“Kilichofanywa na ZEC katika Siku Mbili za Kwanza za Uandikishaji Micheweni”

RIPOTI YA AWALI YA AWAMU YA KWANZA YA UENDELEZWAJI WA DKWK LA ZANZIBAR – WILAYA YA MICHEWENI

 

RATIBA YA UANDIKISHAJI

 

WILAYA TAREHE VITUO VYA UANDIKISHAJI
MICHEWENI 06/07 – 09/08/2009      30
WETE 10/08 – 13/09/2009      31
CHAKE –CHAKE 14/09 – 25/10/2009      31
MKOANI 26/10 – 07/12/2009      28
JUMLA      130

 

UTARATIBU ULIVYO 

 

Kila shehia 6 zitashughulikiwa kwa siku 7: siku 2 za mwanzo ni kuandikishwa wapiga kura wapya na siku tano zinazofuata zitawahusu waliopoteza , ambao shahada zao zimeharibika, wanaotaka kufanyiwa uhamisho wa taarifa zao na watakaobadilishiwa shahada kongwe kwa kupewa shahada mpya.

 

Kila chumba/kituo/shehia kina seti 2 za kompyuta (kits) zinazofanyakazi kwa pamoja kwa madhumuni ya kuondoa msongamano wa watu na kuokoa muda , watu wasisimame katika foleni kwa muda mrefu.

 

  • Siku 2 za awali 6/07/ – 7/07/2009 uendelezwaji wa Daftari katika shehia 6 za jimbo la Konde

 

Jimbo la Konde lina Shehia 6 na Vituo 6 vya uandikishaji: Kilimo kifundi, Skuli ya konde, Skuli ya Makangale “A”, Skuli ya Makangale“B” Skuli ya Msuka “A”, Skuli ya Msuka “B”.

Kwa mujibu wa makisio, katika vituo hivi 6 vya Jimbo la Konde, katika siku hizi mbili za uandikishaji wa wapiga kura wapya, zaidi ya watu 2000 walitegemewa kuandikishwa. Badala yake ni watu 357 tu ndio walioandikishwa.

 

Angalia jadweli ya uandikishaji wa siku 2.

  06/07/2009 07/07/2009 JUMLA
S/N JIMBO

 

 

SHEHIA KITUO WALIOANDIKISHWA WASIOANDIKISHWA WALIOANDIKISHWA WASIOANDIKISHWA WALIOANDIKISHWA WASIOANDIKISHWA
1   Kifundi Kilimo Kifundi 17 60 19 27 36 87
2 Konde Skuli ya Konde 47 96 63 106 110 202
3 Makangale Skuli ya Mk ‘A’ 7 170 20 119 27 289
4 Msuka Magharibi Skuli ya Msuka “A” 21 110 37 100 58 210
5 Msuka mashariki Skuli ya Msuka “B” 34 209 47 118 81 327
6 Tondooni Skuli ya Makangale ‘B’ 7 185 38 114 45 299
      133 830 224 584 357 1414

 

Nini kimesababisha kompyuta 12 kwa masaa 16 (siku mbili za kazi) kuandikishwa watu 357 tu?

 

Si kwa sababu ya kutokuwepo waandikishwaji katika vituo. Ukweli ni kuwa vituo vilifurika na foleni zilikuwa refu. Badala yake ni matangazo ya masheha, wakuu wa vituo vya uandikishaji na askari mbali mbali (wakiwemo polisi, KVZ, na wengine wasiojulikana ambao walikuwa wameshikilia silaha pembeni mwa vituo), ambayo yalikuwa yakisema kwamba kila ambaye hana kitambulisho cha Ukaazi hatakiwi kukaribia katika kituo cha uandikishaji, ndiyo yaliyowasababisha baadhi ya watu wakatawanyika na kuondoka vituoni ingawa baadae walirejea tena.

 

Kutokuwa na vitambulisho vya Uzanzibari vya ukaazi ndio sababu kubwa iliyowafanya vijana wengi wa rika la miaka 18, 19 hadi ishirini na baadhi ya wazee wachache wasiweze kuandikishwa katika siku hizi 2 katika vituo vyote 6.

 

Hata hivyo, watu waliopewa fomu za malalamiko (2KK) ni wachache sana. Kwa mfano, tarehe 6 na 7 Julai 2009, watu waliowahi kuingia vituoni na kupingwa kwa kutokuwa na vitambulisho vya Uzanzibari na kupewa fomu hizo ni watatu katika kituo cha Skuli ya Makangale ‘A’ na wanne katika kituo cha Skuli ya Msuka ‘B’, ingawa waliopingwa walikuwa ni 1,414. Hii ni kusema kuwa katika siku mbili hizi za uandikishwaji wa wapiga kura wapya, kati ya watu 1,414 waliopingwa ni 7 tu ambao wamepewa fomu 2KK.

 

Mantiki ya kutowapatia fomu 2KK waliopingwa kuandikishwa katika vituo maana yake ni kuwazuia watu hao wasiweze kuendelea kudai haki zao mahakamani, tendo ambalo ni kinyume na Sheria ya Uchaguzi wa Zanzibar ya 1984.

 

Ule ukweli kuwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Magogoni ulikuwa ni wa majaribio hapa unaonekana. Vyama vya siasa vilivyoingia katika Uchaguzi wa Magogoni vilijifunza na Tume ya Uchaguzi nayo ilijifunza.

 

Tofauti ni kuwa kama vyama vimejifunza mema, ZEC imejifunza maovu na kuongeza uzoefu wa uchafuzi wa uchaguzi. Kile kitendo cha watu wengi kwenda kudai haki zao Mahakamani katika uchaguzi wa Magogoni kuliathiri sana ZEC  na ndio maana ZEC imekuwa na mtindo mpya hapa Pemba: kuwazuia watu waliopingwa kuwapa fomu 2KK ili usipatikane ushahidi kwamba walikwenda vituoni na kuwazuia wapiga kura hao wasiweze kwenda Mahakamani.

 

Inaonekana kulikuwa na amri iliyotolewa kwamba fomu hizi zisitolewe kwani maafisa wa ZEC katika vituo vyote sita walikuwa hawatoi 2KK, pamoja na kuwa sheria inaeleza wazi wazi kuwa yoyote anaepingwa apewe fomu hizo.

 

  • Mbinu mpya ya kubabaisha/ kuwadanganya watu kwa kukhofia fujo

 

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ilijaribu kuwababaisha wale wote waliopingwa kwa kuwaorodhesha majina yao katika karatasi ya kawaida kuwa watawaandikisha katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Micheweni.

 

Hili lilifanyika siku ya mwanzo 06/07/2009 katika kituo cha Kilimo Kifundi, Skuli ya Msuka ‘A’ (Magharibi) na Skuli ya Msuka ‘B’ (Mashariki) na kwa siku ya pili, 07/07/2009 ni Kituo cha Skuli ya Makangale ‘A’ na kituo cha skuli ya Makangale ‘B’ ndivyo ambavyo vilivyoorodhesha majina ya waliopingwa.

 

Vituo vyengine 4 havikufanaya hivyo. Kama lengo ni kuwaandikisha kwa nini hawakuandikishwa pale pale kituoni au kama lengo ni hilo  kwa nini mpango wa kuwaorodhesha haukuendelea kwa vituo vyote kwa siku zote, huu ni ubabaishaji tu.

 

  • Mawakala wa ZEC –  Sheha na watendaji wengine wa ZEC

 

Katika uandikishaji huu, Sheha kama wakala wa ZEC kwa kiasi kikubwa amepata mapumziko kwa sababu watu wengi waliishia katika mlango wa kuingia kituoni na kuorodheshwa hapo hapo mlangoni bila ya kuonana na Sheha. Hata hivyo kesi chache ziliripotiwa na mawakala wetu zinazohusu masheha na waandishi wasaidizi kuwapinga watu bila sababu za msingi.

 

Mfano mzuri ni huu wa sheha wa shehia ya Tondooni katika Kituo cha kujiandikisha cha Skuli ya Makangale ‘B’ ambapo sheha wa shehia hii na mwandishi msaidizi, Issa Abdalla Said (wa kituo hicho) alimkatalia kumuandikisha Bwana Rashid Khalfan Omar wa shehia ya Tondooni kwa kumuandikia katika fomu 2KK kuwa si Mzanzibari.

 

Na mfano mwengine wa pingamizi ni huu wa Bwana Mohammed Seif Ali wa Msuka aliyepingwa na mwandishi msaidizi, Latifa Kombo Makame wa kituo cha uandikishaji cha Skuli ya Msuka ‘B’. Mohammed amepingwa kwa kuambiwa kuwa amepoteza sifa za kuwa mpiga kura.

 

Sheha kama wakala wa ZEC katika kuisaidia ZEC kuwababaisha watu, tarehe 06/07/2009 sheha wa shehia ya Konde, katika kituo cha uandikishaji cha Skuli ya Konde aliwatangazia watu waliojipanga katika mstari kwa madhumuni ya kwenda kuandikishwa, kuwa ambaye hana kitambulisho cha Uzanzibari, jioni ya siku ile aende   aende nyumbani kwa Sheha kupatiwa fomu, kwa kuomba na baadae kupatiwa kitambulisho cha Uzanzibari ukaazi. Waliokwenda kwa sheha jioni, sheha aliwaambia hana fomu ya aina yoyote. Lengo lilikuwa ni kuwaondosha katika foleni ya kwenda kujiandikisha.

 

Inaonekana ZEC imejitayarisha vya kutosha katika kuendeleza uchafuzi wa uchaguzi kwani wengi kati ya watendaji wa ZEC wazoefu wa kazi hii  ambao wameshafanya kazi za uendelezwaji wa Daftari kwa jimbo la Magogoni, watendaji ambao kwa kiasi kikubwa hawakuwa waadilifu katika kufanya kazi zao wameletwa kufanya kazi hii hapa Micheweni.

 

Mfano mzuri unaonekana katika kituo cha uandikishaji cha skuli ya Konde. (Mwana) Mkuu wa kituo hiki ni mtendaji wa ZEC aliyekuwa anafanya kazi hii Unguja na alishiriki kikamilifu katika uvurugaji wa Daftari katika jimbo la Magogoni.

 

Kabla ya hapo ZEC ilieleza kuwa itakuwa na watendaji 39 watakaofanya kazi ya uendelezwaji wa Daftari kwa Kisiwa cha Unguja na hao wangefanya kazi hiyo Unguja tu na wengine 39 ambao hao nao wangefanya kazi hiyo kwa Pemba.

 

Msimamizi wa uchaguzi wa Wilaya ya Micheweni amethibitisha kuwa hana nakala ya daftari la wapiga kura katika kompyuta katika Ofisi yake. Hii ni kinyume na kif: 13(3) cha sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.

 

Amethibitisha vile vile kuwa kampyuta inapoharibika matatizo hayo yanatatuliwa na fundi/ Mtaalum wao aliyeko Israel, kama anavyoelezwa na Mabosi wake walioko Unguja.

 

Haya ameyaeleza kwa Katibu wa ZEC na Katibu wa CUF wa Wilaya ya Micheweni walipokutana kwa mazungumzo mafupi lilipotokea tatizo kuharibika kompyuta katika kituo cha uandikishaji cha Msuka magharibi  tarehe 08/07/2009 saa 3 asubuhi.

 

Kwa ufupi, zoezi la siku 2 za uandikishaji wa wapiga kura wapya limekuwa na ugumu wake zaidi ingefanana kuitwa zoezi la kutoandikisha kuliko kuitwa zoezi la kuandikisha, kwani kinachotokea ni kuwanyima haki wengi wanaostahiki kuwandikishwa na kuwaandikisha wachache ya waliopaswa kuandikishwa!!

 

Sababu kubwa ni waandikishwaji hao kutokuwa na vitambulisho vya Uzanzibari ukaazi.

 

  • Vikosi vya SMZ

 

Takribani, kwa siku hizi mbili za uandikishaji wa wapiga kura wapya, vituo vyote vilikuwa vimezungukwa na Askari wa vikosi vya SMZ wenye silaha, lengo ilikuwa ni kuwajenga khofu waandikishwaji. Bahati nzuri badala ya khofu, ari na hamasa ya waandikishwaji kudai haki zao iliongezeka na hakuna muandikishwaji aliyesita kwenda kwenye kituo cha uandikishaji kwa khofu ya Askari. Ukiwacha Askari Polisi waliokuwa ndani ya Vituo, Askari wa Vikosi vya SMZ walikuwa wanapita katika foleni za waandikishwaji kuwatangaazia kuwa ambaye hana kitambulisho cha Uzanzibari Ukaazi aondoke kituoni hapo, aende kutafuta kutambulisho hicho.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s