Kauli ya Mhe. Abubakar Khamis Bakary kuhusu kujiuzulu kwa Mhe. Abbas Juma Muhunzi

Abubakar Khamis Bakary,
Kiongozi wa Upinzani
Baraza la Wawakilishi,
P.o Box 902,
Zanzibar

3/03/2009

Mhe. Abass Juma Muhunzi,
Mjumbe wa BLW,
Jimbo la Chambani

KUH: BARUA YAKO ULIYONIPELEKEA YA KUJIUZULU UWAZIRI KIVULI WA
FEDHA NA UCHUMI NA NAKALA MBILI ZA BARUA ULIZONINAKILI MIMI
ULIZOMPELEKEA MHE. SPIKA KUHUSU

(a) WASIA
(b) KUJIUZULU NAFASI YA MWENYEKITI PAC

1. UTANGULIZI
Nilizipata barua nilizozielezea hapo juu, jana tarehe 02.03.2009 saa 8.00 mchana, lakini kichekesho cha mwanzo katika barua hizo ni kuwa zimeandikwa tarehe 03.03.2009. Pole, ni ishara ya kuchoka kwa mawazo mengi ya kujitakia! Kichekesho cha pili, barua uliompelekea Spika pia umetoa nakala kwa Spika!

2. KADHIA ZAKO

(1) Ni vyema sasa tuelezee jinsi ambavyo utu wako umeudhalilisha kwa kutokua muaminifu na kuwa laghai na tapeli mkubwa. Mwanzoni mwa 2006, baada ya Wah. Wawakilishi kupata mikopo, baadhi yao uliwalaghai na kuwambia wakupe pesa zao na utawaletea magari. Hata mimi uliniambia nikupe milioni 18 eti uniletee gari, lakini mimi sie Abubakar wa “Kyambani” mwenye macho ya kurumbiza bali ni Abubakar wa Mgogoni, kama ulivyosema katika message yako moja ulioniletea kuwa, ni mfupi na sitoongezeka kimo, lakini mimi ni mwenye heshima utu na akili timamu na zaidi muaminifu.

Waheshimiwa uliowaumiza kwa njia hiyo ya utapeli na ulaghai ni pamoja na:

1) Mhe. Abdulla Juma 9.5 millioni
2) Mhe. Hija Hassan Hija 21.0 millioni
3) Mhe. Salim Yussuf 18.0 millioni
4) Mhe. Shoka (zilikuwa 11 millioni lakini kwa kelele zake ukamletea skudo 1 ya thamani ya 6.5)anazodai sasa ni 4.5 mill.
5) Mhe. Mwanajuma 7.0 millioni
6) Mhe. Asaa 12.5 millioni

Jumla 72.5millioni

(2) Kadhia ya pili ni ile ya Raza, mfanyabiashara wa hapa Zanzibar, uliemwendea na kumlaghai eti akukopeshe vespa 5 na kila mwezi utamlipa 500,000/-. Miezi kadhaa imepita hajaona 500,000/- wala elfu (5,000/) ndio maana akaja kwangu kunielezea suala hili huku akinungunika kuwa hata simu akikupigia huitikii au kumjibu. Ndio maana hivi karibuni akaandika barua (mnamo tarehe 05/02/2009 hivi) kukudai fedha zake hizo. Barua hio aliipitishia Afisini kwangu, na nikakukabidhi mkononi mwako. Jee kutokulitaja deni hili katika madeni yako sugu unayodaiwa ulisahau au unaficha mgongo wako kwenye shina la njugu? Pesa za watu millioni kumi nazo umezikwapua!

(3) Kadhia ya tatu ya kuwaibia Wawakilishi wa CUF. Pesa zetu tunazozikusanya kila mwezi kwa shughuli zetu za uchaguzi tukijaaliwa na pia kwa mambo yetu mengine hapo 2010, ulituibia. Kwa sababu ni account yetu ya pamoja, uliaminiwa kupewa jukumu la kuweka fedha hzio Benki (PBZ) kwa njia ya hundi. Baada ya kuaminiwa huko, hundi nyingi sana hukuziweka benki katika account yetu ya pamoja. Ulifanya udanganyifu na kuzi “cash” hundi 18 za BOT za shs. 1.8millioni kila moja na hundi 35 za PBZ za shs. 3.2 millioni kila moja na uliziiba kwa njia hiyo baada ya wewe Mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Chambani kuaminiwa na wawakilishi wenzako. Huu, kisheria ni wizi baada ya kuaminiwa! Jumla ya fedha ulizoziiba kwa njia hii basi ni (18×1.8)mill +(35×3.2)mill. Sawa na (32.4)millioni + 112millioni = 144.4millioni

(4) Hata masuala maengine ya aina hii yanatugonga hadi hii leo vichwani mwetu, kama ile suala la kupotea kwa fedha nyingi katika Shirika la Meli Dar-es-Salam

Lakini watu wakasema tu lifunikwe kombe! Nataasaf kusema kuwa hata baada ya kombe kufunikwa, huyo alietakiwa apite hakupita, maana visa na mikasa iliendelea mpaka hii leo!

(5) Sasa Mwakilishi wewe, unaewawakilisha watu huku unafanya utapeli wa zaidi ya millioni mia mbili (200,000,000/-), huwaonei haya hata hao watu wako – wachilia mbali chama chako na wawakilishi wenzako ! Ni aibu kubwa sana.

3. KAULI ZAKO BARAZANI
Siku za bajeti, desturi yetu hukutana nyumbani kwangu kupanga utaratibu wetu, wewe una desturi ya kutohudhuria mikutano hio mara kwa mara kisingizio eti unatayarisha bajeti speech yako. Unajua kuwa bajeti speech zote za Wawakilishi huzipitia kwa pamoja katika kikao hicho isipokuwa yako ambayo huwa hujaiandika. Tunachoshtukizia huwa ni pale unapoisoma Barazani. Sasa suala la bei ya mafuta ulilisema wewe bila ya kuambiwa na chama au sisi wawakilishi. Lakini kwa sababu ulilisema, kwa misingi ya collective responsibility – ni sote tuliosema.

Ni kweli kabisa ulipolisema Barazani na yakatokea yaliyotokea mimi, kwa kukutakia mema nilikwambia umuombe radhi Spika na Baraza ili mambo yamalize. Hukutaka, sasa nifanye nini zaidi ya hapo. Hata hivyo uamuzi uliotolewa tukauchukua kama ni dhidi yetu sote na tukakusaidia kwa hali na mali. Hii tabaan huwezi kukataa.

Kauli yako nyengine ni hiyo ya kuropokwa ovyo kwa kutoa kauli katika hotuba zako bila ya kuishauri Kambi au hata mimi. Na hayo uliyasema mwenyewe ulipokuwa ukisoma hotuba hiyo – ulitaka wawakilishi wote tumtambue Rais mara moja na uliacha kazi ambayo tulitumwa na Chama.

4. UDANGANYIFU WAKO MWENGINE
Katika barua yako uliompelekea Mhe. Spika kuhusu “wasia” ulisema kuwa baada ya kuona kuwa pesa za magari ya waheshimiwa wawakilishi hazikurudi ndio ukachukua fedha zetu za mchango ili ufanye biashara na faida ikwamue matatizo yako.

Huu ni uongo safi maana fedha hii ulianza kuiiba tokea 2005/2006 kabla ya peza za magari kupewa. Jee kwa sababu wewe ni mwana wa “kyambani” ulijua mapema kama utatapeli pesa za magari na itabidi ufanye biashara kwa pesa za wizi baada ya kuaminiwa na ndio ukaanza kuzikusanya tokea 2005? Jee hujui pia kama pesa ulioichukuwa hata ukiifanyia biashara faida ni yetu pamoja maana pesa ni zetu pamoja na kwamba ukichukua faida peke yako ni wizi mwengine huo. Na hii ni fedha ya pamoja utaichukuaje siri siri bila ya wahusika kuwaarifu?.

5. MKUTANO MKUU WA CUF ULIOMALIZIKA JUZI
Wewe uliomba ujumbe wa Baraza Kuu kama walivyoomba wengine wote waliulizwa masuala pamoja na wewe. Aliyekuuliza suala ni Mhe. Asaa kutokana na kumtapeli 12.5 millioni zake na kuiba baada ya kuaminiwa pesa za wawakilishi wengine. Mjumbe wa Baraza Kuu lazima awe mwaminifu na anaeheshimu maagizo ya Chama. Kwa kadhia hizi, uaminifu wako uko wapi? Abass Ibn Juma bin Muhunzi el – Kyambani? Mhe. Asaa alifanya sawa sawa kukuuliza suala hilo. Hata mimi kama nilipata nafasi ya kukuuliza ningalikuuliza. Mbona prof. Lipumba aliulizwa suala baya sana na akalijibu na vivyo hivyo kwa prof. Safari itakuwa wewe Muhunzi usiulizwe?

6. UENYEKITI WA KAMATI NISIYOIJUWA AMBAYO WEWE UNAIJUA.
Si shangai, maana baadhi ya watu wa “Kyambani” huona mengi hata yale yasioonekana. Mimi kwa sababu najiamini kutokuwa na kasoro hiyo ulioisema sijali hata kidogo uongo unaousema wa kutaka kuonekana kuwa na kasoro hizo za kugawa visiwa.

Ikiwa unaoshahidi peleka popote unapotaka kuupeleka. Na napenda uelewe tu kuwa kisheria

“yule mtu anaeona kosa na akaficha au akanyamaza bila ya kutoa taarifa basi naye huwa mkosa sawasawa na yule alietenda kosa”

Sasa wewe ebu Muhunzi unasema unajua kama mimi ndio mwanzilishi na Mwenyekiti wa Kamati ya kuvitenganisha visiwa hivi, kitendo ambacho ni cha uhaini kama unavyosema; mbona ndugu yangu mpenzi uliificha habari hii muhimu siku zote mpaka unaisema hii leo kwa kuambiwa, kwa ushahidi wote uliopo kuwa wewe ni mwizi na tapeli – sijui kama ni wa kimataifa au wa kibaraza – lakini kwa vyevyote ni tapeli?.

Kwa hivyo kisheria madhali Kamati hii unaijua tokea kuanzishwa kwake na ukanyamaza kimya, basi na wewe kisheria umo. Kwa maana hiyo, sasa wewe ni jambazi, tapeli, mwizi na zaidi haini! Masikini wee – “Ngome yakuumiza, na we umumo ngomeni” (najikumbusha kitabu cha Abdillatif Abdulla “Sauti ya Dhiki” alipokuwa kizuizini na kutunga shairi hilo la ngome akiwa ndani).

Lakini uongo huu haunishtuwi hata kidogo maana katika message zako 15 ulizozileta kwangu moja wapo ulinambia kuwa hata kama wewe utakufa kisiasa, lakini damu itanirukia na mimi! Hivyo Mhe. Muhunzi hujui kama jitu likisha kufa huwa halina damu tena ya kumrukia mtu mwengine?.

7. WASIA WAKO FEKI
Karatasi uliomdanganya Spika ati ndio wasia sio wa kweli. Wasia una masharti yake, lazima yatekelezwe na pia uwe “registered” huko Mambo Msiige kwa Mrajis Mkuu wa Serikali. Usitapeli watu na kuwaibia halafu ukaandika wasia feki wa nyumba mbili mbovu zisizofika hata millioni 50 na kiwanja cha nyumba Chake Chake Pemba cha millioni 10 au 15 ukasema ni millioni 30. Akukubali nani na ushaonesha kuwa si muaminifu, hivyo kweli unahisi sisi hatujui kama uliyoyaeleza humo katika wasia feki kuna mengine umeficha. Sote tunajua kuwa umenunua shamba kubwa Kisauni ambalo ndani yake muna nyumba ambayo si nzuri. Lakini sasa kwa pesa za wawakilishi wengi (pengine na zile za Raza) unakiimarisha kwa kujenga nyumba kubwa na kufanya mambo mengine.

Jee unafikiri kuwa hatujui kuwa ndugu yako alieko Japan Haji Juma Muhunzi (Mungu amuepushe na kurithi utapeli kama huu wako) bado munaendelea kufanya biashara za magari.

Jee unafikiri hatujui kama Mhe. Ali Moh’d Bakar alimpelekea ndugu yako pesa za kununulia gari. Gari akainunua, akaitia kwenye Container, na ilipofika Zanzibar ukaiuza bila ya yeye kumwambia na ukamdanyanya kuwa gari haijafika, na baada ya kucheki na nduguyo ndio akajua jinsi uliyomtapeli gari hio!.

Huu si utapeli ni nini? Amma kweli kombe halifunikiki?

8. KUJIUZULU KWAKO
Kujiuzulu Mwenyekiti wa PAC na Uwaziri Kivuli kamwe hakuna maana. Maana kashfa hizi ulizojitia umewakashfu “Wakyambani” wenzio waliokupa kura zao kwa kukuamini. Sasa umewageukia, umewatiwa aibu kubwa kwa kashfa hizo. Hivyo mtu aliemuungwana wa kweli kweli basi huachia ngazi iliompeleka katika wadhifa alionao, na kwa wewe ni Uwakilishi. Mambo yanasema wenyewe (res ipsa loquifa) kwamba sasa sifa za uakilishi kwako wewe hazipo zimekwenda arijojo. Njia nzuri basi ya angalau kujipa heshima ni kwa wewe Abass Juma Muhunzi kujiuzulu Uwakilishi wako ambao ndio kiini cha mambo na sio uwaziri Kivuli wala Mwenyekiti wa PAC, ambazo hazioneshi maana halisi ya uwajibikaji wako. Nakushauri ujiuzulu, ili ionekane kama umechutama baada ya wewe mwenyewe kujivua nguo zake zote.

9. VIAPO VYAKO VYA TALAKA TATU
Nafikiri hapa ulikuwa ukijikumbusha ile michezo ya utotoni “talaka si mke wangu talaka si mke wangu”. Kwani bila shaka hutokufa peke yako katika chama ikiwa wapo wengine wataojivua nguo na kujianika kwa kashfa kama hizi.

Bila shaka wamkumbuka Mapalala, Nyaruba na wenzake, Akwilombe na wengi wengineo. Kweli si wewe peke yako. Wao wameshatangulia, wewe ndio hivyo na wengine wenye sifa mbovu kama hizo watakwenda tu!.

10. HEKIMA NA BUSARA HUKUZITAKA

Ulipowatapeli wawakilishi 7 nilio wataja hapo juu, baadhi yao walikuja kwangu kunilalamikia. Heshima niliokupa kwa sababu ya “usinior” wako katika Kambi yetu nilikwita wewe, mbele ya “senior” wengine wa Kambi kama vile Mhe. Soud Yussuf, Mhe.Hamad Masoud, Mhe. Muhydin na Mhe Mulla na nilikutaka utuelezee ilivyo na jinsi ya kulitatua tatizo hilo.

Jibu lako lilikuwa la kijinga na kijeuri na kuniambia kuwa nisikuingilie katika mambo yako na kwamba wewe utawalipa tu. Niliheshimu jawabu lako, nikarudi kwa walionituma kuwaeleza na baada ya hapo sikukuuliza tena.

Kadhia hii ya pili ya wizi baada ya kuaminiwa niliwaarifu wenzangu baada ya kugundua hayo; kitendo ambacho ni sahihi kwa sababu ni fedha zetu kwa pamoja.

Baada ya hayo tulikubaliana tufanye uchunguzi kwa kuwaandikia Benki halafu tukwite. Kabla hatujapata majibu ya Benki wakati mimi nikiwa Dodoma ukanitumia “message 15” kwenye simu yangu. Message hizo zote ni mbaya ukanitukana ukisema maneno ya kijinga na yasiyomaana kwangu mimi na kwa Wawakilishi wengine. Message zote hizo ninazo”. Massage zote hizo sikuzijibu kutokana na uungwana wangu na heshima yangu, na bado ninazo sijazifuta. Message nilioijibu ni moja tu ulipouliza niko wapi unahaja na mimi; na nikakujibu niko Dodoma, wewe baadae ulisema kuwa hukunikusudia mimi, bali ulimkusudia Mhe. Hamad Masoud.

Bado uliendelea kutuma message kwa Mhe. Asaa tena za vitisho hivyo hivyo na zaidi ukampa maelezo ya mdomo Mhe. Ali Moh’d Bakar aje anielezee “eti utahakikisha kwa vyovyote juu chini kuwa utaniua au kuniweka kilema cha maisha kwa sababu, nimekutolea siri zako na kukukashifu. Aliyekukashifu ni nani? Ni mimi au ni wewe mwenyewe? Kama una uwezo wa kuniuwa au wa kuniweka kilema fanya. Lakini wewe si Mungu na mwenye uwezo huo ni mwenyewe tu Subhanahu Wataala. Hata hivyo siku hizi mara nyingi husikia jambazi fulani huua au kumpiga mtu akamtia kilema. Kwa maana hiyo ninayachukua kwa uzito unaostahiki.

Sasa munkari yote hii, bado tukae tuseme tuzungumze na wewe! Inawezekana?.

11. MZUSHI WA MAMBO
Sina azma ya kumtetea Katibu Mkuu, lakini nina hakika amekwita si chini ya mara 2 (mbili) kukuasa kua utafute njia pesa za watu uzilipe. Leo unazusha kuwa wewe ndie uliekwenda Afisini kwake na ilhali yeye ndie aliekwita! Tafadhali punguza uongo. Katibu Mkuu alikunasihi mara kadhaa, lakini wakati huo kasi ya utapeli na wizi baada ya kuaminiwa umekutanda. Sasa unakamata maji katika mkondo wa maji ambao unakuzamisha! Hayakuokoi maji hayo.

12. WASHAURI WANGU
Mwisho ni vyema ukaelewa kuwa Wawakilishi wote wa CUF ni washauri wangu, na ninawashukuru sana. Hata wewe ulikuwa miongoni mwa washauri wangu. Hao uliowataja nibora tu useme kama una VISA nao. Lakini wote kwa pamoja hukutana na kuamua mambo yetu.

Mimi ninachokuombea kwa niaba ya wenzangu wote ni kuwa Mwenyezi Mungu akupe tauhid uondokane na tabia hii mbovu na mbaya ya utapeli na wizi baada ya kuaminiwa maana mara nyengine unaweza kuwafanyia watu wasio na imani wakakuuzia hata underwear yako. Lakini hii haina maana kuwa na sisi hatutazidai fedha zetu, la hasha!

13. MWISHO.
Nakusudia kuwanakili wale wale uliowanakili wewe kwa mantiki ile ile yako wewe. Lakini mimi ninamuongeza Mwenyekiti wa CUF Taifa ili aone jinsi wawakilishi wake wengine walivyoacha kazi ya kuwakilisha watu na kujiingiza katika utapeli na wizi. Pia ninamnakili Katibu wa Baraza kwa kumbukumbu za Baraza kwani si vibaya pia Baraza kujua kuwa limepata katika kipindi Fulani Mwakilishi mkorofi, tapeli na mwizi.

Ninafunga barua hii kwa kujikumbusha vikatuni vilivyochorwa katika gazeti moja la zamani likionesha watu wawili, mmoja manywele timtim na mmoja wa kawaida. Walikuwa wakibishana kwa makelele. Baadae alipita mtu mwengine na kumuasa yule mtu wa kawaida kuwa aende zake na asibishane na mwandawazimu – maana watu wengine wakiwaona hawatojua tofauti zao!

Waheshimiwa wanakiliwa wote nakusudia kuufunga mjadala huu na kwamba sina nia tena ya kujibizana na mtu ambaye nikiendelea kubishana nae pengine watu hawatojua tofauti zetu.

Ahsante sana,

…………………
Abubakar Khamis Bakary
Kiongozi wa Upinzani
Baraza la Wawakilishi
Zanzibar.

Nakla:

1. Mhe. Mwenyekiti wa Taifa CUF
2. Mhe. Katibu Mkuu Taifa CUF
3. Mhe. Spika, Baraza la Wawakilishi – Zanzibar
4. Mhe. Waziri wa Nchi (AR/MBLM) – Zanzibar
5. Waheshimiwa Wajumbe wote wa CUF, BLW
6. Katibu,Baraza la Wawakilishi – Zanzibar
7. Afisa Mdhamini,Baraza la Wawakilsihi- Pemba

Advertisements

5 thoughts on “Kauli ya Mhe. Abubakar Khamis Bakary kuhusu kujiuzulu kwa Mhe. Abbas Juma Muhunzi

 1. Pingback: Fisadi wa CUF huyu hapa...! - JamiiForums |The Home of Great Thinkers

 2. It reminds me what MALCON X said., THE CHICKENS ARE BACK TO ROOST.
  ikiwa huyu bwana muhunzi vituko vyake mlivijua tangu mwanzo kwa nini mlimbeba?
  Its too late now the devil already is out of the pot

 3. Pingback: Fisadi wa CUF huyu hapa...! - Page 2 - JamiiForums |The Home of Great Thinkers

 4. Kawaida huwezi kumjuwa mnafik at the 1st sight, lakini Mungu hamfichi mnafik, huyu alijivika ngozi ya kondoo, sasa Mungu anamfedhehi, dhulma kafara!!! sasa dhulma imezidi na haiwezi kudumu kwani ikidumu huangamiza.
  CUF MEMBERS Be careful of what you are saying BEHIND THE DOORS and doing! Mnatarajia kuwa na Serikali, ninavyofahamu watu wa serikali wanakuwa makini katika utunzaji wa SIRI, na wanajuwa wanachokifanya, otherwise mtajikuta nyote mmo ndani ya minyororo ya kutapatapa katika kukata roho!!!

 5. Inasikitisha tu kuona mtu aliyepewa wadhifa kama huu na asiweze kuwajibika ipasavyo. Mitihani kila aina inatokea na Insha’Allah mafanikio yapo karibu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s