Baada ya kuanguka Prof. Safari ashutumu wajumbe wa CUF kwa kumdhalilisha

Na Exuper Kachenje
Date::2/26/2009

SIKU mbili baada ya kuangushwa vibaya katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Abdallah Safari amesema wajumbe wa mkutano mkuu walimdhalilisha na kwamba anaandaa kitabu kueleza udhalilishaji huo.

Prof. Abdallah Jumbe Safari, mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa CUF Taifa

Prof. Abdallah Jumbe Safari, mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa CUF Taifa

Profesa Safari alitoa malalamiko hayo jana alipozungumza na Mwananchi kuhusu matokeo ya uchaguzi huo uliomrudisha madarakani Profesa Ibrahim Lipumba, aliyepata kura 646, huku mpinzani huyo akiambulia kura sita tu.

Wakati Profesa Safari akijieleza, wajumbe walikuwa wakimzomea na baadaye kumrushia maswali yaliyomtingisha, ikiwa ni pamoja na kutaka ataje jina la katibu wa tawi lake, swali ambalo alibabaika kulijibu.

“Nimedhalilishwa; nimezomewa; nimeulizwa maswali ya kipuuzi. Ule ni uhuni hakuna kitu pale,” alisema Profesa Safari.

“Wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF wamepotosha na kuharibu maana ya demokrasia ndani ya CUF na kutumia vibaya nafasi hiyo ya kuchagua viongozi.”

Alipobanwa kueleza iwapo anafikiria kuwania tena nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho, Profesa Safari alisema hawezi na hana nia ya kuwania uongozi wa chama hicho.

“Sifikirii wala sina nia tena ya kuwania nafasi yoyote ndani ya CUF. Nitakapoita mkutano na waandishi wa habari, nitaeleza mengi. Mbali ya kuzindua kitabu changu, nitaamua shauri la kufanya pamoja na kesi ya uanachama wangu,” alisema Profesa Safari.

Hata hivyo, wanasiasa wengine wanaona kuwa uchaguzi huo wa viongozi wa CUF umeonyesha kukomaa kisiasa.

Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema CUF imeonyesha demokrasia na kumpongeza Prof. Lipumba kwa ushindi wake wa asilimia 97.

“Inaonyesha jinsi wana CUF walivyo na imani naye. Uchaguzi wa CUF umeonyesha ukomavu wa demokrasia ndani ya chama hicho, nawapongeza pia wana CUF kwa hatua hiyo,” alisema Mrema.

Wakati huohuo, Said Salim anaripoti kuwa viongozi wapya wa CUF, wametoa salamu kali kwa CCM, wakisema kuanzia sasa suala la kuibiwa kura zao katika chaguzi mbalimbali nchini, limekwisha.

Wakizungumza mara baada ya kurejeshwa madarakani katika mkutano mkuu unaoendelea kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini hapa, viongozi hao walisema hawataruhusu tena wizi wa kura.

Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema atahakikisha anatumia ridhaa aliyopewa kukipanga chama na kuhakikisha kuwa wanashinda kila uchaguzi watakaoshiriki.

“Mfano mzuri wa kukataa kwetu kuibiwa kura tutaonyesha katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi katika jimbo la Magogoni Zanzibar… ni jimbo letu lakini tuliibiwa lakini lazima tuligomboe,” alisema Hamad.

“Tunasikia kuwa tayari CCM wameshaandaa kura zao kwa ajili ya kujazia lakini nawapa salamu kuwa, watakavyoipiga ndivyo tutakavyoicheza. Hakuna tena msalia Mtume katika kulinda kura setu”.

Aidha aliwataka wanachama wake kushikamana kwa pamoja na kumaliza tofauti zao ndani ya vikao vya chama ili wakitoka wafanye kazi kwa ushirikiano na mshikamano.

“Tumalize tofauti zetu ndani ya vikao vyetu, tukitoka nje tukisema tuvute kamba basi tuvute kwa pamoja, tukisema tuache tunaacha sote. Nitakuwa nanyi; sitawaangusha hadi tulifikishe jahazi bandarini salama salimini,” aliahidi Hamad.

Naye makamu mwenyekiti mteule wa CUF, Machano Khamis mabaye alikuwa mshitakiwa nambari moja katika kesi ya uhaini iliyokabili viongozi 17 wa chama hicho mwaka 1997 hadi 2001 alisisitiza, kwa kuwa CCM ni wababe na wao lazima wafanye ubabe ili kukataa wizi wa kura.

“Wizi wa kura sasa basi; ikiwa wao ni wababe na sisi ni wababe vilevile; wakitunisha misuli na sisi tutatunisha. Hatutafanya vinginevo kwa kuwa tukifanya vingine, CCM wataendelea kujenga kiburi,” alisistiza Khamis na kuongeza:

“Tukatae CCM kuchukua kura zetu kwa nguvu kwa kuwa wao hawana haki ya kutawala.”

Alisema, ameshakaa jela mara nyingi, kwa hiyo hana tena woga na yuko tayari hata kupoteza maisha kwa kulinda maslahi ya umma.

“Haya ya kuwa siogopi, ndugu wajumbe, yanathibitishwa na kugombea tena nafasi hii. Kwa mateso niliyoyapata kwa kukaa jela, kama ningekuwa muoga ningekwishakaa nje ya chama hiki,” alisema Machano.

“Katika uchaguzi huu, tumewafundisha CCM namna demokrasia inavyotakiwa. Katika chaguzi zao kuna rushwa, kupigana, kuchafuana na makundi lakini kwetu kuna amani, utulivu na upendo baina ya wanachama na wagombea.”

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema amepewa jukumu zito na uzito wake unatokana na chama dola kung’ang’ania madaraka hata kama hakitakiwi nchini.

Alisema, licha ya ugumu huo, atahakikisha kuwa katika awamu hii wizi wa kura unakoma katika chaguzi nchini na wataanzia katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi jimbo la Magogoni na ule wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu.

“Ndugu wajumbe uchaguzi wa Magogoni ndio utakuwa kipimo cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2010… kama tutakuwa na uchaguzi au mapambano; kama uchaguzi au uchafuzi,” alisema Prof. Lipumba.

Uchaguzi mdogo wa jimbo la uwakilishi la Magogoni la kisiwani Zanzibar umepangwa kufanyika Mei 23 baada ya kifo cha aliyekuwa mwakilishi wa Jimbo hilo, Daud Hassan Daud.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s