Prof. Lipumba azindua Operesheni Zinduka

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TAIFA WA CHAMA CHA WANANCHI (CUF), MHE. PROF. IBRAHIM LIPUMBA, KWENYE MKUTANO NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA KUZINDUA ‘OPERESHENI ZINDUKA’
PEACOCK HOTEL, DAR ES SALAAM, 5 JULAI, 2009

Waheshimiwa Wahariri wa Vyombo vya Habari,

Awali ya yote, nachukua fursa hii adhimu kuwashukuru nyote kwa kuthamini mwaliko wetu na kuja kuungana nasi hapa katika mkutano huu maalum. Naelewa wahariri mna kazi nyingi na hasa katika wakati wa mchana ambapo mnapaswa kuwepo katika vyumba vya habari kuangalia yanayoingia ili kuamua mambo yepi yachapishwe na kwa uzito upi. Nasema ahsanteni sana kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkitupa.

Tumewaita hapa ili kuwajulisha juu ya ‘Operesheni Zinduka’ ambayo tuliahidi kwamba tutaizindua mwezi huu wa Julai. Operesheni Zinduka ni operesheni maalum iliyolenga kuwazindua Watanzania na kuwaongoza waweze kufanya mabadiliko ya kisiasa kupitia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwaka huu wa 2009 na kuing’oa kabisa CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Chama Cha Wananchi (CUF) kina historia ya kuwaongoza Watanzania kudai na kuleta mageuzi ya kisiasa. Ndiyo chama pekee cha upinzani chenye misingi ya kitaifa kuwawezesha Watanzania kulifikia lengo lao kuu la kuleta mabadiliko ya kisiasa hapa Tanzania.

Ni vuguvugu la mageuzi la watangulizi wa CUF lililofanikisha kurejeshwa kwa haki ya msingi ya Watanzania ya kuwa na mfumo wa siasa unaowaruhusu kujiundia vyama vya siasa na kuchagua mfumo wa utawala na uongozi wanoutaka kupitia vyama hivyo. Ilikuwa ni vuguvugu la kisiasa la CIVIC MOVEMENT iliyokuwa ikiongozwa na Mheshimiwa James Mapalala kwa upande wa Tanzania Bara na Kamati ya Mageuzi ya Mfumo wa Vyama Huru (KAMAHURU) iliyokuwa ikiongozwa na Marehemu Shaaban Khamis Mloo kwa upande wa Zanzibar lililowazindua Watanzania kudai na kuipata haki yao hiyo ya kuzaliwa.

Tokea wakati huo, CUF haijayumba katika kutekeleza na kutimiza wajibu wake wa kihistoria wa kuwaongoza Watanzania kuleta mabadiliko ya kweli kwa kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuleta Serikali mpya ya Watanzania itakayowekwa madarakani na Watanzania kwa maslahi ya Watanzania.

Tanzania inahitaji mabadiliko. Watanzania wamechoshwa na miaka 48 ya bakora za CCM na sasa wanadai mabadiliko. Lakini mabadiliko hayawezi kuletwa na chama chochote tu cha siasa kinachodai kutaka kuleta mabadiliko. Mabadiliko ili yawe mabadiliko ya kweli na yenye tija na neema kwa Watanzania ni lazima yawe mabadiliko makini. Mabadiliko makini yanaweza kuletwa na Chama Mbadala makini tu.

CCM yenyewe haiwezi kuleta mabadiliko hayo kwa sababu haijali mahitaji ya Mtanzania na pia ndiyo iliyoleta utawala wa kifisadi na kusababisha mripuko mkubwa wa gharama za maisha. CCM haina uwezo wa kuleta ajira na maisha bora. CCM imeleta hofu na ukandamizaji na inatumia vitisho na fujo kubakia madarakani. Kwa hivyo, CCM haiwezi kuleta mabadiliko.

Vyama vingine vya siasa vimejionyesha kuwa ni vyama vilivyopo kwa maslahi ya viongozi wake wachache wanaovifanya kama ni miliki yao na ambao hawawezi kuhojiwa na hivyo kupelekea vyenyewe kuzama katika ufisadi na kushindwa kujiendesha. Vingine ni dhaifu na visivyo na mtandao wa kitaifa wa kuweza kuleta mabadiliko ya maana yatakayoleta tija.

Tofauti na CCM na vyama vingine, Watanzania wameshuhudia kwamba CUF katika miaka 17 tokea kuasisiwa kwake imekuwa ikiimarika siku hadi siku, mwaka hadi mwaka, na imeweza kujenga imani katika nyoyo za Watanzania kwamba ndiyo Chama Mbadala makini, ndiyo Chama kiongozi katika kuleta mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Chama cha CUF kimejipambanua kuwa ndiyo Chama pekee kati ya vyama vya upinzani chenye uwezo wa kuwaongoza Watanzania kuleta mabadiliko ya kisiasa yanayohitajika kwa haraka sana katika nchi yetu.

Kufanyika kwa mafanikio makubwa Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa wa CUF mwezi Februari mwaka huu ni uthibitisho tosha kwamba Chama Cha Wananchi (CUF) ndiyo Chama Mbadala chenye uwezo wa kuwaongoza Watanzania kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) na pia kutoa uongozi makini na imara utakaoleta mabadiliko ya kweli hapa nchini, mabadiliko yatakayotujengea Tanzania mpya yenye haki sawa kwa wote na ujenzi wa uchumi imara wenye kuleta neema kwa Watanzania wote.

Kufanyika kwa Mkutano Mkuu kwa kiwango cha juu cha ufanisi na oganaizesheni ni dalili ya wazi ya uwezo wa CUF. Ni ushahidi wa CUF kuwa ni Chama kilichojijenga kama taasisi kamili ya kisiasa. Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nne ulifanyika miaka mitano kamili tokea ule wa Februari 2004 na hivyo kuifanya CUF ijipambanue kwa kuweza kutekeleza sheria ya nchi inayovitaka vyama vya siasa kufanya chaguzi zake kwa vipindi vilivyotajwa ndani ya Katiba zao.

Kipimo kingine cha chama makini cha siasa ni jinsi kilivyojengeka katika muundo na mtandao wake katika pembe zote za nchi. CUF imefanikiwa kujenga mtandao wake takriban katika pembe zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. CUF ipo kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma, Tanga hadi Mtwara, Bukoba hadi Tabora, Pemba hadi Unguja. CUF imejipambanua kuwa ni Chama cha Kitaifa. Katika maeneo yote hayo, muundo wa Chama unafahamika na umejengeka kuanzia Tawi, Kata/Jimbo, Wilaya hadi Taifa.

Kuleta mabadiliko ya kisiasa katika nchi zinazoongozwa na chama dola kinachong’ang’ania kubaki madarakani kwa njia yeyote ile kunahitaji Chama Mbadala kilicho madhubuti na chenye viongozi na wanachama jasiri, wasiotetereka, wasioyumbishwa na wasio na woga. Viongozi na wanachama wa CUF tokea ngazi ya Taifa hadi Matawini wamejipambanua na kujidhihirisha kuwa ni jasiri na shupavu wasioogopa vitisho wala hujuma za chama tawala katika kutetea haki za Watanzania. Viongozi na wanachama wake wamekamatwa, wamebambikiziwa kesi, wamefungwa, wamepigwa, wamebakwa na hata kuuawa lakini hawakurudi nyuma katika mapambano ya kumkomboa Mtanzania.

Kufichua ufisadi na maovu ya chama kinachotawala ni sehemu ya wajibu muhimu wa chama cha upinzani. CUF imejipambanua kwa kuongoza mapambano ya kupiga vita ufisadi kwa kipindi chote tokea kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini. Tena CUF imejijengea sifa ya kupigana vita dhidi ya ufisadi kwa ujumla wake na siyo vita ya ufisadi inayowalenga watu maalum kwa malengo maalum tu. Tuliachiwa peke yetu vita dhidi ya ufisadi katika miradi ya IPTL, ununuzi wa rada na ndege ya rais, utolewaji wa zabuni katika manunuzi ya vifaa vya kijeshi kwa JWTZ, ujenzi wa minara pacha ya BOT na ufujaji wa fedha zilizotokana na misamaha ya madeni kutoka nje.

Kwa chama makini cha siasa kinachopigania mabadiliko, kufichua maovu na ufisadi au kwa lugha ya mitaani ‘kuripua mabomu’ pekee hakutoshi kuleta ukombozi wa kweli wa Mtanzania. Kauli za hamasa na jazba ni muhimu kuwapa wananchi ari ya kujiletea mabadiliko katika maisha yao baada ya kuangushwa vibaya sana na Serikali za CCM kwa miaka 48 sasa. Lakini ukombozi wa kweli utapatikana kwa kuwa na umma uliozindukana na unaotambua kwa nini unataka mabadiliko na ni mabadiliko gani unayoyataka.

CUF siku zote imejipambanua kwa kuja na sera mbadala zilizofanyiwa utafiti na kutayarishwa kitaalamu kwa kuzingatia misingi ya ujenzi wa uchumi imara wa kisasa. Ni CUF katika miaka mitatu sasa kupitia kwa Kiongozi wake wa Upinzani Bungeni ambayo imekuja na Bajeti Mbadala ambazo zikitekelezwa zitaweza kumkomboa Mtanzania kiuchumi na kuondokana na umasikini walioletewa na CCM ambao hauna sababu. Watanzania wamezindukana kutokana na sera hizi.

Tunawashukuru Watanzania kwa kutupa imani zao na kukubali kwamba sisi katika CUF tumeweza kujipambanua kuwa ni Chama makini kinachopambana kuleta haki sawa kwa wote na kujenga uchumi imara utakaoleta neema na tija kwa wananchi wote.

Lakini mabadiliko makubwa ya kisiasa wanayoyataka Watanzania hayawezi kuja kwa njia za kushtukiza tu. Watanzania wanastahiki kuwa na Dira ya Taifa ya kujenga nchi inayoheshimu haki za binadamu, yenye misingi mizuri ya demokrasia ambapo raia wote watu wazima na wenye akili timamu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa masuala yanayohusu maisha yao na hatma ya nchi yao.

Ni kwa sababu hiyo, CUF ilikuwa ikijipanga na sasa iko tayari na inawapa Watanzania fursa ya kuchagua Dira ya Mabadiliko (Vision for Change) na kuitumia kuongoza harakati za kuing’oa madarakani CCM kwanza kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka huu wa 2009 na kisha katika Serikali Kuu kupitia Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Dira ya Mabadiliko inayopendekezwa na CUF inatilia mkazo mambo yafuatayo:

1. Kila raia popote alipo awe na haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi toka ngazi ya kitongoji/kijiji/mtaa mpaka uongozi wa taifa.

2. Kujenga umoja wa kitaifa wa kweli ambapo hakutakuwa na ubaguzi wa aina yeyote wa jinsia, kabila, rangi, dini au ulemavu. Kuhakikisha kuwa serikali inaheshimu dini zote na inajenga mazingira ya waumini wa dini mbali mbali kuheshimiana na kuvumiliana.

3. Kuhakikisha kuwa kila mwananchi ana uwezo au anawezeshwa kupata milo mitatu kwa siku. Hatua za makusudi zichukuliwe kuhakikisha kuwa kinamama waja wazito na watoto wachanga wanapata lishe bora kwani mtoto mchanga asiye na lishe bora ananyimwa haki ya kujenga mwili, kinga ya mwili na ubongo wake ili aweze kushiriki kikamilifu katika kujielimisha na kujiendeleza na kufikia uwezo wake aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

4. Kuhakikisha kuwa kila raia ana haki na anapata huduma za msingi za afya. Hatua maalum zichukuliwe kuhakikisha kuwa huduma za uzazi anapatiwa kila mama mja mzito ili kupunguza vifo vingi vya kusikitisha vya kina mama waja wazito.

5. Wazee wengi baada ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu wanaishi katika umaskini wa kutisha. Watoto wao hawana kipato cha kutosha na maadili ya kuwalea wazee yameporomoka. Kama taifa ni muhimu turejeshe na kujenga maadili ya kuwaheshimu na kuwaenzi wazee wetu. Tuweke utaratibu wa kitaifa wa hifadhi ya wazee itakayohusisha jamii kuwalea wazee wetu.

6. Elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Ili kujenga taifa linalojiamini, watoto wote wa Tanzania wawe na haki ya kupata elimu bora ya msingi na ya sekondari. Taifa lijenge utamaduni wa kuamini kuwa elimu haina mwisho na kila raia ajiendeleze kielimu hasa kwa kutumia vizuri teknolojia ya habari na mawasiliano.

7. Elimu ya wasichana ni nyenzo muhimu ya kuleta haki sawa kwa wananchi wote na kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa na fursa sawa katika kuleta na kuneemeka na maendeleo. Wasichana wengi hawamalizi masomo yao kwa sababu ya uwezo wa fedha wa wazazi, mila zilizopitwa na wakati zinazowabagua wasichana na wanawake, mazingira mabovu ya shule kama vile kutokuwa na vyoo vya wanawake mashuleni na mambo mengine kama hayo. Motisha maalum utolewa kwa wasichana na familia zao ili wasichana wamalize elimu ya shule ya msingi na waendelee na elimu ya sekondari.

8. Kuwaelimisha wasichana na wanawake kushiriki katika soko la ajira ni nyenzo muhimu ya kuvunja mduara wa umasikini unaorithisha umaskini toka kizazi kilichopo na kinachofuata.

9. Ili kufanikisha mabadiliko ya kiuchumi, kuongeza tija na ajira, Taifa litoe kipaumbele maalum katika kuendekeza elimu ya sayansi na teknolojia.

10. Kujenga uchumi wa kisasa wenye ushindani kimataifa na utakaohimili misukosuko ya utandawazi, unaokua kwa kasi bila kuharibu mazingira na wenye manufaa kwa wananchi wote.

11. Wananchi wahisi na waone kuwa uchumi wa taifa unatoa fursa sawa kwa wananchi wote. Tofauti za vipato vya wananchi visiwe vikubwa mno huku tukizingatia kutoa motisha kwa raia kuwa wabunifu na wajasiriamali hodari. Mikakati ya kukuza uchumi itafanikiwa iwapo itatoa fursa kwa wananchi wote kufaidi matunda ya kukua kwa uchumi.

12. Haiwezekani Watanzania kuondokana na umaskini bila kukuza uchumi unaoongeza ajira. Ikiwa pato la taifa la mwaka 2007 lingegawanywa sawa sawa kwa kila Mtanzania, kila mmoja wetu angepata dola za kimarekani 428 kwa mwaka sawa na dola 1.17 kwa siku au shilingi za Tanzania 1340/- kwa siku.

13. Bila kukuza uchumi umaskini uliokithiri utakuwa tatizo la kudumu. Katika suala la kukuza uchumi hakuna miujiza. Uchumi unakua kwa kuongeza elimu, ujuzi na utaalamu wa wafanyakazi, ongezeko la rasilimali na vitendea kazi, na kuongezeka kwa ufanisi na tija katika uzalishaji na utoaji huduma. Kukua kwa uchumi kunahitaji uongozi imara na utawala bora, mikakati na mipango mizuri ya maendeleo na utekelezaji mzuri wa mikakati na mipango hiyo. Kazi ya kukuza uchumi itakuwa rahisi ikiwa tutatumia raslimali na mali ya asili ya nchi hii kwa manufaa ya wote. Tunapaswa kukipa kilimo nafasi ya pekee katika mikakati ya kukuza uchumi na hivyo kuwaondolea umasikini wananchi wa vijijini ambao wameumizwa vibaya na sera mbovu za CCM zisizotoa kipaumbele kwa kilimo.

Tanzania haiwezi kufikia malengo ya maendeleo ya milenia mwaka 2015 hata baada ya kupata misaada mingi ya kimataifa. Malengo haya ya kimataifa yanakusudia kupunguza umaskini, kutoa elimu ya msingi kwa wote, kupunguza maambukizo ya maradhi kama UKIMWI, Malaria na Kifua kikuu, kupunguza vifo vya watoto na kina mama waja wazito. Ukosefu wa uongozi unaojali maslahi ya Mtanzania wa kawaida ndio kikwazo kikubwa cha kufikia malengo ya milenia (angalia kiambatisho).

Mpaka hivi sasa hatuna Dira ya Maendeleo na mikakati madhubuti ya utekelezaji inayoeleweka kwa wananchi wote. Dira ya Maendeleo ya 2025 ilitayarishwa na wataalamu kuliko kuwashirikisha jamii kwa ujumla, haieleweki kwa wananchi wengi na haitumiwi kuhamasisha wananchi katika ujenzi wa taifa letu. Ukosefu wa uongozi ni kizingiti kikubwa kinachozuia kupitia, kuchambua na kubuni dira ya maendeleo inayozingatia hali halisi ya nchi yetu na mabadiliko ya uchumi duniani.

Chama cha CUF kupitia mijadala na wananchi kimeandaa Dira hii ya Kuleta Mabadiliko (Vision for Change) itakayoonyesha njia ya kuleta haki sawa kwa wananchi wote na kujenga uchumi imara unaokua na kuleta neema na tija kwa wananchi wote. Dira hii ya Mabadiliko itafikishwa kwa wananchi kupitia Operesheni Zinduka.

Operesheni Zinduka itaanza rasmi katika mkoa wa Mwanza tarehe 11 Julai, 2009 na baadaye kuendelea katika mikoa mingine. Ratiba ya awali itatufikisha katika mikoa 11 ya Tanzania Bara kama ifuatavyo:

TAREHE

MKOA
11 – 20 Julai, 2009 Mwanza
21 – 30 Julai, 2009 Kagera
1 – 10 Agosti, 2009 Mara
16 – 25 Agosti, 2009 Shinyanga
1 – 10 Septemba, 2009 Tabora na Wilaya ya Kondoa
16 – 25 Septemba, 2009 Tanga
16 – 25 Oktoba, 2009 Dar es Salaam
1 – 10 Novemba, 2009 Pwani
16 – 25 Novemba, 2009 Lindi
1 – 10 Desemba, 2009 Mtwara
6 – 15 Januari,2010 Ruvuma
21 – 30 Januari, 2010 Mbeya
16 – 20 Februari,2010 Morogoro

Ratiba kama hii itakuwa ikifanyika mfululizo kwa upande wa Zanzibar ukijumuisha Wilaya 10 za visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa nini CUF kiongoze mabadiko?

Chama Cha Wananchi (CUF) ndiyo chama kikuu cha upinzani hapa Tanzania. CUF kinasimamia kuwepo kwa Serikali inayomjali kila mmoja wetu. CUF kinaamini katika uhuru wa mtu na uwezo wa kujisimamia dhamana zake, kinaamini katika haki za binadamu na amani ya kweli, na kinaamini katika haki na utawala wa sheria. CUF ni chama kinachojali na kinachotaka mabadiliko yatakayotupa mustakbali mwema katika hali ya utulivu.

Chama Cha Wananchi (CUF) kikiwa pamoja na familia za Watanzania kinataka kuwepo elimu bure na yenye manufaa hadi sekondari na kutoa mikopo ya asilimia mia moja kwa wanafunzi wa elimu ya juu na pia huduma bure na zinazoridhisha za afya ya msingi kwa wananchi wote.

CUF kinafahamu na kuelewa maisha ya wasiwasi ya familia za Watanzania yanayotokana na kupanda mara kwa mara kwa gharama za maisha, upungufu wa chakula na maji safi na salama, ukosefu wa ajira na usalama wa ajira zilizopo na pia kushindwa kwa Serikali iliyopo madarakani kutekeleza ahadi zake ilizozitoa.

CUF ina sera imara na zenye ufanisi zitakazotujengea uchumi wa kisasa na wenye tija na neema unaotilia mkazo ukuzaji na uimarishaji wa kilimo na kutoa ajira nyingi na bora, wenye kuhakikisha soko za bidhaa za wakulima na kuongeza pato la familia. CUF inawaunga mkono Watanzania wote katika mapambano yao ya kuleta maisha bora na yenye heshima kwa utu wa binadamu.

CUF ni Chama Mbadala kilichodhamiria kuongoza Serikali Mbadala itakayojenga Tanzania mpya isiyo na woga, ukandamizaji, ufisadi, uvunjwaji wa haki za binadamu na vitisho. CUF iko pamoja na wananchi wote wanaoathirika kutokana na kushindwa kabisa kwa serikali isiyo na uwezo na ya kifisadi, na inatoa matumaini mapya kwa wote wanaokandamizwa, kuonewa na kukatishwa tamaa na watawala waliopo.

Wananchi wa Tanzania kwa ujumla wao, bila ya kujali dini, kabila, rangi, tabaka au jinsia zao, wanaweza kuiamini CUF na viongozi wake wa ngazi mbali mbali. Wananchi wote wanaotaka kuleta mabadiliko kwa ajili ya mustakbali mwema wenye kutoa neema, amani, haki na uadilifu wanapaswa kuiunga mkono CUF kwa kujiunga nacho kuleta mabadiliko hayo kuanzia mwaka huu 2009 na kuikamilisha 2010.

Sisi tuko tayari. Tunawaomba Watanzania watuunge mkono tulete mabadiliko.

TANZANIA BILA CCM INAWEZEKANA,
KILA MPENDA HAKI ATIMIZE WAJIBU WAKE.

Ahsanteni sana.

Advertisements

One thought on “Prof. Lipumba azindua Operesheni Zinduka

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s