“Janjaweed wavamia wakaazi wa Kinuni na kujeruhi”

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 5 Machi, 2009

Wapendwa Wanahabari,

Jana tulitoa ripoti ya awali ya namna uandikishaji wapiga kura unavyoendelea katika jimbo la Magogoni na kusema kwamba tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuliharibu zoezi hilo.

Leo tunatuma taarifa hii kwenu kuwajulisha kwamba sasa SMZ imeingia katika hatua nyengine ya pili ya kuuharibu uchaguzi huo kwa kutumia mtindo wake wa 2005 wa makundi ya Janjaweed kuvamia raia, kuwapiga na kuwajeruhi na kuwaibia mali zao kwa lengo la kujenga khofu.

Kuanzia saa 5.30 asubuhi na 8.15 mchana, Waziri wa Nchi (Afisi ya Waziri Kiongozi) Hamza Hassan Juma alikuwa katika eneo la Kinuni ambako alisimamia zoezi la Majanjaweed hao kuvamia na kupiga watu. Matokeo ya zoezi hilo ni kujeruhiwa kwa mapanga watu wawili, Abdallah Mohammed Khamis (47) na Juma Abdi Said (40). Wakati Abdallah amekatwa vidole vinne vya mkono na kichwani, Juma amekatwa kwa mapanga mikononi na mgongoni. Watu wengine watano walipigwa bakora na marungu. Juma na Abdallah wamelazwa katika hospitali ya Al Rahma, mjini Unguja.

Tunaambatanisha picha za majeruhi hawa na tunasisitiza kuwa watu wote hao walivamiwa katika majumba yao. Lengo ikiwa ni kuwatia khofu ili wasishiriki katika uandikishaji na hatimaye uchaguzi.

Sisi, Chama cha Wananchi (CUF), tunalaani vikali hujuma hizi na tunamuhusisha moja kwa moja Waziri Hamza na maafa yaliyotokezea. Damu ambayo imemwagika ina mkono wake. Pamoja na hayo, kwa kuwa Waziri Hamza ni mtendaji wa SMZ, tunachukulia kuwa ametekeleza agizo la serikali hiyo na kwamba, kwa ujumla, kilichofanyika Kinuni ni kazi ya SMZ.

Wapendwa Wanahabari,

Ikumbukwe kwamba mwaka 2005, SMZ ilifanya kazi kama hii katika eneo hili hili la Kinuni na sababu kubwa ni kuwa wakaazi wa eneo hilo wanaaminika na SMZ kwamba wamekataa kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kawaida katika siku za uchaguzi, hali ya usalama hufanywa kwa makusudi iwe mbaya na SMZ, na tunasikitika kwamba Jeshi la Polisi – ambalo ndilo lenye dhamana ya ulinzi wa raia na mali zao – limeanza kuwa sehemu ya uvunjifu wa usalama wa raia.

Leo hii, Jeshi hilo lilikamata vijana wawili, Bakari Ali Hamad na Khamis Ali Mwalimu, wakiwa nje ya mita 200 kutoka kituo cha uandikishaji cha Kinuni, wakawafungia kwenye hema na kuwapiga kwa bakora. Huku ni kuvunja sheria za ulinzi na usalama, ambazo zinataka mtu kutokuteswa wala kupigwa akiwa mikononi mwa Polisi, hasa katika mazingira ambapo mshukiwa hajakataa kutoa mashirikiano.

Kwa hili tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Said Mwema, kuingilia kati utendaji wa jeshi lake hapa Zanzibar ili asije akawa na lawama kama za mtangulizi wake, Omar Mahita, ambaye rikodi yake haipendezi.

Juu ya yote, tunawaomba wakaazi wa Kinuni na wenzao wote wa jimbo zima la Magogoni kuendelea kujitokeza kwa wingi kwenye uandikishaji. Hatimaye haki ndiyo itakayoshinda!

Pamoja na salamu za Chama

Imetolewa na:

Salim Bimani
Mkurugenzi
Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi)
Makao Makuu – Zanzibar
Simu: +255 777 414 112
Weblog: https://hakinaumma.wordpress.com
Website: http://cuf.or.tz

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s