Mwakilishi CUF afariki dunia

Na Gladness Mboma, Godfrida Jola

MJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Soud Yusufu Mgeni, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jana, alikolazwa akitibiwa ugonjwa wa kansa ya mapafu.Ofisa Uhusiano wa Hospitali hiyo, Bw. Jezza Waziri,alisema jana Dar es Salaam kuwa marehemu Mgeni alifariki jana saa 3.50 asubuhi katika wodi ya Mwaisela.

Mdogo wa marehemu, Bw. Ayubu Yusufu Mgeni, alisema maradhi yalimwanza ndugu yake ghafla mwezi mmoja uliopita. Aliondoka salama Pemba kwenda kuhudhuria Mkutano wa Baraza la Wawakilishi, akiwa huko hali yake ilibadilika ghafla. “Marehemu alikwenda Dar es Salaam katika Hospitali ya Regency na kulazwa kwa muda wa wiki tatu kwa tatizo la pumzi, alikuwa anapumua kwa shida na madaktari waligundua kuwa alikuwa na tatizo la moyo,”alisema.Alisema kuwa juzi walimhamishia hospitali ya Muhimbili.

Siku iliyofuata hali yake ilionekana kuwa nzuri na alianza kupumua vizuri na kuwapa matumaini, lakini jana akiwa katika kipimo cha mwisho, alipumua ghafla na kufariki.

Bw. Ayubu alisema mwili wa marehemu ulisafirishwa jana na anazikwa leo katika kijiji cha Wambwa Chake chake Pemba saa 4 asubuhi.

Naye Ali Suleiman kutoka Zanzibar anaeleza kuwa Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa CUF Bw. Salim Bimani alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.”Kwa sasa Soud hatunaye katika dunia hii ndiyo kazi ya Mwenyezi Mungu….amefariki dunia katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar-es-Salaam’alisema Bimani. Alisema kifo cha Mwakilishi Mgeni kimeacha pengo kubwa kwa CUF kutokana na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya siasa.

Bw. Mgeni ni miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mwenye uzoefu mkubwa katika shunguli za Baraza. Amekuwa mjumbe wa Baraza hilo tangu mwaka 1980 akiwa Mwakilishi wa Jimbo la Vitongoji na Waziri katika Serikali ya Rais Idrisa Abdul Wakil.Pia aliwahi kuwa Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi na baadaye Waziri wa Kilimo na Mifugo huku akiwa Mjumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Alifukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi kufuatilia kuchafuka kwa hali ya kisiasa ambayo ilisababisha kufukuzwa viongozi watendaji wakuu wa Serikali na CCM wapatao nane akiwemo Maalim Seif Shariff Hamad mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Hadi anafariki dunia, marehemu Mgeni alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Wawi kupitia tiketi ya CUF na mmoja wa vigogo katika kambi ya upinzani.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Amani Abeid Karume ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha marehemu Mgeni.

Rais Karume ameeleza masikitiko yake na kushitushwa na kifo cha mwakilishi huyo. Alisema Kwa niaba yake binafsi, Serikali na wananchi wa Zanzibar, anatoa mkono wa rambirambi kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Wajumbe na wafanyakazi wa Baraza hilo, familia ya marehemu, ndugu, marafiki na jamaa zake wote.

Rais Karume ameeleza kuwa kifo cha marehemu Mgeni ni msiba kwa wananchi wote wa Zanzibar na marehemu atakumbukwa daima kwa utumishi wake kwa wananchi wa Jimbo lake la Wawi, Pemba na wananchi wa Zanzibar kwa jumla.

Amewaombea subira na ustahamilivu wafiwa wote.Kifo cha Bw. Mgeni kinakuwa cha pili katika Baraza la wawakilishi, kufuatilia kile cha Mwakilishi wa CCM, marehemu Daud Hassan Daud aliyefariki dunia mwishoni mwaka jana.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s