CUF yakhofia mpasuko wa kisiasa

Na Mwanne Mashugu, Zanzibar

WAWAKILISHI wa kambi ya upinzani vsiwani Zanzibar wameonya kuwapo kwa hatari ya kuibuka mpasuko mpya wa kisiasa kama urasimu hautaondolewa katika utoaji wa vitambulisho vya Uzanzibari ukaazi kabla ya kuanza kazi ya kubadilisha shahada za wapiga kura wa kudumu Julai 6, mwaka huu kisiwani Pemba.

haji-faki-shaali

Haji Faki Shaali, mwakilishi wa Mkanyageni.

Wawakilishi hao walitoa onyo hilo baada ya idadi kubwa ya wananchi katika majimbo ya uchaguzi Pemba kujitokeza kuomba fomu za kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi bila ya kufanikiwa kwa viongozi wa serikali za mitaa (masheha) na maofisa wa vitambulisho wa wilaya wakati wakichangia makadirio na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Kiongozi.

Mwakilishi wa Jimbo la Mkanyageni, Haji Faki Shaali (CUF), alisema anazo taarifa kuhusu mpango wa CCM wa kutafuta ushindi katika uchaguzi ujao kwa kupunguza idadi ya watu waliofikia umri wa kuandikishwa katika daftari la wapiga kura kunyimwa haki hiyo.

Alisema viongozi wa serikali lazima waheshimu viapo wanavyokula kwa vile kitendo hicho kinakwenda kinyume cha kifungu cha pili cha katiba ya mwaka 1984, ambayo inatoa haki kwa kila Mzanzibari mwenye umri, kuanzia miaka 18 kuwa na haki ya kushiriki uchaguzi mkuu.

Shaali alisema watu wasiokuwa na sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa Zanzibar ni wale wasio raia, mgonjwa wa akili na mtu aliyepatikana na hatia na kufungwa.

“Tumeupata mpango wenu mapema kuwa mtapunguza kura kwa utaratibu huu, isipokuwa tunawatahadharisha mtaigawa nchi, sisi sote ni ndugu, jambo la msingi, tuheshimu kiapo cha uaminifu,” alisema Shaali.

Alisema CCM ina uwezo wa kupata idadi yoyote ya majimbo Pemba , kwa vile watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar hawana uwezo wa kupinga matakwa ya chama tawala.

Mwakilishi huyo alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar haina uwezo wa kusimamia uchaguzi wa haki, kwa vile matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu uliopita ndiyo yanayojitokeza sasa wakiwamo masheha kuwanyima haki ya kuandikishwa watu walio na sifa za kujiandikisha kikatiba.

“Mheshimiwa Spika, hatutaki Unguja na Pemba itengane, serikali ifanye kila njia watu wenye sifa wapewe haki ya kuandikishwa kikatiba,” alisema mwakilishi huyo.

Naye kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakar, alisema kwamba Mzanzibari ana uwezo wa kuandikishwa kuwa mpiga kura ikiwa ataonyesha cheti cha kuzaliwa, kwa vile ni kielelezo kimojawapo cha kuhalalisha uzanzibari wake.

Alisema kitendo cha kumnyima mtu haki yake ya kujiandikisha kwa kukosa kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi ni kwenda kinyume cha Katiba ya Zanzibar ibara ya 7(1), ambayo imeweka utaratibu mzima wa wenye sifa ya kushiriki uchaguzi wa Zanzibar.

Chanzo: Tanzania Daima

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s