“Serikali ya Muungano haisikilizi”

Sisi wa Kambi ya Upinzani tunaamini kwamba ni kosa kubwa dhidi ya sheria zinazolinda mikataba ya kimataifa na, kwa hakika, ni hatua ya hatari kwa khatima njema ya Muungano huu, kwa ofisi za waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ambayo Zanzibar ni sehemu yake) na Waziri Kiongozi (ambayo ni ya Zanzibar tu kama mwasisi wa Muungano wenyewe) kujadili mustakbali wa Muungano.

Riziki Omar Juma, Mbunge - CUF

Riziki Omar Juma, Mbunge – CUF

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI, MHE. RIZIKI OMAR JUMA (MB), KUHUSU MAKADIRIO NA MATUMIZI YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS MAMBO YA MUUNGANO KWA MWAKA WA FEDHA 2009/2010

1. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
Kwa idhini yako napenda kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Masuala ya Muungano) kwa mwaka wa fedha 2009/2010, kama inavyoelekezwa na Kanuni za Bunge toleo la Mwaka 2007, Ibara ya 99 (3) na (7).

Mheshimiwa Spika,
Natoa shukrani za dhati kwako wewe binafsi kwa kunipa fursa hii ya kutoa mtazamo wa Kambi hii. Naushukuru pia uongozi mzima wa chama changu, Chama cha Wananchi (CUF- The Civic United Front), viongozi wangu wa Kambi chini ya Mhe. Hamad Rashid Mohammed na Mhe. Dk. Wilbrod Slaa kwa imani na ushirikiano wao kwangu.

2. VIKAO BAINA YA OFISI ZA WAZIRI MKUU NA WAZIRI KIONGOZI NA HATIMA YA MATATIZO YA MUUNGANO

Mheshimiwa Spika,
Isingelikuwa ulazima wa kutimiza jukumu la Kambi ya Upinzani la angalau kusema chochote katika kila kikao cha Bunge la Bajeti, basi leo sisi tungenyamaza kimya kuhusu suala hili la Muungano. Sababu ni kwamba, namna serikali ya Muungano inavyofanya kazi kushughulikia matatizo ya Muungano ni kama kwamba haitaki kusikia upande mwengine wa mawazo. Inapenda kujifungia chumbani na kujisikiliza yenyewe ndani ya viambaza vinne.

Mheshimiwa Spika,
Tunasema hivyo kwa kuwa zile hoja za msingi tunazozitoa kuhusu matatizo ya Muungano, hazionekani kabisa kupewa nafasi katika maamuzi ya vipi Muungano huu uendeshwe. Kwa mfano, Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukisema mara kadhaa huko nyuma – na hapa tutarejea – kwamba, tatizo kubwa la Muungano huu ni kutokuheshimiwa kwa Mkataba wake uliouunda. Kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano inakhalifu, kwa kiasi kikubwa, makubaliano hayo na, kwa hivyo, ni katiba iliyokwenda kinyume na msingi iliyoiunda. Kwamba Muungano huu haukuundwa, na wala hautakiwi uongozwe, na katiba. Bali Mkataba. Kile Katiba zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar zilichotakiwa kukifanya, ni kuutafsiri Mkataba ule tu, na si vyenginevyo. Inapotokezea kuwa Katiba imesema kinyume na Mkataba wa Muungano, ni Katiba ndiyo ambayo itakuwa imekosea na lazima irekebishwe mara moja kuondoa kosa hilo.

Mheshimiwa Spika,
Tunasema hivi tukielewa kuna hivi vinavyoitwa vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Muungano na ya Zanzibar kujadili ’kero’ za Muungano. Sisi tunahoji mambo mawili kuhusiana na vikao hivi: kwanza, uhalali wake panapohusika dhati ya Muungano huu na, pili, utayarifu wake wa kushughulikia tatizo halisi lililopo.

2.1 Uhalali wa Vikao vya Pamoja na Dhati ya Muungano

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuzingatia Asili ya Muungano huu, ambayo iko wazi ni kwamba wetu ni Muungano uliotokana na sababu tatu kuu, ambazo ni udugu wa kihistoria baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar, vuguvugu la kulileta pamoja Bara la Afrika, maarufu kama ’Pan-Africanism Spirit’, na zile hisia kwamba Umoja ni Nguvu (United We Stand). Kunatajwa pia sababu za kuipatia ulinzi Zanzibar, ambayo siku mia moja tu kabla ya Aprili 26, 1964 ilikuwa imefanya mabadiliko ya utawala kwa njia ya Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika,
Ama iwe sababu hizo zinatosha kueleza Asili ya Muungano huu au la, ukweli ni kwamba Muungano ulifanyika na Mkataba wake ukasainiwa na mwakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Marehemu Abeid Karume, na wa Jamhuri ya Tanganyika, Marehemu Julius Nyerere. Ukweli huu wa kwamba waliotia saini Mkataba wa Muungano ni wawakilishi wa Tanganyika na Zanzibar, ndio unaojenga hoja ya ukosefu wa uhalali kwa kikao chochote cha kuujadili Muungano ambacho hakihusishi pande husika za Mkataba wenyewe.

Mheshimiwa Spika,
Sisi wa Kambi ya Upinzani tunaamini kwamba ni kosa kubwa dhidi ya sheria zinazolinda mikataba ya kimataifa na, kwa hakika, ni hatua ya hatari kwa khatima njema ya Muungano huu, kwa ofisi za waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ambayo Zanzibar ni sehemu yake) na Waziri Kiongozi (ambayo ni ya Zanzibar tu kama mwasisi wa Muungano wenyewe) kujadili mustakbali wa Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Tunajenga hoja hii kuhusiana na hili: kwanza, wanaostahili kuujadili na kuutolea maamuzi Muungano ni Serikali ya Zanzibar na mwenzake aliyetiliana saini Mkataba wa Muungano, ambayo ni Serikali ya Tanganyika. Uongozi wa Serikali hizo ndio waliokuwa washiriki wa mazungumzo ya kuunda Muungano kwa niaba ya nchi zao. Pili, kilichotokea mwaka 1964 ni Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika kukubaliana kuanzisha ushirika wao unaoitwa Muungano. Katika kulinda heshima za mataifa yao, viongozi hao waliweka saini Mkataba wa makubaliano yao, ambao una kila sifa ya kuwa Mkataba wa Kimataifa unaostahiki kuheshimiwa na pande husika. Na, tatu, kutokana na kwanza na pili hapo juu, kwa hivyo, ni upotoshaji wa makusudi kuuchukuwa mjadala wa nchi mbili zilizoungana na kuukabidhisha mikononi mwa vyombo visivyohusika na kuvipa vyombo hivyo mamlaka ya kufanya maamuzi yote.

Mheshimiwa Spika,
Kwa lugha rahisi ni kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu haina sifa ya kuuwakilisha upande wa pili wa Muungano, maana hii ni Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Zanzibar ni sehemu yake. Ifahamike kwamba, hatuhoji uwezo wa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda, kama mtu binafsi. Tunahoji uwezo wa kisheria wa taasisi anayosimamia kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano. Taasisi hii ni taasisi ya Muungano, ambao ndio unaojadiliwa hapa, na si taasisi ya Tanganyika, ambayo tunaambiwa haipo!

Mheshimiwa Spika,
Tunachelea sana kusema kwamba kile kinachofanywa sasa na ofisi za Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi ni kizungumkuti; maana ni kukichukuwa kiumbe na kukiweka na mmoja kati ya waumbaji wake kukijadili kiumbe hicho. Kiumbe hapa ni Serikali ya Muungano na mmoja wa waumbaji ni Serikali ya Zanzibar. Tutaendelea kufanya kizungumkuti hiki hadi lini huku, kwa makusudi, tukizikengeuka sheria za kimataifa, kama ile ya Common Law na Vienna Convention, ambazo hutakiwa kuongoza mikataba ya kimataifa kama huu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?

Mheshimiwa Spika,
Kambi yetu inasema haya ikijuwa wazi kwamba, kumekuwa na kisingizio kutoka upande wa Serikali ya Muungano kwamba hakuna Serikali ya Tanganyika na, hivyo, haiwezekani kwa Serikali ya Zanzibar kufanya mazungumzo na serikali isiyokuwepo. Sisi tunasema kwamba hiki ni kisingizio dhaifu na cha hila tu. Ni dhaifu kwa kuwa hata kwa kuuliza swali jepesi la “kwani Muungano huu ni wa nani na nani?”, jibu litakuwa ni wa Tanganyika na Zanzibar. Ni cha hila kwa sababu mbili: kwanza, hakuna popote kwenye Mkataba wa Muungano ambapo paliagizwa kufutwa kwa Serikali ya Tanganyika baada ya Muungano huu. Kwa mujibu wa Makubaliano hayo, Serikali ya Tanganyika – kama ilivyo ile ya Zanzibar – imelindwa na Kifungu Na. (v) kinachosomeka kwamba:

“The existing laws of Tanganyika and of Zanzibar shall remain in force in their existing territories.”

Mheshimiwa Spika,
Wataalamu wa Katiba na Sheria wanafahamu kwamba Katiba ndiyo “Sheria Mama” ya sheria zote na, hivyo, Katiba ya Tanganyika imelindwa na inapaswa kuwepo na Serikali yake iwepo pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo ya Tanganyika yasiyokuwa ya Muungano. Katiba na Sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la Tanganyika kwa yale mambo yasiyokuwamo kwenye Muungano. Hiyo ndiyo maana ya ‘respective territories.’

Mheshimiwa Spika,
Kwa hivyo, kilichofanywa na Bunge la Tanganyika tarehe 25 Aprili 1964, siku moja kabla ya Muungano, ‘kuifuta’ serikali ya Tanganyika kwa kutumia Sheria Na. 22 iliyoitwa “Union of Tanganyika and Zanzibar”, kilikuwa kinyume na Makubaliano ya Muungano. Bahati mbaya, kitendo kile mpaka leo kimebakia kikiongeza shaka kwamba Tanganyika ilijiingiza kwenye Serikali ya Muungano na kujifanya nchi mpya yenye jina jipya la Tanzania na yenye mipaka mipya ya kijiografia. Yumkini sana, jibu la Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda la mwaka jana kuwa Zanzibar si nchi, linatafsiri dhamira hii isiyokubalika kwenye mikataba ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika,
Tunasema haya tukijua uzito na uchungu wake. Ni vigumu kukiri kwamba tulifanya makosa, ikiwa kosa hilo linaonekana kuwa na maslahi. Lakini ukweli ni kuwa, kosa haliwezi kuwa na maslahi ya kudumu, hata kama linajaribiwa kufifilishwa kila mara. Kufuta Katiba ya Tanganyika kulikofanywa na vifungu vya sheria hii kulikuwa ni kosa. Kuifuta Serikali ya Tanganyika kulikuwa ni kosa. Na kosa hilo ndilo leo hii lililozaa kosa jengine la kiumbe kuzungumza na mmoja wa waumbaji kuhusiana na hatima ya kiumbe hicho. Na hivi ndivyo tunavyohoji uhalali wa vikao baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano (ambayo inawakilisha kiumbe, Muungano) na Ofisi ya Waziri Kiongozi (ambayo inawakilisha Muumba, Zanzibar).

Mheshimiwa Spika,
Tunapenda kurejea kauli yetu ya mwaka jana, kwamba pale mwaka 1992 Bunge hili tukufu lilipofanya maamuzi ya kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika, lilikuwa limepitisha uamuzi wa busara kama uliopitishwa na chama cha TANU mwaka 1958 kule Tabora kuingia kwenye mfumo wa kura tatu. Bali zaidi ya hapo, Bunge hili tukufu lilikuwa limefanya kitendo cha kisheria na cha kimantiki. Uamuzi ule ulikuwa sahihi wakati ule, ni sahihi leo hii na utakuwa sahihi kesho, maana sio tu kwamba uliakisi matakwa halisi ya Mkataba wa Muungano uliokuwa umetiwa saini zaidi ya nusu karne nyuma yake, bali pia ulikuwa ni kielelezo cha kujitathmini kulikofanywa na waheshimiwa wawakilishi wa Watanzania kupitia chombo chao hiki. Ni bahati mbaya sana kwamba, maamuzi yale ya Bunge yalikuja kuwekwa kando na kuufanya muda, fedha, na busara iliyotumika kuonekana kama si lolote si chochote!

Mheshimiwa Spika,
Ni kutekelezwa kwa azimio lile tu ndiko ambako kungelivipa maana vikao hivi baina ya Ofisi za Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi. Bila ya kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika iliyo hai na inayotambulika, vikao hivi vya mazungumzo vinabakia kuwa vikao vya mazungumzo tu.

2.2 Utayarifu wa Kushughulikia Tatizo Halisi

Mheshimiwa Spika,
Labda kwa manufaa ya mjadala huu, tunaweza kusema tujipumbaze kidogo na tuseme ni kweli vikao vya pamoja kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Waziri Kiongozi vina uhalali wa kisheria kuwepo na vinawakilisha dhati yenyewe ya Muungano. Natukubaliane kutokukubaliana na hilo ili mjadala uende mbele. Hata ikiwa hivyo itakuwa ndivyo, basi bado vikao hivi vitahojika kwamba havikai kwa mnasaba wa kutatua tatizo halisi la Muungano lililopo, bali kwa kuziba dalili za tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika,
Sisi wa Kambi ya Upinzani tumekuwa wazi sana katika hili. Hatujiumi maneno kusema kwamba tatizo kubwa na la msingi ni kutokuheshimiwa kwa Mkataba wa Muungano, ambako kunatokana na ukosefu wa dhamira njema. Tulilisema hilo mwaka juzi, mwaka jana, na mwaka huu tunalirudia. Kwamba wa kujadiliwa ni Mkataba wa Muungano tu na kuona namna gani Muungano uliozaliwa na Mkataba huo unaakisi vipengele vilivyokubaliwa na wale waliouweka saini. Kwamba ni mjadala wa kina juu Mkataba wa Muungano ndio utakaothibitsha kuwa Serikali ya Tanganyika haikutakiwa kufa, na kama imekufa iliuliwa kimakosa, na kama ni kosa basi linaweza kurekebishwa kwa kutangazwa rasmi kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika kama yalivyokuwa maamuzi ya Bunge hili tukufu mwaka 1992. Maana, kwa hakika hasa, hili la kutokuheshimiwa kwa Mkataba wa Muungano ndilo tatizo sugu la Muungano huu, na ambalo vikao hivi vya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi havionekani kuiona haja ya kulishughulikia.

Mheshimiwa Spika,
Tatizo la Muungano si mgao wa asilimia 4.5 kutoka kwa Serikali ya Muungano kwenda kwa Zanzibar. Tatizo si Zanzibar kuwa na au kutokuwa nchi ndani ya Muungano. Tatizo si nishati za gesi na mafuta kuwa na au kutokuwa za Muungano. Tatizo si Zanzibar kujiunga na au kutokujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam Duniani (OIC). Tatizo si Wazanzibari kushikilia nafasi katika serikali ya Muungano katika mambo ambayo si ya Muungano wakati ambapo Watanganyika hawawezi kufanya hivyo katika Serikali ya Zanzibar. Haya yote ni matokeo ya tatizo moja kubwa, nalo ni kutokuheshimiwa kwa Mkataba wa Muungano kuanzia mwanzo kabisa wa Muungano huu.

Mheshimiwa Spika,
Ni hapa ndipo ambapo mjadala wa vikao vya Ofisi za Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi ulikuwa utuwame. Kuuviringisha na kuuelekeza mjadala huu kwengine kokote kule hakusaidii chochote katika kutatua hiki kilichopewa jina la kero za Muungano, bali kuzidi kukitia matata. Hatusemi hivi kwa kuwa tunadharau umuhimu wa kuzungumza, bali kwa kuwa tunatiwa khofu na maendeleo na mwendelezo wa mazungumzo yenyewe. Tunajiuliza: Hivi hawa wenzetu wanakusudia kutupeleka wapi? Pale penye visheni ya ”Tanzania yenye Muungano Imara” au penye misheni ya ”Kuwa na Ufanisi katika Kuimarisha Muungano” kama inavyoelezwa kwenye dira na muelekeo wa Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano)? Na baada ya yote, kwani nini maana ya Muungano Imara na, hivyo, kuimarisha Muungano? Je, si kukichukua kila kitu cha upande mmoja wa Muungano na kukiingiza kwenye Muungano au kukifanya kila cha upande mmoja kuvuuka maji na kuwa cha upande wa pili?

Mheshimiwa Spika,
Baada ya ile Semina Elekezi kwa Watendaji wa Serikali iliyofanyika Ngurdoto, mwanzoni mwa muhula wa uraisi wake, Mheshimiwa Jakaya Kikwete akizungumzia mipango yake ya kuimarisha Muungano, alisema kwamba hakuona kuwa Muungano ulikuwa na tatizo kubwa zaidi ya kukosekana kwa mazungumzo ya mara kwa mara baina ya pande mbili zinazohusika. Kwa hivyo, hima akaitisha utaratibu huu ili ”hata kama hapana jambo kubwa sana, basi angalau watu wakutane kwa kunywa chai na kahawa pamoja na kubadilishana mawazo.”

Mheshimiwa Spika,
Hakika kabisa, kukutana kunywa chai na kuzungumza mambo yanayohusu hatima ya taifa ni jambo zuri sana, lakini mwenendo wa mambo katika kukutana huku unatukumbusha kile kisa cha tarehe 10 Agosti 1957, wakati chama cha kupigania uhuru cha Tanganyika, Tanganyika African Union (TANU), kilipokuwa kinafungua tawi lake katika mtaa wa Mvita, nyumba namba 10, Dar es Salaam. Katika sherehe hiyo muhimu, TANU iliwaalika wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, wengi wao wakiwa machifu kama vile Chifu Kidaha Makwaia, Humbi Ziota, Msabila Lugusha, Mwami Theresa Ntare na wengineo na ikawakirimu waalikwa wao vitafunio, vinywaji baridi na chai. Katika kutoa shukrani za TANU kwa wananchama wa TANU, Mwalimu Nyerere alikamata kikombe cha chai na kukionyesha juu kwa wasikilizaji wake. Akawaambia wasidhani kwamba kitendo cha kumpa mtu chai ni kitu kidogo, maana kuna watu wameiuza nchi hii kwa kupewa kikombe cha chai na wakoloni.

Mheshimiwa Spika,
Wakati tunaheshimu sana na tunaamini njia ya mazungumzo kama suluhisho la pekee kufikia utatuzi wa matatizo yanayolikabili taifa, hatuamini kuwa mazungumzo kwa maana ya mazungumzo tu yanaweza kutufikisha popote. Mazungumzo yenye uwezo huo wa kutoa suluhisho ni yale yanayozingatia nini kinazungumzwa, nani wanazungumza, vipi na kwa nini yanazungumzwa. Kila moja kati ya maswali haya lina maana kubwa kwa hitimisho na suluhisho litokanalo na mazungumzo yenyewe. Tunachelea kusema kwamba, haya yanayofanyika baina ya Ofisi za Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi ni mazungumzo kwa manufaa ya mazungumzo na sio mazungumzo kwa manufaa ya suluhisho. Na kwayo, fedha za walipa kodi wa nchi hii zinateketea lakini tatizo la Muungano halitatuliwi, zaidi ya kulizidisha.

Mheshimiwa Spika,
Turuhusu tupige mfano mmoja wa karibuni, kati ya mingi iliyokwishatokezea, kuthibitisha khofu yetu kwamba mazungumzo haya hayatatui tatizo halisi la Muungano. Mfano huu unakhusu Ripoti ya Baraza la Mapinduzi la Zanzibar ya 2003.

Mheshimiwa Spika,
Tarehe 29 Mei 2003, Ikulu ya Zanzibar ilichapisha Ripoti ya Baraza la Mapinduzi juu ya Matatizo na Kero za Muungano na Taratibu za Kuziondoa, ambapo katika sura yake ya tatu, ripoti hiyo ilitoa orodha ya mambo yanayopaswa kuondolewa katika Muungano. Mambo hayo ni:

i. Mafuta na Gesi Asilia
ii. Elimu ya Juu
iii. Posta
iv. Simu (Mawasiliano)
v. Biashara ya Nje
vi. Kodi ya Mapato
vii. Ushuru wa Bidhaa
viii. Usafiri wa Anga
ix. Takwimu
x. Utafiti
xi. Ushirikiano wa Kimataifa
xii. Leseni za Viwanda
xiii. Polisi
xiv. Usalama

Mheshimiwa Spika,
Katika kuhakikisha kuwa haya yanatekelezeka, SMZ ilitaka kuwepo kwa misingi mitano ya kuzingatiwa, ambayo ni:

a. Masuala ya Muungano yalindwe kwa misingi ya Katiba na Sheria badala ya siasa na maelewano
b. Muungano uwe na maeneo machache yanayoweza kusimamiwa na kutekelezwa kwa urahisi
c. Muungano uanishe washirika wake wakuu, mipaka na haki zao
d. Muungano utowe fursa sawa za kiuchumi kwa pande zote mbili za Muungano
e. Lazima pawe na Muungano unaoweza kuhimili mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi

Mheshimiwa Spika,
Hivi ndivyo SMZ ilivyosema tangu mwaka 2003; na kwa hakika – angalau katika hili – serikali hii imesema vile ambavyo Wazanzibari wamekuwa wakisema tangu siku za mwanzo za Muungano huu. Ni wazi kuwa ripoti hii ya SMZ iko mezani kwa Ofisi zote mbili, ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi. Lakini kinachotokezea kila baada ya kikao cha watendaji wakuu wa serikali mbili, ni taarifa ya kuhuzunisha panapohusika kile hasa kinachohitajika kutatuliwa.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mfano, taarifa ya kikao cha mwisho cha mwezi Mei 2009 iliyotolewa na Ofisi ya Makamu Rais, Idara ya Muungano, ilisema kwamba ’kero’ tatu za Muungano zimeshafutwa na sasa si ’kero’ tena. Kero hizo ni Tume ya Haki za Binaadamu, Uvuvi wa Ukanda wa Bahari na Shughuli za Biashara ya Meli. Katika mawili ya mwanzo, kufutwa kwake kutoka orodha ya kero ni kwa mambo hayo kukubalika rasmi kuwa ya Muungano, ambapo sasa upande wa Zanzibar umeridhia. La mwisho kufutwa kwake ni kwamba Zanzibar inaruhusiwa kuendesha shughuli za biashara ya meli kwa kushirikiana na Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika,
Hii maana yake ni nini? Ni kwamba, kumbe hakuna pendekezo lolote la kupunguza idadi ya mambo ya Muungano, kama yalivyo matakwa ya Zanzibar, linaloweza kuwa linajadiliwa na vikao hivi vya waziri mkuu na waziri kiongozi; maana inaonekana wahusika wa vikao hivi wameshaamua kuwa kupunguza orodha ya Mambo ya Muungano hakuwezi kuimarisha Muungano, bali kinyume chake ndicho sawa! Yaani, kuimarisha Muungano kuna maana moja tu, nayo ni ama kukichukua kila cha Zanzibar na kukifanya cha Muungano na, au, kukifanya kila kilichoko Tanzania Bara kivuuuke maji na kiwe cha Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Naliomba Bunge hili tukufu na Watanzania waniwie radhi kwa kusema kwamba, wakubwa wetu wameufanya Muungano huu ushabihiane sana na kile kisa cha Mfalme Jeta aliyemo kwenye riwaya ya Kusadikika ya Marehemu Sheikh Shaaban Robert. Mfalme huyu alikutwa na mjumbe wa Kusadikika akiwa amekaa katika eneo ambapo mto uliokuwa unakokozoa kila kitu – mawe, magogo, majengo, n.k. – unatiririkia kinywani na kuishia tumboni mwake, lakini kila mara alisikikana akilia: ”Njaa! Njaa! Kiu! Kiu!”

Mheshimiwa Spika,
Hivyo ndivyo Muungano wetu ulivyofanywa, kwamba uwe unakula na kunywa kila kitu na bado kila siku uwe unalalamika kufa njaa na kiu. Na ili kuufanya usife, wakubwa wanaamua kuulisha kila cha Zanzibar na kila cha Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika,
Ikiwa hali ni hii, je si sawa kusema kwamba tunatoka kwenye serikali mbili zilizopo sasa kuelekea serikali moja? Je, jukumu la vikao hivi vya Ofisi za Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi ni kuratibu na kusimamia mchakato wa kubadilisha muundo wa Muungano? Na je, hivyo ndivyo Wazanzibari na Watanganyika walivyotaka yawe matokeo ya vikao hivi ”vya kunywa chai na kahawa?”

Mheshimiwa Spika,
Sisi wa Kambi ya Upinzani hatuoni kwamba vikao hivi vya pamoja vinakuja na suluhisho la tatizo la Muungano huu, bali vyenyewe ni sehemu ya tatizo. Kwa hivyo, ili kutimiza wajibu wetu kama Bunge la Watu lenye jukumu la kusimamia matumizi fedha za walipa kodi, tunaliomba Bunge hili liitake Serikali ya Muungano isitishe mara moja vikao hivi na badala yake Mkataba wa Muungano uletwe Bungeni hapa kama nukta kuu ya mjadala. Hapo ndipo tuanzie na tumalizie kero za Muungano.

3. SIASA ZA SERIKALI YA MUUNGANO KUELEKEA MUUNGANO

Mheshimiwa Spika,
Nimetangulia kusema kwamba, kinachonisimamisha hapa ni utamaduni wa kawaida kwamba kila wizara ya serikali lazima isemewe na wizara kivuli Bungeni baada ya wizara hiyo kuwasilisha bajeti yake, lakini sio kwa imani kwamba hiki tunachokisema kinachukuliwa na Serikali kwa umakini kama sehemu ya mawazo ya Watanzania yanayopasa kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika,
Kambi yetu inaitupia lawama za moja kwa moja serikali ya Muungano kwamba imejiundia siasa zake maalum kuelekea suala la Muungano huu. Siasa hizo zinasomeka katika nukta mbili: moja ni kupuuzia maoni yoyote yanayotolewa na watu kuhusiana na Muungano wenyewe na ya pili ni kuudharau uhalisia wa Muungano wenyewe.

3.1 Kupuuzia Maoni Yanayohusu Muungano

Mheshimiwa Spika,
Nilitagulia kusema kwamba, panapohusika suala la Muungano, Watanzania tuna bahati mbaya ya kuwa na serikali yenye utamaduni wa kujifungia kwenye viambaza vyake vinne, ikajisemesha yenyewe, ikijisikiliza yenyewe na kisha ikatoka na mwangwi wa sauti yake yenyewe kwenda kuufanyia kazi. Bila ya shaka, haya hayakuanza leo, bali ni muakisiko na muendelezo wa utamaduni huo mkongwe; kwamba kila kinachosemwa na Watanzania wengine wowote ambao hawamo kwenye ”Super Structure” ya Muungano, ni kelele za mlango ambazo hazimzuii mwenye nyumba kulala. Kitabu cha bajeti iliyopo mbele yetu sasa ni shahidi wa hayo.

Mheshimiwa Spika,
Ukifuatilia hansard ya tarehe 20 Agosti, 2008, wakati Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Rais (Muungano) akifanya majumuisho ya michangio ya bajeti ya wizara yake, utakuta ahadi ya Mheshimiwa Waziri kuyachukua na kuyafanyia kazi maoni ya Kambi ya Upinzani. Labda nikumbushe tu kuwa, maoni ya Kambi hii mwaka jana yalijikita katika mambo 9 muhimu ambayo ni:

i. Muundo wa Muungano
ii. Shughuli za Muungano
iii. Mambo ya Muungano
iv. Nafasi ya Muungano katika Mpasuko na Muwafaka wa Wazanzibari
v. Mapungufu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
a. Nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
b. Nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
c. Matumizi ya Tanzania Bara Ndani ya Muungano
vi. Akaunti ya Pamoja ya Fedha
vii. Nafasi ya Zanzibar katika Benki Kuu ya Tanzania
viii. Mahakama ya Katiba, Jaji Mkuu na Mahakama ya Rufaa
ix. Hoja ya Serikali Tatu

Mheshimiwa Spika,
Katika kila moja ya mambo hayo, tulionesha tatizo lilipo na tukapendekeza suluhisho lake. Leo hii, mwaka mmoja baadaye, Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano) inawasilisha bajeti yake, ikiwa sio tu kwamba haikutekeleza ahadi yake ya kuyafanyia kazi maoni yetu, bali hata maelezo ya kushindwa kufanywa hivyo hayapo. Katika hali kama hii, ambapo mtu ameshasema kila kile alichopaswa kukisema na bado pakawa hapana mabadiliko, Waingereza wana msemo: ”Need we say more!?” Nasi tunaiuliza Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano), kipi chengine tukiseme hata kitoshe kuisaidia kuuimarisha Muungano huu kwa misingi ya uadilifu na usawa?

Mheshimiwa Spika,
Hizi zimekuwa ndizo Siasa za Muungano kuelekea Muungano wenyewe. Kwamba yeyote ambaye anashauri chochote kuhusu Muungano huu na ikiwa hayumo kwenye ”super structure” ya Muungano wenyewe, basi mawazo yake yaishie hapo hapo anapoyatoa. Serikali ya Muungano haikumsikiliza Mzee Aboud Jumbe aliyekuwa Rais wa Zanzibar, haikulisikiliza hata Bunge hili lilipopitisha Azimio la Kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika, haikusikiliza Tume za Nyalali na Kisanga zilizoshauri muundo wa serikali tatu na haitusikilizi sisi wa Kambi ya upinzani. Nani inayemsikiliza? Inajisikiliza yenyewe.

3.2 Kuudharau Uhalisia wa Muungano

Mheshimiwa Spika,
Tunapozungumzia Muungano wetu, kuna mambo mawili ambayo ndiyo uhalisia wake: kwanza, huu ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, nchi mbili zilizokuwa na mamlaka kamili na ambazo zilisalimisha baadhi ya mamlaka yake hayo kwenye chombo kimoja huku kila upande ukibakia na sehemu nyingine ya mamlaka yake. Huu si Muungano baina ya mkubwa na mdogo panapohusika hadhi ya nchi zilizoungana, maana eneo la kijiografia wala idadi ya watu havikuwa vitu vilivyoamua kuwepo na kutokuwepo kwa Muungano, kwa hivyo haviwezi leo kuamua uendeshwaji wa Muungano wenyewe. Pili, ni ukweli kwamba huu Muungano ni kitu kikubwa na muhimu sana kwa pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Wakati huo ndio uhalisia kuhusu Muungano, siasa ya Serikali ya Muungano inaonesha vyengine. Angalia, kwa mfano, mjengeko wa Serikali hii katika uwiano wa nafasi zinazoshikiliwa na watu kutoka pande hizi mbili kwenye wizara za Muungano. Uwakilishi wa Zanzibar ni wa kulazimisha kama kwamba Zanzibar ni mwalikwa tu na sio mwenza wa Muungano wenyewe. Inapotokea Mzanzibari amepewa nafasi katika wizara hizo, huwa ni kwa kukaribishwa na, au, kukirimiwa tu. Hata hii Idara ya Muungano iliyo chini ya Ofisi ya Makamo wa Rais, mambo ni hayo hayo. Tunamuomba Waziri atakapokuja kufanya majumuisho, alieleze Bunge lako uwiano uliomo kwenye Idara yake panapohusika mizania ya pande mbili za Muungano huu.

Mheshimiwa Spika,
Jambo hili linakwenda sambamba na utatanishi wa makusudi unaofanywa na Serikali ya Muungano na, kwa hakika, hata hili Bunge lako tukufu. Utatanishi wenyewe ni kwamba, kwa upande wa Serikali ya Muungano, imefanya mara nyingi huko nyuma, kumpa Mzanzibari kuongoza wizara ambayo si ya Muungano; ikijua fika kwamba huko ni kinyume cha mantiki ya Muungano wenyewe na kwamba kunachochea malalamiko ya haki kutoka kwa Watanzania Bara.

Mheshimiwa Spika,
Si jambo la haki hata kidogo, kwa mfano, kwa Mzanzibari kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, au Maliasili na Nishati, maana hayo si mambo la Muungano. Wako Watanzania Bara wenye uwezo mkubwa kuongoza wizara hizo. Na hata humu Bungeni, si jambo la haki kwa wabunge kutoka Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanzania Bara ambayo si ya Muungano. Si haki pia kwa Serikali ya Muungano kuunda wizara ambazo zinachanganya mambo yaliyo na yasiyo ya Muungano katika kapu moja, kama ilivyo, kwa mfano, katika suala la elimu ya juu, sayansi na teknolojia.

Mheshimiwa Spika,
Utatanishi wa kwanza unazalisha malalamiko kwamba Wazanzibari wanafaidika na kudekezwa sana na Muungano huu, kama yalivyo mawazo ya wenzetu wengi wa Tanzania Bara, wakiwemo waheshimiwa wabunge wa Bunge hili tukufu – kama ilivyodhihirika mwaka jana katika michangio ya mjadala wa Zanzibar kuwa na kutokuwa nchi. Utatanishi wa pili unazalisha malalamiko kwamba Serikali ya Muungano inafanya hila za makusudi kuinyang’anya Zanzibar kila kile kilichokuwa chake.

Mheshimiwa Spika,
Ukweli ni kwamba huu ni utatanishi wa kimtego na wa kufunika kombe, ambao azma yake kubwa ni kufifilisha ile hoja tunayoijenga kila siku ya kwamba lazima Serikali ya Tanganyika ije juu, ionekane na ifanye kazi zake rasmi kuwakilisha na kusimamia matakwa na maslahi ya Watanganyika yasiyokuwa ya Muungano. Bila ya kuwa na chombo cha kutunga sheria cha Tanganyika kama kulivyo na chombo cha kutunga sheria cha Zanzibar na bila ya kuwa na mamlaka tafauti ya utawala ya Tanganyika kama kulivyo na mamlaka ya utawala ya Zanzibar, tutaendelea kuwa mbali kabisa na uhalisia wa Muungano kama yalivyo matakwa ya Mkataba.

Mheshimiwa Spika,
Kuudharau kwengine uhalisia wa Muungano ni kulidogosha suala zima linalohusu Muungano wenyewe. Angalia, kwa mfano, Muungano mzima umewekwa ni idara tu ndani ya Ofisi ya Makamo wa Rais, ambayo ina idara nyengine kadhaa. Wakati Rais Jakaya Kikwete aliona umuhimu wa kuunda wizara maalum kushughulikia Afrika ya Mashariki, hakuona kabisa umuhimu wa kuwa na wizara kamili kushughulikia Muungano. Hili linaonesha namna Serikali inavyoudharau Muungano kama kwamba ni suala dogo tu.

Mheshimiwa Spika,
Labda hapa linakuja suala la ufundi na la kimantiki kwa wakati mmoja: kwamba katika mjengeko wa utawala serikalini, majina ya vyeo vya wakuu wa vitengo hunasibiana na vitengo vyao, kwa mfano mkuu wa kurugenzi ni mkurugenzi na mkuu wa wizara ni waziri. Sasa, kwa kuwa hakuna wizara ya Muungano, isipokuwa kuna idara ya Muungano kwenye Ofisi ya Makamo wa Rais, mkuu wa idara hiyo ni nani? Ni vyema tukaeleweshwa!

4. HITIMISHO NA MAPENDEKEZO

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na kupuuzwa na kudharauliwa kwa makusudi kwa matatizo ya Muungano huu, hakujawahi kupita muongo ambapo Muungano hautikiswi na kutikisika. Kwa bahati mbaya ni kwamba, kila Muungano unapotikisika, machoni mwa wakubwa huonekana kama kwamba unatikisika kwa kuwa hauna mambo ya kutosha. Na, hivyo, kama vile Mfalme Jeta wa Shaaban Robert alivyokuwa akila na kunywa kila kilichopo, basi nao wakubwa huzidi kuumiminia Muungano kila cha Zanzibar na kila cha Tanzania Bara tumboni mwake.

Mheshimiwa Spika,
Hilo ni kosa kubwa katika sayansi ya utatuzi wa migogoro. Wapemba husema: ”Ganga shina, matawi hayagangika!” kwa maana ya kuwa, kutibu maradhi ni kukitibu chanzo chake na sio dalili zake. Ni kosa kutokujiuliza kwa nini Muungano huu unatikisika (haushibi) na kujiuliza tu vipi unatikisika (unalilia njaa na kiu). La kujiuliza ni ikiwa hivi kweli Muungano huu uliumbwa na roho ya kushiba na kukinai au uliumbwa na uroho wa kufakamia na kusaza kila kitu? Ikiwa hivyo ndivyo, kuna siku kutakuwa na cha Zanzibar tena na, au, cha Tanzania Bara peke yake?

Mheshimiwa Spika,
Katika jumla ya michango iliyotoka hapa mwaka jana wakati wa mjadala wa Zanzibar kuwa na kutokuwa nchi, wabunge wako kutoka Zanzibar walikumbushwa msemo wa Kiingereza usemao: ”You can not eat your cake and have it!” kwa maana ya kuwa mtu hawezi kuila keki yake na bado akaendelea kuwa nayo. Ni ama aile imalizike na asiwe nayo au asiile kabisa ikiwa anataka kubakia nayo. Leo hii nataka nilikumbushe Bunge hili tukufu kwamba kuna pande nyengine za ukweli katika suala hili la keki: nazo ni kuwa, kwanza, kuna mtu kutokuila keki yake na bado asiwe nayo na, pili, kuna mtu kuila keki yake na kuendelea kuwa nayo.

Ripoti niliyoitaja hapo juu iliyotayarishwa na SMZ Mei, 2003 inaweza kabisa kuthibitisha pande hizi za ukweli mwengine kuhusu keki.

Mheshimiwa Spika,
Tumekuwa tukionesha mara zote kwamba chanzo cha matatizo ya Muungano huu ni kutokuheshimiwa kwa Mkataba wake uliouunda. Tunarejea tena kusema hapa kwamba Muungano huu hauongozwi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, bali unaongozwa na Mkataba wa Muungano wa mwaka 1964. Katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar zinatakiwa zitafsiri tu yale yaliyomo kwenye Mkataba na sio kuongeza wala kupunguza.

Mheshimiwa Spika,
Kwa hivyo, basi kama ni suluhisho, sisi wa Kambi ya Upinzani tunatoa jibu kama lile alilowahi kulitoa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1985, alipoulizwa ni kipi kiapumbele chake katika kuijenga Tanzania. Mzee Mwinyi alijibu: ”Barabara!” Alipoulizwa kipi chengine, akajibu ”Ni barabara!”, na alipoulizwa kipi chengine akasema ”Ni barabara!”

Mheshimiwa Spika,
Kwenye Uislam kuna hadithi kwamba Mtume (SAW) aliwahi kuulizwa, ni nani wa kutendewa mema zaidi baina ya wazazi wawili, akajibu: ”Mama!” alipoulizwa kisha nani, akajibu: ”Mama!” na alipoulizwa tena, kisha nani, akajibu: ”Mama!”

Mheshimiwa Spika,
Basi ikiwa Bunge lako hili tukufu litataka kujua ni kipi ambacho sisi wa Kambi ya Upinzani tunaamini kuwa ni suluhisho la matatizo yote ya Muungano huu, tutajibu kuwa ni ”Kurudi kwenye Mkataba wa Muungano!” Tukiulizwa ni kipi chengine, tutasema ”Ni kurudi kwenye Mkataba wa Muungano!” Na hata tukiulizwa mara ya tatu, tutasema ”Ni kurudi kwenye Mkataba wa Muungano!” Si vikao vya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wala si tume zisizokwisha za kuangalia kero za Muungano. Ni kuutekeleza na kuuheshimu Mkataba wa Muungano tu ndiko kunakotakiwa.

Mungu Ibariki Tanzania. Mungu Ibariki Afrika

Naomba kuwasilisha

……………………………….
Riziki O. Juma (Mb)
Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni (Muungano)
29 Juni, 2009

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s