu sana kwa ufugaji wa nyuki kwa Ukanda wa kati Singida inaongoza kwa kuwa na fursa kubwa ya uzalishaji wa asali. Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe.Waziri alieleze Bunge lako tukufu mkakati uliopo wa kuhakikisha kuwa fursa hii inawanufaisha watanzania.

47. Mheshimiwa Spika, kutokana na takwimu zilizopo ni kwamba miaka ya 60 na 70 Tanzania ilikuwa inaongoza kwenye soko la dunia kwa uuzaji wa nta, Kambi ya Upinzani ina uhakika kwa tafiti zilizofanywa tuna uwezo wa kushika soko hilo la dunia kwa uuzaji nta fursa bado ipo.Jambo la kusikitisha ni kuwa baada ya kwenda mbele kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia ya ufugaji wa nyuki sisi tunarudi nyuma.

48. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitishwa sana hili, kwani wataalam wote wanaofanya haya ni watanzania, je ni kwa nini serikali inashindwa kuwatumia wataalam wetu kwa manufaa ya nchi yetu? A u ndio utekelezaji bora wa Ilani ya uchaguzi ya CCM?

UTALII
49. Mheshimiwa Spika, Utalii ni miongoni mwa sekta ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vikiwepo katika maeneo mbalimbali kama vile fukwe maporomoko ya maji, mito mikubwa, chemchem za maji moto (hot spring water), hifadhi za wanyama zilizokusanya wanyama mbali mbali, sura ya nchi na hali ya hewa nzuri, ambayo ni muhimu kwa kuvutia watalii.
50. Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Rais na hotuba ya waziri wa fedha alisema serikali kupunguza gharama za visa kuwa dolla 50 kwa wageni wote ili kuinusuru sekta ya utalii kutokana na mtikisiko wa uchumi.Hata hivyo kabla ya mtikisiko gharama za multiple visa ilikuwa dolla 100 na single visa gharama ilikuwa dolla 50. Serikali inatakiwa kufafanua hapa inakusudia nini hasa?
Mhe spika Kambi ya Upinzani inaona kupunguza gharama za visa pekee haitaleta badiliko tunatakiwa kuangalia mambo mengi kwa upana wake ikiwemo gharama za kuingia kwa parks ( park fee.) Wenzetu wa Kenya wameenda mbali zaidi kwa kupunguza hata nauli kwa ndege zao kwa watalii kuja Kenya, hivyo basi kulifufua shirika letu la ndege (ATCL) ni muhimu sana katika kuifanya sekta ya utalii kuwa kiongozi katika pato la Taifa.

51. Mheshimiwa Spika, Sekta ya utalii ni sekta ambayo kwa kiasi kikubwa imeathirika na mtikisiko wa Uchumi, kwa mujibu wa takwimu inaonyesha kuwa shughuli za utalii, hotel na migahawa zilikua kwa asilimia 4.5 mwaka 2008 ikilinganishwa na asilimia 4.4 mwaka 2007. Japokuwa kulikuwa na ongezeko la asilimia 0.1 kwa shughuli hizo lakini mchango wake katika pato la taifa ulipungua kwa aslimia 0.1.Hii maana yake nini? Tunaomba waziri atupe ufafanuzi wa takwimu hii. Idadi ya watalii waliotembelea hifadhi za taifa na hifadhi ya Ngorongoro kwa mwaka 2008 inaonyesha ilikuwa ni watalii 1,083,113. Idadi ya watalii kutoka nje iliongezeka kwa asilimia 6.4 kwa mwaka 2008. Je ongezeko hili limechangia vipi kwenye pato la Taifa?

52. Mheshimiwa Spika, hakuna nchi yoyote duniani ambayo inategemea watalii wa nje ili kukuza sekta ya utalii. Tanzania bado tunategemea watalii toka nje, hili ni tatizo kubwa kwa maendeleo ya sekta hii na ndio maana likitokea tatizo kidogo nchi za Ulaya sisi tunaathirika sana. Ili kukuza sekta hii inatubidi kuweka mazingira mazuri yatakayo wajengea watanzania utamaduni wa kuwa watalii katika nchi yao.

53. Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa ni gharama za mahoteli yaliyoko mbugani zimewekwa kwa kuangalia watalii toka nje ya nchi na si kwa kuwafikiria watanzania. Kwa hali halisi ya maisha ya watanzania hakuna mwenye uwezo wa kulipa dolla 200- 300 kwa siku kwenye hotel.

54. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza ni kwanini Serikali isiwawezeshe wawekezaji wazalendo wakajenga mahotel huko mbugani ili walipishe gharama zinazoendana na halihalisi ya watanzania? Kwa njia hii watanzania wengi watanufaika na vivutio vyao tofauti na sasa.

55. Mheshimiwa Spika, Kwa kuangalia taarifa ya utendaji iliyotolewa na wizara kuhusiana na mashirika yaliyokuwa yanamilikiwa na wizara kabla ya kubinafsishwa, hasa mahoteli inaonyesha kuwa wengi wa wale walionunua hotel hizo wamevunja makubaliano ya mauzo. Mengi ya mahoteli yaliyobinafsishwa yanafanya kazi chini ya viwango na mengine hayafanyi kazi kabisa.

56. Mheshimiwa Spika, kwa kuyataja machache, ubinafsishaji wa hotel ya lobo wildlife logde ulifanyika April, 2001. Hotel ya Ngorongoro Wildlife lodge ulifanyika Juni, 2000. Lake Manyara ulifanyika April.2001 na Hotel ya Seronera Widlife Lodge ulifanyika Jan.2003, mwekezaji wa mahotel hayo haonyeshi nia ya kuzifanyia ukarabati hotel hizo kwa mujibu wa mkataba wa mauzo, japokuwa anaendelea kufanya biashara nzuri tu.

57. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali kubinafsisha hotel hizo halijafikiwa na sasa ni takriban miaka 10 tangu zoezi hilo limalizike. Kambi ya Upinzani inauliza ni vipi Serikali inalitatua tatizo hilo la mwekezaji huyo kuendelea kuvuna bila ya kuwekeza? Aidha, Kambi inataka maelezo ni kwani mwekezaji huyo asishitakiwe kwa kuvunja makubaliano ya mkataba wa mauzo?

58. Mheshimiwa Spika, mbali na ubinafsishaji wa mahoteli pia kuna ile kampuni iliyokuwa inamilikiwa na shirika la uwindaji (TAWICO) ambayo ilikuwa inajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na nyara za Taifa (KUFUA NYARA) iliyokuwa inaitwa TAXIDERMY. Kwa masikitiko makubwa Serikali imeendelea kutomchukulia hatua zozote mwekezaji wa Taxidermy hadi sasa toka apewe shirika hilo mwaka 1998. Taarifa ya Serikali inasema kuwa mwekezaji huyo amebadilisha biashara na kiwanda hicho cha kufua nyara kimekuwa ni karakana ya kutengeneza magari ambacho ni kinyume cha mkataba.

59. Mheshimiwa Spika, kiwanda hicho kabla ya kubinafsishwa kilikuwa kinafua nyara na kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na ngozi za wanyama, pembe, kwato na vitu vingine, hivyo kuziongezea thamani nyara hizo kabla ya kupelekwa nje ya nchi. Kitendo cha mwekezaji huyu kugeuza matumizi ya kiwanda hiki ni kukosesha Taifa mapato kwani kuendelea kupeleka ngozi ghafi nje ya nchi ni jambo la kulinyima Taifa fedha za kigeni na kudhoofisha uchumi wa nchi.

60. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka ufafanuzi ni kwanini wahusika wasishtakiwe kwa kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wa makubaliano wa mauzo na kuendelea kulitia taifa hasara na kwanini serikali inaendelea kulifumbia macho? Au aioni umuhimu?

61. Mheshimiwa Spika, mwaka jana tulielezea jinsi gani mwekezaji wa Grumeti Reserve aliyemilikisha eneo la wananchi lipatalo hekta 5000 anavyonyanyasa wananchi na hata askari wake kufikia hatua kuwalisha wananchi nyama mbichi. Mwaka huu ameendeleza madhidhi mbalimbali kwa wananchi kiasi cha kuwa kero kubwa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo.

62. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni wananchi wawili wamepigwa risasi kwa kufuatilia ng’ombe wao walioingia kwenye hifadhi na kushikiliwa na mwekezaji huyo. Kama vile haitoshi mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 13 ambaye alikwenda kunywesha ngombe wa baba yake kwenye mto Rubada, ng’ombe wachache walimtoroka, kufuatia hilo askari walimkamata na kumfungulia mashtaka na akahukumiwa kifungo cha miaka 3 jela. Mwanafunzi huyo amepoteza masomo yake na amenyanyaswa ndani ya nchi yake.

63. Mheshimiwa Spika, hivi kweli mwekezaji anafikia hatua ya kukataza wananchi kunywesha mifugo maji kwenye mto ambao umekuwepo miaka yote?

64. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulishughulikia suala hili kwa haraka ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea pale wananchi watakapochoka na unyanyasaji huo.

UWINDAJI

65. Mheshimiwa Spika, Tasnia hii ya uwindaji imekuwa hainufaishi taifa na wananchi wake kwa ujumla kwa sababu ya kukosa mipango madhubuti ya kusimamia. Wawindaji kwenye mapori ya akiba wemekuwa wanawinda idadi kubwa ya wanyama kuliko ile iliyomo kwenye kibali na wakati mwingine kuwinda wanyama tofauti na wale walioruhusiwa.

66. Mheshimiwa Spika, Halimashauri za wilaya zinatakiwa kujua mambo yote yanayotendeka katika maeneo yao. Kwa utaratibu ulipo sasa ambapo shughuli za uwindaji ndani ya mapori ya akiba unaosimamiwa na watumishi wa Wizara bila ya Halimashauri husika kuhusishwa, kunajenga matabaka katika utawala.

67. Mheshimiwa Spika, Wawindaji walitakiwa kuelekezwa na wizara, kuripoti wilayani kwanza wanapokwenda kuwinda na wakati wa kuondoka ili kuhakiki kinachowindwa na nyara zinazochukuliwa. Nakala za leseni ya kila mwindaji “pink copy” sharti ibakizwe wilayani, kama kitalu hicho kipo pori la akiba afisa wanyama pori wilaya husika apate taarifa za uwindaji na vivuli vilivyohusika. Hakuna haja ya mambo haya kuwa ni siri ya Wizara, inatakiwa kuwa ni wazi ili rasilimali zetu ziweze kuvunwa kwa taratibu zilizopo na hivyo kunufaisha Taifa.

68. Mheshimiwa Spika, suala la mgawo wa fedha la 25% kwa uwindaji wa kitalii kwa halimashauri zinazozunguka vitalu vya uwindaji ni suala la kisheria. Cha kusikitisha Serikali inachukulia kama hii ni hisani, kwani inapopenda inatoa isipopenda haitoi. Halimashauri nyingi zimekuwa zinalalamika kwa kutokupewa mgawo huu kwa muda mrefu ambao ni haki yao. Kambi ya Upinzani inauliza ni kwanini Serikali isitoe mgawo huu kwa wananchi wakati fedha zinakuwa zimekwishalipwa? Hii inakatisha tamaa wananchi na kuwanyima motisha kuendelea kuhifadhi wanyamapori wanaowazunguka.

69. Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

………………………….
MAGDALENA H.SAKAYA (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMABI YA UPINZANI-WIZARA YA MALIASILI NA UTALII.
10.07.2009

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s