CUF wasikitishwa na Kikwete

Na Asha Bani

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesikitishwa na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa kuchukua maamuzi thabiti ya kuhakikisha utekelezwaji wa makubaliano ya Kamati ya Mazungumzo ya Muafaka yaliyofanyika Desemba 30 mwaka 2005.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana wakati wa kutoa maazimio ya mkutano mkuu uliofanyika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema CUF inasikitishwa na hatua hiyo kwa kutambua kuwa Rais Kikwete aliahidi kumaliza matatizo ya muafaka wakati akihutubia kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa rais.

Alisema kuwa Rais Kikwete kwa mara kadhaa alikuwa akinukuliwa akiahidi kuupatia ufumbuzi wa haraka mpasuko wa kisiasa Zanzibar kabla ya kumaliza kipindi chake cha urais mwaka 2010.

Profesa Lipumba alisema CUF ikiwa chama mbadala haitakubali kurudi katika meza ya mazungumzo yaliyokwishamalizika, kinachotakiwa ni Rais Kikwete kuingilia kati kwa kuwakutanisha wadau wakuu wa kisiasa Zanzibar ambao ni Rais Amani Abeid Karume na Katibu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ili waweze kupanga utaratibu wa utekelezaji na kuwekeana saini makubaliano hayo.

“Chama cha CUF hakitakubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo yaliyokwishamalizika, labda rais kama anaona kutakuwa na umuhimu wa hilo awakutanishe wagombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif na Rais Karume,” alisema Profesa Lipumba.

Katika maazimio ya chama hicho, pia waliitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kukilipa chama hicho zaidi ya shilingi bilioni 2.2 kama malipo yaliyokwama kufanyika tangu mwaka 1995.

Alisema kuwa mbali na jitihada zilizofanyika za kutaka malipo hayo kulipwa kwa wakati, hakuna kitu chochote kilichofanyika, jambo linaloonyesha urasimu kwa kuwa CCM wao wanaendelea kulipwa ruzuku zao kama kawaida.

“CCM wanaendelea kulipwa ruzuku zao bila usumbufu, lakini sisi tunaendelea kusumbuliwa, tunaogopa suala hili kulipeleka mahakamani kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wakatuzungusha bila kupata mafanikio yoyote kwa vile mahakama zetu zinajulikana zilivyo,” alisema Profesa Lipumba.

Akizungumzia kuhusu ubadhirifu wa rasilimali za umma na vitendo vya ufisadi nchini, alisema kuwa CUF inalaani ‘usanii wa kisiasa’ unaofanywa na serikali kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti za kupambana na ufisadi uliotokana na kashfa ya malipo ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na manunuzi ya rada yaliyofanywa kwa dola milioni 40.

Alisema mbali na ufisadi huo, kuna wa ujenzi wa minara pacha ya Benki Kuu (BoT), manunuzi ya ndege ya rais na helkopta za jeshi ikiwa ni pamoja na mikataba mibovu isiyozingatia maslahi ya taifa.

Maazimio mengine ni kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ambapo wamemtaka Jaji Lewis Makame, kujiuzulu uenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa kushindwa kusimamia vyema chaguzi mbalimbali za marudio ya majimbo ikiwa ni pamoja na Tunduru, Tarime, Kiteto na Mbeya Vijijini.

Alisema kuwa kuna dosari nyingi katika marekebisho ya daftari la wapiga kura badala ya kuboreshwa kwa makusudi na kwa malengo wanayojua NEC, limeharibiwa na kutokuwa na mpangilio madhubuti.

Aidha, Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif Hamad, ametangaza maazimio ya kuundwa kwa kurugenzi mpya ikiwa ni pamoja na kuwa na Kurugenzi ya Utawala, Fedha na Uchumi, Oganaizesheni na Uchaguzi, Siasa Haki za Bindamu na Sheria, Uenezi na Mahusiano ya Umma na Ulinzi na Blue Guards.

Katika kuunda kurugenzi hizo pia kumefanyika mabadiliko mbalimbali ya viongozi wake ikiwa ni pamoja na kubwagwa kwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Winlfred Lwakatare ambaye sasa anakuwa mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Wakati huo huo, majina ya nafasi za wakurugenzi wa kurugenzi mbalimbali za chama hicho yaliyotangazwa jana na Maalim Seif, yalimtaja Joran Bashange kuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa Bara na Ukurugenzi wa Utawala, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi Juma Duni Haji, Naibu Mkurugenzi wa Utawala, Nassor Ahmed Mazrui.

Wengine ni Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Salim Mandari, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi, Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Siasa, Mbaralah Maharagande, Naibu Mkurugenzi wa Siasa, Juma Ameir Muchi, Mkurugenzi wa Haki za Bindamu na Sheria, Julius Mtatiro ambapo naibu wake amekuwa Hemed Said Nassor.

Salim Biman amekuwa Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano ya Umma na naibu wake akiwa Ashura Mustafa, Masoud Abdallah Salim, Mkurugenzi wa Ulinzi na Blue Guard na Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Chama, ambapo naibu wake ni Mzee Rajabu Mazee.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif jana alitangaza nia ya kuwania nafasi ya urais ifikapo mwaka 2010, lakini alisema kuwa kwa hatua yake hiyo haimzuii mwanachama mwingine wa chama hicho kujitokeza kuchukua fomu ya nafasi hiyo.

Wakati Maalim Seif akitangaza nia yake hiyo, Prof. Lipumba alisema yeye bado hajafikia uamuzi wa kama atagombea nafasi hiyo ama la.

Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=2928

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s