Ujumbe wa Maalim Seif kwa Wapemba

”Kila Mzanzibari mwenye haki, ahakikishe anajiandikisha kwenye Daftari!”

• Akagua shughuli za Chama, kuhamasisha Daftari
• Aonya rafu za CCM, ZEC na Afisi ya Vitambulisho
• Amwambia Kikwete hatapata kumweka kibaraka wake kuchimba mafuta ya Wazanzibari
• Afanya mikutano mitano ya hadhara
• Jumapili aunguruma Gombani

Katibu Mkuu wa The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi), Maalim Seif Sharif Hamad, yuko kisiwani Pemba katika ziara ya wiki moja. Ziara hiyo ilianza tarehe 31 Juni na itamalizika tarehe 4 Julai kwa mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya Gombani, Chake Chake.

Hadi sasa, Maalim Seif ameshatembelea na kufanya mikutano ya hadhara katika majimbo ya Micheweni, Tumbe na tarehe 3 Julai atakuwapo kwenye jimbo la Mgogoni.

Mbali na kukagua uhai wa Chama na kuonana na wananchi, Maalim Seif anatumia fursa ya ziara hizi kupeleka ujumbe maalum kwa wakaazi wa Pemba, ambao ni kuwataka wajitokeze kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kuanza katika wilaya ya Micheweni, mkoa wa Kaskazini, Pemba, kuanzia tarehe 6 Julai mwaka huu. Kwamba kila mmoja ahakikishe kuwa anaandikishwa kuwa mpiga kura. Ujumbe huu unakwenda sambamba na azma ya CUF kuhakikisha kuwa Pemba inabakia kuwa ngome yake isiyopenyeka wala kutetereka.

Ujumbe huu wa Maalim Seif unakuja katika wakati ambapo tayari CUF imekusanya ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa kuna ‘utatu’ usio mtakatifu (trinity of the demons) baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Idara ya Vitambulisho Zanzibar, unaopanga njama za kuhakikisha kuwa wakaazi wengi wa Pemba hawaandikishwi kuwa wapiga kura. Katika mtandao huu, njama iliyopangwa ni hii: SMZ iwatumie masheha wake kuhakikisha kuwa hawatoi baru za uthitisho kuwapa watu wanaodai vitambulisho vya Uzanzibari, Idara ya Vitambulisho isimpe kitambulisho hicho mtu ambaye hana barua ya sheha na ZEC isimuandikishe kuwa mpiga kura mtu ambaye hana kitambulisho. Hadi sasa watu 18,000 kisiwani Pemba pekee wamesharipoti kunyimwa vitambulisho hivyo vya ukaazi huku hata zoezi la uandikishaji wapiga kura likiwa halijaanza. Lakini, licha ya kuwepo kwa taarifa hizo, ujumbe wa Maalim Seif kwa wananchi wa Pemba unabakia kuwa ule ule: lazima wahakikishe kuwa kila mwenye haki ya kuwa mpiga kura anaingia kwenye Daftari hilo.

Kwa ZEC, SMZ na Idara ya Vitambulisho, ujumbe wa Maalim Seif ni kwamba kinachofanywa na taasisi hizo kinaipeleka nchi katika machafuko na matatizo makubwa, ambayo ni wao ndio watakaobeba lawama kwa matokeo yoyote yatakayotokea. CUF kila siku itasimama upande wa haki na sio tu kuhakikisha kuwa haki hiyo ipo, lakini kuona kuwa haki hiyo inatendeka.

Kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, ujumbe wa Maalim Seif uko wazi. Kwamba Rais Kikwete ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na kwamba yeye ndiye mwenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao. Kwa hivyo, asijiwache kuchukuliwa na andasa za kihafidhina zilizopo Zanzibar na kuja kusababisha kuvunjiwa heshima yake. Atumie nafasi zake alizonazo kuhakikisha haki inatendeka Zanzibar na sio kutumia nafasi hizo kutafuta wakala wa kumuweka madarakani kwa lengo la kupata wepesi wa kuyachimba mafuta ya Wazanzibari. Hilo halitavumiliwa hata kidogo na Wazanzibari na halitakuwa na manufaa kwake binafsi na kwa nchi nzima kwa jumla. Maalim Seif anamtaka Rais Kikwete asifuate nyayo za mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, ambaye anajuilikana kwenye kama kiongozi aliyesimamia mauaji ya Januari 2001 na kuzalisha wakimbizi kwa mara ya mwanzo katika historia ya Tanzania huru.

Kwa jumuiya za kimataifa, hasa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ambalo linafadhili zoezi hilo la kuandikisha wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu, ujumbe wa Maalim Seif ni kwamba taasisi hiyo ya kimataifa ijitoe mara moja katika ufadhili huo hadi hapo itakapohakikishiwa kwa vitendo kwamba SMZ na ZEC hazitumii nafasi zao kuwanyima haki zao Wazanzibari. Kuendelea kufadhili zoezi hili, anasema Maalim Seif, ni sawa na taasisi hiyo ya kimataifa kushiriki katika mpango wa kuiviza demokrasia Zanzibar, ilhali ilivyotakiwa ni kwamba UNDP isaidie kuimarisha demokrasia na haki za binaadamu.

Imetolewa leo tarehe 1 Julai 2009 na:

Kurugenzi ya Uenezi na Mahusiano na Umma
The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi)
S. L. P 3537
Simu: 0777 414 112
E-mail: cufhabari@yahoo.co.uk
Weblog: https://hakinaumma.wordpress.com

Advertisements

One thought on “Ujumbe wa Maalim Seif kwa Wapemba

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s