MKUKUTA hautekelezeki

Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini unalenga kufanikisha kufikia malengo ya milenia. Hata hivyo utekelezaji wa MKUKUTA umesuasua kwa sababu gharama za mkakati hazikukadirwa mapema. Ukadiriaji wa gharama za MKUKUTA katika baadhi ya sekta muhimu ulikamilika mwishoni wa mwaka 2006 na gharama zake zikabainika kuwa ni kubwa mno kuliko uwezo wa serikali kwa hiyo MKUKUTA hautekelezeki. Kwa mfano gharama za kutekeleza MKUKUTA katika sekta ya nishati ilikadiriwa kuwa wastani wa dola milioni 911 kwa mwaka kati ya 2006/7 mpaka 2009/10. Sekta ya kilimo ilikuwa inahitaji wastani wa dola milioni 300 kwa mwaka. Sekta ya afya ilihitaji wastani wa dola milioni 476 kwa mwaka. Sekta ya barabara ilihitaji wastani wa dola milioni 922 kwa mwaka. Sekta nne za nishati, kilimo, afya na barabara zilikadirwa kuhitaji wastani wa dola milioni 2609 kwa mwaka. Mahitaji haya ya sekta 4 ni zaidi ya asilimia 70 ya matumizi yote ya serikali ya mwaka 2006/07. MKUKUTA haukutekelezwa kama ipasavyo kwa sabababu gharama za mpango hazikukadiriwa mapema, na ukadiriaji ulipomalizika gharama zilikuwa kubwa mno.

Hamad Rashid Mohamed

Hamad Rashid Mohamed

HOTUBA YA KIONGOZI WA UPINZANI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA HAMAD RASHID MOHAMED (MB) WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2009/2010.

I. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba upokee shukrani zetu za dhati kwa kunipa nafasi hii ili nitoe maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2009/2010 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.

2. Mhe. Spika, awali ya yote naomba kutoa shukurani zangu za dhati kwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani kwa ushirikiano wao mkubwa, wakiongozwa na Dr.Wilbrod Slaa (MB), Naibu Kiongozi wa Upinzani waliofanikisha hadi kuniwezesha kusimama mbele yenu kuwasilisha hotuba ya maoni ya Kambi ya Upinzani, kutokana na hoja iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi tarehe 11.06.09. Mhe. Spika, Wabunge wa Upinzani na wabunge wote kwa ujumla wao, kwa pamoja tuna wajibu wa kushirikiana katika kuwatumikia Watanzania kwa lengo kuu la kuwaondolea umasikini uliokithiri, maradhi na ujinga pamoja na kujenga UTAIFA wetu wa dhati. Mwenyezi Mungu aziweke pamoja nia zetu na kuzibariki katika kutekeleza azma hiyo.

3. Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, kukushukuru wewe, naibu Spika, wenyeviti wa Bunge na watendaji wa Ofisi yako, wakiongozwa na Katibu wa Bunge, kwa kutupatia fursa mbali mbali sisi wabunge kujifunza shughuli za mabunge ya wenzetu jinsi ya kuwahudumia vyema wadau ambao ni wananchi na wapiga kura kwa kusimamia vyema utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, Kwa namna ya pekee naomba kuwashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Wawi kwa kuendelea kuniunga mkono na kwa juhudi zao za kujitafutia maisha licha ya vikwazo vikubwa sana na ukiritimba wa kuuza mazao yao ya karafuu. Kama wananchi wa Wawi na Pemba kwa ujumla wangaliruhusiwa kuuza karafuu zao bila pingamizi, wao wenyewe wangepunguza umasikini wao kwa kiwango kikubwa.
4. Mhe. Spika, naomba kumpongeza Waziri wa Fedha Mhe. Mustafa Mkullo (Mb), Manaibu Waziri, Katibu Mkuu na Manaibu wake, pamoja na wakuu wa vitengo na asasi zilizo chini yao kwa kazi nzito ya maandalizi ya Bajeti hii. Kambi ya Upinzani inafanya uchambuzi wake ikiamini kuwa Waziri atakuja kutoa ufafanuzi zaidi katika baadhi ya maeneo kwa kadiri tutakavyoainisha. Uchambuzi wetu nitauelezea baadae kwa kifupi na kwa kirefu utaelezewa na Mawaziri Vivuli wa Wizara mbali mbali.

5. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali ni zaidi ya urari wa mapato na matumizi ya Serikali. Bajeti ni tamko la kisera lenye lengo mahususi katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi. Hivyo maoni haya ya Kambi ya Upinzani yana lengo la kuonesha mapungufu ya Mpango wa Serikali na kutoa sera na mikakati mbadala pale inapowezekana ili kulinusuru Taifa letu. Tunafahamu kwamba Bajeti ya Mwaka huu inakuja wakati mgumu sana kiuchumi katika Taifa. Hivyo, tutajielekeza zaidi katika jinsi ya kuongeza uzalishaji wa ndani ili kuboresha maisha ya wananchi wetu.

MPANGO NA MALENGO YA UCHUMI
6. Mheshimiwa Spika, Kila mwaka, Serikali inaeleza katika hotuba ya bajeti kuwa Misingi na shabaha ya Bajeti imezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo inalenga kuwa Tanzania iwe ni nchi yenye kiwango cha kati cha mapato (middle income country) na hali bora ya maisha kwa wananchi; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005; MKUKUTA; Mpango Maalum wa Kuharakisha Maendeleo ya Tanzania (Tanzania Mini Tiger Plan 2020); na Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Hata hivyo Waziri hafanyi uchambuzi wa kina kuonyesha jinsi sera za bajeti na matumizi ya serikali yanatekeleza mikakati hiyo, mafanikio yaliyofikiwa, vikwazo vilivyopo na vinavyokabiliwa na serikali.

7. Mheshimiwa Spika, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ilibuniwa kwa kuzingatia maendeleo makubwa ya uchumi ya nchi za Kusini Mashariki ya Asia kama vile Malaysia na hususan ukuaji wa sekta ya viwanda, uuzaji wa bidhaa za viwanda nchi za nje na ongezeko kubwa la ajira katika sekta rasmi lililosaidia kupunguza umaskini kwa kasi kubwa. Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ni kuhakikisha kuwa ifikapo 2025, Tanzania itakuwa na uchumi unaotegemea sekta nyingi na ulioendelea kwa kuwa na wastani wa viwanda vingi, uchumi mpana ulio tulivu (macroeconomic stability), miundombinu imara na pato la taifa linakua kwa asilimia 8 au zaidi. Tanzania ya 2025 itakuwa inamudu ushindani wa kikanda na kimataifa kwa kuwa na nguvukazi yenye elimu na ujuzi.

8. Mheshimiwa Spika, Kigezo muhimu cha kupima kama malengo ya Dira ya Taifa yanafikiwa ni ukuaji wa pato la taifa na mabadiliko ya mfumo wa uchumi na hasa ukuaji wa sekta ya viwanda na ongezeko la ajira katika sekta hiii. Wastani wa ukuaji wa pato la taifa kwa miaka minane iliyopita ni asilimia 7, lakini mchango wa sekta ya viwanda bado ni mdogo sana. Viwanda vilichangia asilimia 9.4 ya pato la taifa mwaka 2008 ukilinganisha na asilimia 8.5 mwaka 2000. Katika Nchi za Kusini Mashariki ya Asia, sekta ya viwanda inachangia asilimia 25-30 ya pato la taifa. Katika miaka 4 iliyopita uuzaji wa bidhaa za viwanda umeongezeka kwa kasi kubwa lakini toka kiasi kidogo. Mwaka 2008 thamani ya bidhaa za viwanda zilizouzwa nje (dola milioni 662.3) zilizidi bidhaa asilia (dola milioni 418.4). Katika nchi yenye nguvu kazi ya zaidi ya watu milioni 20, wananchi walioajiriwa katika sekta rasmi ya viwanda mwaka 2008 ni 92015 tu. Lengo muhimu la kubadilisha mfumo wa uchumi kwa kuongeza ajira viwandani halijafanikiwa.

9. Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini unalenga kufanikisha kufikia malengo ya milenia. Hata hivyo utekelezaji wa MKUKUTA umesuasua kwa sababu gharama za mkakati hazikukadirwa mapema. Ukadiriaji wa gharama za MKUKUTA katika baadhi ya sekta muhimu ulikamilika mwishoni wa mwaka 2006 na gharama zake zikabainika kuwa ni kubwa mno kuliko uwezo wa serikali kwa hiyo MKUKUTA hautekelezeki. Kwa mfano gharama za kutekeleza MKUKUTA katika sekta ya nishati ilikadiriwa kuwa wastani wa dola milioni 911 kwa mwaka kati ya 2006/7 mpaka 2009/10. Sekta ya kilimo ilikuwa inahitaji wastani wa dola milioni 300 kwa mwaka. Sekta ya afya ilihitaji wastani wa dola milioni 476 kwa mwaka. Sekta ya barabara ilihitaji wastani wa dola milioni 922 kwa mwaka. Sekta nne za nishati, kilimo, afya na barabara zilikadirwa kuhitaji wastani wa dola milioni 2609 kwa mwaka. Mahitaji haya ya sekta 4 ni zaidi ya asilimia 70 ya matumizi yote ya serikali ya mwaka 2006/07. MKUKUTA haukutekelezwa kama ipasavyo kwa sabababu gharama za mpango hazikukadiriwa mapema, na ukadiriaji ulipomalizika gharama zilikuwa kubwa mno.

10. Mheshimiwa Spika, Mwaka huu wa bajeti ni wa mwisho wa utekelezaji wa MKUKUTA. Waziri kaeleza kwamba serikali inaandaa MKUKUTA namba II. MKUKUTA wa kwanza haujafanyiwa tathmini ya kina ili kujifunza kutoka mapungufu yaliyojitokeza. Ni wazi MKUKUTA wa pili hautakamilika na kuanza kutekelezwa mwaka wa bajeti wa 2010/11. Ikiwa serikali ina lengo thabiti la kuwa na mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini unaotekelezeka inastahili kujipa muda kutathmini MKUKUTA na kushirikisha wadau wote katika kuandaa mpango mbadala wa kukuza uchumi kuongeza ajira za uhakika na kupunguza umaskini.

MALENGO YA MILENIA

11. Mheshimiwa Spika, Malengo ya Maendeleo ya Milenia yamekubaliwa na jumuia ya kimataifa yawe dira ya mipango ya maendeleo ya nchi maskini kama Tanzania. Malengo halisi yako saba na yanakusudia ifikapo mwaka 2015:
a. Kutokomeza umasikini uliokithiri na njaa. Kupunguza kwa asilimia hamsini idadi ya watu masikini ambao kipato chao ni chini ya dola moja kwa siku na kupunguza kwa asilimia hamsini idadi ya watu wanaokumbwa na njaa.
b. Elimu ya msingi kwa wote Kuhakikisha watoto wote wa kike na wa kiume wanahitimu elimu ya shule ya msingi.
c. Usawa wa kijinsia na fursa sawa kwa wanawake Kuondoa tofauti ya uwiano wa wasichana na wavulana katika elimu ya msingi ifikapo mwaka 2005, na katika ngazi zote za elimu ifikapo 2015.
d. Kupunguza vifo vya watoto wachanga Kupunguza kwa theluthi mbili vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano.
e. Upatikanaji wa huduma bora za uzazi Kupunguza kwa robo tatu idadi ya vifo vya uzazi
f. Kupambana na Ukimwi, Malaria na magonjwa mengine Kuzuia kabisa na kuanza kupunguza maambukizo mapya ya ukimwi Kuzuia kabisa na kuanza kupunguza milipuko ya malaria na magonjwa mengine hatari
g. Kulinda mazingira yetu Kujumuisha misingi yote ya maendeleo endelevu katika sera na programu za kila nchi; kuzuia upotevu wa raslimali ya mazingira.
h. Lengo la nane linahimiza ushirikiano wa kimataifa kuziwezesha nchi maskini kufikia malengo haya

12. Mheshimiwa Spika, Uchunguzi wa Bajeti za Kaya wa mwaka 2007 (2007 Household Budget Survey- HBS) unaonyesha kwamba umaskini umepungua kidogo sana toka asilimia 38.6 mwaka 1990, asilimia 35.7 mwaka 2001 mpaka asilimia 33.3 mwaka 2007. Kwa kuwa idadi ya Watanzania inaongezeka kwa asilimia 2.9 kila mwaka. Idadi ya watu maskini imeongezeka kwa milioni moja na nusu toka watu milioni 11.4 mwaka 2001 na kufikia watu milioni 12.9 mwaka 2007. Izingatiwe kuwa kigezo kilichotumiwa na HBS 2007 cha mtu mzima kutohesabiwa kuwa siyo maskini ni kutumia shilingi 641/- au zaidi kwa siku ukiwa Dar es Salaam, shilingi 532/- au zaidi kwa siku ukiwa katika miji mingine na shilingi 469/-au zaidi kwa siku ukiwa vijijini. Ni wazi kigezo hiki ni cha chini mno na bado idadi ya watu maskini imeongezeka.

13. Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha na Uchumi alipowasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika kipindi cha mwaka 2008 alieleza kuwa pato la taifa linakadiriwa kukua kwa asilimia 7.4. Kwa kipindi cha miaka minane 2001-08, pato la taifa limekua kwa wastani wa asilimia 7.1 kwa mwaka. Ikiwa ongezeko la watu ni asilimia 2.9, wastani wa pato la kila mwananchi limeongezeka kwa wastani wa asilimia 4.2 kwa mwaka. Kutopungua kwa umaskini kwa kasi kunaashiria kwamba uchumi wa Tanzania haukui kwa wastani wa asilimia 7.1 kwa mwaka kama takwimu za serikali zinavyoeleza.

14. Mheshimiwa Spika, Kigezo kilichokubaliwa kimataifa kuwa matumizi ya chini kabisa kwa mtu mzima asihesabiwe kuwa ni maskini wa kutupwa ni dola moja kwa siku. Benki ya dunia inakadiria kwa kutumia kipimo hiki, umaskini Tanzania umeongezeka toka asilimia 73 ya Watanzania wote mwaka 1990 mpaka kufikia asilimia 89 mwaka 2000. Kwa kutumia kigezo hiki cha kimataifa na takwimu za uchunguzi wa bajeti za kaya wa 2007, zaidi ya Watanzania 90 katika kila Watanzania 100 ni masikini wa kutupwa. Mheshimiwa Spika hali hii inatisha. Hatuwezi kuwa na mshikamano wa kweli wa kitaifa ikiwa ukuaji wa uchumi unawanufaisha watu wachache na kuwaacha zaidi ya Watanzania milioni 36 wakiwa maskini wa kutupwa. Kwa Watanzania walio wengi kauli mbiu ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzani ni kitendawili cha kejeli kwani maisha yao ni ya dhiki kila kukicha.

15. Mheshimiwa Spika, Malengo ya milenia ni pamoja na kupunguza kwa nusu asilimia ya Watanzania wenye njaa. Watanzania wenye lishe duni na utapiamlo wameongezeka toka asilimia 28 ya Watanzania wote mwaka 1990 na kufikia asilimia 41 mwaka 1995 na kupungua kiasi kufikia asilimia 35 mwaka 2007. Wakati Chama tawala kinaendelea kupongezana kwa kunyeshana vidole gumba, Watanzania wanaolala na njaa karibuni kila siku iendayo kwa Mungu wameongezeka toka milioni 7.4 mwaka 1990 na kufikia milioni 14.4 mwaka 2007.

16. Mheshimiwa Spika, Ili kupunguza umaskini tunahitaji kuongeza ajira bora na za uhakika (decent work). Benki ya Dunia inakadiria kuwa Watanzania wengi mno wanategemea ajira zisizokuwa na uhakika. Watu wenye ajira zenye mashaka wamepungua kidogo toka asilimia 92 ya watanzania wote wenye umri wa kuajiriwa mwaka 2000 na kufikia asilimia 88 mwaka 2007.

17. Mheshimiwa Spika, Lengo la milenia ambalo tunaweza kulifikia ni elimu ya msingi kwa wote na usawa wa kijinsia katika elimu ya msingi. Hata hivyo ni muhimu kuboresha elimu ya msingi ili wanaoanza shule wamalize kwa sababu elimu wanayopata in manufaa. Bila kuiboresha elimu ya msingi tunaweza kurudi nyuma kama ilivyotokea miaka ya themanini kuhusiana na elimu ya UPE.
18. Mheshimiwa Spika, Lengo la milenia kuhusu vifo vya watoto wadogo ni kuvipunguza kwa theluthi mbili kati ya mwaka 1990 na 2015. Vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua toka 96 kwa watoto 1000 waliozaliwa na kufikia 89 mwaka 2000 na 73 mwaka 2007. Lengo la Milenia ni kupunguza vifo vya watoto wachanga kufikia 32 kwa watoto 1000 ifikapo 2015. Kwa miaka 6 iliyobakia, tukiendelea na uzoefu tulionao, lengo hili haliwezi kufikiwa.
19. Mheshimiwa Spika, Vifo vingi vya watoto wachanga vinatokea kwa watoto wenye umri wa chini ya mwezi mmoja. Kila mwaka watoto wanaozaliwa (newborn) 51000 wanafariki kabla ya kufikisha mwezi mmoja. Watoto wengine 43,000 wanazaliwa njiti (still born). Vifo vya watoto wa chini ya mwezi mmoja ni asilimia 29 ya vifo vya watoto wote wa chini ya umri wa miaka 5. Utafiti wa madaktari wa watoto unaonyesha kuwa theluthi mbili ya vifo vya watoto – sawa na watoto 34,000 – vinaweza kuepukika ikiwa huduma za msingi za afya zitawafikia kina mama wajawazito na watoto wao. Serikali inabidi iweke mkakati na fedha kuwahudumia kina mama wajawazito na watoto wachanga.

20. Vifo vya uzazi havijapungua bali vinaongezeka. Kuna vifo vya uzazi 578 katika kila wajawazito 100000 wanapojifungua. Wataalam wa Benki ya Dunia wanakadiria kuwa katika mwaka 2007 kulikuwa na vifo 950 kwa kila kina mama laki moja waliojifungua

21. Mheshimiwa Spika, Kwa mwenendo unaoonekana katika Uchunguzi wa Bajeti za Kaya 2007, na takwimu za Benki ya Dunia, Tanzania, pamoja na kupata misaada mingi toka nje, haitafikia malengo ya milenia ya kupunguza umaskini na kuboresha huduma za afya.

22. Mheshimiwa Spika, Watanzania tunahitaji tutafakari hali halisi tuliyonayo na tubuni sera na mikakati ya pamoja ya kujikwamua toka dimbwi la umaskini. Misingi muhimu ya sera na mikakati hiyo iwe:-

• Kuitumia vizuri mali ya asili ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wote huku tukilinda mazingira yetu
• Kuwekeza kwenye afya ya watoto wa Tanzania toka wakiwa katika mimba za mama zao kwa kuhakikisha kina mama waja wazito na watoto wachanga wanapata lishe bora
• Kuwekeza katika elimu ya watoto wa Tanzania toka shule za chekechea na kuendelea. Kuweka msisitizo maalum katika elimu ya hesabu, sayansi na teknolojia
• Kuwekeza katika kilimo hasa cha chakula kama vile mahindi, mpunga, maharage, jamii ya kunde na mbegu za mafuta kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza masoko ya nje hasa nchi za jirani na hususan Congo,Comoro,Kenya n.k.
• Kuwekeza katika miundombinu ya barabara, umeme, maji na mawasiliano
• Kuweka mkakati madhubuti wa kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi ya ndani na kuajiri watu wengi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu na bidhaa za ngozi, vifaa vya matumizi ya nyumbani na vifaa vya umeme na electroniki.

UCHAMBUZI WA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA SERIKALI

23. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya serikali inaendelea kutegemea wafadhili wa nje bila ya kuweka mkakati wa kujikwamua toka kuwa nchi tegemezi. Theluthi moja ya matumizi ya serikali yanategemea mikopo na misaada kutoka nje. Mikopo na misaada ya nje ya shilingi trilioni 3.2 ni zaidi ya matumizi ya shilingi trilioni 2.8. Kimsingi Serikali haitoi fedha yeyote kugharamia matumizi ya maendeleo na inategemea wafadhili kulipia matumizi ya kawaida. Mfumo huu wa kutegemea nje ni aibu kwa taifa letu hasa ukizingatia kuwa tuna miaka 48 tangu tumejitawala. Alau wahisani wangetusaidia bajeti ya maendeleo na sisi tukaichangia kwa kiasi kikubwa.

24. Mheshimiwa Spika, Tanzania inaweza kukusanya asilimia 20-25 ya pato la taifa kama kodi kwa kundoa misamaha holela ya kodi hasa katika sekta ya madini, kukusanya kodi zinazokwepa katika bidhaa za mali ya asili ikiwa ni pamoja na madini, misitu na samaki. Inakadiriwa kuwa serikali inapoteza mapato ya dola milioni 50 kila mwaka katika sekta ya dhahabu na dola milioni 58 katika sekta ya misitu. Takwimu za biashara zinaonyesha kwamba Uchina imeingiza bidhaa za misitu toka Tanzania ambazo ni mara 10 ya mauzo ya bidhaa hizo zilizo katika kumbukumbu ya takwimu za Tanzania. Kwa hiyo serikali inakusanya asilimia 10 tu ya kodi ya mauzo ya mbao zinazosafirishwa kwenda China. Waziri ameeleza kuwa misamaha ya kodi ni asilimia 3.5 ya pato la taifa. Ikiwa misamaha ya kodi itapunguzwa mpaka kufikia asilimia 0.5 ya pato la taifa, ukusanyaji wa kodi utafikia asilimia 20 ya pato la taifa.

25. Mheshimiwa Spika, Inasikitisha kushuhudia serikali inavyoyaogopa na kuyakumbatia makampuni yanayochimba madini. Serikali imependekezwa kuondoa msamaha wa Ushuru wa Mafuta ya Petroli kwa mafuta yanayotumiwa na kampuni za madini kwa kufuta Tangazo la Serikali namba 99 la mwaka 2005. Marekebisho haya yanahusu kampuni za madini zitakazoingia mkataba na Serikali kuanzia tarehe 1 Julai, 2009. Kwa nini ufutaji wa misamaha hii usiyaguse makampuni yaliyopo hivi sasa. Serikali inaendelea kulinda mikataba ya kifisadi kwa manufaa ya nani?

26. Mheshimiwa Spika, Bunge hili liazimie na liitake Serikali katika bajeti hii kuyatekeleza mapendekezo ya Jaji Bomani ya kuiongezea serikali mapato ikiwa ni pamoja na kufuta misamaha ya kodi.

27. Mheshimiwa Spika, Ushuru wa mazao ni kero kubwa kwa wakulima inawapunguzia motisha wakulima, inachochea rushwa ya watendaji wa vijiji, kata na halmashauri. Waziri anapendekeza kupunguza kiwango cha ukomo cha kutoza ushuru wa mazao kutoka asilimia 5 ya bei ya kuuza mazao shambani hadi asilimia 3 ili kupunguza makali ya athari za msukosuko wa uchumi duniani kwa wakulima nchini. Hata hivyo anapendekeza hatua hii ianze kutekelezwa mwaka wa fedha 2010/11 ili kutoa nafasi kwa Serikali za Mitaa kujiandaa kupata vyanzo mbadala vya mapato. Kwa nini serikali isufute kabisa ushuru wa mazao hivi sasa, na itumie misaada ya mtikisiko wa uchumi kufidia halmashauri kwa mwaka mmoja wakati halmashauri zinajiandaa kutafuta vianzio vingine vya mapato? Badala yake inafidia madeni ya mabenki na wafanya biashara

28. Mheshimiwa Spika, Misamaha yote ya kodi, asilimia 83% inahusu makampuni yaliyosajiliwa T.I.C na asilimia 17 ni mashirika ya umma, taasisi za Serikali, taasisi za dini na asasi zisizo za kiserikali na misaada inayotoka kwa wafadhili. Hivyo sehemu kubwa ya misamaha ni ile ambayo Waziri ameendelea kuisamehe na sio hiyo ya kidini na asasi zisizo za kiserikali.

29. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani kwa kujali huduma zinazotolewa na taasisi hizi, pamoja na mapungufu yaliyopo ya baadhi yao kuitumia vibaya fursa hizi, kwani zipo taasisi zinapata misamaha lakini huduma zake ni ghali kuliko zile zisizo pata misamaha, hata hivyo ni vyema Misamaha hii ikaendelea na wale wanatumia vibaya fursa hizi wanyimwe kabisa fursa hii ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.

MIKOPO YA NDANI

30. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2009/10, Serikali inakusudia kukopa shilingi trilioni 1.08 katika soko la fedha la ndani ili kuziba nakisi ya mapato ya Serikali na kulipia dhamana zinazoiva. Katika mwaka wa bajeti wa 2008/09, Serikali iliendeleza sera ya kutokukopa kutoka vyombo vya fedha kugharamia bajeti yake hasa matumizi ya kawaida. Hata hivyo riba ya Hawala za Hazina (treasury bills) za siku 91 mwishoni wa Desemba 2008 ilikuwa asilimia 11.2. Utafiti wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF umebaini kuwa mabenki ya nje yaliyomo Tanzania yanakula njama kuhakikisha kuwa wanapata faida kubwa kwa kununua Hawala za Hazina. Kuongezeka kwa ukopaji na mapungufu yaliyopo katika kusimamia soko la Hawala za Hazina kutaongeza gharama za riba kwa serikali. Wakati serikali inaongeza kukopa na riba inapanda juu Rais Kikwete ameeleza kwamba “Serikali itayakopesha mabenki fedha kwa riba nafuu ya asilimia 2 ili na wao wawakopeshe wafanyabiashara fedha za mitaji ya uendeshaji kwa riba nafuu.” Serikali itakopa na kulipa riba ya asilimia 11 na kuyakopesha mabenki kwa asilimia 2. Benki Kuu haina mamlaka ya kupanga riba kwa wateja wa Benki za Biashara. Mikopo ya serikali itawaongezea mapato wenye mabenki bila kuwasaidia wafanya biashara wadogo na wa kati kwani mabenki bado inawaona kuwa hawakopesheki..

31. Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kufidia vyama vya ushirika na makampuni yaliyonunua mazao ya wakulima na kuyauza kwa hasara. Katika soko huria kuna kupata faida na kupata hasara. Wafanya biashara makini wa mazao hupanga bei zao za kununulia mazao kwa kuzingatia bei walioipata katika futures market. Hata hivyo wengine hawapendi kuchukua tahadhari kwa kutegemea kwamba bei itapanda na kwa hiyo watapata faida kubwa. Bei imeshuka kwa hiyo wamepata hasara. Jee hakuna wafanya biashara wa mazao waliolipa mikopo waliokopa kwa kujibana. Serikali ina uhakika gani kuwa mikopo hii ilitumiwa vizuri? Mkaguzi na Mdhibiti wa Serikali ayakague makampuni haya kuthibitisha kuwa hasara waliopata haikutokana na matumizi mabaya ya mikopo. Gharama ya ukaguzi huu ulipiwe na mabenki yaliyokopesha. La sivyo serikali inaweza kuliingiza taifa katika EPA namba mbili.

32. Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kusaidia wafanya biashara, makampuni na mabenki yaliyopata hasara. Lakini, hakuna hatua zozote zilizoelezwa za kuwasaidia wafanyakazi waliopoteza ajira na wakulima wanaopata bei mbaya ya mazao isiyorudisha gharama. Hivi sasa wakulima wa pamba hawavuni pamba yao kwa kuwa bei ya pamba ni ya chini sana na hakuna soko la uhakika. Si hotuba ya Rais wala ya Waziri wa Fedha iliyotoa matumaini kuwa walalahoi pia wanakumbukwa na watafidiwa hasara na athari walizozipata kutokana na mtikisiko wa uchumi dunian.

33. Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kutoa udhamini wa madeni ambayo wakopaji kwa sababu ya msukosuko wa uchumi wa dunia wanapata matatizo kulipa kwa wakati. Madeni hayo yanafikia Shs.270 bilioni. Kuna hatari ya serikali kujiingiza katika kudhamini madeni ambayo hatimaye yatabidi yalipwe na serikali. Serikali inajiongezea mzigo wa madeni yanayoweza kutokea (Contigent Liabilities). Serikali imeamua madeni haya yadhaminiwe kwa miaka miwili na siyo mwaka mmoja ili shughuli za Uchaguzi Mkuu wa 2010 ziwe zimemalizika. Hii itatoa mwanya kwa wanaodhaminiwa madeni wachangie kwenye kampeni na baada ya uchaguzi mzigo wa madeni ubebwe na serikali. Kuna hatari ya EPA nyingine kuzinduliwa. Ukaguzi wa kina wa mahesabu ya makampuni husika ufanywe na CAG kwa gharama za mabenki yaliyokopesha kabla ya serikali kuyadhamini makampuni haya.

34.
35. Mheshimiwa Spika, Waziri ameeleza kuwa kauli mbiu ya bajeti hii ni Kilimo Kwanza. Hata hivyo serikali imetenga shilingi bilioni 667 kwa sekta ya kilimo sawa na asilimia 7.0 ya matumizi yote ya serikali. Mwaka wa fedha wa 2008/09 sekta ya kilimo ilitengewa shilingi 513 bilioni sawa na asilimia 7.1 ya matumizi yote ya serikali ya bajeti hiyo. Kibajeti mchango (share) wa matumizi ya sekta ya kilimo umebakia kama bajeti ya mwaka jana. Ubadilishaji wa msamiati toka kilimo ni uti wa mgongo na kuwa kilimo kwanza hauonekani katika fedha zilizotengwa na serikali katika sekta hii.

36. Mheshimiwa Spika, Rais alieleza kuwa Serikali itatoa shilingi bilioni 20 kwa ajili ya mkopo wa riba nafuu kwa zana za kilimo kama matrekta madogo. Fedha hizi hazionekani katika bajeti ya serikali. Fungu lililotengwa kwa ajiri ya Agricultural Mechanization ni shilingi milioni 700 zinazotosha kuagiza matrekta makukuu 18 na zana zake kutoka Uingereza. Waziri kaeleza kuwa “Fedha hizi zitapatikana kufuatia kusainiwa mkataba wa mkopo baina ya Serikali ya Tanzania na India.” Je hana uhakika kiasi ambacho hazikuingizwa kwenye bajeti? Vile vile Rais alieleza kuwa Chini ya mkakati wa kujihami na kunusuru uchumi, Serikali itatoa shilingi bilioni 20 kwa Hifadhi ya Chakula ya Taifa kwa ajili ya kuongeza akiba ya chakula na kudhibiti mfumuko wa bei. Fedha hizo hazikutengwa katika bajeti tunayoijadili. Pia hakuna bajeti ya kuongeza maghala ya kuhifadhia chakula.

37. Mheshimiwa Spika, Tatizo la umeme usio wa uhakika linaeleweka. TANESCO imeishatutahadharisha kuwa nchi inaweza kuingia gizani. Wizara ya Nishati na Madini imetengewa shilingi bilioni 285.5 ikilinganishwa na shilingi bilioni 378.8 zilizotengwa mwaka 2008/09, sawa na upungufu wa asilimia 24.6. Sababu aliyoitoa Waziri ya kupunguza bajeti ya wizara ni “kumalizika mikataba ya kuzalisha umeme kwa makampuni ya kukodi ya Dowans, APR na Aggrekko.” Serikali inatenga fedha ikiwa kuna mikataba ya kuifilisi nchi lakini hatuwekezi raslimali yetu ya kuzalisha umeme wa uhakika. Waziri kaeleza kuwa Serikali itaikopesha fedha Artumas ili waweze kuendelea kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme kwa mikoa ya Mtwara na Lindi ili kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati kwa mikoa hiyo. Hata hivyo fedha za kuwakopesha Artumas hazimo ndani ya bajeti. Kwa nini serikali iikopesha Artumas. Kama serikali ina fedha kwa nini isingie ubia na kununua hisa za kampuni hiyo? Mhes spika Serikali ilikataa kuyapa ruzuku mashirika ya umma hata yaliokuwa yakifanya vizuri, na hatimae kuyauza kwa bei chee,jee sasa inakuwa bora kuzipa sadaka kampuni binafsi kwa kisingizio cha hali mbaya ya uchumi duniani?

38. Mheshimiwa Spika, Bajeti hii haieleweki na haitabiriki. Mkakati wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania dhidi ya Msukosuko wa Uchumi Duniani uliolezwa na Rais Kikwete haukuanishwa waziwazi katika bajeti na kutengewa fedha. Bajeti isiyotabilika inahujumu vipaumbele vya sera na matokeo ya malengo ya matumizi ya Serikali. Misingi mizuri ya Bajeti inataka Bajeti ya Serikali ijumlishe mapato na matumizi yote ya Serikali bila kujali taratibu maalum za kuendesha baadhi ya miradi na programmu, taratibu za kuidhinisha matumizi na vyanzo vya mapato. Kwa ujumla mapato yote yakusanywe na matumizi kupangwa bila kuzingatia chanzo cha mapato. Utayarishaji wa bajeti hii haukufuata misingi muhimu ya bajeti ya serikali.

39. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa utaratibu wa kutumia kadri tunavyopata (cash budget) utaendelea katika mwaka huu wa fedha makadirio yaliyomo ndani ya bajeti hayatafanana na matumizi halisi. Utaratibu wa cash budget unadhoofisha sana nidhamu ya bajeti. Mara kwa mara miradi ya maendeleo inaathirika sana na utaratibu huu kwani ndiyo huwa ya kwanza kupunguziwa matumizi. Utayarishaji wa bajeti unakuwa siyo makini kwani bajeti zilizopangwa haziheshimiwi. Bajeti hii imeweka mianya mipana ya rushwa hasa katika maeneo ya kulipa madeni na kufidia hasara na kudhamini mikopo ya makampuni. Serikali itabeba mzigo mkubwa wa madeni haya, hivyo kuendelea kuwabebesha Watanzania mzigo kila uchao..

MPANGO WA KUHAMI UCHUMI (Stimulus Package)

40. Mheshimiwa Spika, Siku moja kabla ya kusomwa kwa Bajeti, Rais Kikwete aliwahutubia Wabunge na Wazee wa Dodoma kuhusu mtikisiko wa uchumi duniani na jinsi unavyoweza kuathiri uchumi wetu. Hotuba ya Rais ililenga kuelezea hatua zilizochukuliwa na serikali kukabiliana na mtikisiko wa uchumi na ilikuwa inafafanua bajeti ya serikali iliyotangazwa na Mheshimiwa Waziri ambaye alieleza kuwa hotuba hiyo kwa kiasi kikubwa imerahisisha kazi yake ya kuieleza bajeti ya 2009/10.

41. Mheshimiwa Spika, Rais alieleza kwamba serikali iliunda kamati chini ya uongozi wa Gavana wa Benki Kuu. Matokeo ya kamati ya Gavana Ndulu ni kuwepo kwa mkakati wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania dhidi ya Msukosuko wa Uchumi Duniani. Katika mkakati huo mpango wa utekelezaji wa malengo na hatua mbalimbali za kuchukua zimeanishwa.

42. Mheshimiwa Spika, Pamoja na Wabunge kupata fursa ya kujadili Mwongozo wa Mpango na Bajeti mapema mwaka huu ambayo ni hatua muhimu katika maandalizi ya bajeti, kwa kuwa unatoa fursa kwa Waheshimiwa Wabunge kutoa michango yao mapema kabla ya mapendekezo ya bajeti hayajakamilika na kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupitishwa rasmi. Waheshimiwa Wabunge hawakupata fursa ya kujadili Ripoti ya Gavana Ndulu na Mkakati wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania dhidi ya Msukosuko wa Uchumi Duniani. Wabunge kama wawakilishi wa Watanzania wanastahiki kupata na kuujadili Mkakati wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania dhidi ya Msukosuko wa Uchumi Duniani. Kwa bahati mbaya hotuba ya Rais haijatolewa Rasmi kwa maandishi lakini ilikuwa na taarifa nyingi zinazohusu bajeti na baadhi ya taarifa hizo hazimo katika bajeti iliyowasilishwa na Waziri. Rais ameeleza Mpango wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania utagharimu shilingi bilioni 1,692.5 na pesa hizo zimetengwa katika Bajeti. Waziri hakuanisha waziwazi mpango huu katika bajeti yake.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2008/09

a. Mheshimiwa Spika, Mtikisiko wa uchumi ulipoanza mwisho wa mwaka 2007 na kuendelea 2008, Serikali ilieleza kuwa mtikisiko huo hautathiri uchumi wa nchi yetu. Wachambuzi wengine walipoeleza kuwa uchumi wetu utaathirika, serikali haikuwasikiliza na kwa hiyo haikuchukua tahadhari mapema. Takwimu za serikali zinaonyesha kwamba mtikisiko wa uchumi duniani hakuathiri ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Pato la taifa limeongezeka kwa asilimia 7.4. ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 7.1 mwaka 2007. Hata hivyo Waziri ameeleza “Kutokana na msukosuko wa kifedha na kiuchumi unaoendelea duniani, mwenendo wa makusanyo ya mapato umekuwa si wa kuridhisha katika kipindi cha miezi tisa ya mwanzo ya mwaka 2008/09 na mwelekeo ni kwamba hadi kufikia mwisho wa mwaka 2008/09 mapato hayatafikia lengo kwa asilimia 10;” Imekuwaje ukusanyaji wa mapato uathirike kiasi hicho wakati pato la taifa limekua zaidi ya mwaka jana. Hichi ni kitendawili,ni vyema waziri ukakitegua.

b. Mheshimiwa Spika, upungufu wa ukusanyaji wa mapato ya serikali unachangiwa na misamaha holela ya kodi. Kama Waziri alivyoeleza asilimia 30 ya mapato ya serikali sawa na zaidi ya shilingi trilioni 2 yanapotea kwa sababu ya misamaha ya kodi.
c. Mheshimiwa Spika, Naomba kwanza kutoa mtazamo wa Kambi ya Upinzani kuhusiana na Bajeti ya Tshs.9.5trn, wakati Tshs.1.7trn zinarudi kusaidia sekta binafsi kupitia mpango wa kuhami uchumi (stimulus package) ambao kwa jinsi ulivyo ni “stabilization package”. Hivyo bajeti halisi ni Tshs.7.8trn. (kiasi halisi kitakachoelekezwa kwenye shughuli za maendeleo na utendaji wa Serikali).

d. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imefanya utafiti kuona nchi zingine za dunia zinafanya vipi hiyo “stimulus package”. Katika hotuba hii tumeambatanisha mipango hiyo kwa nchi za Asia, sifa moja kubwa ya mipango hiyo ni kwamba mipango hiyo imetungiwa sheria ya Bunge ili utekelezaji wake uweze kusimamiwa na Bunge ili kuzuia matumizi mabaya.

43. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inakataa kutoa “an open blank cheque” kwa Serikali kulipa makampuni binafsi. Tunataka sheria ya “Appropriation Act” iwe na Schedule maalum ya “Stimulus Package” na iseme waziwazi nani atapata nini, kamati ya Fedha na Uchumi iwe inapata taarifa kila miezi 3 ya utekelezaji wa hiyo “stimulus package”

44. Mheshimiwa Spika, Ni ukweli uliowazi kuwa “stimulus package” inazinufaisha benki tu, kwa kuzipa mwanya wa kufanya biashara nzuri na Serikali kwa kutumia fedha za Serikali yenyewe, na ndio maana Nchi nyengine Serikali imelazimika kuwa na hisa ili kuhakikisha kuwa fedha iliyotolewa ambayo inatokana na kodi za wananchi inadhibitiwa na kurudi kwa walipa kodi na wapiga kura.

45. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2007/08 na ile ya 2008/09 Serikali ilikuwa imejizuia kukopa kwenye mabenki, kwa kigezo kikubwa kuwa mabenki yaweze kufanya biashara ya kukopesha Sekta binafsi. Zuio hili liliongeza ufanisi kwa mabenki kukopesha sekta binafsi kwani mikopo kwa sekta binafsi ilipanda hadi kufikia 40% (taarifa ya Sera ya Fedha-Gavana wa Benki Kuu ya Juni, 2009). Stimulus Package itapunguza mikopo ya Benki kwenda kwenye sekta binafsi, na yale mafanikio yaliyokwishafikiwa yatayeyuka, vinginevyo mabenki yawekewe viwango vya kufikia katika kutoa mikopo nje ya “stimulus package”.

46. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya Sera ya Fedha ya BOT Serikali itazikopesha benki kiasi cha Tshs.270Billion kwa minajili ya kuzikopesha Sekta binafsi. Aidha itatoa T.Bill za Tshs. 205 Billion ili kukopa kwenye mabenki hayo hayo. Je mabenki yatashindwa kutumia fedha zile zile ambazo Serikali imeziweka ili kukopesha sekta binafsi kutumia fedha hizo kufanya biashara na Serikali kwa fedha za Serikali? Hili litadhibitiwa vipi? Waziri atueleze.

47. Mheshimiwa Spika, Huu utaratibu wa mwaka huu wa bajeti ni ile inayoongeza matumizi, madhara yake makubwa ni kwamba mpango huu utaongeza “inflation”, na kwa kuwa mfumuko wa bei hapa kwetu hautokani na sera za fedha bali bei za mazao ya chakula, ni dhahiri uwezo wa kudhibiti ni mdogo mno. Hasa tukielewa kuwa kauli mbiu ya “KILIMO KWANZA” kama zile za “Siasa ni kilimo”, “Azimio la Iringa” n.k ambayo hadi leo hatujaweza kuwa na chakula cha uhakika.
48. Mheshimiwa Spika, Wito wa Kilimo Kwanza umeweka vipimo vya ufanisi (Benchmarks) au itakuwa kama Siasa ni Kilimo?
49. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ina wasiwasi mkubwa na kuongezeka kwa mfumko wa bei hadi kufikia asilimia 30. Kama hatua za uhakika za kudhibiti hazikuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuzalisha chakula cha uhakika, kama nitakavyoshauri hapo baadae.

50. Mheshimiwa Spika, Kutokana na taarifa hiyo ya Gavana (Policy Statement ya BOT) inasema kuwa BOT itaikopesha Serikali Tshs.300billion, na kitabu cha mapato (volume I) inaonyesha kuwa mwaka huu BOT haitatoa mrabaha (devidends) kwa wanahisa wake, Kambi ya Upinzani inauliza, hii maana yake ni kuwa zile Tshs 300 Billion ni malipo tangulizi “advance” ya Mrabaha kwa Serikali? Kama ndiyo hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapata nini katika mpango huu? Waziri atueleze.

51. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasema kuwa Serikali haina haja yoyote ya kukopa kutoka kwenye mabenki ya Ndani, jambo la kufanya ni kuweka hisa zake inazomiliki katika makampuni ya fuatayo kwenye soko la hisa. Hii itaenda sambamba na sheria ya kodi ya mapato kifungu cha 73 cha hotuba ya bajeti ya waziri kuwa Kampuni zitakazo jioorodhesha katika soko la mitaji kuuza angalau 30% ya hisa zake itapunguziwa kodi ya mapato toka 30% hadi 25%. Hii ni motisha kwa kampuni kuuza hisa kwa wananchi, inatekeleza sera ya ujasirimishaji wa watanzania na kupanua “middle class income”, hivyo kuongeza uwezo wa watu wetu wa kununua na kupanua wigo wa walipa kodi.

52. Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia ushauri wetu, Serikali itapata kiasi cha Tshs. 475billion kwa kuuza hisa zake kwenye makampuni yafuatayo:
• Celtel (Zain) hisa 25%.. ……Tshs.200billion
• NBC hisa 20% …………………Tshs.150billion
• BP hisa 25% ……………………Tshs. 90billion
• Kilombero sugar 25%………..Tshs.35billion
• Jumla ya Mauzo ni………Tshs. 475billion

53. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona hapa tayari Serikali inawezakupata fedha ambazo walitaka kukopa kwenye mabenki, yaani Tshs.205billion, ambazo zingezidi kutokana na malipo ya riba, hivyo kuongeza deni la Taifa kinyume na sera ya mikopo.

54. Mheshimiwa Spika, Huu ni wakati mwafaka kwa Serikali kulieleza Bunge kuwa ina mkakati gani madhubuti wa kuwawezesha wananchi kuwa na fursa za kukopa katika taasisi za fedha na hasa benki, kwani haitoshi kuiachia Benki kuu kuzipa Benki za Kibiashara kuweka viwango vya riba huku faida yote inayopatikana na biashara hiyo inapelekwa nchi za nje. Ikumbukwe kwamba sekta isiyo rasmi ndiyo yenye mchango mkubwa katika pato la Taifa. Ni kwa njia ya mikopo yenye riba nafuu tu ndio uwiano huu wa mchango wa sekta isiyo rasmi katika pato la Taifa unavyoweza kukua. Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge lako Tukufu riba nafuu ni kiasi gani, ili wasiachie Benki kuamua wakati fedha ni za Serikali.

SEKTA YA AFYA

55. Mheshimiwa Spika, Kuna mapungufu makubwa katika sekta ya afya, pamoja na yale ambayo yanafanyika ukweli ni kwamba viwango vya huduma za afya bado ni duni sana, lakini kubwa zaidi ni uchache wa wataalam wa afya katika ngazi zote. Serikali ionyesha mpango mkakati wa kukabiliana na tatizo hili. Aidha Sera ya afya ina mapungufu makubwa, kwani hadi sasa hakuna mkakati wowote wa kuwa na viwanda vyetu vya madawa, vichache vilivyopo vina kiwango kidogo cha uzalishaji wa dawa.

56. Mheshimiwa Spika, Kuna haja kwa Serikali kuwekeza katika kuwa na Hospitali kuu za rufaa, ambazo zitakuwa na viwango vya kimataifa. Utaratibu wa kupeleka wagonjwa nje kutibiwa ni gharama kubwa kwa Serikali ni vema uwekwe utaratibu mbadala na huo, hivyo basi tuna uhakika hilo linawezekana na faida zake zitaonekana kwa watanzania. Hivyo juhudi zinazofanywa na NSSF na Apollo Hospital ziharakishwe ili kupunguza gharama hizi.

SEKTA YA USAFIRI

57. Mheshimiwa Spika, Uzoefu umeonesha kuwa mabadiliko ya maendeleo hupatikana zaidi pale panapokuwapo mabadiliko ya chama kinachoshika Serikali, hivyo hivyo mabadiliko ya kiuchumi huongezeka kasi pale huduma za usafiri wa watu na mizigo zinapokuwa za kuaminika na kutosha.

58. Mheshimiwa Spika, Inasikitisha kuona kuwa usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia ya reli umeteremka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano usafirishaji wa mizigo wa TRL umepungua toka tani 1,169,000 mwaka 2005 mpaka tani 429,000 mwaka 2008.

59. Mheshimiwa Spika, Kwa takwimu hizi hivi kweli Serikali iko makini katika kutumia jiografia yetu kujiongezea mapato kama program zetu za vision 2025, Mkukuta, Mini tiger n.k zinavyofafanua? Je? nchi yetu itatokana na kilema cha kutegemea mikopo na misaada?
60. Mheshimiwa Spika, Mbali na udhaifu huu Serikali ililipa Tshs.4.4billion kwa RAHCO ili kufuta madeni mbalimbali ya lilikokuwa Shirika la Reli bila ya Idhini ya Kamati ya madeni ya Taifa (NDMC) na hakuna ushahidi kuwa kampuni hizo zilirejesha kiasi hiki (Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Uk.17)
61. Mheshimiwa Spika, Wakati Serikali inatafuta fedha kuokoa shirika (TRL), huku tunatoa fedha bila ya nyaraka muhimu za kuthibitisha malipo, Serikali haijatueleza ni fedha kiasi gani wawekezaji wamewekeza, hadi sasa kwani na ukisoma taarifa ya Utekelezaji wa ahadi za Serikali,inasema Serikali kwa kushirikiana na muwekezaji inaendelea kutafuta fedha ili kutekeleza miradi hii(uk.227)

62. Mheshimiwa Spika, Ni kutokana na uthibitisho kama huu ndio tunataka hii Stimulus Package iwe wazi kwa umma kwa kupitia Bunge lako Tukufu ambalo kwa niaba yake kamati ya Fedha na Uchumi kwa kushirikiana nabaadhi ya wajumbe wa kamati za Kisekta husika wafanye tathmini na kutoa Baraka, vyenginevyo tunaweza kuwa na EPA No.2.

BANDARI

63. Mheshimiwa Spika, Sote tunaona aibu kuambiwa nchi yetu ni maskini huku ikiwa imezungukwa na nchi nane, tuna bandari kubwa na ndogo kadhaa zikiwemo za Dar es Salaam, Mtwara, Zanzibar, Tanga, Pemba, Mafia, Kigoma, Mwanza, Musoma n.k.

64. Mheshimiwa Spika, Wakati tuko katika ushindani wa kibiashara ndani ya Jumuiya yetu ya Afrika ya Mashariki na SADC, bandari yetu ya Dar es Salaam mwaka 2008 ilihudumia shehena yenye jumla ya tani 2,316,000 ikilinganishwa na tani 5,703,000 mwaka 2007 sawa na upungufu wa asilimia 59.4 sababu kubwa ikiwa ni kushuka kwa tija ya kupakua na kupakia mizigo na ushindani wa bandari za jirani, Mombasa, Beira na Durban- Meli zilizohudumiwa mwaka 2008 ni 697 ukilinganisha na 3,038 mwaka 2007 sawa na asilimia 77.1. Hivyo hivyo kwa bandari ya Mtwara ilihudumia tani 82,000 mwaka 2008 kulinganisha na tani 112,000 mwaka 2007, sawa na upungufu wa asilimia 26.8. Meli zilizofika ni 36 mwaka 2008 ukilinganisha na 99 mwaka 2007 sawa na upungufu wa asilimia 63.6. Bandari ya Tanga ilihudumia shehena ya tani 178,000 mwaka 2008 ukilinganisha na tani 542,000 mwaka 2007 sawa na upungufu wa asilimia 67.2%- (Hali ya Uchumi Uk.196/197). Meli zilizokuwa zinasafirisha mizigo na abiria na kutumia bandari ya Dar zimepungua toka 5232 mwaka 2000 na kufikia meli 4154 mwaka 2006, na 697 mwaka 2008.

65. Mheshimiwa Spika, Wakati washindani wetu wanapanua na kuboresha bandari zao, mfano, Kenya wamewekeza US$200 Million kwa upanuzi wa Bandari ya Mombasa, na ina uwezo wa kuingiza meli zenye uzito wa tani 100,000 sisi bandari ya Dar es salaam haiwezi kuingiza meli yenye ukubwa huo, hivyo hata ule mpango wetu wa kuleta mafuta “in bulk” unaweza kuwa ghali ukilinganisha na Kenya, kutokana na ukubwa wa meli inayoweza kufunga gati.

66. Mheshimiwa Spika, Leo hii Malawi wameanza kupeleka mizigo yao Beira-Msumbiji, na Uganda wanatumia bandari yaMombasa sisi tunalaumu hali ya uchumi Duniani. Kama tulipata pesa za kuwapa makampuni binafsi hivi tumeshindwaje kupanua bandari ya Dar es salaam na Mtwara na Pemba? Auntunaendeleza utamaduni wetu wa kutoa sadaka?.

67. Mheshimiwa Spika, Kutokana na sababu za udhaifu wetu wa kusimamia maamuzi yetu, wa Serikali yetu wa kuona fursa zilizopo tuzitumie ili kujijengea uwezo wa haraka wenyewe, tunaimba wimbo wa hali ya uchumi duniani zaidi kuliko kujielekeza kwenye udhaifu wa Serikali yetu katika kuamua na kusimamia utekelezaji wa maamuzi yake haya yataigharimu taifa letu kwani wenzetu wanatenda hawaongei.

68. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka uchambuzi wa kina, uliowazi na wa kushirikishwa Bunge katika kutumia 1.7trillion za “Stimulus Package”.

KILIMO KWANZA

69. Mheshimiwa Spika, Baada ya Utangulizi huo, sasa tuangalie changamoto za bajeti ya Serikali kwa sekta zinazotakiwa kuwa kiongozi katika kuondoa umasikini. Ingawa zipo juhudi kubwa za uhamasishaji na utashi wa serikali kufufua kilimo, bado kuna mapungufu makubwa katika eneo hili. Serikali ambayo haina uhakika wa kuwa na chakula cha kutosha ni sawa na Kiongozi wa familia kutokua na uwezo wa kuilisha familia yake. Hali hii inapunguzia Taifa heshima yake mbele ya Jumuiya ya Kimataifa. Kila inapotokea kipindi kifupi cha ukame, mara moja unaona Serikali na wananchi wake wakihangaika kutafuta chakula kwani akiba haitoshi. Hii ni aibu.

70. Mheshimiwa Spika, Tunapo kumbushana haya hatusemi kwamba Tanzania hakuna maendeleo au mabadiliko, lakini je maendeleo hayo ni endelevu kiasi cha kumhakikishia Mtanzania kwamba baada ya azimio la Iringa la mwaka 1972 la “siasa ni Kilimo” nakufuatiwa na “Sera ya Kilimo ni Uhai” ya Mwaka 1976. Ikaja tena kauli nyingine ya kilimo ni uti wa mgongo, je tunajitosheleza kwa chakula cha kutosha na hata ukame ukitokea tuna chakula cha akiba, au chakula kinapokuwa bidhaa adimu duniani tunaweza kuuza na kubakiwa na akiba? Au bado tunaendelea kuhemea chakula?

71. Mheshimiwa Spika, Katika hayo yote Waziri Mkuu kwa kuanza kuyavalia njuga mapendekezo hayo, lakini Jambo kubwa ambalo tunaliona kuwa litaendelea kuwa kikwazo katika utekelezaji wa mapinduzi ya Kilimo ni Sera ya Kilimo ambayo haiendani na hali halisi ya wananchi wa Tanzania. Katika madhumuni ya Sera ya Kilimo ya mwaka 1997 ni kukifanya kilimo kuwa endelevu na cha kisasa. Katika hali ya sasa pembejeo za kilimo zinapatikana kwa vipindi maalum na pengine nje ya msimu wa kilimo.

72. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Taifa ni chombo muhimu pekee cha kutafsiri na kutekeleza sera za Chama Tawala na Serikali kwa vitendo. Katika bajeti Serikali inapata fursa ya kupanga matumizi ya fedha kidogo zilizopo katika maeneo na sekta zinazohitaji kupewa kipaumbele ili malengo makuu ya Serikali yatekelezwe. Aidha, Rais Mstaafu Mkapa katika hotuba zake za kila mwezi alisema “Bajeti ni kipimajoto cha uhai wa mtu, na afya ya uchumi wa Taifa…………” “Daktari mzuri wa uchumi ataitumia bajeti kutoa tiba ya kupambana na umasikini na kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi.” …..mwisho wa kunukuu.

73. Katika nchi masikini kama Tanzania malengo ya Sera za Serikali yanapaswa kuwa ya kujenga mazingira mazuri ya kukuza uchumi na kuongeza ajira ili kupunguza na kuutokomeza umaskin. Katika kuendeleza uchumi matumizi ya Serikali yanapaswa kuwa na malengo matatu makubwa:-

(a) Matumizi ya Serikali yalingane na uwezo wa mapato ya Serikali matumizi ya Serikali yawe endelevu, pasiwe na nakisi kubwa ya bajeti inayojazwa kwa kuchapisha fedha, kukopa ndani au kukopa nje. Bajeti ya Serikali lazima ilenge katika kupunguza kutegemea misaada na mikopo.

(b) Bajeti ya Serikali igawanywe katika sekta mbali mbali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kutoa kipaumbele katika maeneo yanayokuwa chachu katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umasikini, na kuwa na chakula cha kutosha na nishati ya uhakika.

(c) Matumizi ya fedha za Serikali katika sekta zilizopewa fedha hizo yaendeshwe kwa ufanisi na kwa kuongeza tija. Darasa linalogharimu shilingi milioni moja lisijengwe kwa gharama kubwa zaidi,

74. Mheshimiwa Spika, Je malengo haya ni kwa kiasi gani yamefikiwa na Serikali? Mhe. Spika sote ni mashahidi wa wafanyakazi wetu waliotumikia Taifa hili kwa maagizo na miongozo ya Serikali yao wanavyo sumbuka na kutaabishwa katika kudai haki zao zilizotokana na ahadi za Serikali.

MAPITIO YA BAJETI YA MWAKA 2008/2009

75. Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2008/2009 Serikali ilipanga kutumia jumla ya Tshs. 7.3trn. Kati ya hizo jumla ya shilingi 2.43 trn. zilikuwa ni fedha za wafadhili. Matumizi ya kawaida yalipangiwa Tshs.4.8trn. Matumizi ya Maendeleo yalipangiwa Tshs.2.5trn. kati ya hizo Tsh. 1.55trn. ni fedha za wafadhili. Sambamba na hilo Serikali ilikuwa na upungufu wa ukusanyaji wa mapato yake wa Tshs.330, 080 millioni.

76. Mheshimiwa Spika, Tukiangalia mwenendo wetu wa matumizi na nidhamu nzima ya Serikali kubakia kwenye msitari wa kile ambacho kimepitishwa na Bunge kuwa ndiyo hicho kitakachotekelezwa bado hatujafanikiwa.

77. Mheshimiwa Spika, Matumizi ya kawaida ambayo hayaendani na yale yaliyopangwa na kuidhinishwa na Bunge katika bajeti ni matokeo ya udhaifu wa wazi kwa kushindwa kwa bajeti kama chombo cha kusimamia utekelezaji wa sera za mikakati na maamuzi ya Serikali.

78. Mheshimiwa Spika Ukisoma Hansard ya tarehe 16 Juni, 1994 Uk. 80 na 81 Marehemu Prof. Kighoma Malima akisoma bajeti ya Serikali alitoa suluhisho la jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa kupanda kila mara kwa matumizi ya kawaida dhidi ya makusanyo ya Serikali, kuwa ni kupunguza ukubwa wa Serikali. Serikali iliunda Tume iliyoongozwa na Mhe. Basil Mramba kutatua tatizo hilo. Hadi sasa toka tume ya Mramba iundwe ni takriban miaka19, hakuna lililofanyika na nchi inazidi kuwa na bajeti tegemezi kwa sasa utegemezi wa bajeti ni 33.45% pamoja na kuwakopa wafanyakazi hasa walimu,askari na watumishi wa afya ambao hadi sasa wanaidai Serikali Tshs. 8.46 Billion.

79. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani kwa kuliona hilo na kuendeleza maamuzi ya Serikali ambayo hayakutekelezwa ikaleta hoja ya kubadilisha Katiba ili kuwa na ukubwa wa Serikali unaotajwa na Katiba, lakini kwa masikitiko makubwa Mheshimiwa Spika unaelewa nini kilitokea hata waheshimiwa wabunge hawakupata nafasi yakuona hoja yenyewe kuisoma na kuielewa na kisha kuitolea maamuzi. Kambi ya Upinzani inaona upo umuhimu wa kuwa na kifungu katika Katiba kinachoweka ukomo wa ukubwa wa Serikali.

TAKWIMU ZINAZOTUMIKA

80. Mheshimiwa Spika, Shughuli za kila siku kama vile kuandaa Takwimu za pato la taifa hazipewi kipaumbele kwani hazina posho na magari ya mradi. Mipango yetu ya kukuza uchumi ni dhaifu kwa kutokuwa na takwimu sahihi.

81. Mheshimiwa Spika, Katika bajeti ya mwaka 2007/08 baada ya kuelezea kwa uthibitisho mapungufu katika takwimu zetu za Tiafa tulishuri kuundwa kwa Jopo la Wataalam wa ndani na nje kutathmini usahihi wa takwimu mpya za pato la taifa na kupendekeza taratibu za kuboresha ukusanyaji wa takwimu hizo. Je Mhe. Waziri utekelezaji wake ukoje?

82. Mheshimiwa Spika, Hoja yetu hii inapewa nguvu na mapendekezo yaliyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Uk. 162 kuwa pamoja na mambo mengine Serikali inakuwa na vipaumbele vingine ambavyo haviainishwi kwenye bajeti inayopitishwa na Bunge na hivyo kusababisha matumizi ya Serikali kutokuwa kama vile inavyopitishwa na Bunge.

83. Mheshimiwa Spika, Aidha kwa kuzingatia sheria ya fedha (Finance Act) na Katiba ya nchi ni Bunge tu ndilo lenye mamlaka ya kuidhinisha mapato na matumizi. Inashangaza kuona kuwa baadhi ya Idara za Serikali zinaweza kutumia fedha bila ya kuzingatia utaratibu wa kifedha. Kwa mfano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa uliidhinishiwa kutumia Tshs.34,516,361,130.74 lakini ikatumia Tshs.40,820,717,484.65 ikiwa ni ziada ya Tshs.7,914,996,040.27 kwa balozi zetu bila ya Bunge kuidhinisha. (Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Uk.176)

84. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda ielewe hatua zinazochukuliwa kwa wanaokiuka Katiba, Sheria na Kanuni za Fedha bila ya wasiwasi wowote, kwamba kitendo hicho ni kunyang’anya madaraka ya Bunge lako Tukufu.

KUPUNGUA KWA UWEKEZAJI TOKA NJE

85. Mheshimiwa Spika, Ni kweli kutokana na msuko suko wa kiuchumi duniani, uwekezaji kutoka nje kwa miradi yetu mikubwa kama mradi wa Kabanga-Nikel kule (Kagera) mradi wa uchimbaji Aluminium wenye thamani ya $3.5Billion. Miradi ambayo inaweza kufutwa kabisa ni ujenzi wa Bandari ya nchi kavu Dar, Ujenzi wa kinu cha kuzalishia umeme kwa kutumia gesi ya mnazi Bay pamoja na ujenzi wa kiwanda cha saruji Mtwara.

86. Mheshimiwa Spika, Waswahili wanasema ukiona mawimbi makali ndio unaingia gatini, uhodari ni wa nahodha tu, katika hali hii shirika letu la NDC limeweza kwa mfumo wa PPP kuanzisha mradi wa uchimbaji wa mkaa wa mawe Ngaka, Songea na kuanzia mwezi wa Januari wataanza uzalishaji na wanakisia kutoa tani 1million kwa mwaka. Cha kusikitisha shirika hili halijapewa hata senti moja na Serikali na zaidi hata kuruhusiwa kuendelea kufanya “exploration” kwenye mgodi wa mchuchuma iliwaweze kuzalisha umeme na kuuza mkaa wa mawe nje ya nchi.

87. Mheshimiwa Spika, Hali inaonesha kuwa pamoja na matatizo yaliyopo Duniani lakini zipo bidhaa bado zina soko zuri kama vile dhahabu na mkaa wa mawe kwani, mbiu ya mgambo ya mataifa makubwa ni “Energy” Nishati. Jee tunazitumia fursa hizi vizuri ? au tutaendelea kuimba hali ya uchumi duniani tu?Tunahitaji KUZINDUKA.

MICHANGO YA KISEKTA KATIKA UCHUMI

1. SEKTA YA KILIMO

88. Mheshimiwa Spika, Ukuaji wa uchumi wetu unachangiwa na sekta kadhaa, sekta ya kilimo ikiwa haiongozi ila ni muhimu sana, lakini kwa hali ya kawaida na kwa kufuatana na nadharia za uchumi ni kwamba kadri uchumi unavyokuwa Sekta ya kilimo inatakiwa kupungua na kutoa mwanya kwa sekta nyingine za uchumi kama viwanda kushika kasi, lakini kwa Tanzania ni tofauti.

89. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ina uhakika kuwa kilimo ndiyo sekta pekee yenye nguvu na uwezo wa kuiwezesha nchi yetu kuondokana na lindi la umaskini wa kipato. Hivyo basi ni dhahiri kilimo kinaweza kufanywa kuwa endelevu na chenye manufaa (sustainable agriculture) kwa wakulima na nchi kwa ujumla.

90. Mheshimiwa Spika, Madhumuni ya Sera ya Kilimo ya mwaka 1997 inatamka bayana kuwa ni kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na endelevu. Kwa maana hii ya madhumuni ya sera ni kwamba kilimo kilitakiwa kuwa ni kwa wale wenye uwezo mkubwa kiuchumi na ukweli ni kwamba watanzania wanaojihusisha na kilimo ni wale wenye uwezo hafifu sana kiuchumi na hii ni kasoro ya kisera kwani Sera haikuwapa kipaumbele wakulima,wafugaji na wavuvi wadogo. Mfano mzuri wa sera hii ni kama huu, wa wakulima wawili; mmoja ana uwezo kiuchumi na mwingine hana. Ikitokea teknolojia ya kuongeza uzalishaji imeletwa pale kijijini, ni yule mwenye uwezo atakayeipata na kuzidisha uzalishaji. Na wakulima wenye uwezo katika vijiji vyetu wapo wangapi? Aidha kilimo cha kisasa na endelevu ni kile kisichotegemea mvua na pembejeo hazitakiwi kungojea msimu wa mvua ili matumizi yake yawepo.

91. Mheshimiwa Spika, Matumizi ya serikali yalenge katika kuzindua mapinduzi ya kilimo na hasa kuongeza uzalishaji wa chakula ili tuondokane na aibu na adha ya baa la njaa. Tujifunze kwa wenzetu wa Malawi namna ruzuku ya mbolea ilivyoongeza uzalishaji wa mahindi ambako mfuko mmoja unauzwa kwa Tshs 8000/=. Ni muhimu mbolea na pembejeo za kilimo ziwafikie wakulima kwa wakati. Mbolea husika iwe imefanyiwa majaribio. Wakulima wa Mbeya waliotumia mbolea ya minjingu walipata hasara kwani mimea yao ilikauka. Serikali inawafikiria vipi wakulima waliopata hasara hiyo kutokana na mbolea?

92. Mheshimiwa Spika, ASDP ni programme ya miaka saba ambayo bajeti yake ni Tshs 2.7trillion kuanzia mwaka 2006-2013 hadi sasa ni takribani miaka mitatu imekwishapita, tulitakiwa kuwa tumeshatumia shilingi billion 578.6 sawa na asilimia 21.4, lakini tumetumia Tshs.198 Billion tu sawa na asilimia 7.3 ni jukumu la Serikali kuwaeleza wadau wake hadi sasa mafanikio gani yamepatikana, au programme imeshindwa hata kabla ya ukomo wake kufika?

93. Mheshimiwa Spika, Jambo la kustaajabisha ni kwamba kabla ukomo wa programme hiyo tunaanza tena programme nyingine, ambayo itakuja na kauli mbiu ya “kilimo kwanza” hii maana yake ni nini?

94. Mheshimiwa Spika, Kuna kitu ambacho kinapigiwa upatu nacho ni kilimo cha mkataba “contract farming”, kabla ya kuingia kwanza tuangalie mpango huu umewanufaisha vipi mkulima wa Tumbaku ambaye amekuwa mtumwa wa Makampuni ya Tumbaku kwa miaka zaidi ya 40 sasa. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuliangalia kwa mtazamo wa kuinua hali ya Mkulima na sio kwa upande wa mwekezaji peke yake.

95. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona ni busara kwanza kutumia miundombinu ya viwanda vya mazao ya kilimo iliyopo kwanza kabla ya kuanza kuhamasisha kilimo cha mazao ambayo viwanda vyake vya usindikaji havipo. Mfano viwanda vya bia, viwanda vya ngano, korosho n.k viwanda vya kukoboa na kusaga nafaka na pia viwanda vya kukamua matunda. Kwanza tuangalie viwanda hivyo vinaupungufu kiasi gani ya malighafi, kwa njia hii tutakuwa na uhakika mazao yote ya wakulima yatapata soko. Ni vyema viwanda vya Zana za Kilimo vya UFI (Dar) na ZZK (Mbeya) vifufuliwe kwa gharama yoyote ile ili dhana nzima ya kilimo kwanza iwe na maana kwa wakulima.

96. Mheshimiwa Spika, Kuna zao la muhogo ambalo ni zao linaloweza kustawishwa katika eneo lolote katika nchi yetu, zao hili ni hazina kubwa lakini Serikali bado haijakuwa na Mkakati wa makusudi wa kuhakikisha kuwa linakuwa zao mkombozi kwa kuuzwa nje ya nchi na pia kwa matumizi ya ndani.

97. Mheshimiwa Spika, Tuna uhakika Chuo cha Ukiriguru na Naliendele vikisaidiwa zao hili linaweza kuwa zao kubwa la kuingiza fedha za kigeni kama ilivyo katika nchi za Afrika ya Magharibi hasa Nigeria. Takwimu za uzalishaji wa zao hili kwa kipindi cha takribani miaka 21 iliyopita, kutoka 1986 hadi 2007 inaonyesha tofauti ya tani 88,000. Wakati tofauti ya Idadi ya watu kwa kipindi hicho ni 4,706,612 (kitabu cha hali ya uchumi mwaka 2007). Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani kilimo hicho kisivyotiliwa mkazo. Mfano mzuri wa uzalishaji wa muhogo ni wilaya ya Newala, wananchi wa Newala wanavyotumia zao hilo kuwanusuru wananchi wa Mkoa wa Mtwara katika vipindi vya uhaba wa chakula. Tatizo ni kuwa Serikali haijaona umuhimu wa zao hilo kwa uchumi wa nchi yetu.

98. Mheshimiwa Spika, Wakati sisi tunalalamika kuhusiana na kushuka kwa usafirishaji nje wa mazao asili na mazao ya nafaka, wenzetu Uganda takwimu zinaonyesha kuwa kulikuwa na ongezeko la usafirishaji nje kwa mazao yao, kama ifuatavyo: Kahawa iliongezeka kwa 5.2%, Pamba kwa 8.9%, Chai kwa 7%. Mazao ya nafaka, mahindi na maharage yaliongezeka kwa 55% na 34% kwa mfuatano. Kambi ya Upinzani inajiuliza ni vipi jirani zetu Uganda wanakuwa na ongezeko kama hilo na sisi tunashindwa?

99. Mheshimiwa Spika, kulingana hali ya uchumi ilivyo kwa sasa Duniani, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwekeza katika kilimo hasa cha chakula ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza masoko ya nje hasa nchi za jirani. Swali kubwa la kujiuliza ni kwa vipi bonde la mto Rufiji limetumika kuzalisha chakula? Mito isiyokauka zaidi ya 140 iliyopo katika Mkoa wa Morogoro maji yake yanatumikaje? Ni ukweli ulio wazi kuwa kwa sasa Tanzania inaweza kujivunia soko la takribani watu 100million au zaidi kwa nchi jirani pamoja na zile mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Hii ni pale kama Serikali itakuwa na mtazamo chanya kuhusiana na biashara.

NISHATI

100. Mheshimiwa Spika, Ili kilimo kiende nilazima nishati ya umeme iwe ya uhakika,kwani huwezi kuwa na viwanda vya kusindika mazao bila ya kuwa na nishati. Hivyo kutokana na kauli mbiu ya kilimo kwanza, Kambi ya Upinzani tunasema kwanza “Kilimo na Nishati”.

101. Mheshimiwa Spika, Katika kubuni njia za kumpunguzia mzigo wa maisha Mtanzania, Kambi ya Upinzani imefanya utafiti kuona wenzetu ambao wameamua kubana matumizi wanafanyaje katika kupunguza matumizi ya umeme.

102. Mheshimiwa Spika, Kuna nchi nyingi ambazo wamepanga mipango madhubuti ya kutumia “energy saving bulbs” kwa ajili ya kupunguza gharama za uzalishaji mfano mzuri ni Nchi ya Uganda ambao wana mpango wa kusambaza balbu 800.000 ili kuweza kuokoa kiasi cha zaidi ya US $ 1.000.000 kwa punguzo la MW 30. Na Serikali ya nchi hiyo tayari wameondoa VAT ya asilimia 18 na import duty ya asilimia 25 katika bajeti ya mwaka jana kwa kampuni ya Osram ya Ujerumani kwa uingizaji wa taa hizo ili kupunguza gharama za manunuzi na kutoa bure kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kununua balbu.

103. Mheshimiwa Spika, Kutokana na tafiti zilizofanywa nchini Kenya zinaonesha kuwa nchi hiyo inapoteza kiasi cha sh. Bilioni 10 za Kenya kwa mwaka kwa kutumia taa ambazo zinatumia umeme mkubwa ambazo fedha hizo zingeweza kuwasomesha Wanafunzi wa Shule zote za Msingi Nchini humo. Na laiti kama kila nyumba itatumia “energy saving bulbs” basi wangeliweza kuokoa kiasi cha MW 131 ambazo ni sawa na punguzo la asilimia 80. Hii inaonyesha kwa kupitia mpango huu “line” yenye uwezo wa kuwahudumia wateja wapatao 1.000 basi ingeliweza kutoa huduma kwa watu 5.000.

104. Mheshimiwa Spika, Kutokana na mpango huu pia Nchi ya Ghana wameweza kuokoa kiasi cha fedha US$ 12 milioni kwa kuweza kupunguza GW 2. Nchi ya Australia tayari wameshapitisha sheria ya upigaji marufuku wa uuzaji wa taa za zamani ambazo hutumia umeme mkubwa na badala yake kuhamasisha utumiaji wa “energy saving bulbs” nchi nzima.

105. Mheshimiwa Spika, Wakati tukiona nchi mbali mbali duniani zinafanya juhudi hizo ni dhahiri kuna nafuu kwa mfano, mtu mwenye kipato cha wastani na anae ishi kwenye nyumba ya kawaida yenye familia ya kiafrika huwa anatumia wastani wa unit 380 za umeme kwa mwezi kwa wale wanaotumia balbu ya watt 60 lakini familia hiyo hiyo inapotumia balbu ya watt 20 (energy saving bulb) angetumia wastani wa unit 125, ikiwa ni punguzo la matumizi la asilimia 67. Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali kuifanyia kazi taarifa hii ili tupunguze matumizi ya umeme.

UVUVI

106. Mheshimiwa Spika, Sekta ya uvuvi na hasa ile ya uvuvi wa bahari kuu (deep sea fishing) ni sekta ambayo kwa miaka mingi tumekuwa tukiipigia kelele nyingi sana kuwa Tanzania haijaitumia vizuri katika kukusanya mapato. Haya ni baadhi ya yale tuliyoshauri, Katika kuhakikisha kuwa Sekta Uvuvi inaleta mabadiliko ya kiuchumi kwa nchi na wananchi kwa ujumla, inashauriwa bandari za Mtwara, Dar es Salaam,Tanga na Zanzibar zitenge maeneo ya bandari za samaki (Fish Ports and Fish Processing plants) ili meli zote za uvuvi wa bahari kuu zilazimike kununua mahitaji yao yote ya mafuta, maji, chumvi na vyakula wanapo kuja kukaguliwa kwa ajili ya kukusanya mapato. Aidha njia hii itakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa maana ya kuwepo kwa kile kinachoitwa “forward and backward linkage” Kwa uamuzi huu mapato yanakisiwa kuwa Tshs.3bn ambayo Serikali ingelikusanya.

SEKTA YA MIFUGO

107. Mheshimiwa Spika, sekta hii imekuwa ikichukuliwa kama vile mtoto wa mitaani ilikuwa haipewi heshma inayostahiki.Ni matumaini ya Wafugaji,baada ya kuwa na wizara maalum,hali ya wafugaji ikabadilika kwa kuwa na madawa,majosho na maeneo maalum ya malisho ya mifugo yao.

108. Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa mazo ya baharini na kwenye maziwa,mifigo inaweza kuwa kichecheo kikubwa cha mapato ya haraka haraka kama ushirikiano wa wafugaji na serikali utaimarishwa zaidi ili kutumia masoko kama ya SAUDI ARABIa ambao kwa wastani huagizia ma milioni ya mbuzi,kondoo na nyama kutoka nchi mbali duniani kwa matumizi yao,ibada ya Hijja na Umra.Uganda imepewa order ya mbuzi 10000 kwa mwaka. Na sisi tunaweza kutumia fursa ya masoko hayakama tutawapa hudma stahili wafugaji wetu.

SEKTA YA UNUNUZI NA UGAVI

109. Mheshimiwa Spika, Serikali kama zilivyo Serikali karibu zote Dunia nzima ndiyo mnunuzi mkubwa wa vifaa mbalmbali na huduma kwa wananchi wake kwa kila mwaka. Manunuzi hayo uhusisha kuanzia vifaa vya maofisini hadi mitambo mikubwa ya ma-hospitalini. Manunuzi haya hutumia mabilioni ya shilingi kila mwaka, ambapo hufanywa kwa njia ya kutoa zabuni mbalimbali.

110. Mheshimiwa Spika Katika kadhia hiyo yote ya kufanya manunuzi, Serikali imejikuta ikitumia gharama zisizo za lazima kama vile kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari, kama utaratibu na kanuni za zabuni za Serikali zinavyotaka, uchapishaji wa “tender documents” nakadhalika. Kama hiyo haitoshi muda wa vikao ambao zinatumia kamati za manunuzi katika kuangalia nyalaka za zabuni na vikao hivi wanakaa kada ya juu ya watumishi wa Serikali, maana yake posho za vikao zinalipwa.

111. Mheshimiwa Spika, Tanzania inatumia asilimia 80 ya fedha za, matumizi katika kufanya manunuzi ndani na nje. Kwa kuweka kumbukumbu sawa katika bajeti za Kambi ya Upinzani kwa miaka ya nyuma kuanzia bajeti ya mwaka 2004/2005 tumekuwa tukuishauri Serikali kuanzisha mfumo wa ununuzi kwa kutumia njia ya Mtandao, (e-procurement), ambao ungefanyika vizuri zaidi kama Serikali ingetenga fedha kwa Mkongo wa Taifa.

112. Mheshimiwa Spika, Serikali inatumia takriban 70-80% ya matumizi ya kawaida katika zabuni za bidhaa na huduma. Kwa mwaka wa fedha wa 2005/06 Serikali ilitumia Tshs. 2,018Billion kama matumizi ya kawaida, kati ya hizo Tshs.1,140 Billion zilitumika katika Zabuni.

113. Mheshimiwa Spika, Kama Serikali ingelitumia njia rahisi ya kutoa zabuni ambayo ingepunguza 10% ya gharama nzima ya zabuni ingeokoa Tshs. 141billion kwa mwaka katika ngazi ya Serikali Kuu, na kiwango hicho “kingekwenda sambamba katika ngazi ya Serikali za mitaa.

114. Mheshimiwa Spika, Inaonyesha kuwa Serikali bado haijaelewa ni kwa jinsi gani utaratibu huu utaokoa ubadhirifu na ufisadi wa hali juu unaotokea katika sekta nzima ya manunuzi yanayofanywa na Serikali. Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali ikubali kutumia utaratibu huu wa e-Procurement, wasi wasi wa kuwa wafanyabiashara wetu bado hawajaweza kutumia mtandao ni woga ambao unazidi kutoa mianya ya Serikali kuendelea kupoteza fedha za walipa kodi.

115. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya CAG Uk.122 unaonyesha hasara ya Tshs. 11,233,987,843.37 iliyotokana na udhaifu katika uingiaji na usimamizi wa mikataba ya manunizi. Hizi ni fedha nyingi sana kama zingeingizwa katikamipango ya maendeleo ya nchi.

116. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani itaendelea kuikumbusha Serikali kuwa utaratibu wa Electronic Procurement ndiyo utaratibu pekee ambao utakaoipunguzia Serikali matumizi katika manunuzi ya bidhaa na huduma, na kuiepusha na manunuzi ya bidhaa hewa. Kinyume cha hapo tutaendelea kulalamika upandaji wa gharama kwa watoaji wa huduma na manunuzi ya bidhaa kwa Serikali.

117. Mheshimiwa Spika, Bado Serikali inakusudia kutumia zaidi katika matumizi ya kawaida (shs.6.6 trillion) kuliko matumizi ya maendeleo (shs.2.8 trillion.) zaidi ya hapo katika miaka 12 ya bajeti za nyuma, matumizi halisi ya maendeleo yamekuwa madogo kuliko yalivyoidhinishwa katika bajeti. Hii ni kama tulivyo wahi kusema kuwa ukubwa wa Serikali utasababisha matumizi makubwa ya kawaida. Kambi ya Upinzani inaona kuna kasoro kubwa ya kiuwiano kati ya matumizi ya kawaida na yale ya maendeleo, hivyo kuchelewesha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini. Fedha nyingi zinatumika katika uendeshaji wa Serikali kuliko katika maendeleo na huduma za jamii na hivyo kupanda kwa pato la Taifa kutokuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida.

118. Mheshimiwa Spika, Kutokana na taarifa ya Makaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) katika Wizara na Idara za Serikali tulizochambua mathalani tumebaini kuna upungufu wa makusanyo ya mapato. Mrahaba usiokusanywsa kutoka kampuni ya almasi ya Williamson diamond Ltd ni shilingi 841,137,251. ,Tansort, Tsh.206,662,556. Aidha, misamaha ya Kodi nayo imekuwa ya kutisha, kwani hadi kufikia mwezi huu wa Juni 2008,kiasi cha Tshs.819.9 billion zilikuwa zimesamehewa kama kodi huku misamaha hii mingi ukiondoa ya mashirika ya dini ikiwa haijamnufaisha mwananchi masikini. Hiki ni kiasi kikubwa kwa nchi inayoomba misaada kila kukicha. Kambi ya Upinzani inaona huu ni upungufu mkubwa wa mapato ya wanyonge wa Watanzania kwa kuyatupa bila utaratibu wa wazi na unaoeleweka.

119. Mheshimiwa Spika, Tunaomba kumalizia tathmini yetu kwa kukumbusha kwamba Kambi ya Upinzani mwaka jana ilikataliwa ombi lake la kuunda Kamati ya Bunge kuchunguza EPA, Twin Towers, Mwananchi Gold Mine na Meremeta.

Kambi ya Upinzani, inamtaka waziri tena kutoa ufafanuzi, kuhusu mambo yafuatayo:

(i) Waziri alieleze Bunge lako Tukufu thamani halisi ya gharama za ujenzi wa majengo ya Benki Kuu (Twin Tower) ambayo kwa taarifa ya Benki Kuu gharama imeshazidi USD500 million au wastani wa Tshs. 600 billion. na mjenzi bado hajakabidhi rasmi majengo pamoja na kwamba lilifunguliwa na Rais Mstaafu Mkapa mwaka 2005 kabla ya kustaafu. Aidha kuna wasiwasi kuwa matumizi haya pia yalisabababisha mfumuko wa bei. Tunataka maelezo. Pia tunamtaka atupatie taarifa ya uchunguzi iliofanywa na Benki Kuu yenyewe ili tuweza kulinganisha na taarifa tulizo nazo.

(ii) Bunge lililopita tuliomba Bunge lako Tukufu lipewe maelezo juu ya uwekezaji wa BOT katika Mwananchi Gold Mine wa Dola za Marekani 5,512,398.55 hadi tarehe 30 June, 2006, kwamba je BOT iliendelea kuwekeza katika kampuni hiyo binafsi na kiasi gani cha mapato yaliopatikana hadi sasa? Tunataka Serikali itupatie maelezo ya kina ambayo tuna tumaini yatakuwa tofauti na ya mwaka jana, yatakuwa si majibu ya kisiasa.

(iii) Katika kikao cha bajeti cha 2006/07 Bunge lilielezwa kuwa ule Mradi ulioasisiwa na Marehemu Baba wa Taifa wa kuwapatia wanajeshi wetu fedha kwa ajili ya kuendeshea mradi wa Nyumbu, Meremeta Gold Co. ambayo ilikuwa chini ya uongozi wa Time Mining ya South Africa, na kudhaminiwa na BOT kwa USD100million, iko katika hatari ya kufilisika, lakini tukaambiwa kuwa BOT ilikuwa ikifanya tathmini.. Kambi ya Upinzani inataka kupata taarifa ya kina kuhusu tathmini iliofanywa na BOT juu ya mradi huo .Aidha tunataka kupatiwa taarifa rasmi juu ya umiliki wa mgodi huu sasa. Vinginevyo mgodi huo ukabidhiwe STAMICO kwa fursa zile zile au zaidi ya zinazopewa makampuni ya nje ili watanzania waonje matunda ya raslimali zao.

(iv) (a) Katika Kamati tuliomba kupewa taarifa juu ya JFC, Waziri katika majibu yake (mwaka jana 2007/2008) kwa kamati(uk2.) alijibu “wakati uamuzi kuhusu mapendekezo ya Tume unasubiriwa,bajeti ya 2007/08 imetenga mgao wa Zanzibar kwa utaratibu wa asilimia 4.5 ya misaada ya kibajeti” . Mwaka huu Waziri katika hotuba yake Uk. wa 19 amesema …..”Serikali zote mbili zimekamilisha uchambuzi wa taarifa za Tume na sasa ziko kwenye taratibu za kupatiwa maamuzi na Serikali hizo” mwisho wa kunukuu.

(b) Mheshimiwa Spika, hadi lini Serikali itaendelea na kuvunja Katiba? Naomba Waziri atueleze. Mhe. Spika, kutokutekelezwa kwa hili kumesababisha matatizo mengi katika mgawo wa rasilimali za mapato na matumizi ya Muungano, jambo linalopelekea manung’uniko yasiyokwisha. Kwa mfano, mapato yanayotokana na gesi, mapato ya kodi na pia gharama za kuchangia shughuli za Muungano. Ni vyema Mhe. Spika Bunge lako tukufu likasimama kidete, kukataa katiba kuendelea kuvunjwa.

(c) Kambi ya Upinzani mara hii inataka kupata tarehe ya kuanza mfuko huu, hatuko tayari kuendelea kushiriki kuvunja Katiba ya Nchi.

120. Mheshimiwa Spika, Katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka juzi 2007/08 (uk.59) Serikali ilikusudia “kuanzisha utaratibu wa kupitisha moja kwa moja (fast tracking) bila ukaguzi bidhaa zote zinazoagizwa…” Mhe.Spika, utaratibu huu ni mzuri kama upo uadilifu wa kutosha wa walipa kodi na wakusanyaji wa kodi. Mhe.Spika, Serikali ilipoona kuna udhaifu katika utendaji Bandarini, iliamua kukodisha shughuli za bandari kwa makampuni mbali mbali. Kambi ya Upinzani ilitegemea Serikali kuja na tathmini ya utekelezaji wa makampuni hayo ili iwe rahisi kwa Bunge lako tukufu kuamua, juu ya utaratibu uliopendekezwa na Serikali kama usimamiwe na TRA au kampuni binafsi, kwani kuna mashaka kwamba makampuni yaliyoko bandarini yameshindwa kufanya kazi zao kama ilivyotakiwa.

121. Mheshimiwa Spika,” unaweza kutumiwa Utaratibu wa “fast tracking kuficha udhaifu wa makampuni yaliyopewa kutekeleza shughuli za bandari. Aidha, utaratibu huu unaweza kuwa njia moja ya kuipunguzia mapato Serikali. Kambi ya Upinzani, inamtaka Waziri atupe tathmini ya mpango huu kwa kungalia makusanyo ya kodi kwa walipa kodi hao hao wakati walipokuwa wakikaguliwa na sasa ambapo hawakaguliwi Bandarini.

BAJETI YA SERIKALI YA 2009/10

122. Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza wakati ninachambua matumizi ya serikali ya mwaka wa bajeti 2007/08, matumizi halisi yaliyoainishwa katika hali ya Uchumi wa Taifa na bajeti iliyopitishwa na Bunge ni vitu viwili tofauti. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Uchumi hakufanya uchambuzi wa matumizi halisi kisekta au kwa kila fungu. Mheshimiwa Spika, hatuna sababu ya kuamini kwamba katika bajeti hii matumizi yatafuata makadirio yatakayopitishwa na Bunge hasa ukizingatia kuwa serikali bado inasisitiza kuendelea na utaratibu wa cash budget wa “kutumia tulichonacho.

123. Mheshimiwa Spika, Tukizingatia umaskini wa Tanzania, umuhimu wa elimu na afya katika maendeleo na ujenzi wa nguvu kazi iliyo na tija, nafasi ya mapinduzi ya kilimo katika kuchochea kukua kwa uchumi, kuondokana na baa la njaa na kuutokomeza umaskini, na ulazima wa miundombinu hasa barabara na nishati katika kuiwezesha sekta binafsi kuwekeza na kuzalisha bidhaa na huduma, mfumo wa bajeti utakaokidhi mahitaji ya maendeleo ni kuitengea Elimu asilimia 22, Afya asilimia 12, Kilimo asilimia 12, Miundombinu asilimia 20, Maji 10, Nishati asilimia 9, Mawasiliano,sayansi na teknolojia 5%, Matumizi mengineyo asilimia 10% ya bajeti ya serikali.

a. Mheshimiwa Spika, Kwa wastani bajeti ya serikali itumie asilimia 25 ya pato la taifa. Asilimia 20 ya pato la taifa likusanywe kama kodi na mapato mengine ya ndani ya serikali, na asilimia 5 ya pato la taifa itokane na misaada. Kwa kuanzia ikiwa misaada toka nje itakuwa mikubwa bajeti ya miundombinu iongezwe ili kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi. Uchumi unavyokua mapato ya serikali yataongezeka na kutegemea misaada ya nje kutapungua. Matumizi ya serikali hayafuati mwongozo huu.

b. Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha na Uchumi kaeleza kuwa “mapato ya ndani yamelengwa kufikia shilingi bilioni 4, 728.595 (trilioni 4.728) sawa na asilimia 18.5 ya Pato la Taifa (kwa takwimu za sasa). Hili ni ongezeko la asilimia 31 kutoka mapato yaliyotegemewa kukusanywa mwaka 2007/08.” Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 39 ukilinganisha na makadirio ya mwaka jana. Mheshimiwa Spika, Waziri hakufafanua maeneo yatakayoongeza mapato hayo. Ni vyema angalau Waziri akatueleza vianzio vya mapato haidhuru kwa mafungu makubwa kama vile kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kodi ya ushuru wa forodha, kodi ya mauzo na excise duty, kodi na tozo ya mafuta, kodi ya mapato na kadhalika.

MTAZAMO WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA VIPAUMBELE VYA BAJETI

Kupunguza Bajeti Tegemezi kutoka 34%-31.8%:

124. Mheshimiwa Spika, Katika jambo hili kambi ya upinzani haina budi kuikumbusha serikali kile ambacho tulikisema kwenye bajeti ya mwaka 2007/2008 kuwa tuliweza kupunguza utegemezi wa bajeti hadi kufikia asilimia 31.8%, tunashukuru serikali kwa kufanyia kazi mapendekezo yetu japo haikuweza kufikia lengo tulilokuwa tumeliweka mwaka jana kwani serikali imeweza kupunguza utegemezi hadi kufikia asilimia 34 tuu kwa makadirio ya bajeti ya mwaka huu.

125. Mheshimiwa Spika, Katika mkutano uliopita wa Bajeti tulisema sana juu ya jambo hili la kutegemea wafadhili katika maendeleo yetu. Kambi ya Upinzani inaipongeza TRA kwa kukusanya mapato kwa kiwango marudufu kulingana na miaka iliyopita. Lakini pia tulisema kuwa uwezo wa Serikali kukusanya mapato ni mkubwa zaidi, ila kuna uzembe mkubwa na kutojali (laxity), ubadhirifu,na ufisadi kama inavyodhihirishwa na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali mwaka hadi mwaka. Madhara ya Bajeti ya namna hii ni kwamba tunapopata matatizo inabidi kupita pita na kupunguza matumizi kadhaa (realocation) ili tu kuweka hali sawa ya madhara yaliotokea. Hii ni hatari kwa Maendeleo ya Watanzania kwa kiasi kikubwa kwani hata bajeti ya mwaka huu baadhi ya Wizara zilipunguziwa fedha bila mpangilio.

VYANZO VYA MAPATO

126. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika kuinua uchumi wa nchi na mwananchi imeibua vyanzo vipya vya mapato na vile ambavyo mwakajana tulivisema na baadhi kufanyiwa kazi na serikali kwenye bajeti yake ya 2008/2009 ingawa vyengine imeshindwa kuvifanyia kazi.

a) Uvuvi katika Bahari Kuu
127. Mheshimiwa Spika, Uvuvi katika Bahari Kuu ni moja ya maeneo ambayo kama Serikali ingelikuwa makini na kuchukua maamuzi tunayopendekeza,mapato ya Serikali yangeliongezeka marudufu. Meneo yenyewe ni kama yafuatayo:-

i. Kuongeza ada ya leseni kwa meli za nje zinazovua katika bahari kuu hadi kufikia USD 50, 000 kutoka, inayotozwa sasa ambayo ni USD18, 000 kwa mwaka. Kulingana na takwimu zilizopo ni kuwa kuna meli 140 (japo Kumbukumbu za Bunge-Kikao Cha tatu 5th.Feb.2004 Serikali ilisema kuwa imetoa leseni 193 za Meli za Uvuvi) za nje zilizopatiwa leseni za uvuvi katika bahari kuu ya Tanzania. Kwa maoni haya mapato ya yatakuwa Tshs 9.5bn. Ambayo sasa hayakusanywi. Pamoja na Mhe. Waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi kusema meli zinazovua kinyume cha sheria ni 200, kwa ajili ya kuwa na uhakika wa mapato bado tunabaki na takwimu za mwaka 2007/08

ii. Kuongeza tozo la mrahaba wa mauzo la asilimia 10 katika bidhaa za Samaki zinazovuliwa katika Bahari Kuu. Kila meli kwa mwaka inavua wastani wa tani 200 za samaki, kwa makisio ya chini sana, watavua Tani 2000 kwa mwaka. Bei ya soko kwa kilo ya samaki ni USD2.5 . Kwa wanaojua biashara ya sekta hii, kiwango cha uvuvi ni kikubwa zaidi. Kwa maoni haya Mapato yatakuwa shs. 130bn. ambayo sasa hayakusanywi na Serikali.

iii. Katika kuhakikisha kuwa sekta hii ya uvuvi inaleta mabadiliko ya kiuchumi kwa nchi na wananchi kwa ujumla Bandari ya Mtwara, Dar es Salaam,Tanga na Zanzibar inashauriwa zitenge maeneo ya bandari za samaki (Fish Ports and Fish Processing plants) ili meli zote za uvuvi wa bahari kuu zilazimike kununua mahitaji yao yote ya mafuta ,maji,chumvi na vyakula wanapo kuja kukaguliwa kwa ajili ya kukusanya mapato. (Vyombo vyetu vya ulinzi,vikishirikiana na TRA na Mamlaka ya Uvuvi kudhibiti mapato haya) Kwa uamuzi huu mapato yatakuwa Tshs.3bn. ambayo nayo sasa hayakusanywi na Serikali;

iv. Uvuvi katika maziwa ya Lake Victoria na Tanganyika, haujadhibitiwa vizuri. Hivi sasa kuna uvunaji haramu wa wastani wa Tani 36,000 kwa mwaka,kama uvunaji huu haramu ukidhibitiwa Serikali inaweza kujipatia kiasi cha shilingi 45 bn kwa mwaka. Uganda baada ya breeding stock kupungua mauzo pia yalipungua kwa wastani wa US$30million. Pia uvunaji huu haramu katika maziwa hayo matokeo yake viwanda vyetu vinakosa mali ghafi.Tunataka hatua ya dharura kuikabili hali hii kwa kutumia vyombo vya ulinzi na TRA ili kuongeza mapato na ajira. Zoezi hili litaongeza wingi wa samaki hivyo viwanda vya samaki vitaongeza uzalishaji na kodi itaongezeka. Serikali imeshindwa kushughulikia jambo hili hadi leo.

128. Mheshimiwa Spika, Maoni haya Kambi ya Upinzani sio tu yamepanua wigo wa kodi, lakini pia kwa hatua hizo tutakuwa tumedhibiti uvunaji wa raslimali zetu ambapo sasa hazivunwi kikamilifu.

b) Mapato yanayotokana na Misitu;

a. Mheshimiwa Spika, Chanzo kingine kikubwa ambacho vile vile mapato yake sasa hayakusanywi na Serikali katika sekta ya maliasili, na hasa bidhaa za magogo na mbao. Kutokana na ripoti za kiutafiti kutoka kwa kundi la wahisani na pia asasi kadhaa zisizo za kiserikali, (Kama TRAFFIC) (2005/2006) Serikali ilikusanya asilimia 4 tu ya mapato kwa mwaka 2004 yaliyopaswa kukusanywa kutoka katika bidhaa za magogo na mbao. Wanunuzi wakubwa ni China, India na Japan. Katika utafiti huo, katika kipindi cha 2001/2005 China peke yake ilinunua Cu.mita 18,316 x $150 kwa rekodi za Maliasili Tanzania kwa bei ya wastani wa USD2.7m. sawa na Tshs. 3.5bl. na CU.mita 108,605 kwa rekodi za Forodha za China, kwa maana hiyo ama kwa ufisadi au vyenginevyo Serikali imekosa mapato ya Cu.mita 90,289 x $450 = $40.6m. sawa na Tshs.52.8bn. utafiti huu ulihusu Magogo na mbao zinazotoka Mikoa ya Kusini tu. Taarifa hii inathibitisha Taifa lilikoseshwa fedha kwa kuuza kwa Dola 150 tu wakati bei halisi China ilikuwa Dola 450. Pia kiwango kilichouzwa kimefichwa. Huu ni Ufisadi.

129. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka majibu ya timu ya aliyekuwa Waziri wa utalii na maliasili aliposema kuwa ataituma China kwenda kuchunguza jambo hili ndani ya wiki mbili kwani hadi leo hatuna majibu ya timu hiyo. Pia bajeti ya Waziri haionyeshi kama kuna mapato yeyote yatakayopatikana kutokana na chanzo hiki.

a. Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inashauri hatua zifuatazo zichukuliwe:-

i. Halmashauri za Wilaya zilizo katika maeneo ambayo bidhaa hizi zinapatikana ziwe mawakala wa kukusanya mapato kutokana na bidhaa za maliasili. Uamuzi huu utapunguza kwa kiasi kikubwa ufisadi uliopo sasa katika Wizara ya Maliasili. Kila Halmashauri inayokusanya kodi ipatiwe gawio kutoka sehemu ya makusanyo;
ii. Mapato yote yakusanywe na TRA kwa kutumia stakabadhi za TRA kupitia Halmashauri za Wilaya kama ilivyo elezwa hapo juu;
iii. Mtu yeyote atakayekamatwa kwa kutorosha maliasili afilisiwe kwa mujibu wa sheria kama haipo itungwe;
iv. TRA mbali na kukusanya mapato ishirikiane na Bodi ya Mauzo ya Nje kuhakiki bei za Bidhaa zetu zinazouzwa nje ili kupata mapato halali ya Rasilimali zetu.
b. Mheshimiwa Spika, Kwa hatua hizi mapato ya maliasili misitu yataongezeka kwa asilimia 90 ya mapato ya sasa, makusanyo halisi yatakuwa Tshs 100bn ambazo hazikusanywi sasa.

(C ) Mapato yatokanayo na Utalii
130. Mheshimiwa Spika, Serikali inaona kuwa inakusanya mapato kwa wingi hadi kufikia asilimia 16.8% ya pato la Taifa katika Sekta hii. Hata hivyo, Serikali imeshindwa kufikia malengo ya watalii milioni moja kwa mwaka kama ilivyokuwa imepanga. Idadi ya watalii wanaokuja nchini ni wastani wa laki saba (719,031). Isitoshe, Serikali imekuwa ikipoteza mapato kutokana na watalii kulipia gharama za safari zao na baadhi ya huduma kwa Tour Operator huko huko kwao kwa wastani wa USD200-300 kwa mtu mmoja kwa siku. Mtalii anapo fika Tanzania ,huwa analipa wastani wa USD80-150 tu. Hivyo kuzipunguzia mapato hoteli zetu na kwa maana hiyo na Serikali.Kama watalii hawa wangelikua wanakuja katika “Package Tour” na kuwa tunakusanya wastani wa USD100 kwa siku kwa kila mmoja kwa muda wa siku 7, ukiacha mapato yasio ya moja kwa moja,katika eneo hili Serikali ingelikusanya kama kodi ya mapato 25% sawa ma Tshs 64.5bn ambazo hazikusanywi hivi sasa.

d) Mapato yatokanayo na Uwindaji:

131. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu za Maliasili, kuna vitalu 152. Kwa wakati huu Serikali inakodisha kwa wastani wa USD7500=kwa mwaka (mara nyingi wamiliki nao hukodisha kwa wenye fedha kwa wastani wa USD100,000.kwa mwaka) Ili kuongeza mapato ya Serikali, Kambi ya Upinzani inataka hatua zifuatazo zichukuliwe ili kuongeza mapato kama ifuatavyo:

• Kuwajasirimisha Watanzania vitalu vyote vya uwindaji;
• Ili kupata thamani halisi washauriwe kuingiza Vitalu hivyo katika soko la mitaji kwa kutumia”eletronic commerce.”;
• Kupandisha viwango vya kodi ya Uwindaji;
• Kutoza asilimia 25% ya mapato yatokanayo na Mtanzania atakayekodisha kwa mtu mwingine.

132. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa hatua hizi zinawezekana kwani Tanzania ni Nchi ambayo imejaliwa wanyama wengi zaidi kuliko Nchi nyingine za Bara la Afrika, wanyama wanene zaidi na ambao wanaishi kwenye mazingira halisia,na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipekee na hivyo kuwavutia wawindaji kutoka sehemu mbalimbali za Ulimwengu kutaka kuja na kuwekeza kwenye sekta ya uwindaji.

a. Kwa hatua hii Watanzania watakuwa wamewezeshwa kumiliki rasilimali zao wenyewe na pia kwa kuongeza viwango vya kodi ya uwindaji makusanyo yanakisiwa kuwa Tshs. 81bn ambayo hayakusanywi hivi sasa.

e) MAPATO KATIKA SEKTA YA MADINI

133. Mheshimiwa Spika, Katika sekta ya madini, kwa kulingana na ukaguzi uliofanywa na Kampuni ya Alex Stuart, kwa kipindi cha miaka mitatu Serikali imepoteza shillingi 1.3 trillion. Na hii imetokana na Serikali kutokuwa makini katika kufuatilia nyaraka halali zinazotumiwa na makampuni ya kuchimba madini. Ili kuifanya sekta hii ya madini kuwa na manufaa kwa Taifa na Watanzania wote hatua zifuatazo zikichukuliwa sekta hii itachangia zaidi:

i. Kufanya mapitio ya sheria ya madini na kupandisha asilimia ya mrahaba toka 3% hadi 5% kwa kuanzia;.
ii. TRA kuimarishwa kiutendaji na kukusanya kodi zote katika sekta ya madini;
iii. Katika mpango wa maendeleo wa kampuni husika, maendeleo ya jamii zinazozunguka migodi yaonekane wazi wazi na kuingizwa katika mpango wa mwekezaji;.
iv. Kati ya asilimia 5% za mrahaba utakaotozwa asilimia 2% ibaki katika Halmashauri ya Wilaya/Mji ambamo mgodi upo.
v. Katika masharti ya kuwekeza kwa wageni,ni lazima waingie ubia na Mtanzania au Halmshauri angalau kwa asilimia 10% ikiwa ni pamoja na thamani ya ardhi.
vi. Kuweka sharti ndani ya Mikataba na kubadilisha sheria kwamba atake kiuka mkataba au kusafirisha mali itokanayo na raslimali za nchi kampuni husika itafilisiwa;
vii. Kuhakiki madeni waliyokopa wawekezaji ili kupata kiasi halisi walichokopa, ikiwa ni pamoja na Tax Holiday kwa lengo la kufuatilia muda wa Kusamehewa Kodi.

134. Mheshimiwa Spika, Rais Kikwete aliunda Kamati ya kupitia Miktaba ya madini mwezi Novemba mwaka 2007 kufuatia Hoja Binafsi ya Buzwagi. Kamati imetoa mapendekezo. Swali la kujiuliza ni je? mapendekezo ya kamati yamezingatiwa vipi kwenye bajeti hii ya mwaka 2009/2010? Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuiwasilisha ripoti hiyo ndani ya Bunge mapema iwezekanavyo .

135. Mheshimiwa Spika, Kuna taarifa kuwa serikali imepoteza zaidi ya shilingi 883 bilioni katika kipindi cha miaka 10, kutokana na sheria mbaya ya kodi ya Mapato katika sekta ya madini iliyotungwa na Bunge mwaka 1997. Kupitia Financial Laws (misc. Ammendments) Act, 1997, nafuu ya ziada ya uwekezaji Asilimia 15 iliwekwa na kuleta upotevu huo wa mabilioni ya fedha za kodi. Sheria hii bado ipo katika sheria za nchi kwa kampuni zote zenye Mikataba (MDA) kabla ya mwaka 2001. Kambi ya upinzani Bungeni ilitarajia kuwa serikali ingefuta sheria hii na kuangalia uwezekano wa makampuni ya Madini kulipa fedha hizi kwani nafuu haikuwa na ulazima wowote na haimo katika kanuni za kodi. Kambi ya Upinzani inategemea kukusanya mapato haya kwa kiasi cha shilingi 88.3bn

136. Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inapendekeza kuwa msamaha wa Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta kwa Kampuni za madini ufutwe. Mwaka 2007/2008 Serikali kupitia msamaha huu haikukusanya sh 59bn. kutoka kampuni sita za madini. Waziri wa fedha amesema kuwa wale ambao hawatasamehewa ni wale ambao watawekeza kuanzia mwaka 2009 July, hivyo ni wazi kuwa wale wa zamani hawatolipa hata sentí moja, hivyo kulikosesha mapato Taifa na kupunguza faida ya ukuaji wa sekta ya madini katika uchumi. Kambi ya upinzani inataka kuwa msamaha wa kodi ya Ushuru wa Mafuta kwa kampuni za madini ufutwe mara moja. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iondoe misamaha ya kodi kwa mafuta wanayotumia wazalishaji wa makampuni ya madini katika migodi mikubwa na ya kati na kuanzisha mfuko maalumu wa kufidia punguzo la mafuta yanayopelekwa vijijini. Aidha, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako tukufu pamoja na wananchi kwa ujumla juu ya hali ya uchimbaji wa madini mbalimbali katika machimbo ya KABANGA NIKEL yaliyoko Mkoani Kagera Wilaya ya Ngara na uhalali wa wachimbaji walioko kwenye eneo hilo.

137. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa serikali inafanya mzaha na umuhimu wa sekta ya madini katika mapato ya serikali na kwamba kitendo cha Waziri kutokuzungumzia chochote juu ya Mapendekezo ya kamati ya Rais na utekelezaji wake ni dalili tosha kuwa serikali inatilia maanani zaidi maslahi ya wawekezaji kuliko ya Watanzania. Serikali ituambie kwanini wawekezaji wa madini wanaogopwa?.

f).Mapato kutoka madini ya Vito.

138. Mheshimiwa Spika, Taarifa mbalimbali za kitafiti zinaonesha kuwa Tanzania inapoteza mapato mengi sana katika madini ya vito kwa sababu ya uzembe na ufisadi. Kwa mfano, Katika soko la dunia mauzo ya Tanzanite mwaka 2005 yalikuwa na thamani ya Dola za kimarekani 400m. Hata hivyo rekodi ya Tanzania ni Dola 16m tu.Tuna taarifa kuwa Kenya ilipata tuzo kwa kusafirisha Tanzanite nyingi duniani wakati hawana Tanzanite. Kwa kutumia vito vyetu vya aina mablimbali kama vile Tanzanite,Alexadrite,Safaya,Ruby za aina zote n.k serikali ingeliweka usimamizi madhubuti tungeweza kulipatia taifa fedha kwa ajili ya kuendesha uchumi na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi kuliko hali ilivyo hivi sasa kuwa wananufaika zaidi wawekezaji wakubwa tuu huku wananchi wa maeneo yenye vito hivyo wakibakia kwenye lindi la umaskini mkubwa.

139. Mheshimiwa Spika, kama Serikali ingekubaliana na ushari wa Kambi ya Upinzani, Serikali ingepitia upya kabisa mwenendo mzima wa biashara ya madini haya ili kuwa na chanzo kimoja tu cha mauzo. Udhibiti huu ungeipatia Serikali mapato ya jumla ya Tshs. 150bn. ambayo hayakusanywi hivi sasa.

g). MAPATO KATIKA KODI NYENGINEZO

i) Misamaha ya Kodi
140. Mheshimiwa Spika, Eneo lingine ambalo tumekuwa tukipoteza fedha
nyingi sana ni eneo la misamaha ya kodi. Kama ilivyo katika taarifa ya kamati ya fedha na uchumi ya Bunge, inakadiriwa kuwa takribani shilingi 819.9 billion zilitolewa kama misamaha ya kodi katika mwaka wa fedha unaomalizika. Aidha hali ya misamaha ya kodi kwa upande wa Zanzibar ilikuwa ni ya kutisha kwani mwaka 2008/2009 TRA ilikusanya kiasi cha shilingi 28.1 bilioni huku misamaha ya kodi mbalimbali ikifikia shilingi 18.3 bilioni hili ni jambo la ajabu sana,Kwani misamaha hii ukiondoa ile inayolenga mashirika na madhehebu ya kidini haiwanufaishi wananchi masikini wa taifa hili. Ili kuongeza mapato yetu ya ndani Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ipunguze misamaha ya kodi kwa asilimia 50%. Uamuzi huu utaweza kuongeza mapato na kuwa Tsh. 409.95billion ambazo hazikusanywi hivi sasa.

ii) Kodi katika Posho ‘ALLOWANCES’

141. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato, sheria na.11 ya mwaka 2004 kifungu cha 7(1) na (2) , kila atakachokitoa mwajiri itabidi kikatwe kodi isipokuwa kama mfanyakazi atatumia fedha zake na mwajiri akamrudishia. Kwa mujibu wa sheria hii posho zote za warsha, semina, makongamano, mikutano na vikao zinapaswa kukatwa kodi ya mapato. Hii pia inajumuisha posho wanazopata Waheshimiwa Wabunge kutokana na vikao hapa Dodoma na Dar es Salaam.Ikirekebishwa sheria ya kodi ili kutoza kodi mapato haya kwa kiwango cha VAT yaani 18%. Hatua hizi pia ingelenga kupata manufaa yafuatayo:

(a) Mifuko ya Pensheni itapata wanachama zaidi.
(b) Kodi ya Serikali ambayo ni ya uhakika (P.A.Y.E. itapanda maradufu kwani employment allowance haitozwi).

Mhe. Spika, uamuzi huu Serikali ingepata mapato ya Tshs.6.07bn ambazo hazikusanywi hivi sasa.

h). Mauzo ya hisa za Serikali.

142. Mheshimiwa Spika, Bado kuna makampuni ambayo serikali ina hisa ambayo sasa ingefaa hisa hizo kuuzwa kwa wananchi lakini serikali ipo kimya katika hili. Kwa mfano, ni kwa nini serikali haiuzi hisa zake za kampuni ya simu ya CELTEL, NBC, BP, Kilombero Sugar n.k katika soko la hisa? Kwa nini haiuzi hisa zake ili serikali kupata mapato ya kuendesha uchumi? Iwapo serikali ingeuza hisa zake ingeweza kupata fedha kulipia na kutekeleza mipango mingine ya maendeleo. Soko la Hisa la Dar es Salaama lapaswa kuboreshwa kwa kuingiza kampuni nyingi zaidi ili kumilikisha wananchi hisa za makapuni na kufanya biashara ya hisa kuwa nzuri na yenye kuweza kutabirika. Kwa kuuza hiza za makampuni hayo kama tulivyoainisha mwanzo tungekusanya Tshs.475Billion.

i).Mapato kutokana na Bandari ya Mtwara na Tanga;

143. Mheshimiwa Spika, Eneo lingine ambalo bado halijatumiwa vizuri ni la kuuza mauzo nje ya nchi na hasa nchi jirani (Bonded Goods). Kama bandari ya Mtwara ingejengewa maghala ya kuhifadhia mazao na bidhaa kwa kufanya mauzo ya bidhaa zetu za viwandani kama vile cement na mifugo,mchele na bidhaa nyingine. Katika nchi ya Comoro, ambayo matumizi yao ni saruji tani 70,000, Mchele tani 40,000 kwa mwaka, na ng’ombe ni 4000 kwa wiki. Comoro inaitegemea sana Tanzania katika vyakula na vifaa vya ujenzi. Aidha tutasukuma uuzaji wa bidhaa zetu nje kama Muhogo, korosho,ufuta na samaki. Uimarishaji huu utaweza kutuingizia kiasi cha shilingi 4 billioni kutokana na kodi peke yake ambayo sasa haikusanywi.

j) Kodi itakayo tokana na Leseni za Madereva

144. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa mfumo wa leseni za madereva uboreshwe kwa kutoa leseni mpya kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya komputa. Leseni hizi zitakuwa na uwezo wa kuhifadhi taarifa zote muhimu za madereva. Hii itasaidia kupunguza uhalifu na hasa ajali za barabarani na pia itakuwa ni sehemu ya kitambulisho. Mradi huu uendeshwe kwa utaratibu wa PPP. Kwa makisio ya chini, madereva laki mbili na nusu mwaka huu wa fedha na ada ya leseni kuwa shs. 50,000, tutakusanya jumla ya shilingi 6.25bn ambazo sasa hazikusanywi.

k) Mapato kutokana na kuuza ndege ya Rais

139. Mheshimiwa Spika, Kutokana na dhamira yetu toka mwaka 2003 kwamba ununuzi wa ndege ya Rais ni anasa na gharama zisizo na msingi. Kwa sasa Serikali inatumia Shs 6 Millioni kwa saa ya kuruka ndege hii.Kambi ya Upinzani bado inaendelea na ushauri wake kwamba ndege hii kama alivyofanya Rais wa Ghana Bw. John Kufouri iuzwe kwa mnada. Kwa uamuzi huu Serikali itapata mapato Tshs 30 billion. Pia hatua hii itaiwezesha Serikali kupata fedha za kutengenezea ndege zake.
145. Mheshimiwa Spika, Kuwarahisishia Watanzania kwa kuifanya mamlaka ya manunuzi nchini ijitegemee kwa kutumia utaratibu wa manunuzi wa mtandao (e-Procurement) kwa ajili ya kusajili makampuni katika ngazi za wilaya, Mkoa hadi Taifa na nje zinazotoa huduma kwa Serikali. Kuiboresha mamlaka hii ili isaidie kupunguza rushwa katika manunuzi na kuipunguzia Serikali bei ya manunuzi kwa wastani wa si chini ya 15% ya manunuzi yake yote. Njia hii itatuingizia mapato kiasi cha shilingi 250 bn .

146. Mheshimiwa Spika, Ushauri huu uliotolewa na Kambi ya Upinzani,kama Serikali ingekubali kuufanyia kazi kuhusu sera ya mapato, yangeipatia Serikali jumla ya mapato ya ziada ya Tsh. 1,847.07 bn. Ushauri wa Mapato haya yote ni kutokana na kuboresha Vianzio vilivyopo na Kubuni vipya ambayo Serikali haikuviona.

Mhe.Spika, muhtasari, wa ushauri wetu juu ya vyanzo vipya vya MAPATO ya Serikali ni kama ifuatavyo:-

VYANZO VYA MAPATO
Maelezo Makusanyo(Tshs. Billioni)
1 Uvuvi katika maziwa na mito yetu 45.00
2 Ada ya Leseni-Uvuvi bahari Kuu 9.50
3 Tozo la Mrahaba-Uvuvi Bahari Kuu 130.00
4 Fish port and Processing 3.00
5 Bidhaa za misitu 100.00
6 Vitalu vya uwindaji 81.00
7 Kodi isiyokusanywa katika madini 88.30
8 Ushuru wa mafuta makampuni 6 madini 59.00
9 Mapato ya madini ya Vito 150.00
10 Misamaha ya kodi ya mapato 409.95
11 Kodi katika posho 6.07
12 Mauzo ya hisa za Serikali 475.00
13 Bandari ya Tanga na Mtwara 4.00
14 Leseni za Madereva 6.25
15 Mauzo ya Ndege ya Rais 30.00
16 Electronic Procurement 250.00
JUMLA 1,847.07

147. Mheshimiwa Spika, kwa ushauri wetu wa mapendekezo yetu ya mapato tungeweza kukusanya jumla ya Tshs. 7,091.138bn. au(7.091trillion) kama mapato ya ndani. Makusanyo haya yangekuwa ni ziada ya makusanyo ambayo Serikali imepanga kuyakusanya kwa kiasi cha shs. 5,234.068bn au(5.234trillion) Tofauti ya zaidi ya Shs.1,857.07bn au (1.857trillion) na bila kumuumiza mwananchi wa kawaida

148. Mheshimiwa Spika, Tukizingatia kuwa nchi yetu itapata misaada na mikopo kutoka nje kama jinsi ambavyo imeainishwa katika Makadirio ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2009/2010, Makadirio ya Mapato ya Bajeti hii yangefikia jumla ya Tshs.10,273.086bn au (10.27trillion)
MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU KODI MBALIMBALI.
149. Mheshimiwa Spika, baada ya Kambi ya Upinzani kuainisha vyanzo vipya mbalimbali vya kodi ambavyo havimuumiza mwananchi wa kawaida na pia baada ya mapato ya Serikali kuongezeka kutokana na vyanzo hivyo, hivyo basi tunaitaka Serikali ichukue hatua zifuatazo ili kuweza kuinua uchumi na kukuza ukuaji wa pato la taifa kama ifuatavyo;

Mishahara kwa watumishi wa Serikali;

150. Mheshimiwa Spika, Kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani, Kambi ya Upinzani inashauri kiwango cha chini cha Mshahara Wa wafanyikazi wa Umma kiwe Tshs 315,000 kwa mwezi, kwa ngazi nyingine mshahara ungepanda kwa asilimia ambayo italeta uiwiano baina ya kipato cha chini na cha juu. Ufafanuzi wa kina wa utatolewa na Waziri Kivuli wa Utumishi wa Umma.Kiwango hiki hakitatozwa kodi ili kuweza kumfanya mtumishi wa ngazi ya chini aweze kumudu gharama za maisha ,japo hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi fulani.

151. Mheshimiwa Spika, Kilimo na Nishati ni vipaumbele vyetu vikuu katika mpango mzima wa kuinua uchumi na kuongeza kipata kwa watanzania walio wengi. Kwa maoni ya Kambi ya Upinzani ni kuwa Serikali imejikita zaidi katika hatua ya awali kuwa na shule nyingi,idadi kubwa ya wanafunzi,jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.Kutokana na kazi kubwa iliofanywa na Kambi ya Upinzani ya kutafuta mapato zaidi,muono wetu ni kuimarisha hatua iliofikiwa kwa kuelekeza matumizi yetu katika kuboresha viwango vya elimu ili kuwa na ELIMU BORA Hivyo, tunashauri,kuwa tuhakikishe mkazo mkubwa unawekwa katika kuwaelimisha walimu,katika ule mtindo wa zamani. Pia Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuaondoa kodi kwenye vifaa vyote vya elimu kama vitabu, madaftari,kalamu n.k. Hatua hii itawawezesha wananchi kuweza kumudu gharama za kusomesha watoto wao na kuliendeleza taifa .

USHAURI WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA UTARATIBU WA MGAO WA KUTUMIA FEDHA

152. Mheshimiwa Spika, kama tulivyoshauri katika hatua mbali mbali za maoni yetu, katika kutekeleza mipango ya Serikali, na kuwafanya watekelezaji wa mipango hiyo waweze kutekeleza vyema,, utaratibu wa “cash budget” haufai. Utaratibu uliokuwa unatumika zamani wa ”Warrant system”urudiwe. Aidha Fedha badala ya kutolewa kwa mtindo wa kila mwezi, utaratibu wa kutoa fedha kwa kipindi cha miezi minne minne utumike.

153. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa vipaumbele tulivyo shauri, tumegawa mapato kama ya bajeti hii mbadala kama ifuatavyo:-
Tshs. Billion
1. Kilimo 12% 1232.7703
2. Nishati 9% 924.5777
3. Elimu 22% 2260.0789
4. Miundombinu 20% 2054.6172
5. Afya 12% T. 1232.7703
6. Maji 10 %. 1027.3086
7. Mawasiliano,sayansi na teknolojia5%.513.654
8. Matumizi mengineyo 10% 1027.3086

USHAURI WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA SURA YA BAJETI
Mapato: shilingi bilioni
A. Mapato ya Ndani 7,091.138

B. Mikopo na Misaada ya Nje Ikijumuisha 3,181.948
HIPC/MDRI

JUMLA YA MAPATO YOTE 10,273.086
Matumizi
Matumizi ya Kawaida 5,650.1973
1) Deni la Taifa 1,523.024
2) Wizara, 2,542.588
3) Mikoa 101.7035
4) Halmashauri 1,412.549
5) Matumizi mengine 71.197

C. Matumizi ya Maendeleo 4,623.086
(i) Fedha za Ndani 1,441.138
(ii) Fedha za Nje 3,181.948

JUMLA YA MATUMIZI YOTE 10,273.086

154 . Mheshimiwa Spika, kutokana na mchanganuo huo, tofauti za kimsingi za hoja ya Waziri wa Fedha na Ushauri wa Kambi ya Upinzani ni kama ifuatavyo:-
1. Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii kivuli utaiwezesha Serikali kutumia fedha za ndani kwa miradi ya maendeleo kwa asilimia 31.17%. Hivi sasa bajeti ya maendeleo ya Serikali inategemea wafadhili kwa asilimia 100%.
2. Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii kivuli utaiwezesha serikali kupunguza Bajeti tegemezi. Mikopo na misaada toka kwa wahisani ni asilimia 30.97% ya bajeti nzima kivuli badala ya utegemezi wa asilimia 33.45% uliowasilishwa katika bajeti ya Serikali.
155 . Mhe. Spika, mlinganisho wa kati ya Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti yake kivuli na Sura ya Bajeti ya Serikali ni kama inavyoonekana kwenye Kiambatanisho I.

MWISHO
156. Mheshimiwa Spika, Lengo kuu la Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii kivuli niliyowasilisha ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuondokana na bajeti tegemezi kama Taifa na kuwa na Taifa lililoelimika lenye Utawala unaoheshimika. Katika hotuba yetu nimeonyesha wazi wazi kuwa tunazo fursa kubwa za kupata mapato ya ndani. Tatizo ni mtazamo wa kifikra “MIND SET”. Changamoto kubwa tuliyonayo kama Taifa ni kwa viongozi kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine bila kujali itikadi za kisiasa, ili kwa pamoja tuwaondolee umasikini Watanzania waliokalia rasilimali zinazozidi mahitaji yao.Lazima sote tujiulize kwa nini wageni na wajanja wanatajirika,lakini wakulima na wafanyakazi wetu ni masikini? Taifa hili ni letu. Tusemezane, tujadiliane hatimae tusonge mbele.

157. Tuliyosema yanawezekena, yanahitaji viongozi na watumishi kuweka maslahi ya Taifa mbele. Raslimali tulizonazo zinatosheleza kama zitasimamiwa na kutumika kwa maslahi ya watu wetu. “TUNAHITAJI KUZINDUKANA”

158. Mheshimiwa Spika,Kambi ya upinzani, pamoja na shukrani zake, inapenda kutoa masikitiko yake kuwa imelazimika kutoa hotuba hii kwa dakika 40 tu. Mhe Waziri alitumia saa 4 kutoa hotuba zake. Hali hii imewanyima watanzania kufaidi Bajet mbadala kama ilivyo kwenye Hotuba hii kutokana na ufinyu wa muda. Mhe. Spika, naomba tena kukushukuru na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa kunisikiliza..
Mungu Ibariki Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

HAMAD RASHID MOHAMED (MB)
KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI NA MSEMAJI MKUU WIZARA YA FEDHA.
15 JUNI, 2009.

Kiambatanisho. I
TOFAUTI YA SURA YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA:
Tshs. Billion. BAJETI YA SERIKALI
(Tshs.Bn.)
Tshs.Billion. BAJETI MBADALA
(Tshs.Bn.)
MAPATO
A. Mapato ya Ndani 5234.068 7,091.138
B. Mikopo na Misaada ya nje 3,181.948 3,181.948
JUMLA YA MAPATO 9,513.685 10,273.086

MATUMIZI
C Kawaida:
i. Deni la Taifa 1,523.024 1,523.024
ii. Wizara 3,476.243 2,542.588
iii. Mikoa 123.013 101.704
iv. Halmashauri 1,565.974 1,412.549
v. Mengineyo —— 71.197
vi. Jumla ndogo 6,688.254 5,650.197

Maendeleo
Fedha za Ndani: ——- 1441.138
Fedha za Nje 2,825.431 3,181.948
Jumla Ndogo 2,825.431 4,623.086
JUMLA KUU YA BAJETI 9,513.685 10,273.086

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s