“Bila nishati mbadala, uhifadhi wa mazingira ni ndoto”

“Bila maji hakuna maisha na ili maji yapatikane lazima vyanzo hivyo vya maji vilindwe . Bado tafsiri ya chanzo cha maji kina utata kisheria, kwa kuangalia Sheria ya mwaka 2002 na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004. Sheria zote hizi zina vipengele vya utunzaji au kuhifadhi vyanzo vya maji. Sheria ya maji hairuhusu kufanyika shughuli za kudumu za binadamu katika mita 200 kutoka mto au vijito na mita 500 kutoka kwenye maziwa au bahari, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 yenyewe katika kipengele cha 57(1) hairuhusu kazi za kibinaadamu kufanyika kwenye vianzio vya maji mita 60. Sheria hizo zinakinzana pamoja na kwamba kipengele namba 232 kinaipa uwezo Sheria ya Mazingira kuamua umbali huo.”

Hemed Khamis Salim, Mbunge wa Chambani (CUF)

Hemed Khamis Salim, Mbunge wa Chambani (CUF)

HOTUBA YA MHESHIMIWA ALI KHAMIS SEIF (MB) MSEMAJI MKUU KAMBI YA UPINZANI OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MAZINGIRA KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2009/2010

Mheshimiwa Spika,
Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani juu ya mazingira kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 99(3) na (7) Toleo la 2007.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani kwa viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani, Chama changu cha Wananchi CUF na wapiga kura wangu wa jimbo la Mkoani. Wapiga kura hao ninawaahidi nitaendelea kuwa pamoja nao na sitowaangusha.

Mheshimiwa Spika, mwisho katika shukrani lakini kwa umuhimu mkubwa natoa shukrani na pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote kwa kazi kubwa ya kuliongoza vyema Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, mazingira endelevu yana uhusiano mkubwa na maisha ya binadamu pamoja na viumbe hai wengine. Binadamu anahitaji maji, chakula nishati na kadhalika katika kuendeleza maisha yake ya kila siku.

MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mheshimiwa Spika, Mabadiliko ya tabia nchi ni mabadiliko yanayotokezea juu ya uso wa dunia kwa kasi na kwa muda mfupi (mfano mafuriko, vimbunga, ukosefu wa mvua mfululizo) ama yanayotokea taratibu na yanayochukuwa muda mrefu ambayo ni ya kudumu kutokana na ongezeko la gesi joto zinazozalishwa na shughuli za binadamu.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya mabadiliko hayo ni kina cha bahari kimepanda kwa sentimeta 17 juu ya usawa wa bahari kwa miaka 100 iliyopita. Joto la dunia limeongezeka kwa nyuzi joto 0.740C kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita na gesi joto aina ya karbon dioxide (Carbon Dioxide) limeongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa nchi yetu utafiti uliofanywa nchini kote umeonyesha joto limeongezeka kwa nyuzi joto 0.20C na kwa Nyanda za Juu Kusini ni nyuzi joti 0.60C.

Mheshimiwa Spika, athari ya mabadiliko ya tabia kwa dunia ni kama ifuatavyo:
– Ongezeko la vimbunga na majanga mengine ya kimazingira kama ukame na mafuriko.
– Baadhi ya mazao na mifugo haitaweza kuhimili hali ya joto kubwa
– Upatikanaji wa maji duniani kote utapungua sana, vilele vya milima vitayeyuka.
– Nchi maskini duniani ndizo zitakazoathirika zaidi.
– Wanyamapori watakufa ama kukosa mazingira ya kuzaliana.
– Viumbe vya bahari ikiwa ni pamoja na matumbawe vitaathirika au kupotea kabisa.
– Visiwa vidogo vitamezwa.

Mheshimiwa Spika, athari ya mabadiliko ya tabia nchi yanaanza kuonekana katika nchi yetu kama ifuatavyo:-

– Malaria sasa iko katika maeneo ya baridi ambapo haikuwepo kabisa.
– Ziwa Rukwa limerudi ndani kwa kilometa saba
– Uyeyukaji wa theluthi Mlima Kilimanjaro.
– Maji ya chumvi yanaingia katika visima vya maji baridi katika ukanda wa pwani Bagamoyo, Pangani na Rufiji.
– Kutoweka kwa kisiwa cha Maziwe (Pangani) na Fungu la Nyani (Rufiji).
– Ukuta wa Pangani sasa maji yanapita juu wakati wa maji kujaa na kuhatarisha maisha ya wakazi wa mji huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu lazima iwe na mikakati madhubuti ya kupunguza athari ya mabadiliko ya tabia nchi, haitoshi kuridhia mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi na itifaki ya Kyoto peke yake. Jee, Serikali imefanya miradi gani kama nchi kupunguza athari ya mabadiliko ya tabia nchi?

HALI YA MAZINGIRA KWENYE ARDHIOEVU YA IHEFU NA UZALISHAJI WA UMEME BWAWA LA MTERA.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2006 wafugaji walihamishwa eneo la Ihefu kwa nia ya kuilinda ardhi oevu ya hapo ili hali irejee katika uoto wake wa asili na kuwezesha maji yaweze kutiririka mwaka mzima kwenda Mto Ruaha Mkubwa na hatima yake yafike Bwawa la Mtera kwa kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Spika, mto Ruaha Mkubwa humwaga maji yake kiasi ya 56% kwenye Bwawa la Mtera. Mito mingine Ruaha mdogo (18%) na Mto Kisigo 26%. Bonde la Usangu linapata maji kutoka mito ya Kioga, Mbarali, Kimbi, Mkoji na Ndembera. Mito mingine inayotiririsha maji mwaka mzima ni sehemu ya juu ya Ruaha Mkubwa, Kimani na Chimala.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo hili lina mteremko mdogo sana kati ya (1020m – 1050m) juu ya usawa wa bahari inabidi eneo hilo liwe na maji mengi ili yawezeshe kutiririka kutoka ardhi oevu ya Magharibi – Mashariki – Ihefu Ngiriama Mto Ruaha mkubwa – Mtera – Kidatu kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Spika, Licha ya kuwa eneo hilo lilikuwa likiathiriwa na ufugaji na ndio wafugaji wakahamishwa, hivi sasa katika kupatikana maji ya kutosha ili yaweze kutiririka mwaka mzima kwenda Mto Ruaha mkubwa kunaweza kuathiriwa na kilimo cha mpunga cha wakulima wadogo wadogo kwani maji yanayotumika mengi hayaendi kwenye Mto Ruaha mkubwa.

Hili ni tatizo kwani wananchi wengi wa maeneo hayo, wanategemea kilimo cha mpunga katika maisha yao pia.

Mheshimiwa Spika, katika kulitatua tatizo hilo Serikali iwe makini sana kwa kuona njia gani wakulima hawa hawataathirika na ufumbuzi wa tatizo hilo. Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali hao wananchi watakaoathirika na tatizo hilo wagawiwe kwenye mashamba makubwa yaliyobinafsishwa ili wakulima hao wayaache mashamba yao madogo na kuruhusu maji kuweza kutiririka kwa mwaka mzima kuelekea Mto Ruaha Mkubwa Bwawa la Mtera na Kidatu ili tuweze kupata umeme.

NISHATI YA KUNI NA MKAA NA ATHARI KWA MAZINGIRA

Mheshimiwa Spika, Asilimia kubwa sana ya wananchi wa nchi hii wanatumia nishati ya kuni na mkaa kwa kupikia. Ni dhahiri kabisa ukataji wa miti ili kukidhi haja hiyo ni mkubwa kila mwaka. Inabidi iwe hivyo kwa sababu Serikali haijakuwa na mkakati wa kuwa na nishati mbadala ya kupikia itakayotumiwa na wananchi wengi.

Mheshimiwa Spika, kusamehewa ushuru Moto Poa sio suluhu kuunusuru uharibifu wa mazingira kwa ukataji miti kwani wenye uwezo wa kutumia nishati hiyo ya kupikia ni wachache mno.

Mheshimiwa Spika, Serikali bila ya kuwa makini kwa suala hilo la nishati mbadala ya kupikia badala ya mkaa au kuni, uhifadhi wa mazingira kwa kutokata miti utakuwa ni ndoto.

Mheshimiwa Spika, nchini Malawi kwa kupitia taasisi inayoitwa Habitant for Humanity ilianzisha mradi wa kupunguza ukataji mkubwa wa miti. Taasisi hiyo ilihakikisha upunguzwaji wa bei za saruji ili wanajamii waweze kuhimili hiyo kwa kutumia saruji badala ya miti lakini kama kwamba haitoshi pia walihakikisha bei za umeme zinakuwa chini, pia walianzisha teknolojia ya kutumia majiko ya nguvu ya jua na yanayotumia mkaa kidogo (Solar box cooker and fuel efficient charcoal stoves). Jee, Serikali ina mkakati gani wa uhakika wa kupatikana nishati mbadala ya kupikia tena yenye bei nafuu baadala ya kutegemea kuni na mkaa?

MAJI NA MAZINGIRA

Mheshimiwa Spika, bila maji hakuna maisha na ili maji yapatikane lazima vyanzo hivyo vya maji vilindwe . Bado tafsiri ya chanzo cha maji kina utata kisheria, kwa kuangalia Sheria ya mwaka 2002 na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004. Sheria zote hizi zina vipengele vya utunzaji au kuhifadhi vyanzo vya maji. Sheria ya maji hairuhusu kufanyika shughuli za kudumu za binadamu katika mita 200 kutoka mto au vijito na mita 500 kutoka kwenye maziwa au bahari, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 yenyewe katika kipengele cha 57(1) hairuhusu kazi za kibinaadamu kufanyika kwenye vianzio vya maji mita 60. Sheria hizo zinakinzana pamoja na kwamba kipengele namba 232 kinaipa uwezo Sheria ya Mazingira kuamua umbali huo.

Mheshimiwa Spika, Uhifadhi wa mazingira uendane na uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuyalinda maji yasichafuliwe ili tupate maji safi na salama. Kwa mfano mgodi wa Geita unamwaga taka taka zake zenye sumu katika bwawa la Mtakuja. Mgodi wa North Mara ni hivyo hivyo nao unatoa taka taka za sumu.

Mheshimiwa Spika, Leo hii kijiji cha Nyakabale chenye watu zaidi ya 600 Kaskazini ya machimbo ya Geita watu wake wanaishi kwa wasiwasi mkubwa juu ya maisha yao, kwani wengi wao wanakunywa maji hayo ambayo si salama kwa afya zao.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba zetu za Kambi ya Upinzani mwaka 2007/08 na 2008/09 tulielezea wasiwasi wetu juu ya Mgodi wa North Mara huko Tarime na kemikali zinazotiririka kwenye mto, naomba ninukuu kutoka katika hotuba ya mwaka 2007/08, “madhara mengine ambayo yanatarajiwa kutokea ni yale yanayosababishwa na Mgodi wa North Mara kutupia taka zenye sumu katika mto TIGITI ambao ni tawi la mto Mara unaoingia ziwa Viktoria. Hapa tujaribu kujiuliza ni watu wangapi wanatumia maji na samaki kutoka katika ziwa Viktoria”.

Mheshimiwa Spika,tuliitaka Serikali kuchukua hatua zinazostahili, lakini kwa sababu wasemaji na wapinzani tukapuuzwa. Leo Serikali inatamka nini kuhusu yaliyotokea huko Mara?

Mheshimiwa Spika, ni majuzi tu imeripotiwa na gazeti la Mtanzania Jumapili la tarehe 21/06/2009 kuwa watu 21 wafa kwa kuoga maji ya sumu na watu walinusurika wanachubuka ngozi, mifugo 270 yapoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, tunazidi kuieleza Serikali kuwa uzembe na kutokujali kunakofanywa na wale waliopewa mamlaka kutatupeleka pabaya. Angalizo hili la kuwepo kwa hatari tulikwishalitoa. Hivyo basi Kambi ya Upinzani inawataka walioshindwa kuchukua hatua katika kuhakikisha sumu hizo zinasitishwa kuingia katika mto Tigiti wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Spika,
Hali hiyo inaendelea wakati Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) lipo, na hatujui hatua gani imechukuwa kwa makampuni hayo au inaogopa kuwakera wawekezaji. Serikali itueleze vipi usalama wa afya zao unalindwaje kwa wananchi hao?
Pia Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya fidia wanayotakiwa kupata waathirika wa uharibifu huo wa mazingira toka makampuni ya madini kuwepo maeneo hayo.

BARAZA LA TAIFA LA UHIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA (NEMC)

Mheshimiwa Spika,
Baraza hili ndio chombo kikuu kisheria kinachohusiana na usimamizi wa mazingira. Uwezo huo uko kwenye sheria Na. 20 ya mwaka 2004. Kwa kuwa Baraza hili lina wafanyakazi wachache na karibu wote wako Dar es Salaam ni dhahiri utendaji wake kwa nchi nzima utakuwa hauridhishi.

Mheshimiwa Spika, utumiaji wa mifuko ya plastiki isiyo ruhusiwa hasa kwa mikoa nje ya Dar es Salaam unaendelea kama kwamba haijapigwa marufuku. Hilo linafanyika kwa sababu Baraza halikuenea nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali itueleze kwa uchache wa wafanyakazi kwenye Baraza hili kweli linasimamia suala zima la mazingira?
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya naomba kuwasilisha.

…………………………
Ali Khamis Seif (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani-
Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.
29.06.2009

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s